Tuesday, May 21, 2019

WAKURUGENZI WA HALMASGAURI WATAKIWA KUTENGA FEDHA KUUNGANISHA UMEME TAASISI ZA SERIKALI.

NA HADIJA HASSAN, LINDI.


Serikali imewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kutenga fedha kwa ajili ya kuweka umeme katika taasisi za umma vijijini ambako miradi ya umeme vijijini REA inapita.


Wito huo umetolewa na Waziri wa Nishati Dkt Medardi Kalemani jana mei 20 alipokuwa anazungumza na wakazi wa kata ya Namangale katiaka Halmashauri ya Wilaya ya Lindi Mkoani humo katika hafla fupi ya uwashwaji wa Umeme katika shule ya Msingi namangale kijijini hapo.


Kalemani alisema kama serikali ilipoamua kuanzisha mradi huo wa umeme vijijini REA moja ya Vipaumbele vyake ni kuwekwa katika Taasisi za Umma ambako kwa kiasi kikubwa wananchi wanakwenda kupata huduma katika maeneo hayo.


Alisema ni vyema viongozi hao wakajiwekea utaratibu wa kutenga fedha kwa ajili ya maeneo hayo mapema iwezekanavyo kwani Serikali itaanza kufanya Ziara maalumu ya kukagua majengo hayo ili kuhakikisha kila kijiji ambacho kimepitiwa na mradi huo taasisi zake zimewekewa umeme.


“Kwahivyo wenyeviti wa vijiji, madiwani pamoja na Wakurugenzi tengeni fedha mahususi kabisa kwa ajili ya kupeleka katika Mashule, Zahanati, Vituo vya Afya pamoja na miradi ya maji kote humo lazima kuwekewe umeme kwa kuwa wananchi ndiko wanakokwenda kupata huduma” alisema Waziri Kalemani Kalemani.


Aliongeza kuwa Inasikitisha kuona umeme umefika kijijini lakini wakati unatembelea utashangaa kuona wananchi wananyoosha mikono wanakuambia eti wao kituo chao cha Afya hakina Umeme cha kushangaza unamuuliza mwenyekiti wa kijiji kama ameshalipia umeme kwa ajili ya kuunganishiwa lakini anakosa majibu.


Katika kuunga Mkono jitihada hizo za Serikali Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya State grid inayotekeleza mradi wa REA Vijijini katika Mkoa wa Lindi Charles Mlawa alihaidi kuweka mfumo wa Umeme katika Shule ya Msingi ya Namangale iliyopo katika kata ya Namangale Halmashauri ya Wilaya ya Lindi ili kuifanya shule hiyo kuwa na umeme wa kutosha na wa uhakika

TIF YAGAWA VYAKULA DAR ES SSALAAM.

Image may contain: 6 people, people smiling, beard
Kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa Taasisi ya The Islamic Foundation Aref Nahdi, katika ni Naibu balozi wa umoja wa falme za kiarabu UAE Mohamed Ibrahim Al bahri, na kulia ni  Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Mkaonda, wakati wa zoezi la kugawa vyakula lililofanyika jijini Dar es Salaam.
.....................................

Taasisi ya The Islamic Foundation (TIF) yenye makao yake makuu Mkoani Morogoro nchini Tanzania, kwa kushirikiana na Umoja wa nchi za falme za kiarabu UAE wametoa msaada wa vyakula wa tani Zaidi ya 40 kwa watu Zaidi ya 700 wasiojiweza.


Walengwa wa msaada huo ni wazee, wajane, watu wenye ulemavu pamoja na watu wenye uhitaji, katika kipindi hiki cha Mwezi wa Ramadhani.


Msaada huo umetolewa jijini Dar es salaam na kushuhudiwa na Mkuu wa Mkoa huo, Paul Mkaonda  pamoja na Sheikh wa Mkoa huo Alhad Mussa Salum.


Vyakula vilivyotolewa kwa kila mlengwa ni pamoja na  mchele kg20 unga wa sembe kg20 maharage kg10 sukari kg5 pamoja na mafuta ya kupikia lita 3.


Naibu balozi wa umoja wa falme za kiarabu UAE Mohamed Ibrahim Al bahri ameikabidhi Taasisi ya The Islamic Foundation (TIF) huku akishuhudia ugawaji ukifanyika kwa walengwa.


Akizungumza na wanahabari katika zoezi hilo la ugawaji wa msaada naibu balozi wa umoja wa falme za kiarabu UAE Mohamed Ibrahim Al bahri, amesema kuwa msaada huo ni moja kati ya miradi wanayo itekeleza kwa nchi ya Tanzania lengo likiwe ni kuweza kutoa ushirikiano wa karibu kwa serikali katika kuwahudumia wananchi wa Tanzania katika masuala ya huduma za kijamii ikiwemo kutekeleza miradi ya kutibu moyo watoto wadogo.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Taasisi ya The Islamic Foundation Aref Nahdi amesema kuwa msaada huo ni juhudi za Taasisi ya The Islamic Foundation (TIF) za utekelezaji wa miradi wanayopatiwa na wahisani na wao kuwafikishia wahitaji kwa wakati.


Alisema Taasisi hiyo imekuwa ikitekeleza shughli mbalimbali za kufikisha mahitaji kwa watu wanaokusudiwa hali inayopelekea kujenga uaminifu kwa wahisani dhidi ya Taasisi hiyo.


Alifafanua kuwa, katika kugawa misaada mbalimbali chini ya Taasisi ya The Islamic Foundation (TIF) yapo mambo yanayozingatiwa ili malengo ya watoaji yafikiwe kwa kuwakabidhi walengwa.


Alibainisha kuwa, katika uislamu kuna zaka na sadaka ambapo sadaka hupewa mtu yeyote mwenye uhitaji huku zaka ikitakiwa kutolewa kwa makundi maalum ambayo yame ainishwa katika Qur ani.


Akielezea historia ya The Islamic Foundation katika kutoa misaada ya aina hiyo, Aref alisema hiyo si mara ya kwanza kugawa misaada na kwamba hiyo inatokana na kuaminika na wahisani wa ndani na nje ya nchi.


Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda akizungumza katika zoezi hilo liloandaliwa na Taasisi ya The Islamic Foundation (TIF) amewataka viongozi wa dini kuzidi kusimamia Amani ya nchi.


Aidha amepongeza ushirikiano huo wa Falme za Kiarabu pamoja na nchi ya Tanzania ambao unasaidia kuimarisha mahusiano.
Image may contain: one or more people and crowd 
Vyakula hivyo kama vinavyoonekana pichani, ambapo mtu mmoja ameweza kufungashiwa mchele kg20 unga wa sembe kg20 maharage kg10 sukari kg5 pamoja na mafuta ya kupikia lita 3.

 Magari yaliyobeba vyakula hivyo yakiwa Makao Makuu ya Taasisi ya The Islamic Foundation (TIF) mjini Morogoro kabla ya kuanza safari ya kwenda jijini Dar es Salaam.

DKT. KALEMANI AMUAGIZA MKURUGENZI WA TANESCO KUIMARISHA UPATIKANAJI WA UMEME

Image may contain: 9 people, people standing and outdoor
NA HADIJA HASSAN, LINDI.


Waziri wa nishati Medadi kalemani amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la umeme Tanzania TANESCO kwa kushirikiana na meneja wa Tanesco Mkoa wa Lindi kuhakikisha umeme katika wilaya ya Ruangwa unaendelea kuwa imara na bora wakati wote.


Waziri kalemani ameyasema hayo jana mei 20 alipokuwa katika kata ya chinongwe Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa Mkoani Lindi wakati  akzungumza na wakazi wa kata hiyo katika hafla fupi ya uwashwaji wa umeme kijijini hapo katika shule ya Sekondari chinongwe.


Alisema katika kutekeleza Miradi ya umeme vijijini REA Serikali tayari imeshatoa kiasi kikubwa cha fedha hivyo ni wajibu wa watendaji kusimamia miradi hiyo kwa ufanisi.


“kama serikali tumetumia hela nyingi ili kuondokana na matumizi ya kununua mashine pamoja na mafuta kwa ajili ya kuendeshea mitambo ya kuzalishia umeme ili kurekebisha hali ya upatikanaji wa umeme katika Wilaya ya Ruangwa na maeneo ya jirani”.


Alisema ni muhimu kwa mameneja wa shirika hilo kuhakikisha umeme unakuwa wa uhakika katika vijiji vyote vilivyounganishiwa umeme kupitia mpango wa Umeme Vijijini REA.


Pamoja na mambo mengine Dkt Kalemani aliwataka wananchi wa wilaya ya Ruangwa na maeneo mengine kutumia fursa ya umeme wanaounganishiwa katika kuanzisha shughuli za kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuanzisha viwanda vidogo vidogo Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakazi wa kata hiyo akiwemo mwajuma nambambo na Asha saidi wameishukuru Serikali kwa kuwaletea nishati ya Umeme katika maeneo yao ambao utawafanya kuanzisha shughuli mbalimbali za kiuchumi kwa kutumia umeme huo.

 
Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa REA kwa awamu ya tatu meneja wa Tanesco Wilaya ya Ruangwa Pyuza Samwel alisema kuwa katika kutekeleza mradi huo wilaya ya Ruangwa inatarajia kunufaika katika vijiji 34 ambapo mpaka sasa tayari vijiji 16 vimeshawasha umeme huo, huku akisema kuwa katika mradi huo pia unatarajiwa kujenga njia kubwa ya umeme 33kv(km) 117.74 na kueleza kuwa kazi iliyofanyika mpaka sasa ni km 90.9 sawa na asilimia 77.12%.


Alizitaja kazi zingine zinazotakiwa kufanyika kuwa ni ujenzi wa njia ndogo ya Umeme LV km 106.6 ambapo kazi iliyofanyika ni km 10.15 sawa na 10.18%, Transfoma 50kva 50 ambapo tayari transfoma 18 zimeshawekwa sawa na asilimia 18%

Monday, May 20, 2019

BIL. 29 KUMALIZA TATIZO LA MAJI CHALINZE

Na Omary Mngindo, Ubena


RAIS Dkt. John Magufuli amesikia kilio cha wananchi wa jimbo la Chalinze, wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani, kinachohusu tatizo la maji, ambapo ametenga kiasi cha sh. Bil. 29 kwa ajili ya mradi mpya wa maji kutoka Ruvu kwenda Chalinze.


Mradi huo unaolenga kuwasaidia wananchi hao ambao kwa miaka mingi wamekuwa katika adha hiyo, pia unatarajiwa kufika katika maeneo ya Msata, Mdaula, Msolwa, Ubena, Tukamisasa na kwenda njia ya jeshini kata ya Ubena.


Hayo yamebainishwa na Mbunge wa Jimbo hilo Ridhiwani Kikwete, alipokuwa anazungumza na Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Ubena, Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji wakiwemo Wajasiriamali wa vikundi mbalimbali na waendesha bodaboda.


Alisema kuwa alifikisha kilio hicho kwa Rais Dkt. Magufuli kuhusiana na adha hiyo, ambapo amekubali kisha kutenga kiasi hicho cha fedha zitakazokwenda kufanikisha mradi huo, utakaoambatana na kuiua Chaliwasa kisha kutengeneza Mamlaka moja pamoja na Dawasa.


"Hayo yote anayoyafanya Rais Magufuli inatokana na thamani tunayompa sisi wana-Chalinze, lakini si mimi Mbunge ninayeifanya kazi hiyo, bali na nyinyi ambao kwa umoja wetu tunafanikisha masuala mbalimbali ya kimaendeleo, pia tunajukumu la kutangaza kazi nzuri inayofanywa na Chama Cha Mapinduzi," alisema Ridhiwani.


Alisema kuwa ifike wakati vikundi vinavyopatiwa pesa vitambue kwamba, havipewi kwa sababu wamewachagua, bali serikali ya Chama Cha Mapinduzi inataka kuona mabadiliko ya maisha ya watu wake, huku akitolea mfano vikundi vya bodaboda vinaongeza mifuko yao, pia wakulima watanunua pembejeo za kisasa pamoja na mbolea.


Kuhusu changamoto ya maji inayoikabili jimbo hilo, Ridhiwani alisikitishwa kuwepo kwa taarifa zisizo rasmi zinazodai kwamba, kati ya 2010 mpaka 2015 ndoa nyingi zimepata matatizo, chanzo kikubwa kikiwa ni maji yanayotoka kuanzia saa 6 usiku hali inayoelezwa kuchangia hali hiyo.


"Maji yanawezaje kutoka saa 6 usiku yashindwe kutoka asubuhi, wakati mwingine unaona wazi kuna mazingira ya hovyo kabisa ya kutaka kuharibu nyumba zetu, tushukuru kwamba kuna mpango wa kuiua CHALIWASA, kisha kutengeneza Mamlaka moja pamoja na DAWASA, maana hawa wameshindwa kuendeleza mradi," alisema Ridhiwani.


Kwa upande wake Diwani Nicholas Muyuwa alisema kuwa halmashauri ya Chalinze inaendelea na juhudi za kupunguza kama si kumaliza changamoto zinazowakabili wana- Ubena, kwa kuhakikisha wanaboresha miundombinu ya shule, afya na barabara ambazo kwa sasa baadhi yao zinapitika vizuri.


"Niwashukuru wananchi wa Ubena Zomozi kwa ushirikiano na viongozi wao ambao wamekuwa karibu katika kuibua miradi ya kimaendeleo, inayoanzishwa na wenyewe kisha halmashauri na serikali Kuu kuunga mkono juhudi hizo," alisema Muyuwa.


Mmoja wa wakazi aliyejitambulisha kwa jina Idd Mohamed alikiambia kikao hicho kwamba wanakabiliwa na changamoto ya maji, sanjali na mifugo ambayo imekuwa ikiingizwa kwenye mashamba yao hali inayosababisha usumbufu mkubwa.