Thursday, April 18, 2019

MUHIMBILI WAMPOKEA BINTI MWENYE KIDONDA MGONGONI.

Image may contain: 1 person
Binti mwenye umri wa miaka 25, Mariam Rajab mkazi wa kitongji cha Inung'una mkoani Singida, aliyeteseka kwa muda mrefu na kidonda mgongoni, ambaye video yake ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii akiomba msaada wa matibabu, hatimaye amepokelewa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), saa sita usiku wa jana, Jumatano.


Mariam amepokelewa katika Idara ya Magonjwa ya Dharura, ambapo kwa sasa anaendelea kufanyiwa vipimo vya awali na kisha atalazwa, ili aweze kuonana na jopo la madaktari bingwa wa upasuaji kwa ajili ya kupatiwa matatibu zaidi.


Msemaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Aminiel Algaesha amesema matibabu ya mgonjwa huyo yatagharimiwa na hospitali hiyo.


Kupitia video yake iliyosambaa katika mitandao ya kijamii, binti huyo alijieleza namna anavyoteseka na kidonda hicho.


“Mimi naitwa Mariam Rajabu naishi katika Mkoa wa Singida, Mtaa wa Mnung’una naishi katika familia ya kimasikini, wazazi wangu hawana uwezo wa kunisaidia tatizo langu, tatizo ambalo ninalo, tatizo lenyewe ambalo ninalo ni kidonda ambacho kipo hapa mgongoni, naombeni Watanzania wenzangu muweze kunisaidia niweze kwenda hospitali ya Muhimbili ili niweze kupata matibabu.Sina cha kuwalipa bali Mungu atawalipa, asanteni” 


Baada ya kuonekana kwa video hiyo, Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu aliuagiza uongozi wa MNH kumtafuta Mariam popote alipo ili apelekwe hospitalini hapo kwa ajili uchunguzi na matibabu.


Mariam ameletwa Muhimbili kwa gari la wagonjwa kutoka mkoani Singida, lililoanza safari yake saa 8:00 mchana jana.
Mariam Rajab (25) akipokelewa na wahudumu wa Afya katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

KAMATI YA AMANI PWANI YATEMBELEA MRADI WA UMEME RUFIJI.

Image may contain: 4 people, people smiling, people standing and outdoor  
Kamati ya Amani Mkoa wa Pwani imetembelea eneo la Mradi wa Umeme wa mto Rufiji na kufanya maombi maalum ili utekelezaji wake ukamilike kwa ufanisi na kwa wakati uliopangwa.


Kamati hiyo yenye wajumbe kutoka madhehebu mbalimbali imeshiriki kwenye ziara ya siku tatu iliyoanza April tisa ikijumuisha Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Pwani na ya Wilaya ya Rufiji, Wakuu wa Wilaya sita, Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji pamoja na Viongozi wa Serikali ya Kijiji cha Mloka.


Wakiwa katika eneo la mradi, msafara huo ulioongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Mhandisi Evarist Ndikilo ulipokea maelezo ya utekelezaji wa mradi huo mkubwa wa kimkakati kutoka kwa Wataalamu wa Shirika la Umeme nchini-TANESCO wanaosimamia mradi huo.


Akifafanua lengo la ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Mhandisi Evarist Ndikilo alieleza kuwa sehemu ya eneo la ujenzi wa mradi liko katika Mkoa wa Pwani hivyo ni wajibu wa jamii kuwa na uelewa mpana na wajibu wa kushiriki katika utekelezaji na kulinda miundombinu yake ikiwa ni pamoja na kubaini changamoto zilizopo au zinazoweza kujitokeza na kuzipatia ufumbuzi.


“Asilimia kubwa ya shughuli za utekelezaji wa mradi huu zitakuwa katika eneo la Mkoa wa Pwani hivyo tunataka tuone namna ambavyo Kamati ya Ulinzi na Usalama na Kamati ya Amami itashughulikia maswala yote yaliyoko ili mradi huu usikwame” amesema Mhandisi Ndikilo.


Mkuu wa Mkoa ameongeza kuwa pamoja na kuwa wataalamu wa kitanzania na Mkandarasi wako kwenye eneo la utekelezaji wakiendelea na majukumu yao, bado kuna mambo mengine nje ya eneo hilo ambayo Mkoa kwa kushirikiana na Taasisi nyingine zinawajibu wa kuyasimamia ili kuhakikisha kuwa utekelezaji unafanikiwa na kwa wakati

SERIKALI YASHUSHA GHARAMA ZA URASIMISHAJI

Image may contain: 1 person, smiling
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amesema kuanzia sasa gharama za urasimishaji haitazidi shilingi 150,000 badala ya 250,000 iliyopangwa awali na makampuni yatakayoenda kinyume yatachukuliwa hatua ikiwemo kufutwa.


Lukuvi alitoa kauli hiyo jana Aprili 17, 2019. jijini Dar es Salaam alipokutana na Makampuni ya Upangaji na Upimaji yanayofanya kazi ya urasimishaji katika mitaa mbalimbali nchini pamoja na watendaji wa sekta ya ardhi.


Kwa mujibu wa Lukuvi, baada ya Wizara yake kuona zoezi la urasimishaji linasuasua wamegundua asilimia 30 pekee ndiyo iliyorasimishwa tangu kuanza zoezi hilo na hali hiyo imechangiwa na uwezo mdogo wa wananchi wengi kumudu gharama za urasimishaji.


Waziri Lukuvi alisema, alichotegemea kwa makampuni yaliyopewa kazi ya urasimishaji ni kuwa na uzalendo kwa kushusha gharama lakini yameshindwa kupunguza gharama jambo lililoifanya serikali kuona haja ya kupitia upya gharama hizo na kubaini gharama za msingi ili kumuwezesha mwananchi kupata hati na kusisitiza punguzo hilo halitawahusu waliolipia gharama za urasimishaji.


Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ameyataka makampuni yanaoyoendesha zoezi la urasimishaji kuhakikisha kiasi cha fedha inachowatoza wananchi kinaishia hatua ya Hati na gharama itakayolipwa na mwananchi baada ya kurasimishwa ni kodi ya ardhi na kuyatahadharisha kutochukua muda mrefu kukamilisha zoezi hilo.


Amewataka wananchi wote wanaoishi kwenye maeneo yasiyo rasmi kuhakikisha wanaingia katika zoezi la urasimishaji ili kupata hati itakayowawezesha kiuchumi na kusisitiza kuwa suala hilo linafanyika kwa nia njema kwa nia ya kuwaongezea mtaji wananchi kwa kupatiwa nyaraka itakayowasiadia kukopa fedha benki.

MAGAZETI YA LEO APRILI 18, 2019.

Wednesday, April 17, 2019

WIZARA YA NISHATI YATEKELEZA AGIZO LA MHESHIMIWA RAIS KUHAMIA MJI WA SERIKALI IHUMWA

Image may contain: 1 person, screen and indoorWaziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani, akiwa katika ofisi mpya za wizara hiyo katika mji wa serikali Ihumwa jijini Dodoma.
............................................

Wizara ya Nishati imetekeleza agizo la Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli, alilotoa mwishoni mwa wiki iliyopita kuwa viongozi wote wa Wizara wahamie katika mji wa serikali Ihumwa jijini Dodoma.


Tayari viongozi wote wakuu wa wizara hiyo ambao ni Waziri, Naibu Waziri na Katibu Mkuu wamehamia Ihumwa tangu Jumatatu ya Aprili 15, 2019 ambapo wanaendelea na majukumu yao kama kawaida.


Aidha, zoezi la viongozi wengine pamoja na watumishi wa Wizara hiyo kuhamia Ihumwa linaendelea ambapo wasaidizi wa viongozi hao wakiwemo masekretari, madereva na wahudumu wamekwishahamia pia.


Katika zoezi hilo linaloratibiwa na Idara ya Utawala, linahusisha kuweka vitendea kazi katika ofisi mbalimbali zilizosalia na kuhamisha watumishi waliosalia.
Image may contain: 5 people, people smiling, people standing, suit and outdoor

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani, akisalimiana na watumishi wa wizara hiyo mara alipowasili katika jengo jipya la wizara ya Nishati

 Image may contain: 1 person, standing
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Hamisi Mgalu akiwa katika lango kuu la kuingilia ofisi za wizara hiyo jijini Dodoma
Image may contain: Subira Mgalu, sitting, table and indoor 
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Hamisi Mgalu, akiwa ofisini kwake jijini Dodoma mara baada ya kuhamia rasmi kwenye jengo jipya la wizara hiyo tayari kwa utekelezaji wa majukumu ya Taifa.
Image may contain: 2 people, people standing 
 Watumishi wa Waziri wa Nishati, wakiangalia mabox ambayo ndani yake kuna vifaa kwaajili ya matumizi ya ofisi hiyo vikiwa bado havijapangwa kwenye utaratibu wake unaotakiwa wakati wizara hiyo ilipohamia rasmi katika jengo lake jipya jijini Dodoma.
Image may contain: 3 people, people smiling, people standingWatumishi wa Waziri wa Nishati, wakiwa na nyuso za furaha baada ya kuingia kwenye jengo jipya la wizara hiyo katika mji wa serikali Ihumwa jijini Dodoma.