Tuesday, September 26, 2017

WAZIRI WA AFYA ATOA MIEZI 8 KILA HOSPITALI YA MKOA NA WILAYA KUJENGA JENGO LA HUDUMA ZA DHARULA.



Waziri wa Afya, Jinsia, Wazee na Watoto Umy Mwalimu ametoa miezi nane  kwa hospitali za mikoa na wilaya nchi nzima kuhakikisha wananjenga majengo ya kulea huduma za dharula katika hospitali hizo.

Waziri ummy Mwalimu ametoa agizo hilo mjini Bagamoyo, tarehe 25 Septemba 2017, alipokuwa akiweka jiwe la msingi jengo la huduma za dharula na jengo la wodi ya wazazi katika Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo.

Alisema wananchi wengi wanafariki kabla ya kufika kwa Daktari kutokana na kutokuwepo kwa majengo yanayotoa huduma za dharula katika Hospitali hizo.
alisema anatoa agizo hilo kuhakikisha kila Hospitali ya mkoa na Wilaya inaanza ujenzi wa majengo hayo na mwisho ni tarehe 30 juni 2018 kila Hospitali iwe imekamilisha ujenzi huo.

Ujenzi wa majengo ya huduma za dharula na wodi ya wazazi katika hospitali ya wilaya ya Bagamoyo umefadhiliwa na Taasisi ya Dhi nureyn na kwa kushirikiana na wahisani kutoka saudi Arabia 

Aidha, ujenzi huo ambao utagharimu shilingi milioni mia tani unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba mwaka huu.

Wakati huohuo Waziri Ummy Mwalimu alisema amekipandish hadhi kituo cha Afya cha msoga na kuwa Hospitali na kwamba kilichobaki ni kukabidhi rasmi Barua ya kupandisha hadhi kituo cha Msoga.

Awali Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Alhaj, majid Mwanga alimuomba Waziri wa Afya, kukipandisha hadhi kituo cha afya ili iwe Hospitali kutokana na kukuwa kwa mji wa Chalinze.

Mkuu wa wilaya pia alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungno wa Tanzania Dkt. john Magufuli kwa kukabidhi majengo yaliyokuwa yanatumika na Tan Roads huko msata ili yatumike kwa Halmashauri ya Chalinze.
Alisema kutokana na kufunguliwa kwa Barabara ya Msata Bagamoyo majengo ayo wanakusudia kufanya kituo cha Afya ambacho kitawahudumia wananchi wa Msata na wapita njia.

Waziri Ummy Mwalimu pia amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo kwa kutafuta wafadhili waliofanikisha ujenzi wa majengo ya huduma za dharula na wodi ya wazazi.
Watendaji kutoka Dhi nureyn, Kamati ya ulinzi na Usalama wilaya ya Bagamoyo pamoja na viongozi mbalimbali wa Halmashauri ya Bagamoyo wakifuatilia shughuli ya uwekaji jiwe la msingi katika majengo ya wodi ya wazazi na jengo la huduma za dharula katika Hospitali ya Wilaya bagamoyo.

Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Alhaj, majid Mwanga akizungumza katika shughuli hiyo iliyofanyika viwanja vya Hospitali ya wilaya ya Bagamoyo.

DKT.KIGWANGALLA AKABIDHI GARI LA WAGONJWA MKURANGA



Naibu waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mh. Dk. Hamisi Kigwangalla mapema jana Mei 28.2017 amekabidhi gari maalum la kubebea wagonjwa (Ambulance) na vifaa vya Hospitali ikiwmo vitanda na Magodoro katika Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga, Mkoani Pwani.

Dkt. Kigwangalla ambaye alikuwa mgeni rasmi katika tukio hilo, mbali na kukabidhi gari hilo la wagonjwa na vifaa hivyo vya Hospitali kwa uongozi wa Hospitali na Wilaya akiwemo Mkuu wa Wilaya na Mbunge wa Jimbo hilo, aliweza kufanya ukaguzi wa ghafla kujionea mazingira ya Hospitali hiyo na kubaini mapungufu mbalimbali ambayoo ametoa maagizo kupatiwa ufumbuzi kabla ya kuchukuliwa hatua kwa uongozi wa Hospitali hiyo.

Miongoni mwa changamoto hizo alizobaini katika Hospitali hiyo ni pamoja na kuwa na mfumo mbovu wa uhifadhi wa taka, pamoja na uchafu katika wodi ya wazazi jambo ambalo linaweza kusababisha hatari ya maambukizi kwa Wagonjwa na wahudumu wenyewe wa Afya.

Awali wakati wa kukabidhi gari hilo ambalo limenunuliwa kwa nguvu ya Madiwani kwa kushirikiana na wadau mbalimbali pamoja na Mbunge wa jimbo hilo la Mkuranga, Abdallah Ulega aliwataka kulitumia kwa uangalifu wa hali juu huku likitakiwa kufanya shughuli zilizokusudiwa katika kusaidia wananchi wake.

“Nimesikia kileo chenu ambacho ni kupatiwa mashine ya X-Ray na na vifaa vingine muhimu. Wizara yetu inalishughulikia hilo na tunawaomba muwe na imani na Mbunge wenu ambaye amekuwa akinisisitiza juu ya jambo hilo. 

Hospitali ya Mkuranga ni moja wapo ambayo itafaidika na msaada wa vifaa ikiwemo mashine hiyo ya X-Ray” alisema Dkt. Kigwangalla wakati akizungumza na wananchi mbalimbali ambao pia walipata fursa ya kuuliza maswali katika tukio hilo.

MWAKYEMBE ATAKA MKANDARASI MPYA WAKUTOA TIKETI UWANJA WA TAIFA.

PICHA 1
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (aliyevaa kofia ya pama) akisalimiana na baadhi ya Viongozi wanaosimamia Uwanja wa Nangwanda Mtwara wakati alipofanya ziara kujionea changamoto katika uwanja huo 25 Septemba, 2017 Mkoani Mtwara.
PICHA 2
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (aliyevaa kofia ya pama) akiongea na baadhi ya Viongozi wanaosimamia Uwanja wa Nangwanda Mtwara wakati alipofanya ziara kujionea changamoto katika uwanja huo 25 Septemba, 2017 Mkoani Mtwara.
 PICHA 3
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (aliyevaa kofia ya pama) akiangalia eneo la uwanja wa mpira wa miguu akiwa na baadhi ya Viongozi wanaosimamia Uwanja wa Nangwanda Mtwara wakati alipofanya ziara kujionea changamoto katika uwanja huo 25 Septemba, 2017 Mkoani Mtwara.

 PICHA ZOTE NA BENEDICT LIWENGA-WHUSM
 .................................................

Na Benedict Liwenga-WHUSM.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe amesema kwamba pindi Uwanja wa Taifa Dar es Salaam utakapokamilia kufanyiwa ukarabati atahakikisha anapatikana Mkandarasi Mpya mwenye vigezo na ambaye ataleta mabadiliko hususani katika utoaji tiketi kulingana na namba za viti vilivyopo ndani ya Uwanja huo.

Kauli hiyo ameitoa jana Mkoani Mtwara wakati alipotembelea Uwanja wa Mpira wa Miguu wa Nangwanda ili kujionea miundombinu ya uwanja huo ikiwemo baadhi ya changamoto zinazoikabili kiwanja hicho.

Dkt. Mwakyembe ameeleza kwamba, kumekuwa na changamoto ya kutofahamika idadi kamili ya watu wanaoingia ndani ya uwanja hali inayopelekea watu kukaa ovyo katika sehemu zisizo rasmi na wengine kulundikana nje ya uwanja wakati pesa za viingilio wamelipia ambapo ameweka wazi kuwa hali hiyo inasababishwa na urataibu mbovu wa utoaji tiketi.

Akiongea na Uongozi wa Uwanja huo wa Nangwanda Mkoani hapo alisema kwamba, kwakuwa sasa Uwanja wa Taifa uko katika ukarabati, pindi utakapokamilika Mkandarasi mpya lazima apatikane ili pindi mtu anunuapo tiketi yake iendane na kiti chake atakachokaa na sio vinginevyo kwakuwa kwa kufanya hivyo kutasaidia kuboresha sura za viwanja nchini.

“Napenda kusisitiza suala hili kuwa, ntahitaji apatikane Mkandarasi atakaetoa tiketi kulingana na siti atakayokaa mtazamaji wa mpira, kwasababu kumekuwa na kero kubwa katika utoaji tiketi hapo mwanzo jambo ambalo halileti sura nzuri kwa jamii”, alisema Dkt. Mwakyembe.

Aliongeza kuwa Watanzania hawanabudi kuiga mifano ya nchi nyingine ambazo zimejidhatiti katika masuala ya utoaji tiketi wakati wa michezo.

Sambamba na hayo, Waziri Mwakyembe ameupongeza uongozi wa uwanja huo kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuutunza uwanja wa Nangwanda huku akiaihidi kuzifikisha changamoto za uwanja huo katika Viongozi wa Juu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ili waweze kushirikiana kwa pamoja kuona namna ya kuzitatua.

Uwanja wa Nagwanda ulianzishwa miaka ya 1980 ambapo awali ulikuwa ukiitwa jina la Uwanja wa Umoja Mtwara na baadaye kupewa jina la Uwanja wa Nagwanda lililotokana na jina la mtu maarufu wakati huo.