Na Rashid Mtagaluka, Dar es Salaam
Mwanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na kada maarufu wa chama hicho, Abdul Kambaya, amewatahadharisha Watanzania na wanasiasa wa upinzani wanaotumia mitandao ya kijamii kuhamasisha vurugu kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, akisisitiza kuwa siasa ni mashindano ya hoja, siyo matusi wala fujo.
Kambaya alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam, wakati akihutubia umati wa wananchi katika mkutano wa kampeni uliofanyika kata ya Makurumla, manispaa ya Ubungo, ambapo aliwataka wananchi kuwa makini na viongozi wanaopotosha jamii kupitia mitandao.
“Siasa sio kushindanisha ukubwa wa sauti, hapana. Siasa ni kushindana kwa hoja. Kama wenzetu wana hoja, basi wazilete mezani, siyo kukaa mitandaoni na kuhamasisha watu kufanya maandamano wakati wao wenyewe hawaonekani na hatujui kama bado wako hai au la,” alisema Kambaya huku akishangiliwa na umati wa wananchi.
Kambaya aliongeza kuwa baadhi ya watu wanaomchukia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan hawafanyi hivyo kwa sababu ya mavazi yake au jinsia yake, bali kutokana na uimara wake katika kushughulikia changamoto za wananchi na kasi ya maendeleo ambayo wengi hawakutarajia.
“Wanaomchukia Dkt. Samia wanachukia mafanikio yake. Wamezoea kuona wanawake wakinyamaza, lakini huyu mama ni jasiri, anajituma, anatatua matatizo ya wananchi kwa vitendo,” alisema.
Aidha, Kambaya aliwataka wananchi wa Makurumla kutoingia kwenye mtego wa watu wanaohubiri mambo yasiyotekelezeka, akisisitiza kuwa maendeleo yanayoonekana katika kata hiyo ni matokeo ya uongozi makini wa CCM na Rais Samia.
“Makurumla ya leo sio ile ya mwaka 2020. Dkt. Samia na serikali yake wamefanya kazi kubwa. Tazameni huduma za afya, maji, na elimu mabadiliko ni makubwa. Hata watoto wa shule leo wangeruhusiwa kupiga kura, wangechagua Dkt. Samia kwa sababu wanajua amani yao inayowafanya wasome itaendelea,” aliongeza Kambaya.
Kwa upande wake, Mgombea Ubunge wa Jimbo la Ubungo, Profesa Kitila Alexander Mkumbo, aliwaomba wananchi wa kata hiyo kumpigia kura Dkt. Samia akisema ndiye kiongozi mwenye uzoefu na uwezo wa kusimamia amani, umoja na maendeleo ya taifa.
“Dkt. Samia ni kiongozi mwenye maono. Anatoka katika chama imara chenye historia ya kujenga nchi. Tumuunge mkono kwa kura zetu ili aendelee kuimarisha uchumi na ustawi wa wananchi,” alisema Profesa Mkumbo.
Mkumbo pia aliwaomba wananchi kumpa nafasi ya kuendelea kulitumikia jimbo hilo, akiahidi kusimamia miradi ya maendeleo na kupunguza kero za michango mashuleni.
“Serikali ya Dkt. Samia ilishafuta ada zote, lakini bado kuna wazazi wanalalamika kuchangishwa hovyo. Nikichaguliwa tena, nitahakikisha tatizo hilo linaisha kabisa,” aliahidi Profesa Mkumbo.
Naye Mgombea udiwani wa Kata ya Makurumla, Bakari Kimwanga, alisema akichaguliwa ataendelea kushirikiana na Mbunge na serikali kutatua changamoto za wananchi, ikiwemo miundombinu ya maji na ujenzi wa kingo za Mto China.
“Tutahakikisha mradi wa maji unakamilika kwa wakati na kingo za Mto China zinajengwa ili kuzuia mafuriko. Tayari tumeona mafanikio kwenye mradi wa jengo la kujifungulia kina mama katika zahanati ya kata hii. Huo ndio mwelekeo wa CCM – vitendo, si maneno,” alisema Kimwanga.
Kampeni hizo zimeendelea kuvutia mamia ya wananchi, ambapo viongozi mbalimbali wa CCM katika ngazi ya mkoa na wilaya wamekuwa wakitoa wito wa kudumisha amani na kuendeleza maendeleo yaliyofikiwa chini ya uongozi wa Rais Samia.
No comments:
Post a Comment