Thursday, August 3, 2023

WATU WANNE WAFARIKI AJALINI WILAYANI BAGAMOYO.


Na Athumani Shomari- Pwani
 

Watu wanne wamefariki dunia baada ya magari mawili kugongana uso kwa uso usiku wa kuamkia leo Agosti 03, 2023 wilayani Bagamoyo mkoa wa Pwani.



Ajali hiyo imetokea katika kijiji cha Mapatano, Kata ya Mbwewe, Wilaya ya Bagamoyo, Mkoani Pwani, imepoteza maisha ya Mkurugenzi wa Benki ya ABSA na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Tawi la Dar es Salaam.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi wa Pilisi, ACP.  Pius Lutumo amethibitisha tukio hilo katika Taarifa aliyoitoa kwa vyombo vya habari.


Taarifa hiyo ya jeshi la polisi imesema kuwa ajali hiyo ilitokea jana Agosti 2, saa 2:30 usiku, ikihusisha gari aina ya Toyota Prado yenye namba ya usajili T.104 CBU, likitokea Dar es salaam kuelekea wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro, lililokuwa likiendeshwa na Nechi Msuya, na Scania yenye namba za usajiki T. 881 DWU / T.888 DWU lililokuwa likitokea Arusha kuelekea Dar es salaam, likiendeshwa na Philipo Mtisi mkazi wa Mafinga.



Waliofariki kwenye jali hiyo  wametajwa kuwa ni Nechi Msuya anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 45 hadi 50, Dayana Mageta, mfanyabishara na makazi wa Dar es Slaam anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 40 hadi 45, Nora Msuya anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 40 hadi 45 ambaye ni mwalimu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe Tawi la Dar es Salaam, na abiria wa kike ambaye jina lake halikufahamika na anakadiriwa kuwa na miaka 30 hadi 35.


Jeshi la polisi limesema  chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa Toyota Prado kuhama kutoka upande wa kushoto wa barabara kwenda upande wa kulia kisha kogongana uso kwa uso na lori hilo.



Jeshi la Polisi mkoani Pwani limetoa wito kwa madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazoweza kusababishwa na uzembe.




 









DKT. MOLLEL ASISITIZA KUWEPO MFUMO MMOJA WA TAARIFA KATIKA SEKTA YA AFYA

Na Rayson Mwaisemba WAF- DSM


NAIBU Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel ametoa wito kwa Asasi ya TAHIA kutafakari juu ya kuwa na mfumo mmoja wa taarifa katika vituo vyote kuanzia ngazi ya Hospitali ya Taifa mpaka kwenye zahanati ili kusaidia kuokoa gharama za matibabu kwa mwananchi anayehitaji huduma hasa katika kipindi cha Rufaa.


Dkt. Mollel amesema hayo Jijini Dar es Salaam, katika uzinduzi wa Asasi ya Tanzania Health Information Agency (TAHIA) inayoundwa na Wataalamu wa teknolojia ya Mawasiliano yenye lengo la kuweka rasilimali watu pamoja, rasilimali fedha, teknolojia ili kwa pamoja kuondoa changamoto iliyopo ya mifumo mingi inayoshindwa kubadilishana taarifa kutoka kituo kimoja kwenda kingine.


Amesema, Mfumo huo wa taarifa za mgonjwa utaokuwa unasomana, utahusisha mpaka taarifa za fedha katika vituo, lakini pia huduma zinazotolewa kwa wagonjwa wanaotumia Bima ya afya jambo litalosaidia kuboresha huduma kwa wananchi na kupunguza upotevu wa mapato katika vituo yanayofanywa na watumishi wasio waadilifu. 


Aidha, Dkt. Mollel amesema kuwepo kwa mfumo mmoja unaosomana katika Sekta ya Afya kutasaidia kuboresha matumizi ya taarifa (data) katika ngazi ya vituo na katika ngazi ya Viongozi wa juu wa Sera ili kusaidia kufanya maamuzi sahihi ikiwemo kwenye eneo la kutenga fedha.


Sambamba na hilo, Dkt. Mollel ametoa onyo kwa Wataalamu wanaolenga kutofautisha Sekta ya Afya katika utendaji na kusisitiza kufanya kazi kwa pamoja kwa kushirikiana ili kumhudumia mwananchi aliyechini bila changamoto yoyote. 


Kwa upande mwingine, Dkt. Mollel amewataka Wadau katika Sekta ya Afya kupunguza fedha zinazotumika kwenye mafunzo, semina na warsha na kuelekeza bajeti kubwa zaidi kwenye maeneo yanayoonekana na kugusa zaidi changamoto za mwananchi wa chini mwenye uhitaji wa huduma. 


Kwa upande wake Rais wa TAHIA Bw. Sosthenes Bagumhe amemshukuru Mhe. Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel kwa ushauri alioutoa na kusisitiza tayari TAHIA imeanza kulifanyia kazi suala la kuunganisha mifumo na kuifanya iweze kubadilishana taarifa kwenye vituo kuanzia taifa mpaka zahanati ili kuondoa hadha kwa wananchi. 


Nae, Mkurugenzi wa Tehama Wizara ya Afya Bw. Ilomo Silvanus amebainisha kuwa, moja kati ya vipaumbele 14 katika Sekta ya afya vinaelekeza kuimarisha ubora wa huduma kupitia Tehama hivyo kama msimamizi wa eneo hilo atahakikisha kipaumbele hicho kinatekelezeka ipasavyo.


Bw. Eric Kitali, Mkurugenzi wa Tehama Ofisi ya Rais TAMISEMI amesema, Sekta ya afya ni moja na kuahidi kuendeleza ushirikiano na mshikamano uliopo kati ya Wizara ya Afya na OR TAMISEMI hasa katika eneo la mifumo ili iweze kuleta tija kwa wananchi wanaohitaji huduma bila kuwagharimu pasipo na sababu za msingi.





 

KIPANGA AONGOZA KONGAMANO LA TIMU YA WATALAAMU WANAOTAKA KUJA KUWEKEZA NCHINI WANAOKUTANA RWANDA

KIGALI-RWANDA*


Naibu waziri wa Elimu Sayansi na Teknologia Mhe Qs Omar Kipanga ameongoza timu ya wataalamu wanaotaka kuja kuwekeza Tanzania katika sekta mbalimbali nchini walipokua Kigali Rwanda,


Akiziungumza wakati wa kongamano Hilo Mhe Qs Omar Kipanga amesema Tanzania imebarikiwa kuwa na vyanzo mbalimbali ambavyo vinahitaji kuendelezwa ili jamii ipate faida navyo Hivyo kupitia hapo wawekezaji wanapata kufahamu Maeneo gani Wao wanahijaji Hivyo ni muhimu kuelekezwa alifafanua Mhe Qs Kipanga


*"Hapa Kigali Rwanda tunakutana Wajumbe kutoka Tanzania na nchi mbalimbali zikiwemo hizi za afrika Mashariki na Ulaya Hivyo basi ni muhimu kuelekezwa kwao waweze kuja kwetu kuwekeza maana Serikali ya RAIS Dkt Samia Imeweka Mazingira Mazuri ya Uwekezaji na uendelezaji wenye tija kwa Taifa alimalizia Mhe Qs Kipanga*"


Washiriki wa Tanzania katika kongamano la Afrika la Usalama Mitandaoni linalofanyika Kigali, Rwanda wakiwemo kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), kampuni ya masuala ya usalama mitandaoni ya CHIKITO na Umoja wa WanaTEHAMA Afrika (AfiCTA) wakiongozwa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Omari Kipanga, wameshiriki vikao na wawekezaji kutoka nchi za Romania na Israel, kwa lengo la kushirikiana katika masuala ya TEHAMA na Usalama mitandaoni.


Baada ya vikao hivyo, hatua itakayofuata ni kurasimisha mazungumzo hayo ya ushirikiano baina ya Tanzania na wawekezaji hao, na kisha kuweka bayana makubaliano yaliyofikiwa. 




Washiriki wa Tanzania katika kongamano la Afrika la Usalama Mitandaoni linalofanyika Kigali, Rwanda wakiwemo kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), kampuni ya masuala ya usalama mitandaoni ya CHIKITO na Umoja wa WanaTEHAMA Afrika (AfiCTA) wakiongozwa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Omari Kipanga, wakiwa katika vikao na wawekezaji kutoka nchi za Romania na Israel, kwa lengo la kushirikiana katika masuala ya TEHAMA na Usalama mitandaoni.







 

WAZAMIAJI HARAMU 4, WALAZIMIKA KUNYWA MAJI YA BAHARI ILI WAENDELEE KUISHI.

Wazamiaji haramu 4 wa Nigeria walazimika kunywa maji bahari kwa siku nne ili waendelee kuishi baada ya kudhani wanaenda bara la Ulaya na bila kutarajia wakajikuta wapo bara la America nchini Brazil


Wakihojiwa na shirika la Reuters, mmoja amesema siku ya kuzamia alisaidiwa na rafiki yake mvuvi kumpeleka kwenye meli husika ya mizigo, ila alipoingia kinyemela chini katika rudder ya meli akakutana na Wanigeria wenzie wengine watatu ambao hakuwa akiwafahamu hivyo akaanza kuingiwa na hofu kuwa watamuua kwa kumtosa baharini


Lakini, meli ilipoanza kuondoka wote wakakubaliana watulie kimya ili wafanyakazi wa meli wasije wakawagundua na kuwaua kwa kuwatosa baharini wote


Mmoja wa wazamiaji hao kwa jina la Friday amesema ilikuwa ni safari ya hatari sana kwao hasa eneo la rudder ya meli walipokaa maana hata mtu kulala na kujisahau ilikuwa ngumu unaweza ghafla kujikuta tayari umeangukia baharini bila kutarajia hivyo walifunga neti katika eneo husika na wao wote kujifunga kamba ili yeyote kati yao asije kutumbukia baharini kimakosa maana kuna muda wakiwa kwenye hiyo neti chini yao walikuwa wanaona viumbe hatari vya baharini wakiwemo papa na nyangumi 


Alianza safari tarehe 27 June mwaka huu na amesema siku ya kumi wakiwa ndani ya meli  vyakula na vinywaji walivyokuwa wamebeba viliwaishia hivyo ilibidi kwa siku nne wanywe tu maji ya bahari maana meli ilichukua wiki mbili kufika Brazil huku wakiwa hoi kwa njaa na kutopata usingizi


Amesema walipokuja kuokolewa alijisikia furaha badala ya hofu maana safari yao yenyewe ikiwemo eneo walilokaa kwa siku zote ilikuwa hofu tu muda wowote mtu anaweza poteza maisha


Hata hivyo, walikamatwa nchini Brazil ambapo wawili kati yao kwa hiari yao wameomba kurudishwa nchini mwao Nigeria na tayari wamesharudishwa, ila wawili waliobaki akiwemo Friday na mwenzie wao wamejaribu kuomba hifadhi maalum ya kikimbizi(asylum) ili wabaki nchini Brazil ingawa bado maombi yao hayajibiwa 


Amesema wana matumaini serikali ya Brazil itawaonea huruma na kuwajibu wakae nchini humo akisema kwamba yeye ana familia na amekimbia nchi yake Nigeria kwasababu ya hali ngumu ya kiuchumi, migogoro ya kisiana na uhalifu kuzidi akisema ana familia ambayo inamtegemea na hali yake ya kiuchumi ni ngumu na alikuwa analima shamba lakini mafuriko yaliharibu kila kitu.


Miongoni mwa wazamiaji hao wana miaka zaidi ya 35


Kiongozi mmoja wa kidini nchini Brazil amewatembelea wazamiaji wa nchi mbalimbali wanaoingia kinyemela Brazil ila wazamiaji wa Nigeria huwa na safari hatarishi zaidi






 

DC OKASH ATEMBELEA BANDA LA HALMASHAURI YA BAGAMOYO NANENANE MOROGORO, AHIMIZA WAJASILIAMALI KUTAFUTIWA MASOKO YA UHAKIKA.

 


Na Nurdin Ndimbe, Morogoro.



Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Mhe. Halima Okash ametemblea banda la 

Halmashauri ya Wilaya Bagamoyo katika maadhimisho ya maonesho ya wakulima 

Nanenane 2023 yaliyofunguliwa leo tarehe 1 Agosti, 20223 katika viwanja vya 

kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Manispaa ya Morogoro.


Akizungumza na wajasiliamali katika banda hilo, aliwaomba wajasiliamali kutengeneza bidhaa zenye ubora ili kupata soko la uhakika na kujiongezea mapato ya mtu mmoja mmoja na Halmshauri kwa ujumla wake. 


Aileleza kuwa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Daktari. Samia Suluhu Hassan ipo pamoja katika kuwatafutia mitaji ya biashara na kuweka mazingira mazuri ya kufanya biashara zao.


“Napenda kutoa shukurani zangu za dhati kwenu kwa kujituma na kuja kwenye maonesho haya, hatua hii ni muhimu kwenu kwa ajili ya kujitangaza na  kupata masoko ya uhakika masoko lazima yatafutwe kwa njia zote. Alisema Mhe, Okash.



Aidha Mhe.Okash aliuagiza uongozi wa Halmashauri ya Wilaya Bagamoyo 

kuwatafutia masoko ya uhakika wajasiliamali hao, ili kukuza kipato chao na 

kuendeleza miradi yao. 


Alihaidi kuwa, baada ya maonesho ya Nanenane atapanga kikao maalumu cha kukutana nao ili kujadili kwa kina fursa zilizopo kwa wajisiliamali wadogo Bagamoyo na changamoto zinazowakabili ili kupata ufumbuzi wake.” Nihahidi 

tuu baada ya Nanenane tupange tuonane, kuona uwezekano wa nyinyi kupata 

maeneo ya kuzalishia na kuuza bidhaa zenu”. Alisisitiza.


Kwa upande wao wajasiliamali hao walisema kuwa changamoto kubwa ni 

ukosefu wa masokao ya uhakika hata hivyo, walimshukuru Mkuu wa Wilaya kwa 

kuwatembelea na kujionea bidhaa zao katika maonesho haya ya Nanenane.



Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Nane nane 2023 “ Vijana na Wanawake ni msingi 

imara wa mifumo endelevu ya chakula.





 




TAZAMA MAMBO 6 YA TIF YANAYOISAIDIA SERIKALI.

Na Rashid Mtagaluka

TANGU serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itoe ruksa ya kuanzishwa kwa asasi mbalimbali za kiraia katika historia yake, The Islamic Foundation *(TIF)* ndiyo taasisi pekee ya Kiislamu inayojipambanua kuwa na dhamira ya dhati ya kuisaidia serikali kwa vitendo katika vita dhidi ya Ujinga, Umasikini na maradhi.

*TIF* ambayo makao makuu yake mkoani Morogoro ilianzishwa mwaka 1996 huku ikijulikana kwa jina la Morogoro Islamic Foundation ambayo pamoja na mambo mengine, ilijikita katika ujenzi wa misikiti, kulea yatima pamoja na kusaidia walemavu na watu wasiojiweza.


Uchunguzi wa kina uliofanywa na mwandishi wa makala haya umebaini kuwa, baada ya kuona mafanikio na faida kubwa wanayoipata wananchi wa mkoani Morogoro bila kujali itikadi zao za kidini na kisiasa, busara na hekima za Mwenyekiti wake Alhaj Aref Nahdi pamoja na wasaidizi wake, zikawasukuma kubadilisha jina na kuiita The Islamic Foundation, bila shaka lengo likiwa ni kuinufaisha zaidi jamii kubwa ya watanzania.

Sio lengo langu kutumia jukwaa hili kuelezea kwa kina malengo ya *TIF* hapana, bali nia yangu nikuoneshe jinsi hawa jamaa licha kwamba ni taasisi ya Kiislamu, lakini wanafanya kazi kubwa katika kuisaidia serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.


*Kwanza eneo la Habari.* Sote tunajua kwamba dunia ya leo habari imekuwa ni moja ya tasnia chache zenye nguvu kubwa na thamani nzito kiasi kwamba, nchi zilizoendelea na zisizoendelea, zimeshindwa kuidhibiti.


Kushindwa huko kunatokana na ukweli kwamba, vyanzo mbalimbali vya habari vimegeuka kuwa nyenzo muhimu katika kuongoza na kuelekeza mitazamo, fikra na mawazo ya watu kwenye masuala anuwai ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.


Vyombo vya habari vimekuwa na nguvu kubwa duniani kiasi cha kusababisha baadhi ya watu kudhani na kutamani uwe ni mhimili wa nne wa dola, mbali na Mahakama, Bunge na Serikali.


Umuhimu huu wa teknolojia ya habari na mawasiliano ndiyo ukaufanya uongozi wa *TIF* chini ya Mwenyekiti Alhaj Aref na Mkurugenzi Mtendaji wake Alhaj Sheikh Ibrahim Twaha uwekeze kwenye nyanja hiyo kwa lengo la kuisaidia jamii ya Waislamu, lakini pia kuhakikisha taarifa za uzinduzi na uendelezaji wa miradi mbalimbali ya serikali zinawafikia watanzania kwa wakati kupitia Radio Imaan, Tv Imaan pamoja na gazeti la kila wiki la Imaan.


Pamoja na kuwepo kwa baadhi ya watu kuwa na mtazamo tofauti juu ya vyombo vya habari vinavyomilikiwa na *TIF* , lakini ukweli utabaki pale pale kwamba, tangu kuanzishwe kwa Radio mwaka 2002, TV mwaka 2012 na Gazeti Imaan mwaka 2015, idadi kubwa ya watanzania wamenufaika, kwa sababu vyombo hivi vimejikita katika kutoa elimu bila mipaka.


*Amani na utulivu.* Hakuna kiongozi yeyote wa nchi duniani anayeweza kuongoza nchi yenye watu wa vurugu ambao nyoyo zao zimekosa rutuba ya mawaidha yanayowajengea hofu juu ya Mola wao Muumba.


Kwa kulijua hili, uongozi wa The Islamic Foundation umefanya kila linalowezekana kujenga nyumba za ibada (misikiti) 1612 nchi nzima pamoja na kusambaza walimu na maimamu wanaofundisha namna nzuri ya kuhamiliana na jamii hata isiyo ya Kiislamu ili kulinda umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa!


*Huduma za afya.* Nani hajui kwamba afya ndiyo mtaji pekee unaomnufaisha yeyote katika maisha ya hapa duniani? Ndiyo maana serikali ya awamu ya kwanza iliyokuwa ikiongozwa na Mwalimu Julius Nyerere ilitangaza maradhi kuwa ni ADUI mmojawapo wa maendeleo yetu.


Katika kile kinachoweza kutafsirika kama uzalendo kwa nchi yao, uongozi wa TIF chini ya mwenyekiti Aref umewahi kuendesha kambi maalum za matibabu ya kibingwa ya magonjwa ya moyo katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kugharimu kiasi cha shilingi Milioni 750 za Kitanzania.


Kwa kiongozi mwingine asiye na nia njema, pesa hizi zingemtosha kuendesha maisha yake binafsi, familia yake na viongozi wenzake wa taasisi, lakini kwa Aref Nahdi haikua hivyo!


Aidha kuna zahanati mbili kubwa mkoani Morogoro ninazozifahamu, moja iko Mikumi wilayani Kilosa na nyingine ambayo inafanyiwa ukarabati iwe kituo cha afya iko Manispaa ya Morogoro, lengo likiwa ni kuipunguzia mzigo serikali ya Rais Samia wa kuhudumia wananchi wake.


*Jambo jingine ni elimu.* Baada ya kubaini serikali inahitaji kusaidiwa katika eneo hili, *TIF* ikaona potelea mbali, ebu iisaidie serikali na nchi kwa ujumla kwa kuanzisha shule tano za msingi na shule mbili za sekondari ambazo zinapokea wanafunzi wote bila ubaguzi huku gharama yake ikimzingatia zaidi mwananchi mwenye kipato Cha chini.


Mbali na shule za awali, msingi na sekondari, *TIF* wana Maahad sita kikiwemo na Maahad Imaan cha mjini Morogoro kilichoanzishwa mwaka 2018 na uzinduzi wake rasmi umefanyika Jumapili ya Julai 30,2023, lengo ni kutoa wahitimu watakaolisaidia Taifa katika kujenga nchi yenye maadili pamoja na kuhubiri amani na utulivu wakati wa utoaji elimu ya dini.


*Huduma za kijamii na misaada ya kiutu* . Hili ni eneo jingine muhimu ambalo taasisi nyingi hulisahau. Mpaka sasa *TIF* inajivunia kuhudumia na kuwalea yatima 889 nchi nzima jambo ambalo linapaswa kuigwa na taasisi nyingine.


Mara nyingi taasisi tulizonazo badala ya kuisaidia serikali na jamii kwa ujumla, zenyewe zimejigeuza mzigo kwa kuendekeza tabia ya kuomba omba kiasi ambacho hata misaada ya wafadhili wanayoipata inashindwa kuwafikia walengwa ipasavyo.

Niseme ukweli kwamba, uongozi makini wa *TIF* umehakikisha kwamba, hawajipaki doa hilo pale walipoeneza miradi ya uchimbaji visima virefu na vifupi takribani mikoa yote ya Tanzania Bara.


Miradi hii ya visima ambayo *TIF* wameisambaza mpaka katika majengo ya kutolea huduma ya serikali ikiwemo shule za msingi, sekondari na zahanati inasimamiwa vema na kwa uadilifu mkubwa na Mkurugenzi wake Muhammad Aref Nahdi.


Katika eneo hili *TIF* wanaisaidia serikali kwa kugawa misaada katika maeneo mbalimbali yanayokumbwa na majanga hapa nchini kama vile matetemeko, mafuriko nakadhalika.


Wewe msomaji wangu ni shahidi mwaka 2016 *TIF* ilitoa msaada tani 132 za chakula pamoja na nguo, magodoro vyote vikiwa na thamani ya shilingi Milioni 252 kulipotokea tetemeko la ardhi mkoani Kagera.


Msaada huu ni mbali na ule *TIF* ilioutoa mwaka 2017 wa tani 41 za chakula Pemba visiwani Zanzibar wenye thamani ya shilingi Milioni 112 kufuatia mafuriko yaliyowaacha taabani wananchi wa huko.


Jambo la mwisho kwa leo nalotaka nikujuze ambalo labda *TIF* wenyewe hawalijui ni suala la *AJIRA* .


Tofauti na taasisi nyingine zisizo za kiserikali, hawa jamaa kwa ujumla wake wameisaidia mno serikali ya Rais Samia katika eneo la utoaji ajira.


Fikiria uwekezaji walioufanya kwenye Habari na Mawasiliano pekee ni vijana wangapi wamekamata ajira zinazosaidia mpaka familia zao huko waliko? Achilia mbali madereva na watendaji wengine wanaosaidia uendeshaji wa taasisi.


Kwenye eneo la elimu umeshajiuliza ni walimu wangapi waliokosa ajira serikalini na *TIF* imewapa ajira na maisha yanaendelea huku kipato chao kikisaidia kujenga uchumi wa familia zao na Taifa kwa ujumla?


Bado kwenye afya pamoja na shughuli za ujenzi wa vituo, madarasa, uchimbaji visima huko kote ajira zisizo rasmi zimekuwa zikiwasaidia watanzania kupunguza ukali wa maisha!


Nihitimishe makala haya kwa leo kwa kusema kuwa, mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni, wengi tumezoea kuwasema vibaya wenzetu waliojaribu kadiri ya uwezo wao kuisaidia jamii pale panapotokea mapungufu kidogo ya kibinadamu.


Lakini hatuko tayari kuwapongeza na kuwatia moyo wenzetu hao kwa yale mengi waliyopatia ambayo sisi wengine tumeshindwa hata kujaribu kuyafikiria.


Miaka 27 kwa kupima mafanikio ya taasisi kama *TIF* ni muda mfupi sana ukilinganisha na taasisi nyingine nchini ambazo leo zina miaka zaidi ya 50 lakini kwa kukosa viongozi madhubuti wenye nia njema na jamii, mafanikio yake tunayatafuta kwa tochi.


*Rashid Mtagaluka ni mwandishi wa habari na anapatikana kwa simu 0718406 242.*


MAGAZETI YA LEO TAREHE 03 AGOSTI 2023.

 












Wednesday, August 2, 2023

DIWANI AWAKUMBUSHIA WALIMU UTUMISHI BORA


 NA. ELISANTE KINDULU, CHALINZE


DIWANI wa kata ya Bwilingu ,katika halmashauri ya Chalinze mkoa wa Pwani, Mh. Nassar Karama amesisitiza walimu kufanya kazi kwa bidii na kufuata kanuni za Utumishi wa umma ili kufikia malengo waliyojiwekea.

Mh. Nassar ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na walimu wa shule ya msingi Kibiki katika kata ya Bwilingu, alipowatembelea leo shuleni hapo.

Mh. Nassar amesema Jambo pekee linalomjengea mwalimu heshima ni pamoja uadilifu na ufanisi katika kazi yake ya ualimu vitakavyomfanya kuepuka migogoro na mwajiri wake.

Aidha Mh.Nassar amesema Kuwa kata yake bado inauhitaji mkubwa wa shule shikizi kutokana na wanafunzi wengi kusafiri umbali mrefu kufuata shule kongwe Mahali zilipo.

" Mfano Maeneo ya Kibiki Maziwa na Kitoho Kuna wimbi kubwa la wanafunzi kutembea umbali mrefu kuja kusoma hapa. Lazima tuone namna ya kuanzisha miradi ya Ujenzi wa shule kwenye maeneo yenye changamoto", alisema Diwani huyo.

 Mh. Diwani aliuelekeza uongozi wa shule hiyo kuitisha vikao vya wazazi na wadau wa maendeleo ya elimu kwa ajili ya uhamasishaji wa kuwapatia watoto chakula shuleni, kuhimiza maadili pamoja na masuala ya kitaaluma.

Katika ziara hiyo walimu walitoa changamoto mbalimbali za kikazi zinazowakabili ikiwamo uhaba wa nyumba za walimu, uzio na kuwepo barabara inayopita pembezoni mwa eneo la shule ambayo jamii itakuwa ikiitumia badala ya barabara ya Sasa ambayo inapita katikati ya viwanja vya shule hiyo 










MGOGORO WAMALIZIKA MKANGE; WANANCHI WARIDHIA UJENZI WA BARABARA UENDELEE

Mkange, Chalinze


Mgogoro uliosababisha kusimama kwa utekelezaji wa ujenzi wa barabara ya Afrika ya Mashariki katika kata ya Mkange , umemalizika leo baada ya wananchi wa kata hiyo kukubali kupokea fidia na kupisha ujenzi wa barabara hiyo baada ya kukutana na Mbunge wa jimbo hilo la Chalinze Ndg . Ridhiwani Kikwete.


Mbunge huyo Ndg. Kikwete, ameeleza kufurahishwa kwake na kauli hiyo ya wananchi na amekielezea kitendo hicho kuwa cha kiungwana sana . Akieleza kwenye mkutano huo , Mbunge ameeleza kuwa maamuzi yaliyofikiwa ni wazi yanafungua sio tu milango ya maendeleo katika ukanda huu lakini pia ni ufunguzi mkubwa wa fursa za kukuza kiuchumi kwa wananchi hao.


Wakiongea katika nyakati tofauti, wananchi wa kata hiyo wamemshukuru Mbunge wao kwa kuingilia kati ili kulipatia ufumbuzi jambo Hilo lililodumu kwa muda mrefu. Pia wananchi hao walimshukuru Dr. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuridhia malipo hayo ya fidia.





 

MAKAMU WA RAIS ATEMBELEA BARABARA YA INYALA MKOANI MBEYA


 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akikagua Barabara ya mchepuko katika mlima Inyala mkoani Mbeya
....................................

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ameupongeza uongozi wa Wakala ya Barabara nchini (TANROAD) pamoja na Mkoa wa Mbeya kwa usimamizi mzuri na kukamilisha ujenzi wa barabara ya mchepuko katika eneo la mlima wa Inyala mkoani Mbeya.
 
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akikagua barabara ya mchepuko katika Mlima Inyala iliogharimu shilingi bilioni 6.9 leo tarehe 01 Agosti 2023. Amesema eneo hilo lilikuwa likikabiliwa na ajali nyingi zilizogharimu Maisha ya watu hivyo kukamilika kwa ujenzi wa barabara hiyo utasaidia katika kukabiliana na adha hiyo.
 
Makamu wa Rais ametoa rai kwa madereva na watumiaji wa vyombo vya moto nchini kuwa waangalifu na kufuata sheria za usalama barabarani ili kunusuru Maisha ya watumiaji wa barabara. Ametoa wito kwa madereva kujenga utaratibu wa kukagua magari mara kwa mara ili kuepusha ajali zinazoweza kujitokeza kutokana na ubovu wa vyombo vya moto.
 
Aidha Makamu wa Rais amewataka askari wa usalama barabarani kufanya kazi kwa uadilifu kwa kusimamia sheria za usalama barabarani ili kulinda Maisha ya wananchi wanaotumia barabara hizo.
 
Septemba 11 mwaka 2022 Makamu wa Rais alitembelea eneo la Inyala na kuagiza mambo mbalimbali ili kukabiliana na ajali zilizokuwa zinajitokeza katika eneo hilo ikiwemo kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya mchepuko katika mlima Inyala, kupanua ukubwa wa barabara kutoka mita 6.7 hadi mita 10.5 pamoja na kuweka taa za barabarani katika eneo la kukagulia magari.
 
Halikadhalika Makamu wa Rais amekagua ujenzi wa Zahanati ya Shamwengo iliopo eneo la Inyala ambayo mwaka 2022 aliagiza ikamilishwe ili kusaidia majeruhi waliokuwa wanapata ajali katika mlima Inyala.

Amesema ameridhishwa kwa kukamilika kwa zahanati hiyo na kuwapongeza wananchi wa eneo hilo kwa kujitoa kusaidia watu waliokuwa wakipata ajali katika eneo la mlima Inyala. Ameongeza kwamba serikali itapeleka shilingi milioni 110 kwaajili ya ununuzi wa vifaa tiba na dawa katika zahanati hiyo.