Friday, July 5, 2019

Shirika La Posta Kuanza Kupokea Maombi Ya Fomu Za Mikopo Ya Wanafunzi Julai 8 Mwaka Huu

Na Selemani Magali,

SHIRIKA la Posta Nchini (TPC) kupitia Ofisi zake 170 zilizopo nchini kuanzia Julai 8 mwaka huu litaanza kupokea na kusafirisha vifurushi vyenye fomu za maombi ya mikopo ya wanafunzi wa Juu nchini na kuziwasilisha katika Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).

Akizungumza  Alhamisi (Julai 4, 2019) katika Maonesho ya 43 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, Meneja wa Usimamizi wa Fedha za Kigeni wa TPC, John Tinga alisema fomu zitasafirishwa zikiwa na bahasha maalum yenye nembo za HESLB na TPC.

Tinga alisema ili kurahisha zoezi hilo, TPC imeweka mawakala wake maalum watakaotumika kwa ajili ya kusaidia huduma za usafirishaji wa maombi hayo ikiwemo kutumia pikipiki katika maeneo yaliyopo sehemu za vijijini ili kuwezesha fomuhizo  kufika kwa urahisi katika ofisi za TPC zilizopo katika Ofisi zake za mikoa na Wilaya zote nchini.

Kwa mujibu wa Tinga alizitaja gharama za usafirishaji wa vifurushi hivyo ni Tsh 16,000 kwa fomu za maombi yatakayotumwa  kutoka mikoani ambayo yatawasilisha katika mfumo wa EMS wakati kwa upande wa DSM gharama za kutuma zitakuwa ni Tsh 8000 na hakutokuwa na gharama nyingine zozote zitakazotozwa kwa wateja hao.

Aliongeza kuwa TPC kwa kushirikiana na HESLB zimejipanga katika kuhakikisha kuwa zoezi hilo linaendeshwa kwa ufanisi mkubwa ili kuwawezesha wanafunzi wote nchini kuwasilisha maombi yao kwa wakati na kuepukana na usumbufu wa kutuma maombi hayo katika tarehe za mwisho.

“TPC imejipanga vizuri kwa ajili ya kufanikisha zoezi hili na hakuna fomu yoyote ya maombi itakayopotea tunachokihitaji ni kwa waombaji kukamilisha taratibu zote za msingi ikiwemo kuweka jina lake nyuma ya bahasha zetu” alisema Tinga.

Akifafanua zaidi Tinga alisema malengo ya Shirika hilo ni kutoa huduma bora kwa wananchi na wateja wote nchini ili kuhakikisha malengo ya Shirika hilo yanaweza kufikiwa ikiwemo kutoa huduma bora zinazozingatia viwango vya kimataifa.

Katika hatua nyingine, Tinga alisema Shirika hilo pia limeanzisha huduma ya mfumo mpya wa mawasiliano wa ‘Net Smart’ inayowezesha kutuma na kupokea vifurushi vyote kwa njia ya haraka zaidi.

MBUNGE SEGEREA AISIFU DAWASA



Mbunge wa Jimbo la Segerea Bonna Kamoli amewapongeza Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam DAWASA kwa huduma nzuri wanayoitoa ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam.

Ameyasema hayo alipotembelea banda la DAWASA ndani ya maonesho ya Biashara ya Kimataifa Sabasaba kwenye Viwanja vya Mwalimu Nyerere Barabara ya Kilwa Jijini Dar es salaam.

Bonna ameipongeza DAWASA kwa kuweza kupeleka huduma ya majisafi kwenye maeneo mengi hususani kwenye yale ambayo hayakuwa na mtandao wa maji kwani katika uchaguzi wa mwaka 2015 ilikuwa ni moja ya ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya kufikisha maji kwenye maeneo yote nchini.

Amesema, Dawasa wamejitahidi kufikisha maji ndani ya Jimbo la Segerea ingawa changamoto sehemu nyingine maji bado hayapatikani.

Ameeleza, jitihada kubwa zilizofanywa na Dawasa ni kubadili miundo mbinu ya maji iliyokuwa chakavu na kufanikisha kupatikana kwa maji ndani ya Jimbo la Segerea na viunga vyake.

Mbali na hilo, Bonna ameutaka uongozi wa Dawasa kutoa elimu kwa wananchi namna ya matumizi ya maji hususani kwa wadada wa kazi au watoto wanaowaacha majumbani pia kujaribu kuweka matanki ya maji ili kufahamu matumizi halisi ya maji.

Mhandisi wa Uendeshaji na Matengenezo Mkoa wa Tabata DAWASA Mhandisi Gibson Baragula amemshukuru Mbunge wa Jimbo la Segerea kwa kuona kazi inayofanywa ya kupeleka maji sehemu zote za Mkoa wa Dar es salaam.

Amesema kwa sasa wanatoa maji kutoka bomba la Kimara kwenda hadi Bonyokwa na matarajio ni kuwa na wateja 3000 ila tayari wameshawaunganishia wateja 1400 na wateja 300 wameshafanya maombi ya maunganisho mapya na hivi karibuni wataanza kuwaunganishia.

Dawasa wanaendelea kutoa huduma kwa wananchi wote wa mkoa wa Dar es Salaam katika banda lao ndani ya maonesho ya ya Biashara ya Kimataifa Sabasaba kwenye Viwanja vya Mwalimu Nyerere Barabara ya Kilwa Jijini Dar es salaam.

 Mbunge wa Jimbo la Segerea (CCM)  Bonna Kamoli akipata maelezo kutoka kwa Afisa Huduma kwa kwa wateja  alipotembelea  banda la Dawasa kwenye maonyesho ya sabasaba yanayoendelea na kupongeza juhudi za Mamlaka za kusambaza huduma ya Maji kwenye maeneo mbalimbali Jimboni kwake. 
 Mbunge wa Jimbo la Segerea (CCM) Mhe Bonna Kamoli akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea banda la Dawasa kwenye maonyesho ya sabasaba yanayoendelea na kupongeza juhudi za Mamlaka za kusambaza huduma ya Maji kwenye maeneo mbalimbali Jimboni kwake. 
Mbunge wa Jimbo la Segerea (CCM) Mheshimiwa Bonna Kamoli akipata maelezo kutoka kwa Afisa Huduma kwa kwa wateja  alipotembelea  banda la Dawasa kwenye maonyesho ya sabasaba yanayoendelea na kupongeza juhudi za Mamlaka za kusambaza huduma ya Maji kwenye maeneo mbalimbali Jimboni kwake. 

Wananchi Morogoro wapata muako kujiunga na veta



 Mkufunzi wa Chuo Cha Ualimu wa Ufundi Stadi Morogoro -VETA Mhandisi Anelisa Andungulile akizungumza kuhusu chuo hicho kwenye maonesho ya biashara Sabasaba jijini Dar es Salaam

CHUO cha Ualimu wa  Ufundi Stadi Morogoro VETA kimesema kwa sasa Watanzania wamekuwa na muako mkubwa wa kujiunga na chuo hichohuku akifafanua ili kuwa na Tanzania ya viwanda lazima waandaliwe walimu mahiri watakaofundisha vijana mahiri kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.

Hayo yamesemwa na Mkufunzi kutoka Chuo cha Ualimu wa Ufundi Stadi Morogoro Mhandisi Enelisa Andengulile wakati anazungumza na Michuzi TV kwenye banda la VETA lililopo kwenye maonesho ya biashara Sabasaba jijini Dar es Salaam.

Amefafanua kuwa  chuo hicho ni pekee nchini Tanzania ambacho kinatoa kozi za ualimu wa ufundi stadi ambapo wanapokea wanafunzi wa kada mbalimbali na kisha kuwaandaa kuwa walimu mahiri ambao watakwenda kufundisha vyuo vya ufundi stadi katika maeneo yote nchini.

"Muamko kwa Watanzanani kwa sasa  ni mkubwa kwani zamani tulikuwa tunatafuta wanafunzi na kwamba hata ilikuwa hadi inafika  Aprili hakuna kabisa wanafunzi wa kujiunga na chuo chetu.Lakini leo hii wanafunzi wengi sana wanajiunga na ukweli uwepo wa sekondari za kata umeongeza sana muamko.

 " Tunaweza kutangaza uhitaji wa wanafunzi 200 lakini wanaokuja kuomba kujiunga wanafika kuanzia 1000 au 2000 kutokana na muamko kuongezeka na jamii inaelewa kuwa ufundi ni ajira,"amesema Mhandisi Andengulile.

Ameongeza kuwa siku zote VETA wamekuwa wakitangaza kuwa Tanzania inaingia kwenye uchumi wa kati kupitia viwanda ,hivyo ili kufika huko lazima wawepo walimu mahiri wa kufundisha watanzania katika fani mbalimbali.

Hivyo amefafanua chuo chao kinatoa mafunzo ya ualimu wa ufundi stadi mahiri ambao nao watakwenda kufundisha vijana mahiri ambao watakwenda kufanya kazi katika viwanda.

Kuhusu fani gani muhimu ambazo Watanzania wanaweza kusoma,Mhandisi Andengulile amesema VETA wanafundisha fani zote kwani ni muhimu na kutoa mfano wanafundisha watu kupika maana viwandani watu wnahitaji kula, wanafundisha mashono maana viwandani kunahitajika maovaroli na nguo nyingine za kazi.

"Kila fani kwetu ni muhimu kikubwa mhusika anatakuwa mwalimu wa fani gani.Lazima tufundishe kila aina ya utalaamu na tunafahamu kuwa hakuna fani ambayo ni zaidi ya nyingine.Hivyo wale ambao wanahitaji umeme watafundishwa kuhusu umeme na tunafahamu mitambo mingi inaendeshwa kwa umeme," amesema.

Akizungumzia aina ya wanafunzi wanaowachukua kujiunga na chuo hicho cha ualimu , Mhandisi Andungulile amesema wapo ambao wamemaliza kidato cha nne lakini ni mafundi tayari aidha wana grade ya tatu au wana grade ya kwanza ambao hao wanapewa ualimu wa ufundi stadi ngazi ya cheti kwa muda wa.miaka miwili.

Pia amesema wapo pia waliosoma vyuo vya kati vya ufundi kama DIT, Arusha Tech ,Mbeya Tech na vyuo vingine ambavyo vinafafana na hivyo anbapo hao wanapata diploma ya ualimu wa ufundi stadi na kuongeza kwa mwaka huu wameingia makubaliabaliano na Open Univesirty ambapo watatoa  Post graduate  ya Diploma kwa wanafunzi wote ambao wamesoma Digrii ya Uinjia na hao watafundishwa ualimu kwa njia ya mtandao.
 Mkufunzi wa Chuo Cha Ualimu wa Ufundi Stadi Morogoro -VETA Mhandisi Anelisa Andungulile akizungumza kuhusu chuo hicho kwenye maonesho ya biashara Sabasaba jijini Dar es Salaam
Mhandisi Anelisa Andungulile ambaye ni Mkufunzi kutoka Chuo cha Ualimu wa Ufundi Stadi Morogoro akifafanua jambo

WATUMISHI HOUSING YAWAHAMASISHA WATUMISHI WOTE WA SERIKALI KUNUNUA NYUMBA ZA SHIRIKA HILO AMBAZO BEI YAKE NI NAFUU

MENEJA Masoko na Mauzo kutoka Watumishi Housing ambao wanajishughlisha na uuzaji wa nyumba za bei nafuu Raphael Mwabuponde amewataka watumishi wote wa Serikali  kununua nyumba kutoka shirika hilo  la Watumishi Housing.


Amesema mtumishi wa serikali anapokosa nyumba ya kuishi ni aibu kubwa kwani kuna nyumba za bei  nafuu kutoka shirika hilo.

Akizungumza katika Maonesho ya Sabasaba yanayoendelea viwanja vya Saba saba  jijini Dar es Salaam ,Meneja huyo amesema shirika hilo lina nyumba katika mikoa mingi  hapa nchini, hivyo watumishi wanatakiwa kuchangamkia fursa  hizo ili kuondokana na changamoto  za upangaji.

"Kila mfanyakazi amepanga nyumba huku akisahau kuwa fedha hiyo  anayolipa  kwenye upangaji anao uwezo wa kupata nyumba kutoka Watumishi Housing kwani tuna mpango  unaoitwa  mpangaji mnunuzi na malipo yake utokana na  kipato cha mtumishi huyo,"amesema  Mwabuponde

Aidha  ameongeza ili mtumishi wa umma uweze  kuheshimika ni lazima uwe unamiliki nyumba.

Kwa upande  Juma  Ally ambaye ni mtumishi wa Serikali  ameipongeza Watumishi Housing kwa jinsi inavyopambana kutoa misaada wa uelewa kwa watumishi katika umiliki wa nyumba Kwa watumishi wake.

Amesema kuwa jambo hilo ni njema kwani  watumishi wanapomilikishwa nyumba kwa malipo ya bei  nafuu na masharti ya kawaida, hivyo amewataka wananchi  wengine  kuchangamkia fursa  hizo na si  kutegemea pesa za kustaafu kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Wakati huo huo  Ofisa Uhusiano wa Watumishi Housing Meryjane Makawia amewataka pia wananchi  wote kutembelea mahali pa miradi hiyo  ilipo ili kujionea nyumba za kipee kutoka watumishi housing kwani ni za mfano na za kipekee  na wala  hazijawai kutokea  hapa nchini.

"Siku zote katika maisha hakuna baba mwenye gari bali kuna baba mwenye nyumba hivyo  ni bora watumishi wakakimbilia kununua nyumba na si  magari,"amesema .

Aidha  amewataka vijana na wananawake  kujitokeza kwa wingi  ili kujinyakulia nyumba za bei  nafuu na zisizo na masharti.
 Afisa Uhusiano na Masoko Watumishi Housing,Maryjane Makawia   akizungumza  leo jiji Dar as Salaam na  Michuzi TV kuhusu  wananchi  wote kutembelea mahali pa miradi ya nyumba  ilipo mikoa mbalimbali ili kujionea nyumba za kipee leo  kwenye Maonesho ya 43 ya Kimataifa ya Biashara maarufu kama Sabasaba, jijini Dar es Salaam.
 Mfanyakazi Watumishi Housing Hellen Mwaihojo(kulia)kiwaelekeza wananchi namna kupata nyumba leo katika Maonesho ya 43 ya Kimataifa ya Biashara maarufu kama Sabasaba, jijini Dar es Salaam.
Wananchi wakiwa katika banda la Watumishi Housing katika Maonesho ya 43 ya Kimataifa ya Biashara maarufu kama Sabasaba, jijini Dar es Salaam.(Picha na Emmanuel Massaka wa Michuzi Tv)

TPDC ILIVYOSHEREHEKEA MIAKA 50 TOKEA KUANZISHWA KWAKE,




Na Isack Thadeo; Daresalaam

Ugunduzia wa gesi asilia umechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza gharama za uendeshaji na kusababisha uzalishaji wa umeme kutegemea zaidi gesi asilia.

Akizungumza ijini Dar es Salaam katika Maadhimisho ya Miaka 50 ya Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) Waziri Nishati Dkt. Medard Kalemani alisema awali uzalishaji  wa umeme ulikuwa ukitegemea maji na kwamba mahitaji yalipoengezeka uzalishaji ulihamia katika matumizi ya mashine za mafuta huku akibainisha gesi ilipogunduliwa imechangia kupunguza gharama za uendeshaji na kuchangia kuokoa kiasi hicho cha fedha.

Amesema Mwaka 1992 tulikuwa tunatuimia umeme wa maji mahitaji yalipoengezeka tulilazimika kutumia mashine za mafuta wakati gesi asili ikigunduliwa gharama zimepungua na fedha zimeokolewa
Waziri kalemani aliongeza kuwa matumizi ya gesi yamesaidia viwanda vinavyotumia nishati hiyo kupunguza gharama za uendeshaji tofauti na awali vilivyokuwa vikitegemea umeme wa maji.

Amesisitiza kuwa mafanikio makubwa yamepatikana tangu gesi asili ilipogunduliwa ikiwemo baadhi ya magari kutumia gesi, viwanda na upunguzaji wa matumizi ya mkaa.

Amefafanua kuwa  magunia 500,000  ya mkaa sawa na tani 50 kwa mwaka  hutumika hali ambayo inachangia uharibifu wa mazingira na kuwasisitiza wananchi kuacha nishati hiyo badala yake watumie gesi kupunguza gharama.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi- Ofisi ya Waziri Mkuu na Uwekezaji Angellah Kairuki amewataka watumishi wa shirika hilo kuiga mfano wa wastaafu ambao wamelifikisha lilipo sasa.

Waziri Kairuki amesema kuna haja wizara kuagiza magari yanayotumia gesi kupunguza gharama huku akimpongeza Waziri Dkt, Kalemani kwa utendaji mzuri.

Naye Kaimu Mkurungenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Mhandisi Kapuulya Musonda amesema zaidi ya Sh bilioni 12 zimetumika kutekeleza miradi mbalimbali ya gesi huku akibainisha hadi kufikia Juni 2018 limepunguza hasara kiasi cha  Sh 52 kutoka Sh bilioni 136 za kipindi cha nyuma.

Pia amesema licha ya mafanikio bado kuna changamoto ya upatikanaji wa fedha za utekelezaji miradi, utafiti wa mafuta na gesi huku akisisitiza kuna miradi amabayo imeshatekelezwa ikiwemo ya Songas, Mtwara na Kinyerezi

Katika hatua nyingine Serikali imesema imeokoa takribani Dola Bilioni 13 tangu ilipoanza matumizi ya nishati ya gesi asilia katika uzalishaji wa umeme huku ikibainisha hadi sasa  ya magari 242 yanatumia gesi pamoja na viwanda 44.


OLENASHA ATAKA COSTECH KUSIMAMIA HAKI MILIKI ZA KAZI ZA WABUNIFU

Image may contain: 2 people, people smiling
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha ameitaka Tume ya Sayansi na Teknolojia nchini kusimamia wabunifu kupata haki ya umiliki wa bunifu zao.


Naibu Waziri Ole Nasha ametoa agizo hilo jijini Dar es Salaam, wakati alipotembelea mabanda ya Taasisi za Elimu zilizo chini ya Wizara hiyo ambazo zimeshiriki maonesho ya 43 ya biashara ya kimataifa maarufu kwa jina la Sabasaba na kukutana na mmoja wa wabunifu aliyeomba serikali imtambue kwa kuwa amebuni nyenzo ya kufundishia mfumo wa sayari shuleni.


Alisema ni vizuri wabunifu wanapoandaa kazi zao zikatambuliwa na kupatiwa haki miliki ya bunifu au ugunduzi walioufanya lakini pia kuendelea kuwafadhili ili waweze kukuza bunifu zao.


“Ninyi COSTECH hakikisheni bunifu mbalimbali nilizoziona hapa sabasaba katika mabanda yetu haziishii katika maonesho tu, bali zikuzwe na tumieni nafasi hii ya maonesho kuwakutanisha wabunifu na wafanya biashara kwa ajili ya uzalishaji,” alisema Naibu Waziri Ole Nasha.


Katika hatua nyingine Waziri Ole Nasha ameipongeza Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kwa kazi nzuri ambayo wamekuwa wakiifanya ya kukuza ubunifu na ujuzi na kuwataka kuendelea kusimamia bunifu mbalimbali za wanafunzi ili ziingie katika soko na kutatua changamoto mbalimbali za kijamii.


Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia zilizoshiriki maonesho ya Sabasaba kwa mwaka 2019 ni pamoja na Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE), Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu Mzumbe, Tume ya Nguvu za Atomiki nchini (TAEC), Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE) na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST)


WANANCHI WASHAURIWA KUHUDHURIA KLINIKI ILI KUJUA AFYA ZAO.

NA HADIJA HASSAN, LINDI

Wananchi wilayani kilwa Mkoani Lindi Wameshauriwa kuhudhuria klinik na kuelewa afya zao kwa undani kabla ya mama kuwa mjamzito ili kuepusha matatizo yanayojitokeza kipindi cha ujauzito ambayo yangeweza kuzuilika kabla ya kutokea.


Ushahuri huo umetolewa na Anjelina Abraam muuguzi mkunga kitengo cha Baba Mama na Mtoto wa kituo cha afya kilwa masoko , kilichopo wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi.


Abraam Alisema ili kulinda afya ya Mama Mjamzito pamoja na Mtoto anayetarajiwa kuzaliwa ni vyema wazazi kuanza kuhudhuria katika kituo cha kutolea huduma za afya ya uzazi miezi mitatu kabla ya kuamua kupata mtoto ili kuweza kumlinda mtoto atakaezaliwa.


Alisema hatua hiyo pia itamsaidia mama mjamzito kuuandaa mwili wake kupokea kiumbe anachokitarajia kwa kupewa ushahuri na wahudumu wa Afya waliokaribu nae.


Aliongeza kuwa jamii kubwa ya wananchi wanaoishi maeneo hayo huwa wanahudhuria kliniki baada ya mama kubaini kuwa ni mjamzito jambo ambalo kiafya linaweza kuwa sio salama kwa Mama mwenyewe na hata kwa Mtoto atakae zaliwa.


“jamii kubwa ya Wanawake wa Kilwa hupenda kuhudhuria klinik baada ya kugundua kuwa ni mjamzito na wakati mwingine huja kwa kuchelewa na hata baada ya kujifungua ndipo wanakuja kupata huduma za uzazi wa mpango.


Pia alisema changamoto kubwa kwa Baba na Mama wasipohudhulia katika vituo vya afya Mara nyingi huwenda wakawa na Magonjwa ya zinaa ambayo hupelekea mimba kuharibika ama ukawa ni mwanzo wa kuugua kwa mama huyo baada ya kubeba ujauzito hivyo ni vyema kuwahi kinki mapema ili kukabiliana na hali hiyo pindi utakapogundulika kuwa unatatizo hilo.


Nae Amina Mwaya Mkazi wa kilwa Masoko alisema kuwa kwa mara ya kwanza anahudhuria kliniki alishauriwa na Daktari baada ya kuugua siku kadhaa na kwenda Hospitali kufanyiwa vipimo na kugundulika kuwa mjamzito.


Alisema baada ya hapo alilazimika kuhudhuria Klinik kila Mwezi ili kujua maendeleo ya mtoto aliye tumboni huku akisema kuwa mahudhurio hayo ya klinik yalimsaidia kujua tarehe zake za kujifungua ambazo zilikadiriwa na watoa huuma wa kituo hicho.


Shafihi Hamisi ni miongoni mwa wanaume wachache wa Wilaya ya kilwa wanaowasindikiza wenza wao kwa ajili ya kupata huduma ya uzazi katika kitengo cha Baba Mama na Mtoto katika Kituo cha Afya cha Kilwa Masoko ambapo alisema kuwa suala la wanaume kushiriki na weza wao wanapokuwa wajawazito ni la muhimu kwa kuwa wanaweza kufahamu afya zao kwa pamoja na namna ya kumlinda na maradhi mtoto wanaemtarajia kumpata.


Alisema wanaume wengi hawapendi kwenda Kliniki pamoja na wenza wao kwa kuhofia msongamano wa wanawake katika maeneo hayo pamoja na dhana potofu ya kuwa jukumu la kwenda kliniki ni la mama peke yake jambo ambalo sio kweli.


Hata hivyo Hamisi ametowa Wito kwa akina Baba kujenga tabia ya kwenda na Wenza wao klinik kwa kuwa usimamizi wa afya ya familia ni jukumu la watu wote