Thursday, October 2, 2025

MARUFUKU YA WATAWA, MAPADRE KANISA KATOLIKI HAKI AU KIZUIZI ?

 


ANAANDIKA  RASHID MTAGALUKA


Kauli iliyotolewa Septemba 25, 2025 na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Wolfgang Pisa wa Jimbo Katoliki Lindi, ikiwakataza watawa na waseminari kujihusisha na siasa kwa namna yoyote ile, imeibua mjadala mpana unaohitaji tafakuri ya kina kwa maslahi ya mshikamano wa Taifa letu.



Kwa mujibu wa Askofu Pisa, watawa na waseminari hawataruhusiwa hata kufahamika au kutambulishwa kama washiriki wa chama chochote cha kisiasa, wala kuhusishwa na jambo lolote lenye sura ya kisiasa.



Kauli hiyo imekuja siku moja tu baada ya Masista wa Ndanda kuonekana wakimuombea Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa mkutano wake wa kampeni.



1. *Haki* *za* *Kikatiba* 


Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara ya 20(1), inatamka wazi kuwa:



"Kila mtu anao uhuru wa kukusanyika kwa hiari na kushirikiana na watu wengine, na kwa hiari kuanzisha na kushirikiana na vyama na mashirika mengine kwa madhumuni ya kulinda na kuendeleza maslahi yake".


Vilevile, Ibara ya 21(1) inasema:



" Kila raia ana haki ya kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi, moja kwa moja au kupitia wawakilishi waliochaguliwa".



Kwa mantiki hiyo, marufuku ya jumla ya Askofu wetu mpendwa Wolfgang Pisa kwa watawa na waseminari kujihusisha na siasa inaweza kuonekana kama kupunguza haki zao za kikatiba kama raia wa Tanzania.



2. *Mafundisho* *ya* *Kanisa* (Catholic Social Teaching)



Kanisa Katoliki, kupitia nyaraka zake kuu, mara kwa mara limekuwa likisisitiza wajibu wa waumini kushiriki katika maisha ya kijamii na kisiasa:


Gaudium et Spes (1965), waraka wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatikano, unasema:


"Kanisa linaona ni wajibu wa waumini kushiriki katika ujenzi wa jamii ya kidemokrasia, yenye haki na mshikamano".



Compendium of the Social Doctrine of the Church (2004) linabainisha kuwa:


"Shughuli za kisiasa ni sehemu ya wito wa Kikristo wa upendo na mshikamano; kwa hiyo waumini hawawezi kujitenga nazo".



Hii inamaanisha Kanisa linapaswa kuhimiza uwiano: kulinda heshima ya wito wa kitawa, lakini pia kutambua nafasi yao kama raia wanaoshiriki kwenye maisha ya kijamii.



3. *Data* *za* *Kisiasa* *na* *kijamii* 



Tanzania ina zaidi ya Wakatoliki milioni 12 (takribani 30% ya idadi ya watu  Pew Research Center, 2019).


Katika Uchaguzi Mkuu wa 2020, asilimia 80 ya wapiga kura walihusiana moja kwa moja na taasisi za dini (tafiti za Twaweza 2021).


Utafiti wa Baraza la Maaskofu (AMECEA, 2018) ulionesha kwamba asilimia 65 ya wananchi wa Afrika Mashariki wanaamini taasisi za dini zina mchango mkubwa zaidi katika kudumisha amani kuliko vyama vya siasa.



Kwa data hizi, tukubaliane kwamba, kuwatenga watawa na waseminari kabisa kwenye maisha ya kisiasa kunaweza kudhoofisha nafasi ya Kanisa katika mshikamano wa kitaifa.



4. *Mifano* *ya* *Kimataifa* 


Kenya: Wakati wa uchaguzi wa 2007 na 2013, viongozi wa Kanisa Katoliki na makanisa mengine walihusiana sana na wanasiasa,  mara nyingine kwa kuombewa au kuzungumzia masuala ya uchaguzi.



 Badala ya marufuku ya jumla, Kanisa Katoliki Kenya lilitoa _Pastoral_ _Letters_ likiwataka watawa na mapadre kuwa waangalifu ili kuepuka kuonekana kushabikia chama fulani, huku likiwataka washiriki kwenye majukwaa ya kuhubiri amani na mshikamano.



Poland: Nchini Poland, historia ya Kanisa Katoliki haiwezi kutenganishwa na siasa. Wakati wa utawala wa kikomunisti, Kanisa lilikuwa nguzo ya mapambano ya kisiasa kupitia harakati za Solidarity Movement chini ya uongozi wa Papa Yohane Paulo II. 



Hii ilionyesha kuwa pale ambapo haki na demokrasia zinahusiana, Kanisa linakuwa mstari wa mbele.



Amerika ya Kusini (Brazil, El Salvador): 


Hapa, Kanisa Katoliki limekuwa na utamaduni wa Theology of Liberation (Teolojia ya Ukombozi), likihusisha moja kwa moja mafundisho ya dini na mapambano ya kijamii na kisiasa ya wananchi.



 Viongozi wa Kanisa kama Askofu Oscar Romero (El Salvador) waliuawa wakiwa mstari wa mbele kutetea haki za wananchi dhidi ya ukandamizaji wa kisiasa.



Mifano hii michache inaonesha kuwa kuhusika kwa viongozi wa dini katika masuala ya kisiasa si jambo jipya, na linaweza kufanyika kwa namna yenye kulinda mshikamano badala ya kuupunguza.



5. *Uhalisia* *wa* *jamii* *yetu* 


Mfano wa Masista kumwombea Rais Samia haupaswi kuonekana kama ushabiki wa kisiasa, bali ni tendo la mshikamano na kitamaduni cha kuombea viongozi.



 Viongozi wote wa kitaifa, kuanzia Mwalimu Julius K. Nyerere hadi sasa, wamekuwa wakipokea baraka na sala kutoka kwa taasisi za dini. (Rejea hotuba ya Mwalimu 1985)



6. *Hitimisho* 

Kwa mtazamo wa Katiba, mafundisho ya Kanisa, takwimu za kijamii, na mifano ya kimataifa, kauli ya *TEC* inahitaji kupitiwa upya. 



Marufuku ya jumla inaweza kudhuru mshikamano wa kijamii na kuwapokonya raia haki zao za msingi.


Suluhisho bora ni kuweka mwongozo unaozuia ushabiki wa moja kwa moja, lakini kuheshimu nafasi ya watawa na waseminari kama raia wa Tanzania wanaoshiriki katika maisha ya Taifa.



Kwa maslahi mapana ya Taifa letu, taasisi za dini zinapaswa kuendelea kuwa daraja la mshikamano na mshiriki wa kweli katika ujenzi wa demokrasia na maendeleo ya kijamii.


 Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii 

 Simu 0718 406 242

No comments:

Post a Comment