Thursday, August 6, 2026
Friday, July 17, 2026
JAB YAPOKEA OMBI LA KUTOA MAFUNZO KWA BLOGGERS ZAIDI YA 200
Na Mwandishi Wetu, JAB
Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imepokea ombi kutoka Mtandao wa Mabloga Tanzania (TBN) la kutoa mafunzo kwa wanachama wake zaidi ya 200 kuhusu Sheria ya Huduma za Habari, Maadili ya Uandishi wa Habari na umuhimu wa kupata ithibati.
Ombi hilo limetolewa leo, tarehe 16 Julai, 2026, na Mwenyekiti wa Mtandao wa Mabloga Tanzania, Bw. Beda Msimbe, alipokutana na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JAB, Wakili Patrick Kipangula, katika mazungumzo yaliyofanyika katika ofisi za Bodi jijini Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya mazungumzo hayo, Wakili Kipangula amesema Bodi imepokea ombi hilo na iko tayari kushirikiana na Mtandao huo katika kuwawezesha bloga kupata uelewa wa kina kuhusu Sheria ya Huduma za Habari, maadili ya taaluma pamoja na umuhimu wa kupata ithibati.
Amesema mafunzo hayo yataanza kutolewa kwa bloggers wenye ithibati ili kuimarisha weledi na uelewa wao wa majukumu ya kitaaluma, kabla ya kuendelea kuwafikia wale ambao bado hawajapata ithibati.
"Wale ambao hawana ithibati watapata fursa ya kuelekezwa kuhusu masharti ya kisheria ya kupata ithibati, ikiwemo umuhimu wa kuwa na sifa zinazotakiwa kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari. Wasio na sifa stahiki watashauriwa kujiendeleza kielimu ili waweze kukidhi vigezo vya kupata ithibati," amesema Wakili Kipangula.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtandao wa Mabloga Tanzania, Bw. Beda Msimbe, amesema mafunzo hayo yatawasaidia wanachama wa chama hicho kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, maadili na weledi, sambamba na kuchangia kwa ufanisi katika kuhabarisha umma na kuitangaza Tanzania kupitia taarifa za maendeleo zinazotekelezwa katika sekta mbalimbali.
Amesema ushirikiano kati ya Mtandao huo na JAB utasaidia kujenga uwezo wa bloggers na kuimarisha mchango wao katika sekta ya habari nchini.
Tuesday, June 23, 2026
TANROADS YATANGA BARABARA SITA ZA PPP KUUNGANISHA MIKOA YA DAR, PWANI, DODOMA, SINGIDA NA TANGA KM 969
Katika hatua
nyingine kubwa ya kuharakisha maendeleo ya miundombinu na kuimarisha ukuaji wa
uchumi wa Taifa, Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) umetangaza fursa za
uwekezaji katika miradi sita mikubwa ya barabara yenye urefu wa kilomita 969
kupitia mfumo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP).
Tangazo hilo
la kimataifa la kutafuta wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kwa ajili ya
kubuni, kujenga, kugharamia, kuendesha, kutunza na hatimaye kukabidhi miradi
hiyo kwa Serikali kupitia mfumo wa Design, Build, Finance, Operate, Maintain
and Transfer (DBFOMT), linaendelea kudhihirisha dhamira ya Serikali ya Awamu ya
Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutumia nguvu ya sekta binafsi
kuharakisha utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo.
Hatua hiyo
pia inaakisi mafanikio ya mageuzi makubwa yanayosimamiwa na Kituo cha Ubia kati
ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC) chini ya Mkurugenzi Mtendaji David
Kafulila, ambaye amekuwa mstari wa mbele kuhamasisha ushiriki wa sekta binafsi
katika uwekezaji wa miundombinu na huduma za kijamii nchini.
Miradi
iliyowekwa mezani kwa wawekezaji ni pamoja na upanuzi wa Barabara ya
Morogoro–Dodoma yenye urefu wa kilomita 260 kuwa njia nne, Barabara ya
Handeni–Kiberashi–Chemba–Kwamtoro–Singida yenye kilomita 384, upanuzi wa
Barabara ya Chalinze–Segera–Tanga yenye kilomita 246 kuwa njia nne pamoja na
ujenzi wa Kitonga Escarpment Bypass yenye kilomita 27.
Miradi
mingine ni Dar es Salaam Port–Kibaha Expressway yenye kilomita 42 na Dar es
Salaam CBD–Julius Nyerere International Airport Expressway yenye kilomita 10.
Kwa mujibu
wa TANROADS, miradi hiyo inalenga kupunguza msongamano wa magari, kuboresha
usafirishaji wa watu na mizigo, kuongeza ushindani wa uchumi wa Tanzania na
kuimarisha nafasi ya nchi kama kitovu cha biashara na usafirishaji katika
ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Kwa ujumla,
miradi hiyo ina urefu wa kilomita 969. Kwa makadirio ya wastani ambapo kilomita
moja ya barabara inaweza kugharimu takribani Dola za Marekani milioni moja sawa
na karibu tsh trilioni tatu za Kitanzania kwa zote.
TWPF YAKAGUA ENEO LAKE LA KIMKAKATI DODOMA
Na Oscar
Mbuza, MNRT
BODI ya
Mfuko wa Kuhifadhi Wanyawapori (TWPF) imetembelea kiwanja kinachomilikiwa na
Mfuko huo eneo la Njedengwa katika
Manispaa ya Dodoma ambacho kitapangiwa matumizi yake hivi karibuni.
Msafara wa
Bodi hiyo umeongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya TWPF Profesa Jafari Kideghesho
akiambatana na Mkurugenzi wa Idara ya
Wanyamapori, Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Alexander Lobora na baadhi ya
wajumbe wa Bodi.
Wajumbe
wengine ambao wameshiriki ziara hiyo ni
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) Dkt.
Eblate Mjingo na Kamishna wa Uhifadhi
kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) Mlage Kabange.
Aidha ujumbe
huo pia ulimjumuisha Kamishna Msaidizi
Mwandamizi wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCCA),
Victoria Shayo aliyemwakilisha Kamisha wa Uhifadhi wa NCCA.
Akizungumza
baada ya kukagua eneo hilo lililopo Kitalu Namba 16, lenye ukubwa wa mita za
mraba 39,700, Profesa Kideghesho amesema ameridhishwa na usimamizi na uhifadhi
wa kiwanja hicho ambacho kitapangiwa matumizi yake hususani kwenye maendeleo ya
uhifadhi wa wanyamapori hivi karibuni.
Naye
Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Wanyamapori, Wizara ya Maliasili na Utalii,
Dkt. Lobora amesema wizara italitumia eneo hilo kama eneo la mkakati la
uendeshaji wa shughuli za uhifadhi wa wanyamapori nchini.
Mfuko wa
Hifadhi ya Wanyamapori Tanzania ni wa kudumu maalum kwa ajili ya kusaidia
kutatua baadhi ya changamoto zinazohitaji fedha kwenye uhifadhi.
Madhumuni ya
Mfuko ni kurahisisha na kusaidia uhifadhi wa wanyamapori, ndani na nje ya
maeneo yaliyohifadhiwa. Bodi ya TWPF ina wajumbe tisa.
Monday, June 22, 2026
KATAMBI AWAONYA WAHALIFU NA MAANDAMANO HARAMU YA TAREHE 07
Waziri wa
Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi amewaasa watu wanaotoa kauli za
kichochezi katika mitandao ya kijamii, majukwaa ya kisiasa na maeneo mbalimbali
ambapo kauli hizo za kibaguzi na kichochezi zinahusu Muungano wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Viongozi mbalimbali wa serikali au wa dini.
Waziri
Katambi ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na waumini wa Msikiti wa Mukadam uliopo
Kata ya Chang’ombe iliyopo wilaya ya Dodoma Mjini ambapo kumefanyika Mashindano
ya Quran na Harambee ya Ujenzi wa Msikiti huo.
“Taifa hili
limejengwa kwa maumivu makubwa ya waasisi, limejengwa kwa jasho na hata damu
ilipobidi ili Taifa Tanzania liwepo, nitumie fursa hii kuwaomba sana na kuwaasa
wale wote ambao wanatumia majukwaa ya kisiasa kuchonganisha wananchi, kuwajaza
chuki, kuchochea lakini pia kuhamasisha kufanya uhalifu na wanaounda magenge ya
uhalifu yanayolenga kuharibu taifa letu, niwasihi na kuwaomba waache mara moja
kwasababu kufanya hivyo hakuna ambae atabaki salama tutaathirika sisi
Watanzania wote na athari hii italiathiri taifa kisiasa, kiuchumi na
kiutamaduni.” amesema Waziri Katambi.
“Tutarudi
nyuma kimaendeleo,tutashindwa kuswali, tutashindwa kwenda kanisani, tutashindwa
kufanya kazi za kiuchumi, tutashindwa kujenga nchi yetu, tutashindwa kujenga
uchumi wa mtu mmoja mmoja, tuwakanye na kuwaelekeza vijana wetu wakaishi
mwenendo mwema na uzalendo kwa taifa lao na pale yanapotolewa maonyo na
maelekezo ya vyombo vya ulinzi na usalama wasikaidi kwani kwenda kinyume ni
kuvunja sheria, katiba na taratibu.” aliongeza Waziri Katambi.
VIONGOZI WA REA ZAMBIA, WAWASILI TANZANIA KWA ZIARA YA KIKAZI
Viongozi wa
Mamlaka ya Nishati Vijijini (REA) kutoka nchini Zambia wamewasili nchini kwa
ajili ya ziara ya kujifunza na kubadilishana ujuzi na Wakala wa Nishati
Vijijini (REA).
REA Zambia
ambao wameongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Zambia anayeshughulikia
Umeme, Mhandisi Arnold Simwaba wamewasili Tanzania Juni 21, 2026 katika Uwanja
wa Kimataifa wa Julius Nyerere na kupokelewa na Mwakilishi wa Katibu Mkuu
Wizara ya Nishati Tanzania, Wilson Nyamanga pamoja na Mkurugenzi wa Umeme
Vijijini kutoka REA Tanzania, Mhandisi Jones Olotu, Mkurugenzi wa Rasilimali
Watu na Utawala wa REA Tanzania, Renatus Msangira.
Uongozi wa
REA Zambia utakuwa nchini kwa ziara ya kikazi ya Siku 7 ambapo pamoja na vikao
vya kubadilishana ujuzi, wajumbe hao wanatarajiwa kutembelea miradi mbalimbali
ya umeme vijijini inayotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini.
Saturday, June 20, 2026
SERIKALI YAAHIDI KUSIMAMIA HAKI ZA WAKIMBIZI
Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
Serikali ya Tanzania imeahidi
kuendelea kulinda, kusimamia na kutekeleza haki za binadamu ikiwemo haki za
raia wa Tanzania na Wakimbizi kutoka nchi mbalimbali wanaohifadhiwa hapa nchini
ambapo pia imesema itaendelea kusimamia Amani na Usalama ili madhila
yanayotokea katika nchi nyingine yasitokee hapa nchini.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es
Salaam na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mheshimiwa Patrobas Katambi (MB)
wakati akizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi Duniani ambayo
huadhimishwa kila ifikapo Tarehe 20 ya mwezi Juni, kila mwaka, huku kauli mbiu
ya mwaka huu ikisema “Hadi Kila Mtu awe Salama”
Waziri Katambi akizungumza mbele ya
Wakimbizi wanaoishi jijini Dar es Salaam ambao waliwawakilisha wakimbizi
wanaoishi katika maeneo mbalimbali nchini amesema nchi ya Tanzania inajifunza
kwa yaliyotokea nchi jirani huku akitoa ahadi ya serikali ya kuwahudumia
Wakimbizi.
“Ni agizo la Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia,
watu wote ambao ni ndugu zetu Wakimbizi waliohifadhiwa hapa tutawahudumia hata
pale itakapohitajika rasilimali za nchi yetu tutazitumia, Rais wetu amekua
anafanya hivyo wakati wote hata pale tulipokosa ufadhili na fedha za wadhamini,
UNHCR aliendelea kutushika mkono lakini wapo wengine ambao hawakupata
tuliwaombea kwa Mwenyezi Mungu ili wapate waongeze nguvu lakini zilipokosekana
kabisa Rais wetu hakusita kuweka mkono wake ili Wakimbizi muendelee kuishi kwa
amani na utulivu, tunawapenda ndugu zetu, mmetupa uzoefu mmetupa mifano na
uhalisia na sisi tunajifunza kutoka kwenu” amesema Waziri Katambi
“Mmeeleza sababu zilizopelekea
kukosekana kwa Amani katika nchi zenu, zipo sababu ambazo pengine zinafanana na
zenu ikiwemo rushwa, kujipatia fedha kwa manufaa binafsi, utakatishaji fedha, ukwepaji
kodi na magendo yanayonufaisha wachache na kuumiza walio wengi, ubadhilifu, wizi
wa mali za umma, kughushi na kufanya udanganyifu, uhalifu wa kiuchumi, makosa
yanayoweza kuhatarisha amani ya nchi, uhaini, uchochezi wa vurugu, vurugu za
kisiasa, vyeo na mali, ubaguzi wa kidini, kikabila na ukanda, utapeli na dhulma
kwa wananchi, unyanyasaji wa kijinsia.” aliongeza Waziri Katambi
Waziri Katambi amesema Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Katiba ya Mwaka 1977 na marekebisho
yake chini ya Uongozi wa Dkt.Samia Suluhu Hassan ambae ni Rais na Amiri Jeshi
Mkuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Bunge na Mahakama wataendelea kusimamia
haki za binadamu, utii wa sheria, maslahi ya wananchi wote wakiwepo Wakimbizi.
Tuesday, March 24, 2026
Monday, March 23, 2026
SERIKALI YAHIMIZA MELI YA NEW MV MWANZA KUKUZA UCHUMI, UTALII KANDA YA ZIWA.
Serikali imetoa wito kwa wafanyabiashara, wasafirishaji na wawekezaji mbalimbali kutumia fursa ya meli mpya ya MV New Mwanza kibiashara na kiutalii ili kukuza uchumi wa Kanda ya Ziwa.
Itakumbukwa meli hiyo imejengwa kwa zaidi ya Tsh. Bilioni 120, ikiwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200, tani 400 za mizigo, magari makubwa matatu na madogo, ambapo itafanya safari zake katika bandari zote zinazozunguka Ziwa Victoria ikiwemo Kisumu (Kenya), Port Bay (Uganda) na Kemondo (Bukoba).
Akizungumza Jumapili Machi 22, 2026 na waandishi wa habari katika bandari ya Mwanza Kusini jijini Mwanza ilipoegeshwa meli hiyo, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema kutokana na uwekezaji huo wakazi wa Kanda ya Ziwa, wawekezaji na wafanyabiashara wakubwa na wadogo wanapaswa kuitumia kwenye shughuli zao na kuleta tija ya uwekezaji huo mkubwa.
Amesema Serikali imetimiza jukumu lake la kutekeleza wajibu wa kujenga mazingira mazuri ya biashara, uwekezaji na ustawi wa jamii, hivyo mpira sasa unahamia kwa wananchi kuitumia ili kulinufaisha taifa na malengo yaliyokusudiwa yafikiwe.
"Nawaombeni mkiiona New MV Mwanza, oneni suluhuhisho la uhakika la usafiri na usafirishaji wa abiria na mizigo, oneni fursa muhimu na adhimu ya utalii" amesema Msigwa na kuongeza;
"Serikali inategemea kuona utalii unakua kwa kasi hapa Mwanza, Bukoba na kwingine, watalii waje hapa Mwanza kisha waingie Serengeti, waende Rubondo, Burigi- Chato na kwingineko" amesema.
Ameongeza kuwa, wafanyabiashara na wawekezaji wanapaswa kuiona meli hiyo kama suluhisho la uhakika la kukua kwa biashara mbalimbali za madini, samaki, pamba, nyama na maziwa.
"Katika kanda ya Ziwa, amkeni mkamate biashara za maeneo yote ambayo yanazungukwa na Ziwa Victoria - Tanzania, Kenya, Uganda na kote ambako uwepo wa meli unarahishisha mambo, pia fursa zilizopo DRC, Sudan Kusini, Rwanda, Burundi" amesisitiza Msigwa.
Kwa mujibu wa Msigwa, mafanikio ya ujenzi wa meli hiyo ni moja ya mambo makubwa ya kujivunia kwa watanzania wakiwa na kila sababu ya kutembea kifua mbele kwa kuwa na serikali yenye maono na dhamira ya kuwekeza katika mambo makubwa ambayo yatatoa mchango mkubwa katika mageuzi ya kiuchumi.
"Hii inafanya meli hii sio tu kuwa kubwa kuliko zote katika ziwa Victoria na maziwa makuu bali pia hii ndiyo meli kubwa kuliko zote katika maji baridi barani Afrika" amesema



.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)












.jpeg)











































