Sunday, October 12, 2025

DC BAGAMOYO, AWATAKA WANANCHI WAMILIKI ARDHI KISHERIA KUEPUKA UTAPELI.

 


MKUU wa Wilaya ya Bagamoyo, Shaibu Ndemanga, amewataka wananchi kurasimisha ardhi ili wapate umiliki kisheria waepukane na utapeli na migogoro ya ardhi.


Ndemanga ameyasema hayo Chalinze wakati akizindua Mradi wa Kuboresha Usalama wa Miliki za Ardhi katika Halmashauri ya Chalinze.


Amesema kuwa mfumo wa hati za kisasa hauwezeshi mtu kutumia ujanja ujanja kupata hati na kumiliki ardhi kinyume cha utaratibu hivyo kupunguza utapeli na migogoro ya ardhi ambayo ilikithiri.


Naye Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Pwani Rugambwa Banyikila amesema kuwa hadi sasa jumla ya wananchi 515 wamekwisha hudumiwa kupitia kliniki ya ardhi ya wiki ya huduma kwa wateja. 


Banyikila amesema kuwa zoezi la kliniki ya ardhi kwa wananchi wa wilaya ya chalinze lilianza tarehe Oktoba 7 mwaka huu na linafanyika ikiwa ni kuadhimisha wiki ya huduma kwa wateja, ambapo limerahisisha utoaji na upatikanaji wa huduma za kisekta kwa wananchi katika maeneo yao.


Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Ardhi Halmashauri ya Chalinze Deo Msilu  akisoma taarifa ya kamishna wa ardhi Mkoa wa Pwani amesema kuwa vipande vya ardhi 24,730 vimetambuliwa na viwanja 23,936 vimepimwa kwenye Kata tatu za Bwilingu na Vigwaza.


Msilu amesema kuwa viwanja 22,022 vya matumizi mbalimbali vimesanifiwa kwenye mfumo wa e–Ardhi na viwanja 20,257 vimepimwa na kuidhinishwa kwenye mfumo huo na zoezi la umilikishaji na viwanja 3,135 vimesajiliwa kwa ajili ya hatua ya umilikishaji.


No comments:

Post a Comment