Sunday, May 26, 2019

AMANA BANK, VODACOM WAZINDUA HUDUMA MPYA YA HALAL PESA.

Amana Bank kwa kushirikiana na Mtandao wa simu za mkononi wa Vodacom kwa pamoja wamezindua huduma mpya ijulikanayo kama ''halal pesa''.


Huduma hii mpya sasa itapatikana kwa wateja wa Vodacom wanaotumia M-Pesa na wale wa Amana Bank kwa kuzingatia misngi ya sheria ya kiislamu.


Akizungumza katika uzinduzi wa huduma hiyo, Mkurugenzi mtendaji wa Amana Bank, Dkt. Muhsin Salim Masoud, alisema kwa muda mrefu wamekuwa wakifikiria jinsi ya kuwafikia wateja wengi zaidi ambao wanapenda kutumia miamala ya kifedha kwa mujibu wa sheria ya kiislamu.


Dkt. Muhsin alisema Amana Bank imekuwa ikibuni njia mbalimbali za kuwafikia wateja wake wazamani na wapya hivyo wameweza kuanzisha huduma hiyo ya halal pesa ambapo wateja wa Vodacom wanaotumia M-pesa wataipata huduma hiyo mpya inayozingatia misingi ya sheria ya kiislamu.


Alisema katika huduma ya halal pesa mteja wa Amana Bank anaweza kufanya miamala yake kwa kutumia Vodaco M-Pesa huku akiwa bado yupo kwenye sheria za uislamu kuhusu miamala ya kifedha.


Akifafanua zaidi Dkt. Muhsin alisema Amana Bank imetimiza miaka minane mpaka sasa na kwamba katika kipindi chote hicho toka kuanzishwa kwake imekuwa ikiendesha shughuli zake kwa mujibu wa sheria za kiislamu.


Alisema Benki hiyo ndio benki pekee hapa Tanzania ambayo mfumo wake wa kifedha umesimamia sheria za benki za kiislamu.


Hata hivyo aliongeza kwa kusema kuwa, licha ya Benki hiyo kufuata sheria za kiislamu katika uendeshaji wake, bado inaendelea kuwahudumia wateja wake bila ya kubagua dini, rangi wala kabila hivyo amewataka wateja wao kutambua kuwa Benki hiyo ipo kwaajili ya kila mtu.


Alisema kuanzishwa kwa huduma ya halal pesa kwa kushirikiana na mtandao wa simu wa Vodacom kutasaidia watu wengi zaidi kufikiwa na huduma giyo ambayo inafuata sheria za kiislamu.


Kwa upande wake Mkuu wa kitengo cha huduma za M-Pesa kutoka Vodacom, Tulisindo Rashid alisema, halal pesa imelenga zaidi ya robo tatu ya waislamu nchini Tanzania ambao kwa kupitia mfumo wa M-Pesa wataweza kuweka fedha na kupata faida kihalali (bila ya riba).


Alisema kwa muda mrefu waislamu wamekuwa na uhitaji mkubwa wa huduma za kuweka fedha zinazfuata sheria za dini ya kiislamu ambapo huduma hiyo itawezesha watumiaji wake kuweka fedha kwa njia rasmi ya halal pesa.


Alisema Vodacom itaendelea kutoa ufumbuzi wa mambo mbalimbli ili kukidhi mahitaji ya wateja wake katika mfumo wa kifedha kwa kutumia teknolojia ya kidigitali yenye gharama nafuu na uwezo wa hali ya juu.


Aliongeza kwa kusema kuwa, halal pesa ni huduma rahisi na ya kipekee inayoendana na sheria za kiislamu ambayo imegawanyika katika mafungu mbalimbali.


Alifafanuwa kuwa, mafungu hayo ni pamoja na kuweka pesa binafsi, kwaajili ya kwenda hija, watoto au kuweka pesa kwa muda mrefu kuanzia miezi 3 hadi 12.


Aidha, alitumia nafasi hiyo kutoa wito kwa maimamu wa misikiti kufungua Akaunti kupitia halal pesa ambapo msikiti utapewa namba maalum ya utambulisho (Code number) itakayowawezesha waumini kuchangia michango ya msikiti hata kama hawapo msikitini.


Alisisitiza kuwa, huduma hiyo ni salama na kwamba inafuata misingi ya kiislamu kwa kupata muongozo kutoka kwa wanazuoni wa kiislamu kuhusu masuala ya kifedha.


Sheria ya kiislamu imeharamisha riba na kuhalalisha biashara hivyo muislamu anapofanya miamala ya kifedha huchunga mipaka ya kisheria na kujiepusha na riba.


Kwa huduma hii mpya ya halal pesa iliyozinduliwa kwa ushirikiano wa Amana Bank na Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom itamuwezesha muislamu kuweka fedha Amana Bank na kuzitoa kwenye M-Pesa huku akiwa hakutani na riba na badala yake atapata gawio la faida ambalo limeruhusiwa katika sheria ya uislamu.
 
Mkurugenzi mtendaji wa Amana Bank, Dkt. Muhsin Salim Masoud, akizungumza katika uzinduzi huo ulifanyika katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.
    
Mkuu wa kitengo cha huduma za M-Pesa kutoka Vodacom, Tulisindo Rashid akizungumza katika uzinduzi huo ulifanyika katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.

 Mkuu wa Maendeleo ya Biashara na Masoko wa M-Pesa, Polycarp Ndekana, akizungumza katika uzinduzi wa halal pesa uliofanyika katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.
 
Mkuu wa kitengo cha huduma za M-Pesa kutoka Vodacom, Tulisindo Rashid (kushoto) wa pili ni
Meneja mfawidhi huduma kwa wateja kutoka Amana Bank, Juma  Msabaha wakiwa katika picha ya pamoja.
 

MPANGO WA MATUMIZI BORA YA ARDHI KATIKA MRADI WA BOMBA LA MAFUTA GHAFI WAZINDULIWA.

Image may contain: 11 people, including Subira Mgalu, people smiling, people standing Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi (katikati) akiwa tayari kukata utepe ikiwa ni ishara ya kuzindua Mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa Vijiji, Wilaya na Mikoa itakayopitiwa na mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) wa tatu kushoto ni Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanry  aliyeshika kipaza sauti.
...................................... 

Serikali imezindua Mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa Vijiji, Wilaya na Mikoa itakayopitiwa na mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) ikiwa ni hatua nyingine katika utekelezaji wa mradi huo.


Mpango huo umezinduliwa katika Kijiji cha Sojo, Kata ya Igusule, wilayani Nzega, Mkoa wa Tabora tarehe 25/5/2019 na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi aliyeambatana na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanry na Meneja Mradi wa EACOP, Mantin Tiffen.


Akizungumza na wananchi wa Sojo, Waziri Lukuvi, alisema kuwa, mpango huo wa matumizi ya ardhi unahusisha Mikoa Nane, Wilaya 24 na Vijiji 226 ambapo vijiji 30 vipo katika Mkoa wa Tabora.


" Mpango huu unazinduliwa katika Kijiji cha Sojo kwa niaba ya Vijiji vyote nchini kwa kuwa hapa Sojo ndipo patakuwa na kituo kikubwa cha kutoa huduma katika mradi wa bomba la Mafuta kuliko vituo vingine kwani kutakuwa na Kambi Kuu na kiwanda cha kutayarisha mabomba yatakayotumika kusafirisha mafuta kitajengwa hapa." alisema Lukuvi.


Katika hatua nyingine, Waziri Lukuvi, alitoa onyo kwa wavamizi wa ardhi iliyotengwa kwa ajili ya mradi huo kuwa, tayari mkuza wote ulishapigwa picha za anga hivyo fidia itatolewa kwa wananchi wanaostahili tu.


Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, alisema kuwa, kazi za mradi wa EACOP zilizopangwa kufanyika katika Kijiji hicho cha Sojo zina uwekezaji wa shilingi bilioni 600 na matarajio ni kuwa kazi hizo zitaanza mwezi wa Tisa mwaka huu.


Alisema kuwa, kutakuwa na ajira zitakazozalishwa hivyo alitoa wito kwa wananchi kuchangamkia fursa zitakazojitokeza kutokana na uwekezaji huo.


Alisema kuwa, mpaka sasa mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi umeshatoa ajira zaidi ya 200 na matarajio ni kuwa utaendelea kutoa ajira zaidi kwa watanzania.


Kuhusu umeme, alisema kuwa, Wizara iko katika Mpango wa kusambaza umeme kwenye Vijiji vyote vinavyopitiwa na mkuza huo kwa gharama ya shilingi elfu 27,000 tu ili kuweka mazingira wezeshi ya kutekeleza mradi husika.


Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri, alisema kuwa, Mkoa huo utaweka mazingira wezeshi ili mradi huo wa Bomba ufanyike kwa ufanisi na ameahidi kusimamia matumizi bora ya ardhi iliyotengwa kwa ajili ya mradi husika.


Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa Bomba la Mafuta kutoka Tanzania, Salum Mnuna, alisema kuwa, Rais John Pombe Magufuli amefanya jitihada mbalimbali zilizowezesha mradi huo kuanza kutekelezwa nchini hivyo ni muhimu kwa wanachi wakafanya bidii kuchangamkia fursa zinazotokana na mradi.


Aliongeza kuwa, mradi huo licha ya kutoa ajira za ujuzi wa juu, kati, chini na vibarua, utaboresha pia baadhi ya miundombinu kama vile Reli na Barabara pamoja na huduma za kijamii katika maeneo ambayo mradi utapita.
Image may contain: 4 people, including Subira Mgalu 
 Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, akizungumza wakati wa kuzindua Mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa Vijiji, Wilaya na Mikoa itakayopitiwa na mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP)
Image may contain: 7 people, including Subira Mgalu, people smiling, people standing, sky, cloud and outdoor

RIDHIWANI NA MIRAJI FOUNDATION WAGAWA FUTARI

Katibu wa Mbunge Jimbo la Chalinze, Iddi Swala (kulia) akikabidhi futari kwa wakazi wa cha Magome kata ya Pera Halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo, futari imetolewa na Taasisi ya Miraji Foundation.
............................................
 
Na Omary Mngindo, Chalinze

MBUNGE wa Jimbo la Chalinze wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani, Ridhiwani Kikwete, akishirikiana na Taasisi ya Miraji Foundation wamegawa futari kwa waumini wa dini ya Kiislamu Msikiti wa Swafiyyah uliopo Kitongoji cha Magome kata ya Pera jimboni humo.


Katika hafla hiyo fupi iliyofanyika msikitini hapo, Idd Swala Katibu wa Mbunge ndiye aliyakabidhi kwa niaba ya Mbunge Ridhiwani Kikwete, huku Abdilah Makuluta akiiongoza Taasisi ya Miraji ambayo ni rafiki wa mbunge kwa kusaidia kwenye nyanja mbalimbali za kijamii.


Akizungumza kabla ya ugawaji futari hiyo ambayo ilikuwa na ujazo wa tani moja ya, Makuluta alisema kuwa Taasisi yao chini udhamini wa Muft Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Aboubakar Zuber ikiongozwa na Mkurugenzi Halifa Abdurahamaan, imejiwekea utaratibu wa kugawa futari kila mwaka kipindi cha mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.


"Kwaniaba ya uongozi wa Miraji Foundation chini ya udhamini wa Muft Sheikh Mkuu Aboubakar Zuber ikiongozwa na Mkurugenzi Halifa Abdulhaman, tumekuwa na utaratibu wa kugawa futari kila mwaka kipindi cha mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, leo tupo hapa Magome Kata ya Pera halmashauri ya Chalinze," alisema Makuluta.


Kwa upande wake Iddi Swala akizungumza kwa niaba ya Mbunge, alianza kuishukuru taasisi hiyo kwa misaada mbalimbali  inayotoa jimboni humo, huku akieleza kwamba Msikiti wa Swafiyyah uliopo kitongojini hapo pia umejengwa na taasisi hiyo.


"Ndugu zetu wa Miraj Foundation wamekuwa karibu nasi kusaidia maendeleo ya jimbo letu katika nyanja mbalimbali, huu msikiti tunaofanyia shughuli hii fupi leo, wameujenga wao, tuendelee kuwaombea Mwenyezimungu awazidishie kila la kheri, ili mwakani inshaaAllaah watuletee zaidi ya hiki tulichokipata" alisema Swala, katibu wa Mbunge wa Chalinze.


Kwa upande wake Tatu Mkenge kwa niaba ya wana-Magome alianza kumshukuru mbunge Ridhiwani Kikwete na washirika wake, kwa kuona umuhimu wa kuwafikia katika kuwaunga mkono kwenye mfungo huo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.


Mwenyekiti wa Kitongoji hicho Idd Mbato aliishukuru taasissi hiyo na mbunge Ridhiwani, huku akimuomba mbunge aendelee kuwatafutia wahisani wengine wasaidie nyanja nyingine ndani ya Kitongoji chake na Kata kwa ujumla.
 
Katibu wa Mbunge Jimbo la Chalinze, Iddi Swala akikabidhi futari kwa Mgaza Makunja, mkazi wa cha Magome kata ya Pera Halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo, futari imetolewa na Taasisi ya Miraji Foundation.
 
 Katibu wa Mbunge Jimbo la Chalinze, Iddi Swala akikabidhi futari kwa mkazi wa cha Magome kata ya Pera Halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo, futari imetolewa na Taasisi ya Miraji Foundation.

Picha zote na Omary Mngindo.
  

Friday, May 24, 2019

BAGAMOYO YAKOPESHA VIKUNDI SH. MIL. 57

Na Omary Mngindo, Bagamoyo
HALMASHAURI ya wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani, imevikopesha vikundi vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, kiasi cha shilingi milioni 57 kupitia mapato yake ya ndani.


Katika hafla fupi iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo chini ya Mkuu wa wilaya Zaynabu Kawawa, taarifa ya Mkurugenzi Fatma Latu imeeleza kwamba, halmashauri yao imetenga shilingi milioni 488.5 kwa ajili ya zoezi hilo.


"Halmashauri tunaendelea na utekelezaji wa sera kwa vitendo, ambapo kwenye maeneo ya kiuchumi ikiwemo kilimo, ufugaji, biashara na sanaa, bajeti ya 2018/2019 tumetenga shilingi milioni 489,532, kati ya hizo milioni 248,911 ni asilimia kumi ya mapato ya ndani," iloeleza taarifa ya Latu. 

Imeongeza kwamba katika mchakato huo kiasi cha shilingi milioni 240,421 ikiwa ni marejesho ya mikopo ambayo vikundi mbalimbali vilikopeshwa kupitia ailimia 4 za wanawake, 4 za vijana huku mbili zikiwa za watu wenye ulemavu. 


Kwa upande wake Kawawa alitanabaisha kwamba kati ya fedha hizo za halmashauri shilingi milioni 57, imezinufaisha vikundi vinne vya wanawake vilivyopewa milioni 16.3, vikundi vinane vya vijana millioni 28.7 wakati kikundi kimoja cha watu wenye ulemavu kikipatiwa shilingi milioni 2.5. 


Aidha amewataka viongozi wa halmashauri zote mbili za Bagamoyo na Chalinze kupitia maofisa maendeleo jamii kuwa naa utamaduni wa kuwapatia mafunzo ya ujasiriamali wanavikundi, yatayowasaidia kitumia vema mikopo wanayopatiwa ili Marengo ya serikali yafikiwe. 


"Nitumie nafasi hii kuwapongeza wote mlioona umuhimu wa kujiunga kwenye vikundi kisha kuomba mikopo kutoka halmashauri, mtumie vizuri mikopo yenu ili mrejeshe kisha kuwapatia fursa wengine kukopa, kumbukeni mikopo hii haina riba," alisema Kawawa.


 Wakizungumza na waandishi wa habari baada ya zoezi hilo, Grace Vision Mhazini vikundi cha Faraja alisema kuwa huo ni mikopo wa pili tangu waanzishe kikundi hicho, huku wakiishukuru serikali kwa mikopo isiyokuwa na riba. 


Nae mmoja wa mwanakikundi cha wenye ulemavu Dunia Abdalaah alisema kwamba huo ni mkopo wao wa kwanza wa shilingi milioni 2.5 tangu kuanzishwa kwake, ambapo wanajijusisha na kilimo cha mpunga na ufugaji wa kuku.

Wednesday, May 22, 2019

RIDHIWANI KIKIKWETE ATOA NENO KWA WA ISLAM.

 
 Na Shushu Joel, Chalinze.

MBUNGE wa jimbo la chalinze wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani, Ridhiwani Kikwete amewataka waislamu kutumia nafasi hii katika kipindi hiki cha mfungo wa Ramadhani kuwaombea viongozi ili waweze kutekeleza majukumu yao vizuri na kuleta maendeleo kwa jamii yote hapa nchini.

Rai hiyo ameitoa alipokuwa akizungumza na viongozi mbalimbali wa dini ya kiislamu katika Kata ya Pera kitongoji cha Magome alipokuwa akikabidhi Msikiti wa Masjid Swafiya uliojengwa kwa msaada wa Mbunge huyo kwa kushirikiana na Taasisi ya Miraji Islamic Center.

"Kipindi kama hiki cha mfungo tunatakiwa kumcha Mwenyezimungu na kusaidia masikini kwani funga inamaana kubwa sana hapa duniani hivyo kila mwislamu aliyefanikiwa kupata nafasi hapa duniani ni lazima amsaidie mwenzake japo futali" alisema Kikwete.

Alisisitiza kuwa mwezi huu wa Ramadhani ni mwezi ambao tunasisitizwa kusoma sana Qur'an kwasababu ndio mwezi ambao Qur'an iliteremshwa kupitia kwa Mtume Muhammad Swalla llaahu Alayhi Wasalaam ili uwe muongozo kwa watu wote hapa duniani, pia usomaji huo unamalipo makubwa sana kwa Mungu.

Aliongeza kuwa kutokana na jinsi viongozi wa Serikali wanavyopambana kufanikisha maendeleo kwa wananchi wanyonge kwa kubana wenye kutumia raslimali za wananchi vibaya ni lazima viongozi hao wachukiwe na baadhi ya watu.

Aidha mbunge huyo amempongeza Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kwa juhudi zake anazozifanya katika utekelezaji wa ilani ya chama cha mapinduzi (ccm) kwa ufanikishaji wa maendeleo kwa wananchi wanyonge.

Kwa upande wake Shehe Mohamed amempongeza Mbunge huyo kwa kutambua thamani ya uislamu na hata kujitolea kwa hali na mali katika ufanikishaji wake wa ujenzi wa msikiti huo katika Kata ya pera.

Hivyo amemuhakikishia Kikwete kuwa wao kama viongozi wa dini wataendelea kuliombea Taifa hili ili liondokane na majanga ya aina yeyote ile na wananchi wake kuweza kunufaika zaidi na maombezi ya viongozi wao wa dini.

Naye Tatu Mkenge amemshukuru Mbunge wa jimbo hilo katika dhamira yake ya kupambania ujenzi wa msikiti wa Magome ili kuwaondolea changamoto ya mahali pa kumuomba Mwenyezimungu.

Aidha amewataka waislamu kote kuongeza juhudi za kuwaombea viongozi mbalimbali ili utendaji wao wa kazi uendelee kutukuka na uwe wenye kumuogopa Mungu.