Saturday, March 30, 2019

SERIKALI YAIAGIZA BMT KUHAKIKISHA UCHAGUZI WA KLABU YA YANGA UNAFANYIKA NDANI YA SIKU 30

Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa Bw.Alex Nkenyenge (Kulia) akizungumza na Waandishi wa Habari leo Machi 30, 2019 Jijini Dodoma kuhusu kutekeleza maagizo ya Serikali kwa  Baraza hilo kusimamia Uchaguzi ndani ya Klabu ya Dar es Salaam Young Africans (Yanga) ndani ya siku 30 kuanzia leo.Kushoto ni Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Michezo wa Wizara ya Habari utamaduni Sanaa na Michezo Bw.Yusuph Singo.
.....................................


Na Shamimu nyaki –WHUSM

Serikali imeliagiza Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kushirikiana na Shirikisho la mpira wa Miguu (TFF) kuhakikisha uchaguzi ndani ya Klabu ya Dar es Salaam Young Africans (Yanga) unafanyika ndani ya siku 30 kuanzia leo.


Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Michezo Bw.Yusuph Singo katika mkutano na Waandishi wa Habari leo Jijini Dodoma ambapo amesema kuwa migogoro iliyokuwepo huko nyuma imeshafika tamati hivyo uchaguzi ndani ya Klabu hiyo ni lazima ufanyike.


“Nailekeza BMT iwaelekeze TFF kuhakikisha taratibu zote za uchaguzi zinafuatwa na uchaguzi ndani ya Klabu ya Dar es Salaam Young Africans unafayika ndani ya siku 30 kuanzia sasa”.amesema Bw.Singo.


Aidha Bw.Singo amewahisi Viongozi, wanachama na wapenzi wa Klabu ya Dar es Salaam Young Africans kutoanzisha migogoro wala vikwazo vingine bali kutumia siku 30 hizo kufanya uchaguzi ili kupata viongozi watakaoisimamia na kuiongoza Klabu hiyo kuendelea kufanya vizuri katika mpira wa miguu ndani na nje ya nchi.


Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Bw.Alex Nkenyenge amesema amepokea maagizo na atayafanyia kazi mara moja ili kipindi kilichowekwa na Serikali cha siku 30 Klabu ya Yanga iwe tayari ina uongozi.


Bw.Nkenyenge ameongeza kuwa atahakikisha Kamati ya Uchaguzi ya TFF inapanga utaratibu unaotakiwa kufuatwa kulingana na Katiba ya Shirikisho hilo ili Uchaguzi huo ufanyike hatimaye migogoro iliyodumu kwa muda mrefu ndani ya Klabu hiyo ifikie mwisho na Klabu iendelee kufanya vizuri katika mpira wa miguu.


Klabu ya Dar es Salaam Young Africans (Yanga) ni miongoni mwa Klabu kubwa za mpira wa miguu hapa nchini ambayo kwa muda mrefu haijatekekeleza uchaguzi kwa mujibu wa Katiba yao.

MOTO MKUBWA OFISI ZA TANESCO MLANDIZI

Image may contain: outdoor
 Na Omary Mngindo, Mlandizi - Machi 30

MOTO mkubwa umezuka katika Kituo kidogo cha kupozea umeme cha Kanda ya Mlandizi Kibaha Mkoa wa Pwani, ulioanza kuwaka saa moja asubuhi ya leo  Machi 30, 2019.

Moto huo ulioleta taharuki kubwa kwa wananchi waishio jirani kabisa na mtambo huo, umezuka ghafla saa moja asubuhi, na kusababisha watu kukimbia kutoka kwenye nyunba zao kwa kuhofia usalama wao.

Mitambo hiyo iliyopo jirani na mashine za Maji Mlandizi, pia eneo hilo kuna uwanja wa Mpira wa Miguu Maarufu uwanja wa DAWASA, ambapo kwa muda huo vijana walikuwa wanafanya mazoezi hivyo kulazimika kukimbia kuhofia usalama wao.

Baadhi ya vijana waliokuwa wanacheza mpira katika uwanja huo uliopo mita chache na kituo hicho, walisema kwamba walisikia muungurumo mkubwa kutoka ndani ya uzio kabla ya kuona moto mkubwa ukianza kuwaka.

"Tulifika hapa saa 12 asubuhi kama kawaida yetu kwa ajili ya kufanya mazoezi, ghafla tukasikia muungurumo mkubwa unaotokea kwenye uzio wa Tanesco kabla ya kuanza kuripuka moto mkubwa," alisema Juma Ramadhani.

Aliongeza kwamba ghafla hali ilibadilika kutokana na moto mkali ukiambatana na moshi mzito uliotanda angani huku watu wakitaharuki wengine wakitoka katika nyumba zao wakikimbia kwa kuhofia usalama wao.

"Leo nimeona kwanini Tanesco imepiga marufuku watu kujenga jirani na miundombinu yao, kwa moto huu kama kungekuwa na nyunba jirani sana na ulipo moto, mji wa Mlandizi ungeteketea, ni moto mkali sana," alisema.

Nae mkazi aliyejitambulisha kwa jina la Mariamu Hussein alisema kuwa yeye anaishi mbali na kituo hicho cha kupozea umeme lakini aliona moshi mkubwa angani ndipo alipokimbilia ili nae ajionee hali ilivyokuwa.

"Nikiwa nyumbani nimeshuhudia moshi mwingi mzito angani, nikaona nije kujionea kilichotokea nimekuta moto na moshi mzito, nimeamini miundombinu ya Tanesco inapaswa kuachwa mita nyingi na makazi ya watu," alisema Mariamu.

Mkazi mwingine dereva wa bodaboda ambaye hakupenda kutaja jina lake alisema kuwa, katika eneo la Mlandizi kuna baadhi ya transfoma zimekuwa zimesababisha miripuko ya mara kwa mara, lakini wahusika wanashindwa kuzibadilisha hivyo miripuko hujirudiarudia.

"Katika maeneo yetu kuna siku mbili tumekosa umeme lakini hakuna taarifa zilizotolewa na viongozi wa Tanesco, tunawaomba wafanye juhudi za kuzibadilisha baadhi ya Transfoma ambazo wanaona zimechoka, zinaweza kugharimu maisha ya watu," alisikika dereva huyo.

Juhudi za kuuzima moto huo zilifanyika ambapo Jeshi la zimamoto na uokoaji limefanikiwa kuuzima bila ya kuleta madhara makubwa.

Chanzo cha moto huo bado hakijafahamika

Hata hivyo juhudi za mwandishi wetu kumpata msemaji wa Tanesco kuzungumzia ni hasara kiasi gani imepatikana hazikufanikiwa.
 Image may contain: one or more people, people standing and outdoor 
Kikosi cha Jeshi la zimamoto na uokoaji wakiendelea kuudhibiti moto huo uliotokea mapema hii leo Machi 30, 2019. katika Kituo kidogo cha kupozea umeme cha Kanda ya Mlandizi Kibaha Mkoa wa Pwani.
Image may contain: 3 people, people standing and outdoor 

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo akishuhudia hali ilivyokuwa mara baada ya moto kuzimwa.

Friday, March 29, 2019

OFISI YA MAKAMU WA RAIS YAPONGEZWA NA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA VIWANDA, BIASHARA NA MAZINGIRA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba (katikati) akiongea na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge wa Viwanda, Biashara na Mazingira Mhe. Suleiman Murad Sadick katika moja ya ziara za kikazi za Kamati hiyo hivi karibuni.
....................................


Na Lulu Mussa,Dodoma

Serikali imesema itaendelea na juhudi za kushawishi wadau wa maendeleo na Jumuiya za Kimataifa ili kupata fedha za kusimamia uratibu wa shughuli za mazingira na kukabiliana na Athari za Mabadiliko ya Tabianchi nchini.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba ameyasema hayo hii leo Jijini Dodoma wakati wa kuwasilisha taarifa ya Utekelezaji  wa Mpango na Bajeti kwa mwaka wa fedha 2018/2019 na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2019/2020 kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira. Amesema Tanzania ni Mwanachama kwenye Mifuko na Mikataba mbalimbali duniani hivyo kuna fursa za kunufaika na fedha zitolewazo na mifuko hiyo akitoa mfano wa Green Climate Fund.


Aidha Waziri Makamba ameainisha mafanikio yaliyopatikana katika Ofisi yake kwa kipindi cha mwaka 2018/2019, kuwa ni pamoja na kufanya Mapitio ya Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 1997 na Mkakati wa Utekelezaji wake,  kuandaa rasimu ya Mpango wa Taifa wa Mazingira wa mwaka 2019 – 2023, na Maandalizi ya Mkakati wa Taifa wa Kudhibiti Viumbe Vamizi (Invasive Alien Species).


Pia, katika kipindi cha mwaka 2018/19, Ofisi ya Makamu wa Rais imekamilisha rasimu ya mwisho ya Ripoti ya Tatu ya Hali ya Mazingira Nchini baada ya kupata maoni ya wadau kabla ya kuwasilishwa Bungeni kwa mujibu wa matakwa ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004.


Waziri Makamba amesema katika kuhakikisha usimamizi na utekelezaji wa Sheria ya Mazingira unazingatiwa jumla ya miradi 1,254 ya maendeleo imefanyiwa Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) na Ukaguzi wa Mazingira na katika kuharakisha uwekezaji katika sekta ya viwanda nchini, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira linatoa Kibali cha Awali cha Mazingira (Provisional Environmental Clearance) ili kuwawezesha wawekezaji kuendelea na maandalizi ya awali ya mradi wakati mchakato wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira unaendelea.


Kwa upande mwingine Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Viwanda, Biashara na Mazingira Mhe. Suleiman Sadick amepongeza uongozi wa Ofisi ya Makamu wa Rais kwa jitihada za kuhifadhi mazingira nchini. ” Kamati inatambua jitihada za Ofisi yenu katika kuhifadhi mazingira, sisi tunawaunga mkono” alisisitiza Mhe. Sadick.

LINDI: WADAI VYOO VILIVYOEZEKWA VINAWAKOSESHA KUPUMUA.

Na HADIJA HASSAN, LINDI.

BAADHI  ya kaya zinazoishi katika Manispaa ya Lindi Mkoani humo zinatumia vyoo ambavyo havijaezekwa kwa madai kuwa wanashindwa kupumua vizuri wakati wa kujisaidia

Hayo yameelezwa na Afisa afya wa Manispaa hiyo jana alipokuwa anazungumza na Bagamoyo kwanza blog afisini kwake ilipotaka kufahamu juu ya namna ya kampeni ya “USICHUKULIE POA NYUMBA NI CHOO” inavyotekeleza na ilipofikia

Seiph alisema kuwa licha ya Kampeni hiyo kufanikiwa kwa kiasi kikubwa lakini bado baadhi ya Wananchi wa maeneo hayo hawana uelewa wa umuhimu wa kutumia Vyoo bora

  Ni jambo la kushangaza kuona   kuwa wakati tukiendelea na Kampeni hii tukitembea mtaa kwa  mtaa, kata kwa kata nyumba kwa nyumba tuliweza kubaini kuwa zipo baadhi ya kaya zikitumia vyoo ambavyo havijaezekwa kwa madai kwamba wanashindwa kupumua vizuri wakati wa kujisaidia

 “ wakati tunaanza kampeni hii ya usafi wa Mazingira kwa ujumla Manispaa yetu ya Lindi ilikuwa na asilimia 36 ya wakaazi kwa maana ya nyumba zenye vyoo Bora, lakini mpaka sasahivi tumeweza kufanikisha zoezi hili  kwa kuongeza idadi ya kaya ambaozo zina vyoo bora kwa zaidi ya  asilimia 55 sawa na kaya 8339 kati ya kaya 20006” alisema Seiph

Hata hivyo Seiph alisema  mpaka sasa Manispaa hiyo  kaya ambazo zina vyoo pasipo kuzingatia ubora ni kaya  asilimia 99.3 ambapo kati ya hizo kaya zenye vyoo bara ni asilimia 55.2 na  kaya asilimia 44.4 zinavyoo ambavyo havina ubora huku asilimia 0.2 zikiwa hazina vyoo kabisa 

Aidha Seiph aliongeza kuwa   pamoja na mafanikio hayo wapo baadhi ya wananchi ambao bado wamekuwa wakijisaidi vichakani kwa wale wanaoishi pembezoni mwa mji na wapo baadhi ya wananchi wanaojisaidia ufukweni kwa wale  ambao wanaishi pembezoni mwa bahari

Seiph pia alitumia fulsa hiyo kuwahasa wananchi wa Manispaa ya Lindi kuacha tabia ya kujisaidia vichakani sambamba na kwenye fukwe za bahari kwani kwa kufanya hivyo kunaweza kuhatarisha afya zao hii ni kutokana na hata wale waliojenga vyoo bora wanaweza kuwahatarini  kupata ugonjwa wa matumbo