Friday, November 28, 2025

MKURUGENZI WA MAWASILIANO IKULU AKUTANA NA MTANDAO WA WANABLOGU TANZANIA (TBN) NA WAANDISHI WA HABATI ZA MTANDAONI.

 

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bw. Bakari Machumu akizungumza na Waandishi wa Habari wa Mtandaoni pamoja na Wanablogu mbalimbali, Ikulu Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujitambulisha na kupokea maoni yao, ikiwa ni mfululizo wa mikutano na wadau wa Tasnia ya Habari kwa ajili ya kuboresha masuala mbalimbali ya Mawasiliano baina ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu na Vyombo vya Habari, tarehe 27 Novemba, 2025.

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bw. Bakari Machumu akiwa na viongozi mbalimbali kwenye picha ya pamoja na Waandishi wa Habari wa Mtandaoni, pamoja na Wanablogu mbalimbali, Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 27 Novemba, 2025.




Viongozi mbalimbali wakizungumza katika Kikao cha pamoja cha Waandishi wa Habari wa Mtandaoni, Wanablogu mbalimbali pamoja na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bw. Bakari Machumu, Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 27 Novemba, 2025.




Waandishi wa Habari wa Mtandaoni, pamoja na Wanablogu mbalimbali wakizungumza katika Kikao cha pamoja na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bw. Bakari Machumu, Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 27 Novemba, 2025.

Monday, October 13, 2025

BASUTA YATOA TAMKO KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2025

 

Amiri wa Baraza Kuu la Jumuiya za Ansaar Sunna Tanzania (BASUTA) Sheikh Ally Zubeir.

Mkuu wa wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule, akiongea kwenye Mkutano huo ambae alimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam.
...............................

Baraza Kuu la Jumuiya za Ansaar Sunna Tanzania (BASUTA) limetoa tamko kuelekea uchaguzi mkuu, unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi Oktoba mwaka huu 2025.


Tamko hilo la BASUTA limetolewa katika Mkutano wake Mkuu uliofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa Juliasi Nyerere jijini Dar es salaam siku ya tarehe 11 Oktoba 2025.






Sunday, October 12, 2025

KAMBAYA ATAHADHARISHA SIASA ZA FUJO

 


Na Rashid Mtagaluka, Dar es Salaam


Mwanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na kada maarufu wa chama hicho, Abdul Kambaya, amewatahadharisha Watanzania na wanasiasa wa upinzani wanaotumia mitandao ya kijamii kuhamasisha vurugu kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, akisisitiza kuwa siasa ni mashindano ya hoja, siyo matusi wala fujo.


Kambaya alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam, wakati akihutubia umati wa wananchi katika mkutano wa kampeni uliofanyika kata ya Makurumla, manispaa ya Ubungo, ambapo aliwataka wananchi kuwa makini na viongozi wanaopotosha jamii kupitia mitandao.


“Siasa sio kushindanisha ukubwa wa sauti, hapana. Siasa ni kushindana kwa hoja. Kama wenzetu wana hoja, basi wazilete mezani, siyo kukaa mitandaoni na kuhamasisha watu kufanya maandamano wakati wao wenyewe hawaonekani na hatujui kama bado wako hai au la,” alisema Kambaya huku akishangiliwa na umati wa wananchi.


Kambaya aliongeza kuwa baadhi ya watu wanaomchukia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan hawafanyi hivyo kwa sababu ya mavazi yake au jinsia yake, bali kutokana na uimara wake katika kushughulikia changamoto za wananchi na kasi ya maendeleo ambayo wengi hawakutarajia.


“Wanaomchukia Dkt. Samia wanachukia mafanikio yake. Wamezoea kuona wanawake wakinyamaza, lakini huyu mama ni jasiri, anajituma, anatatua matatizo ya wananchi kwa vitendo,” alisema.


Aidha, Kambaya aliwataka wananchi wa Makurumla kutoingia kwenye mtego wa watu wanaohubiri mambo yasiyotekelezeka, akisisitiza kuwa maendeleo yanayoonekana katika kata hiyo ni matokeo ya uongozi makini wa CCM na Rais Samia.


“Makurumla ya leo sio ile ya mwaka 2020. Dkt. Samia na serikali yake wamefanya kazi kubwa. Tazameni huduma za afya, maji, na elimu mabadiliko ni makubwa. Hata watoto wa shule leo wangeruhusiwa kupiga kura, wangechagua Dkt. Samia kwa sababu wanajua amani yao inayowafanya wasome itaendelea,” aliongeza Kambaya.


Kwa upande wake, Mgombea Ubunge wa Jimbo la Ubungo, Profesa Kitila Alexander Mkumbo, aliwaomba wananchi wa kata hiyo kumpigia kura Dkt. Samia akisema ndiye kiongozi mwenye uzoefu na uwezo wa kusimamia amani, umoja na maendeleo ya taifa.


“Dkt. Samia ni kiongozi mwenye maono. Anatoka katika chama imara chenye historia ya kujenga nchi. Tumuunge mkono kwa kura zetu ili aendelee kuimarisha uchumi na ustawi wa wananchi,” alisema Profesa Mkumbo.


Mkumbo pia aliwaomba wananchi kumpa nafasi ya kuendelea kulitumikia jimbo hilo, akiahidi kusimamia miradi ya maendeleo na kupunguza kero za michango mashuleni.


“Serikali ya Dkt. Samia ilishafuta ada zote, lakini bado kuna wazazi wanalalamika kuchangishwa hovyo. Nikichaguliwa tena, nitahakikisha tatizo hilo linaisha kabisa,” aliahidi Profesa Mkumbo.

Naye Mgombea udiwani wa Kata ya Makurumla, Bakari Kimwanga, alisema akichaguliwa ataendelea kushirikiana na Mbunge na serikali kutatua changamoto za wananchi, ikiwemo miundombinu ya maji na ujenzi wa kingo za Mto China.


“Tutahakikisha mradi wa maji unakamilika kwa wakati na kingo za Mto China zinajengwa ili kuzuia mafuriko. Tayari tumeona mafanikio kwenye mradi wa jengo la kujifungulia kina mama katika zahanati ya kata hii. Huo ndio mwelekeo wa CCM – vitendo, si maneno,” alisema Kimwanga.


Kampeni hizo zimeendelea kuvutia mamia ya wananchi, ambapo viongozi mbalimbali wa CCM katika ngazi ya mkoa na wilaya wamekuwa wakitoa wito wa kudumisha amani na kuendeleza maendeleo yaliyofikiwa chini ya uongozi wa Rais Samia.


KIKWETE ASHIRIKI MAPOKEZI TUZO YA SHUKRANI KWA DKT. SAMIA.

 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Ridhiwani Kikwete, ameshiriki mapokezo ya Tuzo ya Shukrani kwa Dr. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jitihada kubwa alizozifanya akiongoza mapambano kuwatetea na kuwahudumia Watu wenye Ulemavu , zilizopokelewa na Ndg. Kassim Majaliwa Majaliwa , Waziri Mkuu wa JMT kwa niaba yake Jana tarehe 11 Oktoba Dar- Es Salaam. 


Tuzo hii ambayo inabeba mrejesho wa shukrani kwa kazi nzuri ambayo Mheshimiwa Rais. Dkt Samia ameifanya kwa watu wenye Ulemavu katika kipindi cha miaka yake minne ya uongozi wake, ni alama ya shukrani toka kwa watu wenye Ulemavu. Kwa upande wake waziri Kikwete, ametumia nafasi hiyo kumshukuru Mh. Rais kwa jinsi anavyoleta heshima kwenye nchi  na  matunda yake yanaonekana.


Naye Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Kasim Majaliwa, amewashukuru watu wenye ulemavu kwa kutambua mchango huo wa Mh. Rais na kuwapa salamu pia za Mh. Rais kuwa ataendelea kushirikiana nao.



DC BAGAMOYO, AWATAKA WANANCHI WAMILIKI ARDHI KISHERIA KUEPUKA UTAPELI.

 


MKUU wa Wilaya ya Bagamoyo, Shaibu Ndemanga, amewataka wananchi kurasimisha ardhi ili wapate umiliki kisheria waepukane na utapeli na migogoro ya ardhi.


Ndemanga ameyasema hayo Chalinze wakati akizindua Mradi wa Kuboresha Usalama wa Miliki za Ardhi katika Halmashauri ya Chalinze.


Amesema kuwa mfumo wa hati za kisasa hauwezeshi mtu kutumia ujanja ujanja kupata hati na kumiliki ardhi kinyume cha utaratibu hivyo kupunguza utapeli na migogoro ya ardhi ambayo ilikithiri.


Naye Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Pwani Rugambwa Banyikila amesema kuwa hadi sasa jumla ya wananchi 515 wamekwisha hudumiwa kupitia kliniki ya ardhi ya wiki ya huduma kwa wateja. 


Banyikila amesema kuwa zoezi la kliniki ya ardhi kwa wananchi wa wilaya ya chalinze lilianza tarehe Oktoba 7 mwaka huu na linafanyika ikiwa ni kuadhimisha wiki ya huduma kwa wateja, ambapo limerahisisha utoaji na upatikanaji wa huduma za kisekta kwa wananchi katika maeneo yao.


Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Ardhi Halmashauri ya Chalinze Deo Msilu  akisoma taarifa ya kamishna wa ardhi Mkoa wa Pwani amesema kuwa vipande vya ardhi 24,730 vimetambuliwa na viwanja 23,936 vimepimwa kwenye Kata tatu za Bwilingu na Vigwaza.


Msilu amesema kuwa viwanja 22,022 vya matumizi mbalimbali vimesanifiwa kwenye mfumo wa e–Ardhi na viwanja 20,257 vimepimwa na kuidhinishwa kwenye mfumo huo na zoezi la umilikishaji na viwanja 3,135 vimesajiliwa kwa ajili ya hatua ya umilikishaji.


Thursday, October 2, 2025

SERIKALI YAHIMIZA TAASISI ZA KULEA YATIMA KULINDA IMANI YA WAHISANI

 

Na Albert Kawogo,

Bagamoyo 


SERIKALI imezitaka taasisi zinazosimamia malezi ya watoto yatima na wale wanaoshi katika mazingira magumu kusimamia miongozo,taratibu na sheria katika matumizi ya misaada mbalimbali wanayopewa ili kujenga imani ya wahisani wanaotoa misaada hiyo


    Wito huo umetolewa hivi karibuni  na Afisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Bagamoyo Abuu Yasin wakati wa sherehe ya miaka 25 ya kuadhimisha kituo cha kuelelea watoto yatima cha Moyo Mmoja kilichoko mjini hapo


   Yasin amesema kumekuwa na matatizo ya baadhi ya vituo vya watoto yatima kutumia vibaya misaada ya wahisani hasa fedha jambo ambalo linawakatisha tamaa watoa misaada na madhara yake yanakwenda moja kwa moja kwa walengwa wakuu wa misaada hiyo ambayo ni yatima.


   "Sisi kama serikali taratibu na sheria zetu ziko wazi na kazi yetu sisi ni kuwahimiza kufuata miongozo hiyo ili kulinda imani ya wafadhili" Amesema


  Aidha Yasin alikisifu kituo cha Moyo Mmoja Trust kuwa kama mfano wa vituo vingine katika kuendesha shughuli zake kwa usahihi jambo ambalo limevutia wahisani kukisaidia kwa muda wa miaka 25 sasa.


  Kwa upande wake Meneja wa Moyo Mmoja Trust Shilinde Masangu amesema kwa zaidi ya miaka 25 Taasisi hiyo imeweza kusaidia kwa ufanisi mkubwa watoto waliopoteza wazazi kutokana ajali magonjwa na hali ngumu za maisha.


   Shilinde amesema wamelea watoto wengi zaidi ambao wamepata elimu ya Chuo Kikuu na ile ya ujuzi wengine wakiajiriwa na wengine wakijiajiri.


  Meneja amesema pamoja na changamoto mbalimbali za malezi ya kielinu lakini kubwa ni Ile ya watoto wanaolelewa hapo kukosa mikopo ya elimu ya juu pindi wakiwa vyuo vikuu.


  "Ugumu wa kupata mikopo ya elimu ya juu kwa watoto wetu walioko vyuo vikuu limekuwa ni tatizo licha ya kujaribu mara kwa mara".Amesema Shilinde


  Naye Meneja wa Taasisi ya Ushirikia wa Tanzania na Norway TANO Olav Holten amesema Norway kupitia TANO kwa muda wa miaka 25 imekuwa mstari wa mbele kusaidia Moyo Mmoja kwenye misaada ya kufanya kituo hicho kiweze kuendelea kutoa huduma zaidi 


  Holten amesema TANO inaamini kuwa kila mtoto anahitaji kupata huduma zote muhimu za makuzi ikiwemo upendo elimu afya na uhifadhi hata kama amepoteza wazazi au walezi.


  Amesema amefurahi sana kuona watoto wakiwa na sehemu wanayoweza kuita hapa ni nyumbani kwao.


  Pia Holten amesema TANO itaendelea kudumisha ushirikiano na kituo hicho kwenye jitihada zote kuimarisha malezi ya watoto ili kulinda ustawi wa utu.

MARUFUKU YA WATAWA, MAPADRE KANISA KATOLIKI HAKI AU KIZUIZI ?

 


ANAANDIKA  RASHID MTAGALUKA


Kauli iliyotolewa Septemba 25, 2025 na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Wolfgang Pisa wa Jimbo Katoliki Lindi, ikiwakataza watawa na waseminari kujihusisha na siasa kwa namna yoyote ile, imeibua mjadala mpana unaohitaji tafakuri ya kina kwa maslahi ya mshikamano wa Taifa letu.



Kwa mujibu wa Askofu Pisa, watawa na waseminari hawataruhusiwa hata kufahamika au kutambulishwa kama washiriki wa chama chochote cha kisiasa, wala kuhusishwa na jambo lolote lenye sura ya kisiasa.



Kauli hiyo imekuja siku moja tu baada ya Masista wa Ndanda kuonekana wakimuombea Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa mkutano wake wa kampeni.



1. *Haki* *za* *Kikatiba* 


Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara ya 20(1), inatamka wazi kuwa:



"Kila mtu anao uhuru wa kukusanyika kwa hiari na kushirikiana na watu wengine, na kwa hiari kuanzisha na kushirikiana na vyama na mashirika mengine kwa madhumuni ya kulinda na kuendeleza maslahi yake".


Vilevile, Ibara ya 21(1) inasema:



" Kila raia ana haki ya kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi, moja kwa moja au kupitia wawakilishi waliochaguliwa".



Kwa mantiki hiyo, marufuku ya jumla ya Askofu wetu mpendwa Wolfgang Pisa kwa watawa na waseminari kujihusisha na siasa inaweza kuonekana kama kupunguza haki zao za kikatiba kama raia wa Tanzania.



2. *Mafundisho* *ya* *Kanisa* (Catholic Social Teaching)



Kanisa Katoliki, kupitia nyaraka zake kuu, mara kwa mara limekuwa likisisitiza wajibu wa waumini kushiriki katika maisha ya kijamii na kisiasa:


Gaudium et Spes (1965), waraka wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatikano, unasema:


"Kanisa linaona ni wajibu wa waumini kushiriki katika ujenzi wa jamii ya kidemokrasia, yenye haki na mshikamano".



Compendium of the Social Doctrine of the Church (2004) linabainisha kuwa:


"Shughuli za kisiasa ni sehemu ya wito wa Kikristo wa upendo na mshikamano; kwa hiyo waumini hawawezi kujitenga nazo".



Hii inamaanisha Kanisa linapaswa kuhimiza uwiano: kulinda heshima ya wito wa kitawa, lakini pia kutambua nafasi yao kama raia wanaoshiriki kwenye maisha ya kijamii.



3. *Data* *za* *Kisiasa* *na* *kijamii* 



Tanzania ina zaidi ya Wakatoliki milioni 12 (takribani 30% ya idadi ya watu  Pew Research Center, 2019).


Katika Uchaguzi Mkuu wa 2020, asilimia 80 ya wapiga kura walihusiana moja kwa moja na taasisi za dini (tafiti za Twaweza 2021).


Utafiti wa Baraza la Maaskofu (AMECEA, 2018) ulionesha kwamba asilimia 65 ya wananchi wa Afrika Mashariki wanaamini taasisi za dini zina mchango mkubwa zaidi katika kudumisha amani kuliko vyama vya siasa.



Kwa data hizi, tukubaliane kwamba, kuwatenga watawa na waseminari kabisa kwenye maisha ya kisiasa kunaweza kudhoofisha nafasi ya Kanisa katika mshikamano wa kitaifa.



4. *Mifano* *ya* *Kimataifa* 


Kenya: Wakati wa uchaguzi wa 2007 na 2013, viongozi wa Kanisa Katoliki na makanisa mengine walihusiana sana na wanasiasa,  mara nyingine kwa kuombewa au kuzungumzia masuala ya uchaguzi.



 Badala ya marufuku ya jumla, Kanisa Katoliki Kenya lilitoa _Pastoral_ _Letters_ likiwataka watawa na mapadre kuwa waangalifu ili kuepuka kuonekana kushabikia chama fulani, huku likiwataka washiriki kwenye majukwaa ya kuhubiri amani na mshikamano.



Poland: Nchini Poland, historia ya Kanisa Katoliki haiwezi kutenganishwa na siasa. Wakati wa utawala wa kikomunisti, Kanisa lilikuwa nguzo ya mapambano ya kisiasa kupitia harakati za Solidarity Movement chini ya uongozi wa Papa Yohane Paulo II. 



Hii ilionyesha kuwa pale ambapo haki na demokrasia zinahusiana, Kanisa linakuwa mstari wa mbele.



Amerika ya Kusini (Brazil, El Salvador): 


Hapa, Kanisa Katoliki limekuwa na utamaduni wa Theology of Liberation (Teolojia ya Ukombozi), likihusisha moja kwa moja mafundisho ya dini na mapambano ya kijamii na kisiasa ya wananchi.



 Viongozi wa Kanisa kama Askofu Oscar Romero (El Salvador) waliuawa wakiwa mstari wa mbele kutetea haki za wananchi dhidi ya ukandamizaji wa kisiasa.



Mifano hii michache inaonesha kuwa kuhusika kwa viongozi wa dini katika masuala ya kisiasa si jambo jipya, na linaweza kufanyika kwa namna yenye kulinda mshikamano badala ya kuupunguza.



5. *Uhalisia* *wa* *jamii* *yetu* 


Mfano wa Masista kumwombea Rais Samia haupaswi kuonekana kama ushabiki wa kisiasa, bali ni tendo la mshikamano na kitamaduni cha kuombea viongozi.



 Viongozi wote wa kitaifa, kuanzia Mwalimu Julius K. Nyerere hadi sasa, wamekuwa wakipokea baraka na sala kutoka kwa taasisi za dini. (Rejea hotuba ya Mwalimu 1985)



6. *Hitimisho* 

Kwa mtazamo wa Katiba, mafundisho ya Kanisa, takwimu za kijamii, na mifano ya kimataifa, kauli ya *TEC* inahitaji kupitiwa upya. 



Marufuku ya jumla inaweza kudhuru mshikamano wa kijamii na kuwapokonya raia haki zao za msingi.


Suluhisho bora ni kuweka mwongozo unaozuia ushabiki wa moja kwa moja, lakini kuheshimu nafasi ya watawa na waseminari kama raia wa Tanzania wanaoshiriki katika maisha ya Taifa.



Kwa maslahi mapana ya Taifa letu, taasisi za dini zinapaswa kuendelea kuwa daraja la mshikamano na mshiriki wa kweli katika ujenzi wa demokrasia na maendeleo ya kijamii.


 Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii 

 Simu 0718 406 242

Wednesday, September 3, 2025

WANANCHI WINDE BAGAMOYO, WASHANGAZWA NA KUPANDWA MAWE MAPYA KWENYE ENEO LAO.

 

Wananchi wazawa wa eneo la Winde lililopo kitongoji cha Mkwajuni kata ya Makurunge wilayani Bagamoyo wameshangazwa na uwepo wa mawe yanayoashiria mipaka mipya ndani ya eneo lao.


Wakiongea siku ya tarehe 30 Septemba 2025 katika mkutano ulioitishwa na wananchi hao ili kujadili mambo mbalimbali yanayohusu eneo lao wamesema wao ndio wenye eneo hilo na tayari baadhi ya familia wamefuata taratibu za kupima eneo hilo kisheria lakini chakushangaza yanaonekana mawe katika eneo hilo.


Mwenyekiti wa Wananchi hao, Muharami Seleman amesema kuwa eneo hilo ni mji wa Kale ambao una historia kubwa hivyo kuna haja ya kuuenzi kwa kuurasimisha na kuweka huduma za kijamii.


Seleman amesema kuwa moja ya vitu vya kihistoria ni uwepo wa kaburi lililopo hapo tangu mwaka 1,532 la mtu mweusi, visima vya maji ambayo yanatumika hadi hivi sasa.


Amesema kuwa pia eneo hilo maarufu kama namba 56 kuna mji ambao umezama baharini kwani unapakana na bahari, magofu ya kale, vyungu vya kupikia na kuna maeneo kwa ajili ya mila na tamaduni.


Aidha amesema kuwa Mji huo ulitambuliwa na Waingereza hata kwenye ramani ya maeneo waliyoyatawala unaonekana mji huo ambapo wao wamerithi kutoka kwa wazee wao ambao ni kaya 45 ndizo zinazomiliki ambapo ni jumla ya watu 4,500 kutoka vizazi vilivyotokana na wazee wa eneo hilo lenye ukubwa wa hekta 6,000.


Miraji Miraji ambae ni miomgoni mwa viongozi wa wananchi hao  wa eneo la Winde alisema kuwa amefuatilia sakata hilo kwa muda mrefu huku akieleza kuwa wakati linafikia hatua nzuri wanashangaa kuona maeneo hayo yamepandwa mawe.


"Cha kushangaza mawe yamepandwa na hata Mwenyekiti wa Kitongoji hana taarifa ya kupandwa kwa mawe hayo," alieleza Miraji.


Kwa upande wake mwana Winde,  Mussa Iddi amesema kuwa yeye alikuwepo eneo hilo mwaka 1953 akiwa anasoma hivyo historia ya hapo anaijua vizuri na kupitia wazazi wao walidai uhuru wa Tanzania.


Mussa amesema wanaomba eneo hilo lipimwe ili kuwe na huduma za kijami ili kuwe na makazi ya watu kwa kufuata utaratibu wa urasimishaji ardhi ili watu wamiliki kisheria.


Naye Wasaka Mnane mwenyekiti wa Kitongoji cha Mkwajuni lilipo eneo hilo amesema kuwa wanatambua eneo na kwamba  kinachotakiwa ni kufuata taratibu za urasimishaji ardhi  zilishaanza ambapo pia kuna baadhi ya watu wameingia kinyume cha utaratibu.


Mnane amesema kuwa wana Winde wanapaswa kuwa wamoja na kushirikiana ili waweze kuleta maendeleo yao na familia zao.


Katika kikao hicho walifanya uchaguzi wa kusimamia mambo yao ambapo Muharam Selemani amechaguliwa, kuwa Mwenyekiti mpya wa wana Winde.




Monday, September 1, 2025

DUA MAALUM KWA TAIFA NA RAIS SAMIA YAFANA DAR

 


Na Rashid Mtagaluka


Tukio la Dua ya kuiombea Taifa na Rais Samia Suluhu Hassan lililofanyika Tarehe 31 Agosti 2025 katika ukumbi wa DRIMP, Ilala Boma, ni kielelezo cha namna Watanzania wanavyotambua dhamana kubwa aliyoibeba Rais katika kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025. 


Dua hiyo iliyoongozwa na Sheikh Adam Mwinyipingu wa BAKWATA Ilala, imekusanya makundi mbalimbali ya kijamii wanawake, wanaume, vijana kwa wazee, ikiwa ni alama ya mshikimano wa kitaifa.


Kinachovutia zaidi ni kwamba tukio hili limeandaliwa na mwanadada jasiri na mwandishi wa habari anayeheshimika, Fatma Jalala, kupitia taasisi yake ya Seed of Changes. 


Hii ni ishara kwamba vijana, hususan wanawake, wanajitokeza mbele sio tu kama wachambuzi wa habari, bali pia kama wabunifu wa matukio yenye tija kubwa kwa taifa. 


Licha ya changamoto za kiutekelezaji, Fatma hakusita kuchukua jukumu la kuandaa tukio kubwa la kuliombea taifa na kiongozi wake mkuu jambo linaloonyesha uthubutu, uzalendo na imani ya dhati katika uongozi wa Rais Samia.


 Katika kuliombea taifa, Dkt. Samia na viongozi wengine wote  wa vyama 18 vyenye wagombea waliotia nia. 


Aidha dua hiyo iliyojulikana kwa jina la Munajjat ya Samia na Taifa ilibeba Kauli mbiu inayosema, " Bila Amani hakuna ndoto inayotimia"


 ujumbe ambao umebeba dhamira ya dhati ya kuwasisitiza Watanzania kuwa na wivu mkubwa na amani waliyonayo, hivyo wailinde na kuzidi kumuomba Mungu ajaalie amani na utulivu uliopo nchini udumu.


Kwa upande wa Rais Samia, dua hii ni ujumbe mzito kwamba wananchi wanamuona kama dira ya matumaini, kiongozi anayebeba maono ya mshikamo na maendeleo ya Watanzania wote. 


Ni heshima na upendo wa wananchi kwa kiongozi wao, wakimuombea apate nguvu, ulinzi na ujasiri wa kukabiliana na vikwazo vinavyoweza kuibuka katika safari ya kuelekea uchaguzi.


Kwa hakika, tukio hili linapaswa kuwa somo kwa vijana wengine nchini: kwamba mabadiliko na mafanikio makubwa hayahitaji kusubiri misaada ya nje, bali uthubutu, dhamira na moyo wa kujitolea kwa ajili ya taifa.




 

Sunday, August 31, 2025

MLIPUKO WAUA WAWILI BAGAMOYO

 


Watu wawili wamefariki dunia na mmoja kujeruhiwa baada ya kutokea mlipuko ambao bado haujafahamika ni wa kitu gani.


Akitoa Taarifa kwa vyombo vya habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Salim Morcase, amesema tukio hilo limetokea leo tarehe 31 Agosti 2025 Mtaa wa kichemchem kata ya Nianjema wilayani Bagamoyo majira ya saa moja na dakika ishirini asubui.


Amesema chanzo cha vifo hivyo ni mlipuko wa chuma ambacho Doto Mrisho (Marehemu) alikuwa anakikata kwenye karakana yake ya kuchomelea mageti.


Waliofariki katika tukio hilo ni Doto Mrisho mwenye umri wa miaka 24 fundi wa kuchomelea mageti mkazi wa kichemchem kata ya Nianjema na Saidi Ramadhani mwenye umri wa miaka 53 mkazi wa Sanzale Bagamoyo, na aliyejeruhuwa katika tukio hilo ni  Hassan Omari, mkazi wa Sanzale Bagamoyo.


Kamanda Morcase amesema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea kufanyika na jeshi la polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama ili kubaini chanzo cha mlipuko huo na ni wa kitu gani.



Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linatoa wito kwa baadhi ya wananchi wenye tabia ya kuokota vyuma ambavyo hawavijui na pia waache tabia ya kukata vyuma ambavyo ni aina ya mitungi ya gesi, au chochote chenye duara au mfano wa kibuyu kidogo kilichozibwa ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza.