Monday, December 8, 2025
TANZANIA NA MAREKANI ZASONGA MBELE KUKAMILISHA MAKUBALIANO MAKUBWA YA UWEKEZAJI
TPA YASAINI MAKUBALIANO KUANZA UJENZI WA BANDARI YA BAGAMOYO
Na Albert Kawogo
MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania ( TPA) imesaini hati ya Makubaliano ( MoU) na Kampuni ya Africa Global Logistics ( AGL) Tanzania Ltd yenye Makao Makuu yake Nchini Ufaransa ambayo ni kampuni tanzu ya MSC, kwa ajili ya usanifu, Ujenzi na uendeshaji wa gati mpya tatu katika Bandari ya Bagamoyo.
Hati hii ya makubaliano ( MoU) imesainiwa tarehe 6 Disemba,2025 Makao Makuu ya TPA Jijini Dar es Salaam kati ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA Bw. Plasduce Mbossa na Rais wa AGL Philippe Labonne.
Bw. Mbossa amesema, kusainiwa kwa hati ya Makubaliano ni ishara ya utayari wa kuanza kwa mradi wa Bandari mpya ya Bagamoyo ambapo kwa kuanzia AGL itaanza usanifu na Ujenzi wa gati tatu mpya za Kisasa kati ya 28 zinazotatajiwa kujengwa katika Bandari hiyo pamoja na gati mbili mpya za Kisasa katika Bandari ya Dar es Salaam.
“Tunategemea kuanza Ujenzi wa gati mpya tatu katika Bandari ya Bagamoyo mapema mwezi Januari na pia tunawakaribisha Wawekezaji wengine wa ndani na wa nje katika Mradi huo ambapo lengo ni kuleta mapinduzi makubwa katika Shughuli za Kibandari Nchini” Amesema Bw. Mbossa.
Kwa upande wake Rais wa AGL Bw. Philippe Labonne anasema wameamua kuingia makubaliano na TPA na kuwekeza Tanzania kutokana na kuwa nchi yenye Amani, Usalama na mazingira bora na tulivu ya uwekezaji iliyosehemu sahihi kijiografia kwa Sekta ya Uchukuzi na kuwa lango la Biashara Kitaifa na kimataifa.
“ Ninaamini Tanzania ni nchi inayokuwa kwa kasi kimaendeleo ikiwa na mtaji Mkubwa wa watu wakatimu na mtazamo Chanya na pia ni lango la kuingilia nchi nyingi barani Afrika na kuyafikia masoko ya kimataifa, Naamini ushirikiano huu utafungua mambo mengi ikiwemo kutengeneza Ajira ambazo ni muhimu sana kwa maendeleo ya Mtu mmoja mmoja na Taifa kwa Ujumla” Amesema Bw. Labonne.
Mradi wa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo kwa gati mpya tatu utajengwa kwa miezi 36 ( miaka mitatu) na Kampuni ya AGL imepata nafasi hii ya kushirikiana na TPA katika Ujenzi huo kutokana na uzoefu wao kama kampuni kubwa ya huduma za usafirishaji na logistiki, inayotoa huduma kamili za usafirishaji, usimamizi wa mizigo, usafirishaji wa kimataifa na huduma za forodha, ikihudumia sekta mbalimbali kama uchimbaji, mafuta, chakula, na misaada ya kibinadamu, ikiwa sehemu ya kundi la kimataifa la AGL (zamani Bolloré T&L) na sasa wakiwa chini ya MSC.
Wednesday, December 3, 2025
BARA LA AFRIKA TUNAHITAJI WANAHABARI MAHIRI KUKUZA SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UBUNIFU.
Na Veronica Mrema - Pretoria
Uandishi wa habari za sayansi kwa umakini na umahiri ni nyenzo muhimu ili kufikisha ujumbe sahihi kwa jamii, kusaidia kukuza maendeleo ya tafiti na vumbuzi mbalimbali.
Bara la Afrika bado lina uhitaji mkubwa wa waandishi wa habari ambao wamejikita na wapo na umahiri katika kuwasilisha masuala ya sayansi kwa lugha rahisi zinazoeleweka kwa jamii.
“Kazi yoyote ile tunayoifanya [katika] sayansi ina maana tu pale inapofahamika vizuri kwa watu na jamii nzima,”.
Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu wa Afrika Kusini Profesa Blade Nzimande amesema hayo alipokuwa akifungua rasmi Mkutano wa 13 wa Waandishi wa Habari za Sayansi Duniani.
Mkutano huo WCSJ2025 unafanyika Pretoria Afrika Kusini kuanzia Disemba 1-5, 2025 ukiwa na kauli mbiu isemayo 'Uandishi wa sayansi, unaojenga uelewa na uthabiti wa sayansi na haki za kijamii'.
“Nilipoombwa kuja kufungua mkutano huu nilikubali mara moja kwa sababu ya umuhimu wa nafasi ya waandishi wa habari za sayansi katika kukuza sayansi,” amesema.
Ameongeza “Kwa hiyo waandishi wa habari ni daraja muhimu sana [lakini] hatusemi daraja lisilo na ukosoaji, hapana bali daraja muhimu la kuielimisha jamii kuhusu sayansi.
“Kama bara, tunahitaji waandishi wa habari za sayansi wengi kwa sababu bado tunalo jukumu la kuendeleza sayansi, teknolojia na ubunifu barani Afrika.
“Na mawasiliano ni sehemu muhimu ya hilo. Kwa mfano, tunayo mkakati wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kwa Afrika [STISA 2034].
“.., ambao unalenga kukuza sayansi, utafiti na maendeleo barani Afrika jambo muhimu sana. Kwa hiyo tunathamini kazi mnayofanya, na ni muhimu sana,” amesema.
Amesema waandishi wa habari wanapaswa kusaidia Bara la Afrika kupambana na dhana potofu na ubaguzi katika namna sayansi inavyowasilishwa.
“Lazima tuwahusishe pia makundi yaliyotengwa wanawake, watu waliodhulumiwa au waliokuwa na historia ya ukandamizaji ili nao wawe sehemu ya mawasiliano ya sayansi.
“Moja ya hatari kubwa inayoweza kuua umuhimu wa sayansi ni kuifanya kuwa mradi wa viongozi au watu wachache.
“Sayansi haipaswi kuwa mradi wa tabaka la juu; lazima iwe mradi unaoeleweka na watu wote. Tunawahimiza kuhakikisha mnazingatia hilo kama waandishi wa sayansi,” amesema.
Prof. Nzimande ameongeza “Waandishi wa habari mnapaswa kukabiliana na changamoto ya taarifa za uongo [fake news].
“Hili ni mojawapo ya mambo hatari sana katika mawasiliano leo, mitandao ya kijamii ina mazuri na mabaya.
“Ni mazuri kwa kuwa kila mtu anaweza kupata taarifa siku hizi karibu kila mtu anasema,” amesema na kuongeza
“Mimi ni mtengeneza maudhui.” Lakini pia mitandao ya kijamii inaweza kusambaza taarifa za uongo haraka sana, jambo ambalo ni hatari.
“Katika sayansi, tunapaswa kupambana na taarifa za uongo, si tu katika jamii kwa ujumla, bali katika sayansi haswa kwa sababu inaweza kusababisha madhara makubwa.
Amesisitiza “Je, mnakumbuka wakati wa COVID jinsi taarifa za uongo zilivyosambaa?
“Leo kuna watu katika nchi kubwa wanaodai kwamba chanjo husababisha autism jambo la uongo kabisa.
“Lakini likirudiwa na watu wenye mamlaka, linakuwa hatari zaidi. Hii ina maana kwamba lazima muwe jasiri kama waandishi.
“Mnapaswa kuwa jasiri na msiogope kuuliza maswali makubwa na muhimu,” amesema.
Teknolojia ya Akili Unde [AI] katika sekta ya habari pia si suala la kuliacha nyuma, amesisitiza,
“Tunahitaji kuingiza teknolojia mpya kama akili bandia katika kazi yenu, ili kuimarisha weledi na uwazi katika taaluma yenu.
“Tunapaswa pia kushughulikia tofauti katika namna sayansi inavyoripotiwa. Bara letu bado linatengwa katika mambo mengi.
“Mnachukua jukumu la kuhakikisha masuala ya sayansi yanawafikia Waafrika si hivyo tu.
“Bali pia kuhakikisha ubunifu, uvumbuzi na miradi ya sayansi kutoka Afrika inatambulika ndani na nje ya bara,” amesema Prof Nzimande.
Diplomasia ya sayansi pia waandishi wa habari wanalo jukumu la kusaidia kuikuza ndani ya Bara la Afrika.
“Sayansi haina mipaka, na kwa sababu hiyo ina uwezo mkubwa wa kujenga mahusiano ya kidiplomasia baina ya nchi na mabara.
“Kama Afrika Kusini, tunaamini sana katika sayansi huria kwamba sayansi inapaswa kufikika zaidi na iwe wazi.
“Lakini lazima niseme kwamba waandishi wa habari za sayansi ni sehemu muhimu sana mjue au msijue katika kazi tunazofanya katika sekta ya sayansi.
“Bila ninyi, hatuwezi kuwafikia wale tunaopaswa kuwafikia,” amesema Prof Nzimande.
Tuesday, December 2, 2025
KARNE YA AI: 'SADC BADO KUNA PENGO LA MAWASILIANO YA SAYANSI'
Na Veronica Mrema - Pretoria
Ulimwengu wa sayansi na teknolojia unasonga kwa kasi ya ajabu.
Mataifa makubwa duniani yanawekeza kwenye ubunifu, utafiti wa kisayansi, na teknolojia za kisasa.
Teknolojia kama akili unde, kilimo cha kisasa na tiba za kibunifu zaidi zinabadilisha maisha katika mataifa makubwa duniani.
Karne ya akili unde [AI], roketi zinavuka anga, kuna uvumbuzi na gunduzi nyingi katika teknolojia mpya kwa kasi ambayo dunia haijawahi kushuhudia.
Mataifa makubwa yanawekeza, yanashirikiana, na yanapasha habari za sayansi kwa umma wao kwa kasi.
Lakini upande mwingine wa dunia, ndani ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika [SADC], bado kuna pengo kubwa katika mawasiliano ya sayansi.
Watafiti wanagundua, Serikali zinafanya miradi, taasisi zinavumbua, lakini taarifa 'hazitembei' kwa kasi inayohitajika.
Bado haziwafikii vema wananchi wake, hazijengi uelewa na hazifanyi sayansi kuwa sehemu ya maisha ya kila siku.
Ndani ya SADC, bado kuna pengo kubwa kati ya maendeleo ya ki-sayansi na jinsi ambavyo taarifa hizo zinavyowafikia wananchi.
"Kwa sababu nchi nyingi za SADC bado hazina mkakati wa mawasiliano katika masuala ya sayansi,".
Yameelezwa hayo na Mkurugenzi Mkuu wa Ushirikiano wa Kimataifa na Afrika, Wizara ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (DSTI), Afrika Kusini Mwampei Chaba.
Ni wakati alipokuwa akifungua mdahalo wa siku moja wa waandishi wa masuala ya sayansi kutoka nchi 18 wanachama wa SADC.
Amesema kutokana na pengo lililopo katika upashanaji habari kuhusu maendeleo ya sayansi katika nchi hizo, ndiyo maana DSTI iliona vema kuwaleta pamoja waandishi wa habari na kufanya mdahalo huo.
Ni katika mkutano wa kimataifa wa waandishi wa habari za masuala ya sayansi [WCSJ2025] unaofanyika Pretoria nchini Afrika Kusini.
Akifungua mjadala huo, aliweka wazi changamoto kubwa wanazokutana nazo waandishi wa sayansi katika ukanda huu.
“Nchi nyingi katika SADC bado hazina mkakati wa ushirikiano katika mawasiliano kuhusu sayansi. Hiyo ndiyo sababu upashanaji habari za sayansi unakumbwa na changamoto nyingi.”
Ameongeza "Ukosefu wa mkakati huo unawafanya waandishi wengi kukosa ushirikiano wanaohitaji kutoka kwa Serikali zao.
"Mnashindwa kuwa karibu na watafiti, mnakosa mazingira rafiki ya kupata habari, pamoja na fursa za ufadhili au mwaliko kwenye matukio muhimu yanayohusu sayansi na uvumbuzi.
Amesisitiza "Kwa hivyo, katika nchi yako na unataka kupata ushirikiano kutoka Serikali [kuandika kuhusu habari fulani inayohusu sayansi] au unataka watambue kazi yako.
"Unataka kufadhiliwa kwa baadhi ya kazi zako. Unataka kualikwa kwenye matukio [kwa wengi wenu], itakuwa ngumu kwa kuwa hawana mkakati wa ushirikiano kuhusu hilo," amesema.
"Mkirudi nchini mwenu kafuatilieni hili kwa undani, nendeni mkaulize wizara [zinazohusika na masuala ya] sayansi, wizara za mawasiliano [iwapo] wameandaa mkakati?.
Hii ni mara ya kwanza kwa Bara la Afrika kuwa mwenyeji wa mkutano wa kimataifa wa waandishi wa habari za sayansi, afya, mazingira na mambo mengine yanayohusiana na hayo.
Mdahalo huo kwa ajili ya waandishi wa habari kutoka SADC ulilenga kuwaleta pamoja kujadiliana namna gani watasukuma mbele masuala ya sayansi ndani ya nchi zao kwa upashanaji habari.
"Hii ni warsha ya mafunzo yenye umuhimu mkubwa kwetu. wazo hili lilikuja kwetu mwaka 2022 tulipoandaa Mkutano wa Sayansi Duniani (World Science Forum).
"..,, ambao ulikuwa wa kwanza kuandaliwa barani Afrika. Kwa hivyo, tulitengeneza historia mwaka 2022 kwa kuandaa mkutano wa Sayansi Duniani barani Afrika.
"Kisha tukaamua kuwa kuleta fursa kama hii barani Afrika bila waandishi, waandishi wa sayansi kuwa kwenye chumba, kungekuwa kupoteza.
Ameongeza "Tunawezaje kuwasilisha kile tunachofanya katika mkutano, kama idara, kama serikali barani Afrika, kama taasisi zinazofanya utafiti, ikiwa hatuna uandishi wa sayansi kwenye chumba?
"Pia tuligundua kuwa waandishi wa sayansi bado hawana uwezo wa kutosha kuhusiana na uandishi na kuandika makala za sayansi.
"Hivyo basi, tuliona hitaji la kuunda ushirikiano. Na Stellenbosch alishirikiana nasi kwa kiwango kikubwa.
Amesema walianza kupanga warsha ya mafunzo, yenye vipengele vingi, ambayo itasaidia kujenga uwezo wa waandishi wa habari katika kuwasilisha kazi tunazofanya kwa ufanisi zaidi.
"UNESCO ilifadhili baadhi ya wajumbe mwaka 2022, na imeendelea kuwa mshirika wetu tangu wakati huo.
"Sekretari ya SADC pia imekuwa mshirika wetu, na tunashukuru sana michango waliyotoa kwa waandishi wa SADC kuungana nasi.
"Chama cha Waandishi wa Sayansi wa Afrika Kusini (SASJA) pia kimeungana nasi, na sisi pia tuko kwenye mshirika mkubwa katika mkutano mwingine wa kihistoria," amebainisha,
Amesema mkutano wa WCSJ2025 walioandaa mwaka huu unatengeneza historia mpya nyingine na walitaka kuwa sehemu ya historia hiyo.
Amesema Afrika Kusini waliunda mkakati wa mawasiliano na ushirikiano katika masuala ya sayansi tangu mwaka 2015 na kwamba walichelewa mno kuunda.
"Taasisi yetu ilianzishwa Juni 2004, hivyo karibu miaka 11 baadaye, tu wakati huo tu tulikuwa na mkakati wa ushirikiano wa sayansi unaotekelezwa kwa sasa, na mchakato wa ukaguzi upo.
Amebainisha "Mwaka huu SADC ilishiriki katika G20. Tulikuwa Rais wa G20 na GSTI ilipanga kile kinachoitwa Wiki ya Utafiti na Ubunifu [Research and Innovation Week].
"Pia tulipitisha hati maalumu inayoitwa Azimio la Ushirikiano wa Sayansi wa G20 (G20 Science Engagement Resolutions).
"Hati hiyo inahimiza nchi za G20 kuweka sayansi kati-kati ya jamii inahimiza kuongeza ufahamu katika jamii zetu kuhusu thamani ya sayansi, na kuwasilisha sayansi kwa njia jamii zinaweza kuelewa.
"Kwa nini tunapaswa kufanya hivyo? Ni kwa nini hii ni muhimu? Sayansi haifadhiliwi vya kutosha, na hili ni changamoto katika jamii nzima.
Amesisitiza "Ikiwa thamani ya sayansi haifahamiki, ikiwa athari ya sayansi haijulikani kwa serikali zetu, jamii zetu, wafadhili wetu na wachangiaji.
"Basi mpango wa kufafanua ni ninyi walioko hapa. Ninyi ndio midomo yetu. Ninyi ndio mabalozi wetu wa kuwasilisha sayansi kwa jamii.
"Mara sayansi itakapofahamika, mara thamani ya sayansi itakapothibitishwa kwenye hatua za vitendo, kwenye jamii, kwenye vijiji.
"Basi mna nafasi nzuri ya kupata ufadhili kutoka Serikalini, ufadhili kutoka kwa wafadhili na kadhalika.
"Kwa hivyo, jukumu lenu ni muhimu sana, na tunategemea ninyi kusaidia kuunganisha pengo," amesema na kuongeza,
"Napenda kuwahimiza kwamba katika wiki hii, mchukue fursa ya warsha nyingi zinazofanyika kuhamasisha sayansi.
"Matumizi ya data, sita-sita kusema kwamba sayansi inapaswa kuwa kati-kati ya jamii, elimu, viwanda, ili kuendesha maendeleo kwa ujumla.
"Na haiwezi kuwa katikati ikiwa ninyi hufahami jinsi ya kuwasilisha sayansi. Nami naamini hatuhitaji kuwa wanasayansi ili kuelewa sayansi.
"Sayansi inapaswa kufafanuliwa kwa mtu wa miaka 85 na mtoto wa miaka 5. Bila kutumia maneno magumu.
Amesisitiza "Ikiwa mtu hawezi kueleza, ikiwa mwanasayansi unayemhoji hawezi kueleza sayansi yao kwa njia unayoielewa, basi hawafanyi kazi nzuri.
"Na pia unapaswa kuwa na uwezo wa kuhimiza wanasayansi kuzungumza na kuwasilisha sayansi kwa njia kila mtu anaweza kuelewa.
Amehoji "Je, unajua waandishi mashuhuri wa sayansi barani Afrika? Kwa nini haingewezekana iwe wewe?
"Kwa nini haingewezekana iwe wewe?” aliuliza, akiwahimiza washiriki kuwa wao wenyewe wanaweza kuwa waandishi mashuhuri wa sayansi Barani Afrika.
“Kuna waandishi wa sayansi mashuhuri duniani kote, lakini sio barani Afrika. Afrika inahitaji sayansi kwa maendeleo zaidi kuliko kanda nyingine yoyote duniani.
"Hivyo basi, tufanye lengo letu kuwa na waandishi mashuhuri wa sayansi katika jamii zetu, nchi zetu, ndani ya SADC na barani kote.
Amesisitiza "Vinginevyo, mbona mko hapa? Kwa nini mko hapa ikiwa hatutumiwe kile tulicho nacho kuwasilisha sayansi na kuifanya iwe ‘fashionable’?”
Amehimiza waandishi wa habari kutumia vema majukwaa ya kidigitali kama fursa ya kufikisha taarifa muhimu zinazohusu sayansi kwa kundi la vijana ambalo kubwa lipo kwenye majukwaa hayo.
"Kila mtu yupo TikTok, kila mtu yupo YouTube, lakini lazima tuone maudhui ya sayansi pia kwenye TikTok au YouTube.
"Tumia majukwaa haya maarufu kuwasilisha sayansi. Tuwafikie vijana walipo kwenye YouTube, Instagram na mitandao mingine na kuwapa elimu ya sayansi kwa njia wanayoielewa.”
Monday, December 1, 2025
TBN. YANG'ARA KIMATAIFA, VERONICA MREMA AINGIA JOPO LA MDAHALO MKUTANO MKUU WA DUNIA WA WAANDISHI WA SAYANSI.
PRETORIA, AFRIKA KUSINI
Kilele cha utambuzi wa uandishi wa habari za kidijitali nchini Tanzania kimethibitishwa baada ya Bi. Veronica Mrema, Mwanzilishi wa chombo cha habari cha M24 TANZANIA MEDIA na mwanachama mahiri wa Tanzania Bloggers Network (TBN), kuingia rasmi kwenye jopo la mdahalo katika Mkutano wa 13 wa Kimataifa wa Waandishi wa Habari za Sayansi (WCSJ2025) unaofanyika jijini Pretoria.
Hili si tu fahari kwa Mrema binafsi, bali ni heshima kubwa kwa TBN na tasnia nzima ya habari nchini, ikionesha kuwa kazi ya uandishi wa kidijitali inatambulika katika majukwaa makuu duniani.
Mrema yuko Afrika Kusini kuhudhuria mkutano huo mkuu unaotarajiwa kudumu hadi Desemba 5, 2025, baada ya kukabidhiwa udhamini maalum wa safari (Travel Grant) na Wizara ya Sayansi, Teknolojia, na Ubunifu ya Afrika Kusini (DSTI). Udhamini huu ulikuja kama matunda ya utambuzi wa utendaji wake wa kipekee katika uandishi wa habari za kisayansi na afya, akibainishwa kuwa miongoni mwa wachache barani Afrika waliochaguliwa kwa heshima hiyo. Uwepo wake kwenye jopo la mdahalo unampa fursa adhimu ya kushiriki moja kwa moja katika kuunda mwelekeo wa mustakabali wa habari za sayansi duniani.
Akiwa anahutubia jukwaa la WCSJ2025 ambalo linakutanisha waandishi, watafiti, na wataalamu mashuhuri kutoka kote duniani, Veronica Mrema anatarajiwa kusisitiza kuwa tasnia ya habari za sayansi na afya barani Afrika inakua kwa kasi na kwa hivyo inahitaji sasa zaidi ya wakati mwingine uandishi wa weledi wa hali ya juu, ubunifu, na ushahidi wa ki-sayansi ili kufikisha ujumbe sahihi na wa kuaminika kwa jamii.
Lengo lake kuu ni kuhakikisha uelewa sahihi wa sayansi unakuza maamuzi yanayoleta maendeleo, huku akitumia uzoefu wake kama kiongozi, ikiwemo nafasi yake kama Naibu Afisa Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam (DAR-PC) na Afisa Habari wa Jumuiya ya Watu Wanaoishi na Selimundu Tanzania (SCDPCT), kutetea uandishi wenye tija.
Kutambulika huku kwa Mwanachama wa TBN kunaimarisha nafasi ya Tanzania katika uwanja wa uandishi wa habari za kisasa, kuashiria kwamba mchango wake katika upashanaji habari ni wa kiwango cha kimataifa.
Friday, November 28, 2025
TBN YAFAFANUA MKUTANO NA MKURUGENZI WA MAWASILIANO IKULU.
Mtandao wa Wanablogu Tanzania (TBN) Unatoa Ufafanuzi Kuhusu Mkutano wa Ikulu
Dar es Salaam. Mtandao wa Wanablogu Tanzania (TBN) unapenda kutoa ufafanuzi rasmi na kuweka mambo wazi kufuatia taarifa zisizo sahihi na zinazoleta utata zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu mkutano uliofanyika hivi karibuni Ikulu.
TBN inakanusha vikali madai yanayosambazwa na baadhi ya watu wanaojiita wanaharakati, wakidai—bila uthibitisho wowote—kuwa wanahabari wa maudhui ya mtandaoni waliitwa Ikulu jijini Dar es Salaam kwa lengo la "kupewa maelekezo" kuhusu maandamano yanayodaiwa kupangwa kufanyika tarehe 9 Desemba.
Kusudi Halisi la Mkutano
TBN inathibitisha kuwa madai haya si sahihi na yamekuwa yakipotoshwa.
Kusudi la kweli na la moja kwa moja la wito wa Ikulu lilikuwa hili: Mkurugenzi mpya wa Mawasiliano Ikulu, Bw. Bakari Machumu, alifanya mkutano wa utambulisho rasmi na wadau muhimu wa sekta ya habari, akianza na wanahabari wa maudhui ya mtandaoni.
Mkutano huu ulikuwa ni hatua muhimu ya kuweka msingi wa ushirikiano na mawasiliano bora. Hakukuwa na ajenda iliyofichwa, wala mchezo wa nyuma ya pazia. Taarifa zozote zinazozungushwa kinyume na ukweli huu zinapaswa kuchukuliwa kama za uzushi na zisizo na msingi.
Wito wa Utulivu na Maadili
TBN inasikitishwa na kitendo cha kusambazwa kwa kipande kifupi cha video cha mkutano huo na baadhi ya watu, ikiwemo wanasiasa, kwa nia ya kujenga utata na kashfa kutoka kwenye kikao cha kawaida cha kiutendaji.
Tunasisitiza umuhimu wa kukuza utamaduni wa majadiliano ya kitaifa yenye staha na ukweli. Vitendo vya kubuni uongo na kupotosha taarifa vinadhoofisha tasnia ya habari na jitihada za kujenga uelewa katika jamii.
TBN inatoa pongezi kwa Bw. Machumu kwa kuonyesha nia ya kushirikiana na wadau wote wa habari. Tunamsihi aendelee na utendaji wake, huku tukiamini kuwa uwazi na utulivu ndio silaha bora dhidi ya upotoshaji.
Tunawaomba wananchi na wadau wote kutanguliza hekima, ukweli, na uzalendo na kukataa taarifa zozote zinazoweza kuleta mgawanyiko au kuchochea taharuki nchini.
MKURUGENZI WA MAWASILIANO IKULU AKUTANA NA MTANDAO WA WANABLOGU TANZANIA (TBN) NA WAANDISHI WA HABATI ZA MTANDAONI.
Viongozi mbalimbali wakizungumza katika Kikao cha pamoja cha Waandishi wa Habari wa Mtandaoni, Wanablogu mbalimbali pamoja na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bw. Bakari Machumu, Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 27 Novemba, 2025.
Waandishi wa Habari wa Mtandaoni, pamoja na Wanablogu mbalimbali wakizungumza katika Kikao cha pamoja na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bw. Bakari Machumu, Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 27 Novemba, 2025.
Monday, October 13, 2025
BASUTA YATOA TAMKO KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2025
Baraza Kuu la Jumuiya za Ansaar Sunna Tanzania (BASUTA) limetoa tamko kuelekea uchaguzi mkuu, unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi Oktoba mwaka huu 2025.
Tamko hilo la BASUTA limetolewa katika Mkutano wake Mkuu uliofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa Juliasi Nyerere jijini Dar es salaam siku ya tarehe 11 Oktoba 2025.
Sunday, October 12, 2025
KAMBAYA ATAHADHARISHA SIASA ZA FUJO
Na Rashid Mtagaluka, Dar es Salaam
Mwanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na kada maarufu wa chama hicho, Abdul Kambaya, amewatahadharisha Watanzania na wanasiasa wa upinzani wanaotumia mitandao ya kijamii kuhamasisha vurugu kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, akisisitiza kuwa siasa ni mashindano ya hoja, siyo matusi wala fujo.
Kambaya alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam, wakati akihutubia umati wa wananchi katika mkutano wa kampeni uliofanyika kata ya Makurumla, manispaa ya Ubungo, ambapo aliwataka wananchi kuwa makini na viongozi wanaopotosha jamii kupitia mitandao.
“Siasa sio kushindanisha ukubwa wa sauti, hapana. Siasa ni kushindana kwa hoja. Kama wenzetu wana hoja, basi wazilete mezani, siyo kukaa mitandaoni na kuhamasisha watu kufanya maandamano wakati wao wenyewe hawaonekani na hatujui kama bado wako hai au la,” alisema Kambaya huku akishangiliwa na umati wa wananchi.
Kambaya aliongeza kuwa baadhi ya watu wanaomchukia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan hawafanyi hivyo kwa sababu ya mavazi yake au jinsia yake, bali kutokana na uimara wake katika kushughulikia changamoto za wananchi na kasi ya maendeleo ambayo wengi hawakutarajia.
“Wanaomchukia Dkt. Samia wanachukia mafanikio yake. Wamezoea kuona wanawake wakinyamaza, lakini huyu mama ni jasiri, anajituma, anatatua matatizo ya wananchi kwa vitendo,” alisema.
Aidha, Kambaya aliwataka wananchi wa Makurumla kutoingia kwenye mtego wa watu wanaohubiri mambo yasiyotekelezeka, akisisitiza kuwa maendeleo yanayoonekana katika kata hiyo ni matokeo ya uongozi makini wa CCM na Rais Samia.
“Makurumla ya leo sio ile ya mwaka 2020. Dkt. Samia na serikali yake wamefanya kazi kubwa. Tazameni huduma za afya, maji, na elimu mabadiliko ni makubwa. Hata watoto wa shule leo wangeruhusiwa kupiga kura, wangechagua Dkt. Samia kwa sababu wanajua amani yao inayowafanya wasome itaendelea,” aliongeza Kambaya.
Kwa upande wake, Mgombea Ubunge wa Jimbo la Ubungo, Profesa Kitila Alexander Mkumbo, aliwaomba wananchi wa kata hiyo kumpigia kura Dkt. Samia akisema ndiye kiongozi mwenye uzoefu na uwezo wa kusimamia amani, umoja na maendeleo ya taifa.
“Dkt. Samia ni kiongozi mwenye maono. Anatoka katika chama imara chenye historia ya kujenga nchi. Tumuunge mkono kwa kura zetu ili aendelee kuimarisha uchumi na ustawi wa wananchi,” alisema Profesa Mkumbo.
Mkumbo pia aliwaomba wananchi kumpa nafasi ya kuendelea kulitumikia jimbo hilo, akiahidi kusimamia miradi ya maendeleo na kupunguza kero za michango mashuleni.
“Serikali ya Dkt. Samia ilishafuta ada zote, lakini bado kuna wazazi wanalalamika kuchangishwa hovyo. Nikichaguliwa tena, nitahakikisha tatizo hilo linaisha kabisa,” aliahidi Profesa Mkumbo.
Naye Mgombea udiwani wa Kata ya Makurumla, Bakari Kimwanga, alisema akichaguliwa ataendelea kushirikiana na Mbunge na serikali kutatua changamoto za wananchi, ikiwemo miundombinu ya maji na ujenzi wa kingo za Mto China.
“Tutahakikisha mradi wa maji unakamilika kwa wakati na kingo za Mto China zinajengwa ili kuzuia mafuriko. Tayari tumeona mafanikio kwenye mradi wa jengo la kujifungulia kina mama katika zahanati ya kata hii. Huo ndio mwelekeo wa CCM – vitendo, si maneno,” alisema Kimwanga.
Kampeni hizo zimeendelea kuvutia mamia ya wananchi, ambapo viongozi mbalimbali wa CCM katika ngazi ya mkoa na wilaya wamekuwa wakitoa wito wa kudumisha amani na kuendeleza maendeleo yaliyofikiwa chini ya uongozi wa Rais Samia.
KIKWETE ASHIRIKI MAPOKEZI TUZO YA SHUKRANI KWA DKT. SAMIA.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Ridhiwani Kikwete, ameshiriki mapokezo ya Tuzo ya Shukrani kwa Dr. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jitihada kubwa alizozifanya akiongoza mapambano kuwatetea na kuwahudumia Watu wenye Ulemavu , zilizopokelewa na Ndg. Kassim Majaliwa Majaliwa , Waziri Mkuu wa JMT kwa niaba yake Jana tarehe 11 Oktoba Dar- Es Salaam.
Tuzo hii ambayo inabeba mrejesho wa shukrani kwa kazi nzuri ambayo Mheshimiwa Rais. Dkt Samia ameifanya kwa watu wenye Ulemavu katika kipindi cha miaka yake minne ya uongozi wake, ni alama ya shukrani toka kwa watu wenye Ulemavu. Kwa upande wake waziri Kikwete, ametumia nafasi hiyo kumshukuru Mh. Rais kwa jinsi anavyoleta heshima kwenye nchi na matunda yake yanaonekana.
Naye Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Kasim Majaliwa, amewashukuru watu wenye ulemavu kwa kutambua mchango huo wa Mh. Rais na kuwapa salamu pia za Mh. Rais kuwa ataendelea kushirikiana nao.































