Wednesday, January 9, 2019

JESHI LA POLISI PWANI LATOA MSAADA KWA WATOTO YATIMA.

 Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani, katika kuukaribisha mwaka mpya, limetembelea kituo cha watoto wenye uhitaji maalum cha Fadhila kinacholea watoto yatima eneo la Misugusugu Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani na kutoa msaada wa vitu mbalimbali kwa watoto waliopo kwenye kituo hicho. 

Msaada huo umekabidhiwa na Dr. Mkuu wa Polisi Mkoa wa Pwani ASP Festo kwa niaba ya Af Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Kamishina Msaidizi Wankyo Nyigesa ni:- Dawa za chooni box 3, Sabuni za kuoshea vyombo box 2, Pampers box 3, Sabuni ya unga ndooo 2, Sukari kilo 50, Kalamu box 6, Sabuni ya miche box 5, Mafuta ya kupaka box 3, Mafuta ya kula lita 20, Madaftari katoni 1, Chumvi katoni 1, Juice katoni 1, Mchele kilo 100, Unga kilo100 na mbuzi wa 2. 

Mbali ya vitu hivyo, watoto hao waliweza kupatiwa flana za usalama barabarani na vipeperushi vya usalama barabarani na vya kupinga vitendo vya ukatili baada ya kuwa wamepatiwa elimu ya usalama barabarani na dawati la elimu kutoka ofisi ya mkuu wa usalama barabarani Mkoa wa Pwani wakishirikiana na mabalozi wa usalama barabarani (RSA) pamoja na ofisi ya dawati la Jinsi Mkoa wa Pwani juu ya kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia na kuripoti vituoni pale wanapofanyiwa vitendo hivyo.

 Aidha, Dr wa Polisi aliweza pia kuonana na watoto wenye matatizo mbalimbali ya kiafya kutoka katika kituo hicho na kuweza kuwapatia tiba, ambapo amefungua milango kwa uongozi wa kituo hicho kuwapeleka kwenye matibabu kwenye zahanati ya Polisi watoto wenye uhitaji maalumu wa kuonana zaidi na Daktari kwajili ya matibabu ya kina. 

Dr. Festo ameongeza ofisi yake itaweka utaratibu wa kupita na kuwajulia hali kila baada ya wiki mbili kituoni hapo ikiwa ni katika kujenga mahusiano bora baina ya Polisi na jamii yenye uhitaji maalum. 

Awali, akizungumza na viongozi wa kituo hicho cha Fadhila pamoja na watoto wanaolelewa hapo, Mkuu wa Usalama barabarani Mkoa wa Pwani Mosi Ndozero-ASP ameeleza kuwa, Jeshi la Polisi kikosi cha usalama barabarani Mkoa wa Pwani limelenga katika mwaka 2019 kutoa elimu ya usalama barabarani kwa makundi maalum na kufungua klabu za mabalozi wa usalama barabarani kwenye maeneo mbalimbali na kwa kuanzia wameamua kuendesha mafunzo ya usalama barabarani kwenye vituo vya watoto wenye uhitaji maalum kundi ambalo limekuwa likisahaulika kwa muda mrefu. 

Kadhalika, mbali ya utoaji wa elimu katika kituo hicho pamoja na utoaji wa msaada, Mkuu huyo wa usalama barabarani Mkoa wa Pwani alitumia muda wake kula pamoja na watoto wa kitu hicho ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa.

Kwa upande wake, mkurugenzi wa kituo hicho bi Suleiha amelishukuru Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani kwa msaada wanaoendelea kukipatia kituo chake mara kwa mara. "Tunaomba mtufikishie salam zetu kwa viongozi wote wa Jeshi la Polisi kwa msaada wenu wa mara kwa mara katika kituo chetu, mbali ya kuwa mna majukumu mengi ya kufanya lakini mmekuwa mkisaidia sana jamii kama wazazi kwenye malezi ya watoto wetu hawa".

Vitu mbalimbali vilivyotolewa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani kituo cha watoto wenye uhitaji maalum cha Fadhila kinacholea watoto yatima eneo la Misugusugu Wilaya ya Kibaha Mkoani humo.
  
 Dr. Mkuu wa Polisi Mkoa wa Pwani, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Festo akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kukabidhi msaada huo.
 
 Dr. Mkuu wa Polisi Mkoa wa Pwani, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Festo akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kukabidhi msaada huo.
 
 Picha zote Na Jeshi la Polisi Pwani.

Thursday, January 3, 2019

DC MUHEZA: NITASHIRIKIANA NA WANAMICHEZO KUHAKIKISHA TUNAPATA TIMU YA LIGI KUU

Mkuu wa wilaya ya Muheza Mhandisi Mwanasha
Tumbo akizungumza wakati akifunga Mashindano ya Kombe la Kabunda Cup
........................................


Mkuu wa wilaya ya Muheza Mkoani Tanga Mwanasha Tumbo amesema atashirikiana na wanamichezo ili kuhakikisha wanaweza mazingira mazuri yatakayowezesha kupatikana timu ambayo itaweza kushiriki ligi madaraja ya juu ikiwemo Ligi kuu.

Mwanasha aliyasema hayo wakati fainali michuano ya kombe la Kabunda Cup iliyokuwa ikichezwa kwenye viwanja vya Vikonge Mtindiro wilayani Muheza ambapo alisema ili kuweza kuhakikisha wanafanikisha jambo hilo wataendelea kuhamasisha vijana kujikita kwenye michezo.

Alisema licha ya kuhamasisha michezo kutokana na kwamba ni ajira ambayo inaweza kuwainua vijana kuichumi na kupata maendeleo lakini pia aliwahaidi kuwajengea kiwanja cha mpira chenye matofali ili waweze kuonyesha umahiri wao na hatimaye wilaya hiyo iweze kupata mafanikio kwenye soka.

“Leo nimekuja hapa kuhimitisha Ligi hii kwanza nimefurahishwa sana na viwango ambavyo mmekuwa mkivionyesha kwenye mchezo huu nimeongeza na Diwani wenu hapa na niwahaidi kwamba nitawajengea kiwanja chenye matofali ili hari ya kushiriki kwenye michezo muweza kuendelea nayo na tunaamini siku zijazo tutairudisha Muheza kwenye ramani ya soka “Alisema DC Mwanasha.

Alisema kwamba anafanya hivyo ili kuweza kuchochea maendeleo ya mchezo huo ambao vijana wakiweka bidii
na nia wanaweza kufika mbali ikiwemo kuitangaza wilaya hiyo lakini pia kupata manufaa kama walivyokuwa Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu ambao wanacheza soka la kulipwa nje ya nchi.

Awali akizungumza katika fainali hiyo Katibu Msaidizi wa Kamati ya Mashindano hayo Salehe Mwinjuma alisema lengo la mashindano hayo yalikuwa ni kuweza kuinua vipaji vya wachezaji wachanga kwenye Kata hiyo yaliyoanzishwa na mdau wa michezo Seif Kabunda kwa kushirikisha timu 20 zilizocheza kwa mtindo wa makundi.

Alisema kwamba msimu ujao ligi hiyo itakuwa na mabadiliko makubwa kutokana na mdhamini wa mashindano hayo kuamua kujipanga upya na kuja kinyengine lengo kubwa likiwa kuhakikisha michezo inapata mafanikio.

Katika fainali hiyo timu ya Ushirika FC waliweza kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 na kutawazwa kuwa mabingwa wapya wa Kombe la Kabunda Cup baada ya kuibamiza Kwarabuye FC mabao 2-1 katika mchezo wa fainali uliochezwa kwenye uwanja wa Vikonge Mtindiro na kujiny’akulia kombe na kitita cha sh.milioni moja . 

Katika mchezo huo ambao ulikuwa mkali na wenye ushindani mkubwa uliohudhuriwa na Mkuu wa wilaya ya Muheza
Mwanasha Tumbo ambaye ndie alikabidhi zawadi kwa washindi kwenye michuano hiyo.
 

Mkuu wa wilaya ya Muheza Mhandisi Mwanasha
Tumbo kushoto akimkabidhi Kitita cha Milioni moja Nahodha wa timu ya Ushirika Amiri Nko baada ya timu yao kuibuka na ushindi kwenye michuano ya Kombe la Kabunda Cup kushoto ni Afisa Michezo wa wilaya ya Muheza Anania Sama

MKUU wa wilaya ya Muheza Mhandisi Mwanasha Tumbo kushoto akimkabidhi Kombe la Ubingwa wa Mashindano ya Kabunda Cup Nahodha wa timu ya Ushirika Amiri Nko kushoto ni Afisa Michezo wa wilaya ya Muheza Anania Sama.

Katibu Msaidizi wa Kamati ya Mashindano hayo akisoma risala.

MKUU wa wilaya ya Muheza Mhandisi Mwanasha Tumbo katika akiwa kwenye picha ya pamoja na wachezaji

DC BAGAMOYO ATAKA KASI YA KUKUSANYA MAPATO IONGEZEKE.

Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Zainabu Kawawa, akizungumza na katika kikao cha Kamati ya ushauri ya wilaya (DCC).
................................. 

Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Zainabu Kawawa, amewataka wahasibu wa Halmashauri za Chalinze na Bagamoyo, kuacha kukaa ofisini muda mrefu na badala yake wafike kwenye vyanzo vya mapato ili kujionea hali halisi ya mapato halisi katika maeneo husika.

Agizo hilo amelitoa wakati akizungumza kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) kilichofanyika Ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Bagamoyo.

Amesema kazi ya kukusanya fedha inahitaji ufuatiliaji hivyo ni wajibu wa wakuu wa idara kuhakikisha mnafuatilia walipa ushuru kwenye vyanzo ili kujiridhisha endapo malipo wanayolipa yanalingana na kile walichobeba au kuzalisha.

Amesisitiza swala kuongeza mapato ndani Halmashauri zote mbili kwakuwa fedha hizo zinaweza kutatua baadhi ya changamoto zilizopo ikiwemo upungufu wa vyumba vya madarasa.

Awali Afisa Mipango wa Halmashauri ya Chalinze, Shabani Milao, akisoma taarifa ya utendaji kazi shughuli za Halmashauri hiyo, alisema mapato yameendelea kukua mwezi hadi mwezi na kufikia milioni 600, kwa mwezi wa Oktoba na Novemba 2018 kutoka milioni 400 mwezi Julai 2018.

Milao alisema ongezeko hilo limetokana na juhudi za Mkuu wa wilaya kufuatilia kwa karibu vyanzo vya mapato na namna watumishi wa Halmashauri wanavyokusanya hali iliyoleta msukumo na kuongezeka kwa mapato.

Aidha, Milao alitaja changamoto zinazowakabili katika kufikia lengo ikiwa ni pamoja uelewa mdogo wa wafanya biashara juu ya ulipaji kodi ya huduma za mji pamoja na uhaba wa vyombo vya usafiri.

Hata hivyo, Afisa mipango huyo amesema Halmashauri imejiwekea mikakati ya kuhakikisha inaendelea kuwahamasisha wananchi juu ya umuihmu wa kulipa kodi ya huduma na kuwachukulia hatua wale wote wenye madeni sugu.

Katika hali hiyo, Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, ameonyesha kutoridhishwa na mapato hayo na kutaka kasi iongezwe katika ukusanyaji ili kufikia milioni mia tisa kutoka mia sita za sasa.

Alisema tayari ameshafanya uchunguzi na kubaini fedha nyingi zinazopotelea kwenye mifuko ya watu na kwamba hatokubali mapato ya Halmashauri yapotee.

Aliwaagiza wakurugenzi wa Halmashauri zote mbili za Chalinze na Bagamoyo kuhakikisha wanasimamia ukusnyaji wa mapato na kwamba ikitokea mkuu wa idara husika anazembea katika kufuatilia na kukusnaya mapato atahakikisha anamuwajibisha.
 
 Wajumbe wa kikao cha Kamati ya Ushauri ya wilaya ya Bagamoyo wakiendelea na kikao. 


 Afisa Mipango Halmashauri ya Chalinze, Shabani Milao akisoma Taarifa ya utendaji kazi wa Halmashauri hiyo kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC).
 
Afisa Mipango Halmashauri ya Bagamoyo, Malboard M. Kapinga akisoma Taarifa ya utendaji kazi wa Halmashauri hiyo kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC).

JAFO APONGEZA UJENZI OFISI ZA HALMASHAURI KIBITI.

Muonekano wa Jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti linaloendelea kujengwa.
...................................

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Selemani Jafo amewapongeza viongozi wa Wilaya ya Kibiti kwa Ujenzi mzuri wa Ofisi za Halmashauri ya Wilaya Kibiti mradi unao tarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi bilioni tatu. 

Waziri Jafo alitoa pongezi hizo Leo hii alipokuwa katika ziara ya kikazi Wilayani Kibiti Mkoani Pwani.  

Ujenzi huo unaojengwa na mkandarasi SUMAJKT chini ya Mshauri Chuo Kikuu cha Ardhi umemridhisha sana Waziri Jafo kutokana na kuzingatiwa kwa viwango vya ubora katika ujenzi huo. 

Hata hivyo Jafo ameagiza kuongezwa kwa kasi ya ujenzi ili mradi huo ukamilike kabla ya mwezi Julai, 2019.

Katika ziara hiyo ya kikazi wilayani Kibiti Waziri Jafo alifanikiwa kutembelea mradi huo pamoja na mradi wa ujenzi wa kituo cha Afya Kivinja “A” ambao unagharimu shilingi milioni 400.

Katika kuhitimisha ziara yake wilayani humo waziri Jafo ameutaka uongozi wa wilaya hiyo kutumia fursa waliyonayo ya tofali nzuri zenye ubora zinazo zalishwa na SUMAJKT katika ujenzi wa hospitali ya wilaya ambayo wameshapokea shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo. 

Aidha, Mbunge wa Jimbo la Kibiti Mhe. Seif Ungando ameishukuru sana Serikali ya DKT. John Pombe Joseph Magufuli kwa msaada mkubwa wa miradi ya maendeleo inayo elekezwa wilayani Kibiti.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa Na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo(katikati) akitoa maelekezo wakati akikagua ujenzi wa Ofisi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo aKiwa na viongozi wa Wilaya ya Kibiti wakati wa ziara yake Wilayani humo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa Na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo(katikati) akitoa maelekezo wakati akikagua ujenzi wa Ofisi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti.

MAKOSA YA UBAKAJI NA KUPATIKANA NA SILAHA YALIONGEZEKA MKOANI PWANI 2018.

NA MWAMVUA MWINYI, PWANI 

MAKOSA ya ubakaji yametajwa kuongezeka kutoka 206 kwa mwaka 2017 na kufikia 271 mwaka 2018, mkoani Pwani .

Aidha kupatikana na silaha mwaka 2017 yalikuwa makosa tisa ambapo mwaka uliopita 2018, yameongezeka na kufikia 26 .

Akielezea tathmini ya hali ya uhalifu katika kipindi cha mwaka 2018 ikilinganisha na mwaka 2017, kamanda wa polisi mkoani Pwani Kamishna Msaidizi wa Polisi, (ACP)  Wankyo Nyigesa alisema tathmini ya kijumla inaonyesha wamepunguza matukio 151 makubwa .

Alisema, makosa ya ubakaji yameonekana kupanda kutokana na uelewa kwa jamii na mwamko wa kuripoti matukio hayo polisi. 

Wankyo alieleza, matukio ya mauaji yalikuwa 61 ikilinganisha na matukio 70 yaliyoripotiwa mwaka 2017 .

“Makosa ya kufanya biashara ya kusafirisha binadamu mwaka 2018, yalikuwa 03 ikilinganishwa na makosa 05 yaliyorekodiwa mwaka 2017″alifafanua Wankyo. 
Kamanda huyo alisema kuwa, makosa ya unyang ‘anyi wa kutumia silaha mwaka 2017 yalikuwa 21 na mwaka 2018 makosa hayo ni 13.

Unyang’anyi wa kutumia nguvu mwaka 2017 yaliriporiwa makosa 126 ,wakati mwaka 2018 makosa ya namna hiyo yameripotiwa makosa 52 .

Alisema, jeshi hilo pia limefanikiwa kudhibiti uingizaji bidhaa kupitia bandari bubu wilayani Bagamoyo kwa kukamata makosa 27,watuhumiwa 31 pamoja na madumu 5,435 ya mafuta ya kula aina mbalimbali .
“Sukari kutoka nchi za nje mifuko 78, mabello 20 ya nguo za mitumba aina mbalimbali ikiwemo manne ya khanga na vyombo vya moto vilikamatwa ikiwa ni pamoja na pikipiki sita na magari matatu. “alieleza Wankyo.