Wednesday, April 10, 2019

RIPOTI ZA MDHIBITI NA MKAGUZI MKUU WA HESABU ZA SERIKALI KWA MWAKA WA FEDHA ULIOISHIA TAREHE 30 JUNI, 2018

MDHIBITI na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) Prof. Mussa Juma Assad,akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dodoma wakati akitoa Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha Ulioishia Tarehe 30,Juni,2018.
..................................


MDHIBITI na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) Prof. Mussa Juma Assad,amesema kuwa katika ukaguzi uliofanyika kwa mwaka 2017/18 Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA  haikujumlisha shilingi bilioni 18.95 ambazo ni Vocha za Misamaha ya Kodi kutoka Hazina.


Prof.Assad ameyasema hayo leo Aprili 10, 2019. jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ripoti ya za Mdhibiti na Mkaguzi  Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha ulioishia juni 30 mwaka 2018.


Amesema  kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilikusanya shilingi trilioni 15.38 ikilinganishwa na malengo yaliyowekwa ya kukusanya shilingi trilioni 17.31; hivyo kuwa na nakisi ya makusanyo kwa shilingi trilioni 1.93 ambazo ni sawa na asilimia 11 ya malengo.


 Hivyo, makusanyo halisi ya mwaka 2017/18 ni shilingi trilioni 15.40 yakijumuisha na Vocha za Misamaha ya Kodi kutoka Hazina.


“Kodi zilizoshikiliwa katika Kesi za muda mrefu kwenye Mamlaka za Rufaa za Kodi Mamlaka ya Mapato Tanzania ina Mashauri ya Kodi ya Thamani ya shilingi trilioni 382.6 kwenye Mamlaka za Rufaa za Kodi ikiwa ni ongezeko la kiasi cha shilingi trilioni 378.2 (asilimia 8595) ikilinganishwa na shilingi trilioni 4.4 kwa mwaka wa fedha 2016/17”amesema Prof Assad.


Aidha amesema  kuwa ongezeko hili limechangiwa kwa kiasi kikubwa na mashauri manne yenye thamani ya shilingi trilioni 374.7 yanayoihusu Kampuni ya Uchimbaji Madini ya ACACIA.


“ Kutokukusanywa kwa mapato yatokanayo na kodi ya Kiasi cha Shilingi Bilioni 46.81 na Dola za Marekani Milioni 2.74, ukaguzi wangu ulibaini kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania ilishindwa kukusanya mapato zaidi ya shilingi bilioni 46.81 kutoka kwa walipakodi mbalimbali.


 Kwa upande mwingine Prof.Assad amesema  kuwa wakati wa uhakiki wa bidhaa zinazoingizwa Nchini na Nchi jirani ili zisafirishwe kwenda Nchi nyingine, Mamlaka ya Mapato Tanzania ilishindwa kumpatia ushahidi kuthibitisha kuwa kodi ya shilingi bilioni 57.09 ililipwa.


“ Aidha, nilibaini kuwa bidhaa zilizosafirishwa kutoka nchini kwenda nchi nyingine zilizopaswa kutozwa kodi ya ongezeko la thamani ya shilingi milioni 649.45 ziliruhusiwa kwenda nje ya nchi bila kukamilisha taratibu za Forodha”amesisitiza


“Mamlaka ya Mapato Tanzania ilishindwa kutoa ushahidi wa nyaraka za kuthibitisha kuwa kodi stahiki zilikusanywa. 3.2.2 Usimamizi wa Deni la Serikali Kufikia tarehe 30 Juni, 2018, deni la Serikali lilikuwa shilingi trilioni 50.92, ambapo deni la ndani lilikuwa shilingi trilioni 14.73 na deni la nje shilingi trilioni 36.19; kiasi hiki ni ongezeko la shilingi trilioni 4.84 sawa na asilimia 10.5 ikilinganishwa na deni la shilingi trilioni 46.08 lililoripotiwa tarehe 30 Juni, 2017”ameongeza Prof.Assad


Hata hivyo amesema  kuwa “Katika ukaguzi wangu, nilibaini masuala ya msingi yafuatayo kuhusu Deni la Serikali na usimamizi wake:


(a) Mapungufu katika usahihi wa taarifa kutokana na udhibiti wa ndani usiojitosheleza katika kuweka kumbukumbu na kutoa taarifa za Deni la Serikali.


(b) Serikali kuchelewa kulipa madeni ya Benki Kuu ya kiasi cha shilingi bilioni 212.7. Kati ya hizo, shilingi bilioni 199.79 zinatokana na riba ya nakisi ya Serikali, na shilingi bilioni 12.9 ikiwa ni sehemu ya Serikali ya gharama za kudhibiti ukwasi kuanzia mwaka 2015/16 hadi 2017/18.


(c) Kutokuwapo kwa uwianishaji wa taarifa za mfumo wa malipo (Epicor) na Mfumo wa Utunzaji wa Taarifa za Deni la Taifa wa Jumuiya ya Madola (Common Wealth Secretariat-Debt Record Management System – (CS-DRMS)). Hii inasababisha taarifa za fedha kutowiana na vyanzo vyake, hivyo kuhatarisha uadilifu wa taarifa za Deni la Serikali.


Akiongelea  ukaguzi maalumu wa Mfumo wa Utambuzi wa Alama za Vidole (AFIS) alisema ulibaini mambo yafuatayo:


(a) Mahitaji ya kitaalamu kutoka idara inayotumia mfumo huo hayakuzingatiwa wakati wa kutathmini na kutoa zabuni.


(b) Malipo ya shilingi bilioni 3.30 yalifanyika kwa mzabuni kwa ajili ya huduma ya matengenezo na msaada wa kitaalamu wa Mfumo wa Utambuzi wa Alama za Vidole kwenye mikoa nane ya Kipolisi ya Temeke, Mwanza, Simiyu, Rukwa, Tabora, Kigoma, Geita, na Kinondoni lakini Jeshi la Polisi lilishindwa kuthibitisha kuwa matengenezo hayo na msaada wa kitaalamu ulifanyika. 45


(c) Vifaa vya Utambuzi wa Alama za Vidole vyenye thamani ya shilingi bilioni 1.73 havikufungwa kwenye magereza 35 yaliyoainishwa. Badala yake vilihifadhiwa katika Ofisi ya Upelelezi, Makao Makuu ya Jeshi la Polisi.


(d) Malipo ya shilingi milioni 604.39 kwa ajili ya mafunzo kwa wataalamu 30 hayakufanyika.


(e) Jeshi la Polisi lilishindwa kuionesha timu yangu ya ukaguzi zilizo monita 58 za kompyuta aina ya Dell zenye thamani ya shilingi milioni 159.16 zilizopelekwa kwenye Kitengo cha Uchunguzi wa Kisayansi cha Makao Makuu ya Jeshi la Polisi (Forensic Unit). Pia, monita 213 za kompyuta aina ya Dell zililipiwa kiasi cha shilingi milioni 195.22 kwa mzabuni Lugumi Enterprises Limited lakini mzabuni hakuzileta.


Udhaifu katika Ukusanyaji wa Shilingi Bilioni 97.58 za Madeni ya
Alisema kuwa “Nilibaini kuwepo kwa kiwango kidogo cha kukusanya marejesho ya madeni ndani ya Mamlaka za Maji, kwa kuwa mapato mengi yalikuwa hayajakusanywa na yamezidi muda uliowekwa kwenye Sera ya Mikopo ya Mamlaka husika.


Katika jumla ya deni hilo la shilingi bilioni 97.58, nilibaini kuwa shilingi bilioni 39.59 (sawa na asilimia 41) ni Madeni ya Serikali, na shilingi bilioni 57.99 (sawa na asilimia 59) ni madeni ya wateja wengine.


Ongezeko hili la madeni limesababishwa na ufuatiliaji hafifu wa wadeni na kutokufuata Sera ya Mamlaka za Maji ya kukata huduma za maji kwa wateja wanaokiuka taratibu.


Hata hivyo amesema kuwa katika ukaguzi wangu, nilifanya tathmini ya utekelezaji wa mapendekezo ya kiukaguzi yaliyotolewa miaka iliyopita na kubaini kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kuyafanyia kazi.


Tathmini ya utekelezaji wa mapendekezo hayo inaonesha kuwa kati ya mapendekezo 350 yaliyotolewa miaka iliyopita, mapendekezo 80 sawa na asilimia 22.9 yametekelezwa kikamilifu. Mapendekezo 124 sawa na asilimia 35.4, utekelezaji wake unaendelea.


 Prof.Assad amesema  kuwa, mapendekezo 72 sawa na asilimia 20.6 utekelezaji wake haujaanza; na mapendekezo 74 sawa na asilimia 21.1 yamepitwa na wakati.


Aidha amesema  kuwa katika Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo iliyokuwa inatekelezwa na Taasisi mbalimbali kwa mwaka wa fedha 2017/18, “nimetoa jumla ya Hati za Ukaguzi 469. Kati ya hizi, Hati zinazoridhisha ni 455, sawa na asilimia 97; na Hati zenye shaka ni 14, sawa na asilimia 3” 

Zaidi Tembelea .http://www.nao.go.tz/?p=2081

 

Monday, April 8, 2019

MAKOSA YA USALAMA BARABARANI YAPUNGUA MKOANI LINDI

NA HADIJA HASSAN, LINDI

JESHI la polisi mkoa wa lindi limefanikiwa kupunguza makosa ya usalama wa barabarani kwa asilimia 26 kwa kipindi cha miezi mitatu januari hadi machi 2019 ukilinganisha na makosa yaliyotendeka kwa kipindi kama hicho mwaka uliopita wa 2019


Hayo yameelezwa na kamanda wa Polisi Mkoani humo Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP) Pudensiana  Protas alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni ofisini kwake


Kamanda Protas alisema kuwa kipindi cha mwezi Januari hadi Machi 2019 makosa ya Barabarani yaliyoripotiwa yalikuwa 7,096 ikilinganishwa na makosa yaliyoripotiwa kwa kipindi kama hicho mwaka 2018 ambapo yalikuwa 9,550 hivyo kuwa na upungufu wa matukio 2,454 sawa na asilimia 26


Akieleza sababu za kupungua kwa makosa hayo Kamanda Protas alisema kuwa makosa hayo yamepungua kutokana na kufanyika kwa oparesheni za mara kwa mara za kushitukiza kwa kukamata Magari mabovu yanayoendelea kuendeshwa pamoja na yale yanayokiuka sheria za barabarani


Hata hivyo kamanda Protas alisema kuwa katika kipindi hicho  cha Mwezi Januari hadi Machi 2019 pia makosa ya jinai yaliyoripotiwa yamepungua kwa asilimia 8% kutoka1,687 kwa mwaka 2018 hadi kufikia 1,556 kwa 2019  ukilinganisha na makosa yaliyofanyika kwa kipindi kama hicho na kufanya upungufu wa makosa 131 

JELA MIEZI 6 KWA KUVUNJA MLANGO WA BABA YAKE.

Kijana mmoja mwenye umri wa miaka 21 Mkazi wa Mianzini B kata ya Kisutu wilayani Bagamoyo (jina linahifadhiwa) amehukumiwa kwenda jela miezi sita kwa kosa la kushambulia mlango na kuvunja kioo cha mlango huo nyumbani kwa baba yake mzazi.


Upande wa mashtaka ulidai mbele ya mahakama ya mwanzo Mwambao mjini Bagamoyo kuwa, mnamo tarehe 19 mwezi Machi 2019 majira saa tano na nusu usiku huko nyumbani kwa baba wa mshitakiwa  Kitongoji cha mianzini B kata ya Kisutu wilayani Bagamoyo mshtakiwa kwa makusudi alitenda kosa hilo na kusababisha hasara ya shilingi 150,000.


Akitoa maelezo ya kosa mbele ya mahakama, mlalamikaji ambae ni baba mzazi wa mshitakiwa alisema mwanae huyo kutokana na matukio yake yasiyomridhisha alilazimika kumuwekea utaratibu maalum wa makubaliano ili waweze kuishi kwa pamoja kama baba na mtoto.


Alisema miongoni mwa masharti hayo ni pamoja na muda wa kurudi nyumbani katika mkataba waliosaini wote waili (baba na mtoto) ambao ulisema mwisho wa kurudi nyumbani kwa mtoto huyo ni saa nne kamili usiku na sio zaidi ya hapo.


Mara baada ya kusaini mkataba huo ambao nakala yake ilipelekwa kituo cha polisi Bagamoyo kama ushahidi, mtoto huyo kwa siku kadhaa alikuwa anakiuka yale waliyokubaliana kwenye mkataba na hasa muda wa kurudi nyumbani na kwamba amekuwa akirudi nyumbani zaidi ya saa nne kinyume na makubaliano na bila ya kutoa maelezo yoyote yenye kuridhisha .


Kufuatia hali hiyo tarehe 19 mwezi machi 2019, ambapo ni siku ya saba toka kusainiwa kwa mkataba huo wa makubaliano, kijana huyo alirudi nyumbani saa tano na nusu usiku, ambapo alikuta milango imefungwa hali iliyomlazimu kugonga ili afunguliwe.


Aidha, mara baada ya kijana huyo kugonga mlango baba yake alisema "sikufungulii mlango kwakuwa umekiuka mkataba wetu kuhusu muda wa kurudi nyumbani ambao mwisho ni saa nne kamili usiku".


Kufuatia majibu hayo ya baba yake, kijana huyo hakuweza kujitetea kwa kuongea chochote na badala yake alichukua mawe na kuyapanga kwaajili ya mashambulizi ambapo alipiga mlango kwa mara kadhaa na kusababisha majirani kutoka ili kushuhudia kinachoendelea kutokana na kishindo kikubwa kilicholia hapo nyumbani.


Kijana huyo aliendelea kushambulia mlango huo huku akisema kuwa "nitaingia ndani kwa namna yoyote ile na kwamba wewe (baba) huna uwezo wa kunizuia"alisikika kijana huyo akimjibu baba yake.


Katika harakati zake za kuvunja mlango alifanikiwa kuvunja kioo cha juu ya mlango na kuingia ndani huku akiahidi kuendeleza mashambulizi kwa siku zinazofuata ikiwa atawekewa masharti na kufuatwa fuatwa katika maisha yake.


Kesi hiyo ya jinai Namba 120 ya mwaka 2019 iliyosikilizwa na hakimu Japheti Angilile Masebo wa Mahakama ya mwanzo Mwambao mjini Bagamoyo ilihukumiwa siku hiyo hiyo baada ushahidi kukamilika na mahakama kumtia hatiani mshitakiwa.


Akisoma hukumu hiyo Hakimu Masebo alisema anamuhukumu mshitakiwa kwenda jela miezi sita ili iwe fundisho kwa vijana wengine wenye tabia za kudharau wazazi wao na kuvunja sheria za nchi.


Aliongeza kwa kusema kuwa, mshitakiwa alifanya kosa hilo kinyume na kifungu cha 326 kifungu kidogo cha (1) sura ya 16 kanuni ya adhabu iliyorejewa mwaka 2002.


Awali mshitakiwa alipotakiwa kujitetea alisema alilazimika kuvunja mlango ili aingie ndani akalale baada ya baba yake kukataa kumfungulia huku ikizingatiwa kuwa, hana sehemu nyingine ya kulala.


"Mheshimiwa Hakimu, huyu mie ndio baba yangu na pale ndio nyumbani kwangu nilivunja mlango ili nikalale kwakuwa sina sehemu nyingine ya kulala" alisema kijana huyo mara baada ya kutiwa hatiani.


Hakimu Masebo alimtaka ajitetee ni kwanini Mahakama isimpe adhabu mara baada ya kumtia hatiani, mshitakiwa alijibu "hapo nimemaliza, mheshimiwa utaamua wewe"


Akizungumza na mwandishi wa habari hizi nje ya Mahakama, baba mzazi wa kijana huyo ambae hakutaka jina lake litajwe alisema amechukua uamuzi wa kumpeleka mahakamani mwanae, baada ya njia tofauti za kumrekebisha kitabia kushindikana.


"Nimetumia njia nyingi kumrekebisha kijana wangu lakini imeshindikana, huenda hii ikawa njia sahihi ya kujifunza nidhamu kwa kijana huyu" Alisema baba huyo huyo wa mshitakiwa.


Aliongeza kwa kusema kuwa ninao uwezo wa kutengeneza kioo pamoja na huo mlango wote lakini kilichonifanya nimpeleke mahakamani kutaka ajifunze utii wa sheria ikiwa ni pamoja na sheria za nchi za mungu na zile mnazokubaliana na wazazi wako pia ni sheria zinazopaswa kutiiwa.


"sio kwamba siwezi kutengeneza huo mlango, au sio kwamba simpendi mwanangu hapana, nimefanya hivyo baada ya njia nyingi za kumrekebisha kufeli nadhani hii ndio njia sahihi kwake, Alisema mzazi huyo.

Sunday, April 7, 2019

TAKUKURU LINDI YAMTAKA MSAMBAZAJI WA VIFAA VYA UJENZI KUONGEZA UBORA.

NA HADIJA HASSAN, LINDI

TAASISI ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU)Mkoa wa Lindi imemshauri msimamizi wa mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Lindi Mkoani Humo kuwataka wasambazaji wa vifaa  kuongeza ubora wa vifaa vya ujenzi huo ama Halmashauri kutafuta wasambazaji wengine wa 


Hayo yamesemwa na kamanda wa TAKUKURU Mkoani humo Stephen Chami mwishoni mwa wiki iliyopita alipokuwa anazungumza na Waandishi wa habari ofisini kwake  lengo likiwa kutoa Taarifa ya utekelezaji wa majukumu yao kwa kipindi cha miezi mitatu ' januari hadi machi 2019


Chami alisema katika kipindi hicho Taasisi yao imefuatilia  matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo mbalimbali inayoendelea katika Mkoa huo yenye thamani ya Tsh. Bilioni 8,180,718,289 ambapo ufuatiliaji huo umefanyika ili kutanzama na kujilidhisha na miradi husika pamoja na kuona thamani ya fedha zilizotumika katika miradi hiyo


Chami aliongeza ushauri huo umekuja baada ya Ya Taasisi hiyo kufanya ufuatiliaji katika mradi huo na kubaini kuwa kunabaadhi ya vifaa vinavyotumika katika mradi wa ujenzi wa Hospitali hiyo vina ubora mdogo


Mradi huo wa Hospitali hiyo ya Wilaya ya Lindi  unajengwa katika eneo la Kiwalala ambapo mpaka kukamilika kwake utaghalimu kiasi cha Tsh. Bilioni 1,500,000,000 ukiwa unasimamiwa na Halmashauri husika kwa kutumia mfumo wa Force Accout


Pia Chami pia alisema kuwa Taasisi yao bado inaendelea kufuatilia kwa ukaribu kila hatua ya ujenzi huo mpaka utakapokamilika kwa asilimia 100%