Saturday, August 5, 2023

RATIBA YA LIGI KUU BARA.

Wakati wadau na mashabiki wa soka nchini wakisubiri kuanza kwa Ligi Kuu msimu wa 2023/24 bodi ya ligi hiyo nchini (TPLB) imesema ratiba ya mashindano hayo wataiachia siku mbili zijazo.

Ligi Kuu inatarajia kuanza Agosti 15, huku ikishuhudiwa baadhi ya timu zilizokuwapo msimu uliopita zikikosekana, huku zikitokea mpya tatu kwa michuano hiyo.

Timu za Mbeya City, Ruvu Shooting na Polisi Tanzania zilizokuwapo msimu huo, hazitakuwapo baada ya kushuka daraja, huku Tabora United, Mashujaa na JKT Tanzania zikichomoza msimu ujao.

Hadi sasa timu, mashabiki na wadau wa soka nchini wanasubiria kujua rariba inatoka lini ili kujua nani anaanza na nani na wapi ili kuanza mipango na mikakati rasmi.

Ofisa Habari wa bodi ya Ligi Kuu chini (TPLB), Karim Boimanda amesema hadi sasa ratiba imeshakamilika na muda wowote kuanzia kesho Jumapili au Jumatatu wataiachia rasmi.

Amesema wamechelewa kuitoa kutokana na shirikisho la soka Afrika (CAF) kuchelewesha kalenda yao huku akibainisha wameboresha na huenda changamoto za kusimamisha au kusogeza mechi zisijitokeze kama ilivyokuwa msimu uliopita. "Kuanzia kesho hadi Jumatatu ratiba itatoka rasmi kujua nani anaanza na nani na wapi, tumechelewa kutokana na kutopata mapema kalenda ya CAF, lakini tumezigatia ratiba ya michuano ya kimataifa hivyo zile changamoto za msimu uliopita hatutarajii kujitokeza"

"Ni ngumu ligi kukosa mapungufu kwa sababu kuna ratiba zinaweza kujitokeza za dharula, lakini sisi tumejitahidi kurekebisha kadri ya uwezo wetu ili kuondokana na hilo" amesema Boimanda.

Ofisa habari wa Tanzania Prisons, Jackson Mwafulango amesema wao wapo tayari kukutana na yeyote na popote kwani kikosi chao kipo fiti kwa ajili ya msimu ujao.

"Sisi hatuna presha wala wasiwasi tumejipanga kuanza na yeyote na popote, iwe nyumbani au ugenini, tupo kambini mazoezi yakiendelea tangu Julai 3," ametamba Mwafulango.

https://www.mwanaspoti.co.tz/ms/soka/ratiba-ligi-kuu-bara-hiyoooo-4327534



 

NAIBU WAZIRI: IJA NI CHUO MUHIMU KWENYE MAMBO YA HAKI.

 

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul amesema kuwa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA) ni Chuo muhimu katika kuwajenga watu wanaosimamia masuala ya haki hapa nchini.


Naibu Waziri Mhe. Pauline Gekul amesema hayo leo Jumamosi tarehe 05/08/2023 wakati akizungumza na wajumbe wa Menejimenti ya IJA, Halmashauri Tendaji ya Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia, Habari na Utafiti (RAAWU) tawi la Lushoto pamoja na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Lushoto, hapa Chuoni wilayani Lushoto.


Amesema kuwa Chuo cha IJA kinapotoa maarifa kwa watu wa kada mbalimbali, basi kinasaidia katika masuala ya haki, akibainisha kuwa wananchi mbalimbali bado wanakabiliwa na ukosefu wa haki.


"IJA ni Chuo muhimu, nimefurahi kuona kumbe tuna Taasisi nzuri hapa," amesema Naibu Waziri na kuongeza,
"Sisi ambao tuna husika na wananchi moja kwa moja kama wabunge, madiwani na wenyeviti ni mashahidi kwamba wananchi wetu bado wana ukosefu wa haki zao hasa masuala ya kisheria, kwa hiyo nina imani ninyi mkiwapa maarifa watu wanaokuja kusoma hapa mnakuwa mnasaidia kwenye eneo la haki."


Pia Naibu Waziri huyo wa Katiba na Sheria ameongeza kuwa amejifunza masuala mengi ya Chuo cha IJA na kuhusu changamoto za Chuo Cha IJA, amebainisha kuwa atakwenda kuzifanyia kazi pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria na viongozi wengine.


"Mhe. Waziri wa Katiba na Sheria alikuja hapa akapokea changamoto zenu, nami niwaambie tutakwenda kuzifanyia kazi na kazi yetu sisi ni kuwa kiungo ili kuona mnafanya kazi vizuri," amebainisha Mhe. Naibu Waziri.


Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha IJA ambae pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul F.Kihwelo amesema kuwa Chuo ni kitovu cha elimu na Utafiti kwa upande wa Mahakama na kwamba kimeendelea kuzalisha watu muhimu kwenye eneo la usimamizi wa haki.


Pia Mhe. Jaji Kihwelo amesema kuwa Chuo kimefarijika na ujio wa Naibu Waziri hapa Chuoni na kwamba ziara hiyo imekuwa na tija.


Awali katika ziara hiyo, Mhe. Naibu Waziri huyo wa Katiba na Sheria alitembelea maeneo kadhaa ya Chuo, ikiwemo Maktaba, Hosteli ya Wanaume ya Benjamini Mkapa pamoja na viwanja vya michezo vya Chuo.





MAJALIWA: MFUKO WA WATU WENYE ULEMAVU HAUJAUNGANISHWA NA MIFUKO MINGINE

 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Mfuko wa Taifa kwa Watu wenye Ulemavu haujaunganishwa na mifuko mingine ya makundi maalum kama ambavyo inadaiwa.

“Katika risala yenu mmeomba Mfuko wa Taifa kwa Watu wenye Ulemavu usiunganishwe na mifuko mingine ili uweze kutekeleza majukumu yake yaliyoainishwa kwenye Sheria ya Watu wenye Ulemavu Na. 9 ya mwaka 2010. Nitumie fursa hii kuwafahamisha kuwa mfuko huo haujaunganishwa na mifuko mingine na kama mlivyosikia, mfuko huo umetengewa kiasi cha shilingi bilioni moja kwa ajili ya utekelezaji wa afua mbalimbali kwa watu wenye ulemavu,” amesema.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumamosi, Agosti 5, 2023) wakati akifungua kongamano la siku moja la watu wenye ulemavu Dar es Salaam lililofanyika kwenye ukumbi wa JNICC, jijini humo.

Alikuwa akijibu hoja kuu ya kwenye risala ilisomwa na Mwenyekiti wa SHIVYAWATA, Ernest Kimaya ambaye alitaka wapate majibu ya Serikali kuhusu hatua iliyofikiwa ya uanzishwaji wa Mfuko wa Maendeleo wa Watu wenye Ulemavu kwani wanaona ukiunganishwa na mifuko mingine, utasababisha masuala yao yafunikwe na kundi lao halitanufaika ipasavyo.

Hata hivyo, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuainisha changamoto zitakazowakabili kwenye matumizi ya fedha hizo endapo hawatajipanga kwa vile wana makundi mengi ambayo inabidi yaainishwe ili kila kundi liweze kunufaika na mfuko huo.

“Watu wenye ulemavu mna makundi mengi mno kama walivyo wasanii. Kuna wasanii wa muziki wa bongo fleva, orchestra, muziki laini, wa kufoka foka, bongo movie, wachoraji na wachongaji. Na hapa nimeona huo mchanganyiko. Mwenyekiti inabidi mkae na kuainisha haya makundi ili muweze kunufaika,” amesema.

Akitoa ufafanuzi kuhusu mkwamo wanaoupata watu wenye ulemavu katika maombi ya kazi kupitia utaratibu wa kidijitali wa Sekretarieti ya Ajira, Waziri Mkuu amesema Serikali inatambua uwepo ya changamoto hiyo na tayari imeweka utaratibu maalum kwa ajili ya watu wenye ulemavu.

“Waombaji wanatakiwa wawasilishe maombi kupitia Vyama vya Watu wenye Ulemavu ili wapate usaidizi kwa kuwa ofisi hizo tayari zina miundombinu rafiki kwa ajili ya watu wenye ulemavu. Mkurugenzi wa Idara, Kitengo cha watu wenye ulemavu upo hapa, simamia utaratibu huu ili kila nafasi za kazi zinapotangazwa wapelekee taarifa Vyama vya Watu wenye Ulemavu ili wapate usaidizi kwa wale wenye sifa zinazolingana na nafasi za ajira zilizotangazwa. Wekeni utaratibu mzuri wa kuwafikia ili nao wanufaike na fursa hizo.”

Akifafanua kuhusu ombi lao la kutaka kuharakishwa kwa utaratibu mpya wa kutoa na kurejesha mikopo inayotolewa na Halmashauri, Waziri Mkuu amesema Kamati ya Kitaifa iliyoundwa kuandaa utaratibu mpya wa usimamizi wa mikopo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri kwa mfumo wa kibenki iko katika hatua za mwisho za maboresho ya taarifa yake. “Niwasihi sana mvute subira na pindi Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI atakapotoa miongozo yake basi miongozo hii itagusa namna nzuri ya kurejesha mikopo hii.”

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa kongamano hilo, Naibu Waziri (OWM - Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Patrobas Katambi alisema Serikali imeanza kukusanya fedha za kufanya mapitio ya Sera ya Maendeleo na Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2004.

“Sera hii ni ya mwaka 2004, ni takriban miaka 20 sasa. Tumeanza kutafuta fedha ili kuibadilisha sera hii badala ya kuboresha sheria kwa kutumia sera iliyopo. Ili upate sheria nzuri ni lazima uwe na sera nzuri. Tumedhamiria kwamba kutakuwa na ushirikishwaji wa makundi tofauti kulingana na ulemavu walionao kwa sababu kila kundi lina mahitaji tofauti.”

Alisema Serikali imetoa sh. milioni 35 kugharimia upatikanaji wa hati ya kiwanja katika eneo la Mtumba, jijini Dodoma kwa ajili ya kujenga Ofisi za Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu. Vilevile, Serikali kupitia Ofisi ya Rais - TAMISEMI inaendelea kuratibu upatikanaji wa ofisi za vyama vya watu wenye ulemavu kwenye Mikoa na Halmashauri zote nchini.

Naye Mwenyekiti wa Keysha Empowering Development Foundation (KEDEF) ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum (Walemavu), Khadija Shaban Taya alisema kongamano hilo ni la tatu na kwamba amekwishaandaa makongamano kama hayo kwenye mikoa ya Dodoma na Mwanza.

“Nia ya makongamano haya ni kuwaleta pamoja watu wenye ulemavu ili watoe maoni yao na kuelezea changamoto zinazowakabili. Pia, tutawapa elimu juu ya sheria ya manunuzi ambayo inataka asilimia 30 itengwe na Halmashauri zote ili zitumike kuendeleza shughuli za watu wenye ulemavu.”








MAGAZETI YA LEO AGOSTI 05, 2023.

 















Friday, August 4, 2023

TBA YATAKIWA KUHAKIKISHA UBORA WA MAJENGO WANAYOJENGA ILI KUKIDHI MAHITAJI YA SOKO.



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia viongozi mbalimbali pamoja na wananchi wakati wa hafla ya Ufunguzi wa Jengo la Makazi la Kibishara la Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) lililopo katika eneo la Sekei Jijini Arusha leo tarehe 04 Agosti 2023.
......................................

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amewataka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kuhakikisha nyumba zinazojengwa zinakidhi mahitaji ya soko kwa miaka mingi ijayo ikiwemo ubora wa nyumba hiyo na sehemu za kupata mahitaji.


Makamu wa Rais amesema hayo mara baada ya kufungua Jengo la Makazi la Kibiashara la Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) lililopo katika eneo la Sekei Jijini Arusha, Jengo lililogharimu shilingi bilioni 6.86.


 Amewahimiza TBA kuzingatia tija na viwango katika miradi mingine kama ilivyofanyika katika jengo hilo pamoja na kuwasihi kutekeleza kikamilifu Mpango Mkakati wa Wakala wa Majengo wa mwaka 2021/22 hadi 2025/26 ili kutimiza mahitaji ya makazi bora kwa Watumishi wa Umma na wananchi kwa ujumla. Amesema kukamilika kwa miradi mingi ya nyumba kutawezesha TBA kujiendesha kibiashara badala ya kutegemea ruzuku kutoka serikalini.


Halikadhalika Makamu wa Rais amewaagiza TBA kuhifadhi na kutunza mazingira kwa kupanda miti katika maeneo yote inapotekelezwa miradi ya ujenzi wa nyumba ikiwemo uwekaji wa miundombinu sahihi ya ukusanyaji takangumu ili kuwezesha ukusanyaji na utupaji wake. 


Amesema kila inapowezekana TBA ihakikishe inaweka miundombinu ya kuvuna maji ya mvua kwa matumizi mbalimbali ikiwemo umwagiliaji wa miti na maua.



Makamu wa Rais ametoa rai kwa wapangaji wanaotumia nyumba hizo kuzingatia masharti ya mkataba wa upangishaji kwa kulipa kodi kwa wakati ili kuepukana na usumbufu unaoweza kujitokeza kutokana na teknolojia mpya ya uwekaji vitasa janja (Smart locks) ambavyo hujifunga pindi mpangaji anapofanya ulimbikizaji wa kodi. Pia amewasihi wapangaji kutunza nyumba hizo ili zibaki katika hali ya ubora kwa muda mrefu.



Vilevile Makamu wa Rais ametoa wito kwa sekta binafsi kuchangamkia fursa adhimu ya kushirikiana na TBA katika kutekeleza miradi ya ujenzi wa nyumba nchi nzima kwa kuwa Serikali tayari imeiruhusu TBA kushirikiana na Sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi mbalimbali kwa ubia. Aidha amewasihi TBA kuendelea na mpango wa kuyaendeleza maeneo yote yaliyorejeshwa Serikalini kwa kujenga majengo ya ghorofa kama ilivyoelekezwa kwenye Ibara ya 55(h)(ii) ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya 2020.



Makamu wa Rais amewaasa wananchi wa mkoa wa Arusha kutunza mazingira kwa kuepukana na tabia ya kutupa taka ovyo kwani jambo hilo litaleta athari katika masuala ya utalii mkoani humo.


Amewaagiza viongozi wa mkoa huo kusimamia suala hilo kwa kuhakikisha usafi unafanyika katika maeneo yote na kudhibiti utupaji taka ovyo hususani chupa za maji.



Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa ameishukuru serikali kwa kuendelea kuiamini Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi inayotekeleza miradi mbalimbali ikiwemo miradi ya ujenzi wa nyumba na majengo ya serikali katika maeneo mbalimbali hapa nchini.



Prof Mbarawa amesema kukamilika kwa ujenzi wa mradi huo kutasaidia upatikanaji wa makazi ya uhakika kwa wakazi wa jiji la Arusha. Ameongeza kwamba mradi huo umesaidia wataalamu wazawa wa fani za ujenzi kujengewa uwezo wa taaluma kwa vitendo pamoja na kusaidia kuendelea kukua kwa kasi kwa jiji la Arusha, kuongezeka kwa mapato ya serikali pamoja na huduma za kijamii katika jiji hilo.



Awali akitoa taarifa kuhusu mradi huo Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Arch. Daud Kondoro amesema Chimbuko la mradi huo ni katika kuiwezesha Wakala kuwa na uwezo wa kujiendesha kupitia vyanzo vyake vya mapato na kupunguza utegemezi kwa Serikali. Ameongeza kwamba mapato yatakayopatikana kwenye miradi kama hiyo yatatumika kujenga nyumba nyingine za watumishi wa umma.


Arch. Kondoro ameongeza kwamba pamoja na mradi huo, Wakala wa Majengo Tanzania unaendelea kutekeleza miradi mingine kwa fedha za ndani ikiwemo Ujenzi wa Majengo ya Makazi eneo la Canadian Village, Masaki, Dar es Salaam ambapo jengo moja lenye uwezo wa kuchukua familia 12 limekamilika na majengo mengine mawili utekelezaji wake umefika asimilia 35. Wakala pia umeanza ujenzi wa Jengo la Makazi eneo la Ghana Kota jijini Mwanza ambalo utekelezaji wake umefikia asilimia 12.


Ujenzi wa Jengo hilo lenye uwezo wa kuhudumia familia 22 umeleta faida mbalimbali ikiwemo kutoa ajira kwa wataalam wa ujenzi, mafundi, vibarua, baba na mama lishe ambapo ajira zipatazo 171 zilipatikana hadi kukamilika kwa mradi huo. Mradhi huo unatarajia Kuongeza mapato ya ndani kwa Wakala kupitia kodi ya pango itakayokusanywa kwa makadirio ya Shilingi milioni mia mbili na kumi (210,000,000.00) kwa mwaka.

IMETOLEWA NA
OFISI YA MAKAMU WA RAIS
04 AGOSTI 2023
Arusha. 





Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akikata utepe kuashiria Ufunguzi wa Jengo la Makazi la Kibiashara la Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) lililopo katika eneo la Sekei Jijini Arusha leo tarehe 04 Agosti 2023.

 Wengine katika picha ni Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof Makame Mbarawa, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angelina Mabula, Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongela, Mtendaji Mkuu wa TBA Arch. Daud Kondoro pamoja na wawakilishi wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma.




Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof Makame Mbarawa pamoja Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angelina Mabula katika sebule ya moja ya nyumba iliopo katika Jengo la Makazi la Kibiashara la Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) lililopo katika eneo la Sekei Jijini Arusha mara baada ya kufungua jengo hilo leo tarehe 04 Agosti 2023.





SITA WAKAMATWA KWA HLKUHIFADHI WAHALIFU SAME


Watu Sita wanashikiliwa na Polisi wakituhumiwa kuwaficha kwa kuwahifadhi wahalifu walioingia kinyemela na kujihusisha na uchimbaji wa madini eneo ambalo ni chanzo tegemeo cha Maji kwa wakazi zaidi ya 22,000 wa kata nne za Vudee,Mwembe,Mhezi na Mbangalala Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro.


Kukamatwa kwa watuhumiwa hao Sita ni matokeo ya Oparesheni ya kamati ya Usalama Wilaya ya Same iliyo ongozwa na mwenyekiti wake ambae ni mkuu wa Wilaya Kasilda Mgeni, waliolazimika kufanya msako kwa kushtukiza baada ya kupata taarifa za kuwepo watu zaidi ya 70 wanaoendesha shughuli za uchimbaji madini Aina ya Dhahabu bila vibali.


Kwa mujibu wa mkuu wa Wilaya ya Same taarifa zilizo mfikia ni kwamba mbali na wachimbaji hao kufanya shughuli zao kinyemela, pia wameharibu miundombinu ya Maji na kuhatarisha Usalama wa watumiaji kwakua wanasafisha madini moja Kwa moja kwenye Bwawa wakitumia Mercury ambayo ni hatari kwa binadamu.


“Kuingia huku kinyemela na kuharibu miundombinu ya Maji NI hujuma, hatutavumilia vitendo kama hivi, niwatake Jeshi la Polisi kuweka kambi kwenye eneo hili kuimarisha ulinzi kuhakikisha shughuli za uchimbaji zinakoma na waliohusika kuihujumu Serikali lazima watafute popote na wachukuliwe hatua”.Alisema Kasilda Mgeni mkuu wa wilaya ya Same.

Awali kaimu Afisa Mtendaji wa kijiji cha Mteke Felix Ngeti amesema kwa sasa asilimia kubwa ya watu wamelazimika kuacha kutumia Maji hayo kwakua Uharibifu ni mkubwa na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi kulazimika kutafuta huduma ya majinsafi maeneo ya mbali.

"Hapa mnapoona kuna wachimbaji zaidi ya sabini na viongozi wa kijiji walikuja baada ya kupata malalamiko kwa wananchi juu ya uchaguzi unaofanyika lakini wachimbaji hao kwakua waliokua wengi waliwafukuza viongozi”.Alisema Ngeti.

Baadhi yao wakazi wanaoishi jirani na eneo hilo kulikofanyika Uharibifu wamepongeza hatua za haraka zilizochukuliwa na kamati ya Usalama, wakisema Hali ilizidi kuwa mbaya kwakua kumekua na ongezeko la idadi ya watu wanaotoka maeneo mbalimbali na kuingia kinyemela katika eneo hilo la chanzo cha Maji na kuanza uchimbaji wa madini.





 






SAHANI YA MLO UNAOFAA.


 

Sahani ya Mlo Unaofaa.

Swahili Healthy Eating Plate

Sahani ya Mlo unaofaa, ambayo imebuniwa na wataalamu wa lishe kutoka Chuo Kikuu cha Afya ya Jamii, Harvard na kuhaririwa na wataalamu kutoka Harvard, ni muongozo wa mlo kamili unaofaa kwa afya-ikiwa utatumiwa kwenye sahani ya mlo ama kama chakula cha kufunga kwenye box. Bandika nakala kwenye fridge au kabati ili ikukumbushe kuandaa mlo kamili wenye afya!

  • Sehemu kubwa ya mlo wako uwe mbogamboga na matunda – ½ ya sahani

Hakikisha unaweka aina mbalimbali zenye rangi tofauti. Viazi mbatata havihesabiwi kama mbogamboga katika Sahani ya Mlo unaofaaa kwa sababu ya madhara yake kwenye kiwango cha sukari mwilini.

  • Tumia vyakula vya nafaka isiyokobolewa – ¼ ya sahani

Vyakula vinavyotokana na nafaka isiyokobolewa kama vile ulezi, mtama, mchele wa brown vinaathari kidogo katika kiwango cha sukari mwilini na utengenezaji wa insulini kuliko vyakula vinavyotokana na nafaka iliyokobolewa.

  • Nguvu itokanayo na protini – ¼ ya sahani

Samaki, Kuku, maharagwe, njugu, vyote ni vyakula vinavyoleta afya kutokana na protini-vinaweza kuchanganywa na kachumbari, na pia kwenye Sahani ya Mlo Unaofaa vinafaa kuchanganywa na mbogamboga. Punguza matumizi ya nyama nyekundu and epuka nyama za kusindikwa kama beconi na soseji.

  • Mafuta yatokanayo na mimea kwa kiasi

Chagua mafuta yanayofaa ambayo yanatokana na mimea kama vile mizeituni, soya, mahindi, alizeti, karanga na mengineyo na epuka kutumia mafuta ambayo yameganda. Kumbuka kuwa alama ya “low-fat” kwenye makopo ya mafuta haimaanishi “mafuta yafaayo kwa afya”

  • Kunywa maji, kahawa au chai

Epuka vinywaji vyenye sukari, punguza matumizi ya  maziwa na vyakula vitokanavyo na maziwa mpaka  mara moja au mbili kwa siku, punguza matumizi ya juisi mpaka glass ndogo moja kwa siku.

  • Shughulisha mwili

Picha nyekundu ya mtu anayekimbia kwenye Sahani ya Mlo Unaofaa inakumbusha kuwa, kuweka mwili katika hali ya mazoezi ni muhimu pia katika kupunguza uzito.

Ujumbe muhimu wa Sahani ya Mlo Unaofaa ni kusisitiza kuhusu Aina ya Mlo unaofaa

  • Aina ya wanga kwenye mlo ni muhimu zaidi kuliko kiwango cha wanga kwenye mlo, kwa sababu baadhi ya vyakula vya wanga mfano mbogamboga, matunda, nafaka zisizokobolewa na maharagwe vina manufaa kiafya kuliko zingine.
  • Sahani ya Mlo unaofaa pia inashauri watumiaji kuepuka vinywaji vyenye sukari, ambavyo ni chanzo kikubwa cha kalori kwenye mwili, wakati vikiwa na faida ndogo kiafya.
  • Sahani ya Mlo unaofaa inasisitiza utumiaji wa mafuta ya kupikia yatokanayo na mimea na haijamuwekea mtu kiwango cha juu cha asilimia ya kalori  kutoka kwenye mafuta yanayofaa.





MAGAZETI YA LEO TAREHE 04 AGOSTI 2023.