Wednesday, September 3, 2025

WANANCHI WINDE BAGAMOYO, WASHANGAZWA NA KUPANDWA MAWE MAPYA KWENYE ENEO LAO.

 

Wananchi wazawa wa eneo la Winde lililopo kitongoji cha Mkwajuni kata ya Makurunge wilayani Bagamoyo wameshangazwa na uwepo wa mawe yanayoashiria mipaka mipya ndani ya eneo lao.


Wakiongea siku ya tarehe 30 Septemba 2025 katika mkutano ulioitishwa na wananchi hao ili kujadili mambo mbalimbali yanayohusu eneo lao wamesema wao ndio wenye eneo hilo na tayari baadhi ya familia wamefuata taratibu za kupima eneo hilo kisheria lakini chakushangaza yanaonekana mawe katika eneo hilo.


Mwenyekiti wa Wananchi hao, Muharami Seleman amesema kuwa eneo hilo ni mji wa Kale ambao una historia kubwa hivyo kuna haja ya kuuenzi kwa kuurasimisha na kuweka huduma za kijamii.


Seleman amesema kuwa moja ya vitu vya kihistoria ni uwepo wa kaburi lililopo hapo tangu mwaka 1,532 la mtu mweusi, visima vya maji ambayo yanatumika hadi hivi sasa.


Amesema kuwa pia eneo hilo maarufu kama namba 56 kuna mji ambao umezama baharini kwani unapakana na bahari, magofu ya kale, vyungu vya kupikia na kuna maeneo kwa ajili ya mila na tamaduni.


Aidha amesema kuwa Mji huo ulitambuliwa na Waingereza hata kwenye ramani ya maeneo waliyoyatawala unaonekana mji huo ambapo wao wamerithi kutoka kwa wazee wao ambao ni kaya 45 ndizo zinazomiliki ambapo ni jumla ya watu 4,500 kutoka vizazi vilivyotokana na wazee wa eneo hilo lenye ukubwa wa hekta 6,000.


Miraji Miraji ambae ni miomgoni mwa viongozi wa wananchi hao  wa eneo la Winde alisema kuwa amefuatilia sakata hilo kwa muda mrefu huku akieleza kuwa wakati linafikia hatua nzuri wanashangaa kuona maeneo hayo yamepandwa mawe.


"Cha kushangaza mawe yamepandwa na hata Mwenyekiti wa Kitongoji hana taarifa ya kupandwa kwa mawe hayo," alieleza Miraji.


Kwa upande wake mwana Winde,  Mussa Iddi amesema kuwa yeye alikuwepo eneo hilo mwaka 1953 akiwa anasoma hivyo historia ya hapo anaijua vizuri na kupitia wazazi wao walidai uhuru wa Tanzania.


Mussa amesema wanaomba eneo hilo lipimwe ili kuwe na huduma za kijami ili kuwe na makazi ya watu kwa kufuata utaratibu wa urasimishaji ardhi ili watu wamiliki kisheria.


Naye Wasaka Mnane mwenyekiti wa Kitongoji cha Mkwajuni lilipo eneo hilo amesema kuwa wanatambua eneo na kwamba  kinachotakiwa ni kufuata taratibu za urasimishaji ardhi  zilishaanza ambapo pia kuna baadhi ya watu wameingia kinyume cha utaratibu.


Mnane amesema kuwa wana Winde wanapaswa kuwa wamoja na kushirikiana ili waweze kuleta maendeleo yao na familia zao.


Katika kikao hicho walifanya uchaguzi wa kusimamia mambo yao ambapo Muharam Selemani amechaguliwa, kuwa Mwenyekiti mpya wa wana Winde.




No comments:

Post a Comment