Tuesday, March 26, 2019

POLISI PWANI YAPATA MILIONI 500 ZA KUJENGA NYUMBA.

NA MWAMVUA MWINYI, PWANI

JESHI la polisi mkoani Pwani, limepatiwa sh. milioni 500 ikiwa ni ahadi ya Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi ya Ulinzi na Usalama, Dkt. John Magufuli, ili kuhakikisha wanajenga makazi ya kuishi askari polisi.


Ahadi hiyo aliwahi kuitoa Dkt. Magufuli April 7 mwaka jana akiwa Arusha akizindua nyumba za askari katika mkoa huo.


Akizungumzia kuhusu fedha hizo, kamanda wa polisi mkoani Pwani, Kamishna Msaidizi wa Polisi, ACP -Wankyo Nyigesa, alisema mkoa huo ni miongoni mwa mikoa ambayo askari wake wana changamoto ya makazi hali inayosababisha kupanga uraiani ama kuishi Dar es salaam.


“Tatizo hilo hupelekea endapo kukitokea dharula askari huchukua masaa hata wakati mwingine matano kuitikia wito wa dharula “alisema Wankyo.


Wankyo alielezea, mpango huo utawezesha kuanza kwa kujenga nyumba 20 pamoja na kukabiliana na changamoto hiyo na askari kuweza kuitikia wito kwa haraka.


Alibainisha, kwasasa hatua iliyopo ni kusafisha kutoa visiki, vichuguu, vichaka na kusawazisha eneo la ujenzi ambapo wanamshukuru mdau Said Salum Bakhresa kwa kutoa katapila aina ya CAT -7R kwa ajili ya kusafisha.


Alieleza, katika kufanya hivyo ,mdau huyo ametumia milioni 75.

Kamanda huyo, aliwaomba wadau wengine kushirikiana na kuunga mkono juhudi za Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya ulinzi na usalama, kwa kutoa vifaa vingine ili kuendeleza zoezi hilo na kufanikisha ujenzi huo haraka iwezekanvyo.

Sunday, March 24, 2019

RAIS WA MSUMBIJI AISHUKURU TANZANIA KWA MISAADA YA DAWA NA CHAKULA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Rais wa Msumbiji, Mhe. Filipe Nyusi na Wananchi wake  wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Wananchi wa Tanzania kwa kuwa miongoni mwa nchi za mwanzo kabisa kutoa misaada ya Madawa, Magodoro na vyakula kwa watu wa Msumbiji walioathirika na kimbunga.

Kimbunga kilichopita katikati ya Jamhuri ya Msumbiji  kilicho anza tarehe 14 Machi 2019,  kimesababisha madhara makubwa katika mji wa Beira ambao ni wa tatu kwa ukubwa na wa pili kibiashara baada ya Maputo.

Upepo uliambatana na mvua uling’oa miti, mapaa ya nyumba za mabati na vigae na kuvunja madirisha ya vioo bila huruma katika mji huo.

Kufuatia janga hilo ambalo limezikumba pia nchi za Malawi na Zimbabwe, Rais Magufuli alitangaza kutoa msaada wa haraka ambapo ndege kubwa za JWTZ zilipeleka misaada hiyo kama inavyoonekana katika picha. 

Mjini wa Beira na wilaya  za jirani ziko kwenye uwanda wa tambarale. Mji huo pia una mito miwili mikubwa inayoingia katika bahari ya Hindi na hiyo ndiyo sababu ya mara kwa mara unakabiliwa na mafuriko.

Tanzania inaomba Mungu mvua zipungue kwa majirani hao ili waweze kuidhibiti hali hii ya mafuriko inayoendelea sasa baada ya Kimbunga kupita.

Mji wa Beira umeharibika vibaya ambapo asilimia 97 ya majengo, miundombinu, na mali za wananchi zimeathiriwa na kimbunga hicho.

Balozi wa Tanzania nchini Msumbiji, Mhe. Rajab Luhwavi ambaye alipokea shukrani hizo kwa niaba ya Serikali ameihakikishia Msumbiji kuwa, Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi hiyo  kwa hali na mali. 

Aidha, Mhe. Balozi ametoa pongezi kwa Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na wadau wengine kwa kufanikisha msaada huo.


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, 
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, 

Dodoma, Tarehe 24 Machi 2019

WAZIRI LUGOLA AWASILI ZANZIBAR, KUFANYA MKUTANO WA HADHARA UNGUJA

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (kushoto) akimsalimia Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Thobias Sedoyeka, wakati alipokuwa anawasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume, mjini Unguja, Zanzibar, kwa ajili ya ziara ya kikazi. 

Lugola anatarajia kufanya mkutano wa hadhara katika Viwanja vya Komba Wapya, mjini humo, leo, na atafungua Mkutano wa Kuzuia Biashara Haramu ya Kusafirisha Binadamu, utakayofanyika katika Hoteli ya Ngalawa, mjini humo, kesho.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (kushoto) akimsalimia Naibu Kamishna wa Uhamiaji, Ali Nassor, wakati alipokuwa anawasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume, mjini Unguja, Zanzibar, kwa ajili ya ziara ya kikazi. 

Lugola anatarajia kufanya mkutano wa hadhara katika Viwanja vya Komba Wapya, mjini humo, leo, na atafungua Mkutano wa Kuzuia Biashara Haramu ya Kusafirisha Binadamu, utakayofanyika katika Hoteli ya Ngalawa, mjini humo, kesho.  

Picha zote na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.  

VIJANA MOROGORO WATAKIWA KUCHANGAMKIA FURSA.

Vijana wa Morogoro wametakiwa kuchangamkiaa fursa za kilimo zilizopo katika Mkoa huo ili kujiwezesha kujiinua kiuchumi


Hayo yamebainishwa na Naibu waziri wa Kilimo Omary Mgumba wakati akizungumza katika uzinduzi wa Jukwaa la Vijana wa Mkoa wa Morogoro uliohudhuriwa na Vijana wa Mkoa huo pamoja viongozi mbalimbali 


Naibu waziri Mgumba amewataka Vijana hao kuchangamkia fursa hizo ikiwepo kupata mkopo kutoka  Bank ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) na mikopo ya Matractor kutoka Shirika la Maendelo la Taifa (NDC) Pale Kibaha ili kuweza kujiari katika sekta hiyo.


Alisema kuwa Mkoa wa Morogoro umepata bahati ya kuwa na viwanda vikubwa ambavyo vinahusika katika sekta ya Kilimo ikiwemo Kiwanda cha  Mtibwa Sugar, kilombero sugar, Mkulazi one na two, Mansoor industry cha kutengeza Sigara, ujenzi wa Kiwanda cha kukoboa Mpunga na Kiwanda cha kuchakata  mazao ya jamii ya Mikunde cha Mahashree


Naibu waziri wa Kilimo Omary Mgumba amewataka Vijana kutosubiri ajira tu za kuajiwa ofisini na badala yake waungane kwa pamoja kwa kuanzisha mashamba, kushiriki katika ujasiliamali wa mazao ya kilimo, kutoa huduma kwenye sekta ya kilimo na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo ili kutengeza ajira kwao vijana na kuajiri vijana wenzao na kuweza kujikomboa kiuchumi.


Akizungumza na mamia ya Vijana wa Mkoa wa Morogoro katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Waislam MUM mkoani Morogoro Naibu waziri wa Kilimo Omary Mgumba amewahakikishia Vijana kuwa serikali chini ya Mh Dkt. John Pombe Magufuli imedhamiria kuwakomboa wakulima kupitia mazao ya Kimkakati program aliyoizindua mwaka Jana na Mhe Raisi Dkt. John pombe Magufuli kubadilisha kilimo toka cha kujikimu na kuwa cha kisasa na cha kibiashara.


Mgumba ameongeza kuwa ni vyema Vijana hao wakashirikiana na wataaalam mbalimbali ili kuhakisha wanalima Kilimo chenye tija, na kujiunga kwenye Vikundi na kwenda kuomba ardhi serikali za vijiji na kuzipima kupata hati za umiliki ardhi zitakazo tumika kwa ajili ya uzalishaji mali na kuwa dhamana kwenye taasisi za fedha kupata mitaji ya kuwekeza kwenye kilimo.


Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe Steven Kebwe amesema kuwa Mkoa huo umebarikiwa kutokana asilimi kubwa ya mazao mbalimbali kustawi vizuri.


Dkt. Kebwe alisema kuwa Mkoa huo pia una ardhi kubwa ambayo inafaa kwa kilimo ikiwemo cha umwagiliaji kutokana na kuwepo na mito mingi ambayo itamuwezesha mkulima kulima kwa kipindi chote.


Hata hivyo ametumia fursa hiyo kuwapongeza Vijana wanaohitimu chuo kikuu cha Kilimo SUA kwa jitihada zao za kujiingiza katika Kilimo na kutosubiri ajira za serikali.


Jukwaa la Vijana Mkoa wa Morogoro limezinduliwa na Waziri wa nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Suleiman Jafo ambapo amewataka Vijana hao kuhakisha wanatumia vyuo vya Kilimo vilivyopo katika Mkoa huo kubalidisha hali ya Mkulima. 


Jukwaa hilo la Vijana Mkoa wa Morogoro limezinduliwa likiwa na kauli mbiu "Fursa Zetu Mkoa Wetu"