Thursday, December 6, 2018

WATENDAJI KATIKA SEKTA YA UMMA WATAKIWA KUJIEPUSHA NA MGONGANO WA MASLAHI ILI KUJENGA UCHUMI IMARA WA TAIFA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George Mkuchika (Mb), akizungumza na washiriki wa mjadala kwenye maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu Kitaifa, kabla ya kumkaribisha Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Mhe. Mohamed Chande Othman kufungua rasmi mjadala huo jijini Dodoma.
....................................

Viongozi, watumishi na wataalam mbalimbali nchini, wametakiwa kujiepusha na mgongano wa maslahi kwa kutotumia nyadhifa zao au ofisi zao kujinufaisha wao wenyewe, kuwanufaisha ndugu zao au jamaa zao na watu wengine ili waweze kutekeleza wajibu wao ipasavyo katika ujenzi wa uchumi imara wa taifa.

Wito huo umetolewa na Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Mhe. Mohamed Chande Othman wakati akifungua mjadala kwenye maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu Kitaifa, jijini Dodoma.

Mhe. Othman amesema, mgongano ya maslahi ni lazima udhibitiwe kwa nguvu zote kwani unailetea sifa mbaya serikali, taasisi, idara na sekta binafsi ambazo mgongano wa maslahi unajitokeza, na kuongeza kuwa unamletea pia sifa mbaya ya kiutendaji kiongozi au mtumishi kwenye fani au taaluma aliyobobea.

Mhe. Othman ameainisha njia za kuweza kuepukana na mgongano wa maslahi, njia hizo ni kujiuzulu au kujitoa endapo kiongozi anaona kuna maslahi binafsi kwenye jambo atakalolitolea maamuzi kwa ajili ya kulinda maslahi ya umma.

Mhe. Othman amesisitiza kuwa, ni jukumu la mtendaji mwenyewe kutamka mapema, kukiri kwa hiari na kwa uwazi kwamba ana mgongano wa maslahi kwenye suala atakaloenda kulitolea maamuzi badala ya kungoja kuambiwa ajiuzulu na kushutumiwa kuwa na mgongano wa maslahi kwenye suala aliloshiriki kutoa maamuzi.

Naye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George Mkuchika amesema, moja kati ya mambo ambayo ofisi yake inapambana nayo ni kuhakikisha inaondoa uwezekano wa kuwepo kwa mgongano wa maslahi katika taasisi za umma.

Mhe. Mkuchika amefafanua kuwa, kiongozi au mtumishi yeyote katika sekta ya umma hatakiwi kufanya biashara na taasisi yake kwasababu kuna uwezekano mkubwa wa kupendelea kampuni yake kuipatia zabuni na kuiongezea malipo ili aweze kujinufaisha na hatimaye kuitia hasara serikali.

Aidha, Mhe. Mkuchika ametoa wito kwa washiriki wa mjadala kuhakikisha wanatoa maoni na mapendekezo ambayo yataondoa changamoto ya mgongano wa maslahi katika sekta ya umma.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) amesema, viongozi na watumishi ambao wanasimamia maadili wanapaswa kuyaisha yale wanayoyasema, na ni muhimu pia ni wajibu wao kuonyesha njia katika uzingatiaji wa maadili ili wanapohubiri maadili mema wawe na ushawishi kwa umma.

Mhe. Dkt. Mwanjelwa ameongeza kuwa, vitendo vya mmomonyoko wa maadili vinatakiwa kukemewa bila kusita wala kuonewa haya kuanzia kwenye ngazi ya familia ili kujenga taifa lenye uadilifu.

Mada zilizojadiliwa katika mjadala huo ni pamoja na, Mgongano wa masilahi katika utumishi wa umma, Ulinzi wa haki za binadamu na mgongano wa maslahi na matumizi mabaya ya madaraka yanayopelekea mgongano wa maslahi na uwepo wa rushwa nchini.

WAZIRI UMMY AAGIZA AFISA AFYA WA WILAYA ACHUNGUZWE KWA TUHUMA YA RUSHWA

 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu akiongea na Wananchi wakati akifanya uhamasishaji kwa Wananchi kujiunga na mfuko wa Bima ya Afya katika mji wa Kitangali Wilaya Newala Mkoa wa Mtwara.
............................................

Na WAMJW-NEWALA, MTWARA

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amemwagiza Mkuu wa Wilaya ya Newala Mhe. Aziza Mangosongo, Kumchunguza Afisa Afya wa Wilaya hiyo maarufu kwa jina la Mama Flora kwa tuhuma ya Rushwa aliyochukua kutoka kwa Bw.Shaib Mussa kama adhabu ya kutupa taka hovyo.

Hayo yamefuatia baada ya Mwananchi aliyejitambulisha kwa jina na Shaibu Musa kutoa malalamiko yake mbele ya Mhe.Waziri ya kilipishwa shilingi elfu 50,000 na Bibi Afya huyo mwaka Jana.

Waziri Ummy alisema kuwa Watumishi wa Serikali hasa wa Sekta ya Afya ni lazima wajiepushe na vitendo vya Rushwa na kuacha tamaa zinazopelekea kuminywa kwa haki kwa baadhi Wananchi wanaotaka kupata huduma.

“Namtafuta mmoja ili nimtolee mfano kwa Tanzania nzima, bahati nzuri Mimi ni Mwanasheria, Kosa LA jinai halina muda, hata kama ni 2017, tunataka huyu mtu afuatiliwe, achunguzwe kama kweli shilingi 50,000 iliingizwa kwenye Halmashauri au haijaingia, tunataka Mazingira masafi lakini ile hela iende Serikalini” alisema Waziri Ummy.

Nae Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bw. Bernard Konga amesema kuwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umeanza rasmi kampeni ya uandikishaji ya kijiji kwa kijiji katika Mikoa ya Mtwara na Lindi ili kuwawezesha wananchi hao kuwa kwenye utaratibu mzuri wa kupata huduma za matibabu.

Bw. Bernard Konga aliendelea kusema kuwa, Wananchi wamekuwa wakiingia katika umasikini mkubwa kwa kulazimika kuuza mali za familia kwa lengo la kupata fedha za kugharamia huduma za matibabu.

“Nikuhakikishie Mheshimiwa Waziri na wananchi wote walioko hapa, timu yangu inaanza rasmi kampeni ya kijiji kwa kijini kuanzia wiki ijayo kwa lengo la kumfikia kila mkulima aliyeko katika Mkoa wa Mtwara na Lindi ili wananchi hawa wawe kwenye mfumo bora wa kupata huduma za matibabu wakati wowote, alisema Bw. Konga.

Konga aliendelea kusema kuwa zaidi ya asilimia 80 ya wananchi wote wako kwenye sekta ya kilimo hususan maeneo ya vijijini na kwa kutambua umuhimu wa kulitunza kiafya kundi hili, Mfuko ulianzisha mpango maalum unaojulikana kwa jina la Ushirika Afya unaowawezesha kujiunga na huduma za NHIF kwa gharama nafuu.

Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto yupo Mkoani Mtwara kwa ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma za Afya Pamoja na uhamasishaji kwa Wananchi kujiunga na mfuko wa Bima ya Afya ya Taifa (NHIF) na Leo hii yupo Wilayani ya Newala.

DC BAGAMOYO AWAONYA WAPITISHA MAGENDO.

  Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Zainbau Kawawa, akizungumza na wafanyabiashara wanaoagiza mafuta ya kupikia kupitia Bandari ya Bagamoyo katika ukumbi wa mikutano ofisi ya Mkuu wa wilaya, kulia ni
Mkuu wa Takukuru wilaya ya Bagamoyo, Raymond Katima na kushoto ni Mkuu wa Polisi wilaya ya Bagamoyo, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi-SSP Rajabu Shemndolwa
......................................
Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Zainbau Kawawa amewaonya wanaopitisha magendo katika wilaya hiyo kuwa hawako salama.

Zainabu alitoa kauli hiyo alipokutana na wafanyabiashara ya mafuta ya kupikia wanaopitishia bandari ya Bagamoyo.

Katika kikao hicho ambacho kimewashirikisha waagizaji wa mafuta ya kupikia kutoka Zanzibar kupitia Bagamoyo, maafisa wa forodha, Afya, Biashara, TFDA na TRA lengo likiwa kuangalia changamoto zinazowakabili wafanyabiashara waagizaji mafuta ya kupikia, na maafisa wa serikali wanaohusika kukusanya tozo mbalimbali za serikali.

Katika kikao hicho wafanyabishara wa mafuta wamelalamikia kukamatwa na polisi hali inayopelekea kukwamisha biashara zao kwa siku kadhaa licha ya kuwa vibali vyao vimekamilika.

"tunapata tabu na polisi wanatukamata, wanakuja nyumbani na bunduki mpaka sasa mtoto wangu anaogopa kwenda shule kwa hofu ya polisi kwanini hawatukamati wakati tunatoa mizigo wanatufuata nyumbani?"  alisikika akilalamika mmoja wa wafanyabiashara hao aliyejitambulisha kwa jina Shabani Hamsini (chavurugu)

Kufuatia kauli hiyo, Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo aliwataka wafanyabiashara hao kutoa ushirikiano katika kuwafichua wale wote wanaotumia Bandari bubu kupitisha mizigo yao.

Alisema serikali itaendelea kuwasaka wale wote wanaokwepa ushuru na kodi za serikali na kuhakikisha inadhibiti Bandari bubu.

Aliongeza kuwa, ili kuepuka usumbufu wanaotumia Bandari na kulipa ushuru na kodi wanapaswa kuwataja wenzao wanakwepa kulipa kodi za serikali ili washughulikiwe vinginvyo serikali itawakamata wale wote wanawatilia mashaka ili kukagua mizigo yao kama imepitishwa kihalali.

" Labda niwaambie ndugu zangu, hii kadhia ya kukamatwa kamatwa haiwezi kuisha hapa Bagamoyo kama hamtatupa ushirikiano, ushirikiano tunaotaka wale wote wanaotumia Bandari bubu waache, mnafanana nao wengine mlitokea huko na bidhaa ni hizo hizo sasa ili tuikomeshe tabia hii watajeni vinginevyo tutkamata anaehusika na asiyehusika" Alisema Mkuu wa wilaya Bi Zainabu.

Kwa upande wao wafanyabiashara hao wamekiri kuwa awali walikuwa wanatumia Bandari bubu kupitishia bidhaa zao na sasa wameacha wanatumia njia rasmi ya Bandari na kulipa kila kinachohitajika.

Aidha, wametoa rai kwa mamlaka zinazohusika kuweka mazingira rafiki kwa wafanyabiashara wadogo ili nao waweze kutumia Bandari rasmi kupitishia mizigo yao kihalili.

Walisema ni wazi kuwa mazingira yakiwa mazuri kwa wafanyabiashara hakuna atakaepitia porini kwani porini kuna hatari nyingi ikiwemo kukamatwa na kupoteza mzigo wako.

Mkuu wa wilaya aliwataka wataalamu kutoka TFDA, TPA, TRA na FORODHA, kutoa elimu kwa wafanyabiashara hao ili kila mmoja awezekutumia njia sahihi kwa wakati sahii kuepuka usumbufu.

Alisema kila mmoja ana wajibu wa kukomesha Bandari bubu kwani Bandari bubu sio tu zinapitisha mafuta lakini pia vinaingizwa vitu vya aina mbalimbali ambavyo vingine ni hatari kwa usalama na afya.

Akizungumza katika kikao hicho Mkuu wa Polisi wilaya ya Bagamoyo, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi-SSP Rajabu Shemndolwa, alisema polisi inapotekeleza majukumu yake haina lengo la kumkomoa raia bali inatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria na kanuni.

Aliwataka raia wote wilayani humo kutii sheria bila ya shuruti ili kila mmoja afanye shughuli zake kwa amani na utulivu.

Akizungumzia kukamatwa kwa magari yanayobeba bidhaa zinazotoka Bandalini, SSP Shemndolwa alisema hiyo ni katika kuhakiki mzigo uliobebwa umefuata taratibu za kisheria au la.

Aliongeza kwa kusema kuwa Polisi ndio wenye mamlaka ya kisheria kusimamisha gari na kisha ukaguzi wa nyaraka mbalimbali za mzigo utafanywa na idara husika ili kujiridhisha kilichobebwa kama kinafanana na nyaraka zilizooneshwa.

Alisema tayari ameshatoa maelekezo kwa askari polisi juu ya utaratibu wa kukamata magari yaliyobeba mizigo na kusema kuwa polisi watakagua kinachowahusu na maafisa wa idara nyingine za serikali watakagua vinavyowahusu ili kila mmoja atekeleze wajibu wake kwa ufasaha.
 Mkuu wa Polisi wilaya ya Bagamoyo, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi-SSP Rajabu Shemndolwa, akizungumza katika kikao hicho.

Wafanyabishara waagizaji wa mafuta ya kupikia kutoka Zanzibar kupitia Bagamoyo,wakiwa katika kikao kilichoitishwa na Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili.
 
Baadhi ya Wafanyabishara waagizaji wa mafuta ya kupikia kutoka Zanzibar kupitia Bagamoyo, wakiwa nje ya Ukumbi baada ya ndani kujaa katika kikao kilichoitishwa na Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili.


 Wa kwanza kulia ni Afisa Mwandamizi wa Kituo cha Forodha Bandari ya Bagamoyo Noeli Makere, na wapili ni Meneja wa Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini (TFDA) Kanda ya Mashariki, Emmanuel Alphonce
 Kutoka kushoto ni Afisa Mfawidhi wa Kituo cha Forodha Bandari ya Bagamoyo, Raymond Mwanisawa, wa pili ni Meneja wa Mamlaka ya mapato nchini (TRA) wilaya ya Bagamoyo, Farence Mniko wa tatu ni Mkuu wa Polisi wilaya ya Bagamoyo, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi-SSP Rajabu Shemndolwa, wa nne ni Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Zainbau Kawawa, na watani ni Mkuu wa Takukuru wilaya ya Bagamoyo, Raymond Katima.

MAGAZETI YA LEO DESEMBA 06, 2018.

HATUNA CHA KUMLIPA JPM -WAKULIMA WA KOROSHO KIBAHA

WAKULIMA wa zao la korosho wilayani Kibaha mkoani Pwani .
........................................................
NA MWAMVUA MWINYI, KIBAHA 

WAKULIMA wa zao la korosho wilayani Kibaha mkoani Pwani ,wamesema maamuzi ya serikali chini ya Rais Dk John Magufuli kununua korosho ni mkombozi kwao. 

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mwenyekiti wa umoja wa vyama vya ushirika wa zao la korosho wilaya ya Kibaha (UVUKI) Adhu Mkomambo alisema ,hatua hiyo itasaidia kuondoa ubabaishaji wa malipo uliokuwepo kipindi cha nyuma. 

Alifafanua,  maamuzi hayo ni faida kubwa kwa wakulima kwani bei elekezi ni nzuri ya shilingi 3,300 kwa daraja la kwanza ambapo wafanyabiashara walisema watanunua kwa shilingi 2,700 hali ambayo ilikuwa ni mbaya.

“Manufaa ya maamuzi haya ni kunufaisha wakulima ambao wamekuwa wakitaabika kwa muda mrefu ambapo wafanyabiashara walikuwa wanaangalia maslahi yao binafsi,” 
“Hatuna cha kumlipa mh Rais, ila tunamuombea azidi kutetea wanyonge “alisema Mkomambo.

Nae mwenyekiti wa chama cha ushirika Kongowe Amcos Deo Joseph alisema, maamuzi hayo yataondoa usumbufu mkubwa waliokuwa wanapata wakulima katika malipo Mara wanapopeleka korosho kwenye minada.

Mzee Mwinshehe ambaye ni mwenyekiti wa chama cha ushirika Misugusugu Amcos alieleza, wakulima tegemeo lao ni korosho hivyo kuwalipa fedha ndogo ni kuwakwamisha kimaisha kwani wanategemea zao hilo kusomesha na shughuli nyingine za maendeleo na bei elekezi itapunguza gharama za pembejeo.

DC MSHAMA AKABIDHI SHAMBA PORI MIKONONI MWA WANANCHI WAKATI AKISUBIRI TARATIBU NYINGINE KUCHUKULIWA

 MKUU wa wilaya ya Kibaha, Assumpter Mshama.
.........................................
NA MWAMVUA MWINYI, KIBAHA 

MKUU wa wilaya ya Kibaha, Assumpter Mshama amesema ataandika ombi la kufuta hati ya shamba la mmiliki Siemens, lililopo kata ya Pangani, kutokana na kuwa pori na kugeuzwa jalala la kutupwa miili ya marehemu pamoja na kutumika kwa uhalifu. 

Hatua hiyo inakwenda pamoja na kuwakabidhi wananchi kulitumia kwa masharti ya kulima mazao ya muda mfupi wakati serikali ikiendelea na taratibu za kupima viwanja na kuuza kwa gharama nafuu. 

Akitoa maamuzi hayo wakati alipokuwa akizungumza na wananchi wa kata hiyo, Assumpter alisema ifikie mwisho kujaza viwanja na mashamba pori wilayani hapo. 

Assumpter alitoa rai kwa wamiliki wenye mashamba na viwanja pori kuanza kuyaendeleza na kama watakaidi wananchi wakiyavamia ataruhusu wagawiane maeneo. 

“Hii ni salamu tuu, mwenzio akinyolewa wewe anza kutia maji, wananchi wamechoshwa kulinda maeneo ya watu, kama mmeyashindwa yaacheni”alifafanua Assumpter. 

Awali diwani wa kata ya Pangani, Agustino Mdachi aliomba serikali ,kuangalia namna ya kufuta umiliki wa mashamba ambayo hayaendelezwi na kusababisha kutumika vificho vya wahalifu .

Alisema, kwa kipindi cha miezi sita miili zaidi ya kumi zimeokotwa kwenye mtaa huo ambapo kati yao wengine walinusurika kifo na kuokolewa na wengine wakiwa wamefariki dunia. 

Nae mwenyekiti wa mtaa wa Pangani Jitihada Ndiali alisema maeneo hayo yamegeuzwa dampo au sehemu ya kutupia maiti pia madereva bodaboda kuporwa pikipiki zao kisha kutupwa .

Kwa upande wa wananchi akiwemo Lillian Godfrey alimpongeza mkuu wa wilaya kwa maamuzi yake. 

Alisema, wamekubali kulima mazao ya muda kama mihogo, mbaazi, maharage na mbogamboga hadi hapo serikali itakapofanya maamuzi ya moja kwa moja. 

Wednesday, December 5, 2018

RIDHIWANI AWALAZA WABUNGE WA UGANDA NA VIATU.

Na Shushu Joel,
MBUNGE wa Tanzania  anayetokea  jimbo la Chalinze mkoani Pwani Ridhiwani Kikwete amewalaza wabunge wa uganda na viatu mara baada ya kuwachachafya mabeki wa timu hiyo katika mchezo wao wa kwanza katika mashindano ya wabunge yanayoendelea huko nchini Burundi.

Katika mechi hiyo ilichezwa juzi katika uwanja wa amavumbi nchini humo timu ya Bunge la Tanzania ilipoteza mchezo huo kwa kufungwa goli 2 kwa 1.

Akizungumza kwa njia ya simu kutokea nchini Burundi Ridhiwani Kikwete alisema kuwa mchezo huo ulikuwa mziri na wa kuvutia ingawa walipoteza mechi hiyo kwa wabunge walio wengi hawana mazoezi ya kutosha hivyo pumzi uwaishia na kupelekea kuwapatia nafasi wenzetu ambao wanaonekana kuwa na mazoezi ya muda mrefu katika kujiandaa na michezo mbalimbali.

“Tumefungwa na wenzetu wa Uganda lakini kazi wameiona kwani tulifanikiwa kuwashambulia mara kwa mara ingawa bahati haikuwa ya kwetu ila mabeki wamelazwa na viatu kutokana na jinsi walivyochoka kwa mashambulizi ya Bunge la Tanzania”Alisema Kikwete.

Kwa upande wake mbunge wa Sengerema Ezekiel Ngereja alisema kuwa kilichowafungisha ni kutokuwa na mazoezi ya muda mrefu ila kama tungekuwa na pumzi kama alizozionyesha mbunghe mwenzetu wa jimbo la chalinze amabye muda mwingi alionekamna kuwa ni mwiba katika lango la wapinzani wetu.

Aliongeza kuwa kupoteza mechi moja si hoja bali meci zijazo lazima tutashinda kutokana na hali yaliyonayo kambi wabunge wa Tanzania.

“Tunawaomba watanzania wote huko nyumbani waendelee kutuombea ili mechi zijazo tuweze kushinda na kuchukua kombe na kurudi na heshima nyumbani ili wachezaji wetu waweze kujifunza katika mechi zao”Alisema Ngereja.

Akizungumza kwa njia ya simu kaptain wa timu ya bunge la Uganda aliyejitambulisha kwa jina moja la Pentagoni ambaye anacheza nafasi ya kiunga mshambuliaji alisema kuwa ingawa wameshinda kwa gori 2 kwa 1 dhidi ya wapinzao wao wa Bunge la Tanzania ila kazi pevu wameiona kutoka kwa mbunge wa chalinze ambaye alikuwa anawapa shida kubwa kwa jinsi alivyokuwa akicheza katika mechi hiyo.

Aliongeza kuwa timu ya Bunge ya Tanzania iko vizuri sema tu wabunge walio wengi hawafanyi mazoezi hivyo wanakosa pumzi na kupelekea kufungwa lakini mbunge Ridhiwani Kikwete anaonekana anafanya mazoezi sana ndio maana anaonekana kuwa ni msumbufu sana katika kumkaba na kumpora mpira pindi anapokuwa nao.

DUNDA KINARA WA ELIMU BAGAMOYO

 Diwani wa Kata ya Dunda Dickson Makamba akizungumza katika hfla hiyo.
..................................
Na Omary  Mngindo, Bagamoyo

JUMUIA ya Wazazi wilaya ya Bagamoyo  Mkoa wa Pwani inatarajiwa kuandaa harambee kubwa katika Kata ya Dunda inayolenga kupatikana kwa fedha zilizotumika kumalizia Bweni sekondari ya Kata. 

Mjumbe Kamati ya Utekelezaji jumuia hiyo Wilaya Yahya Msonde, aliyemwakilisha Mwenyekiti wa Jumuia hiyo wilaya Aboubakary Mlawa, katika hafla ya kupongezwa walimu katani humo kwa kufanikisha Kata hiyo kuwa ya kwanza kiwilaya. 

"Nilipopewa taarifa na Mwenyekiti wangu Mlawa kuja kumwakilisha kwenye hafla hii,  nilijiuliza mara milimbiko nini cha kuzungumza,  lakini kwa kuwa nami ni mdau wa elimu siwezi kukosa la kuzungumza,  lakini la kwanza niwasilishe hili la Harambee inayohimizwa ifanyike wiki ya kwanza mwezi Januari, " alisema Msonde. 

Akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, diwani wa Kata ya Dunda Dickson Makamba alianza kwa kuwapongeza walimu kwa kazi kubwa wanavyoendelea kuifanya katani humo,  akisemaa kwamba huu ni mwaka wa tatu mfululizo kushika nafasi hiyo.

"Niwashukuru walimu kwa kujitoa kikamilifu katika kuhakikisha Kata ya Dunda inaendelea kuwa kinara katika imu, pia wazazi, walezi na wadai mbalimbali wanaoendelea kusaidia katika nyanja tofauti za kuhakikisha elimu inaendelea kuboreshwa katani hapa," alisema Makamba. 

Akizungumzia changamoto ya Bweni kwenye shule ya Kata,  Makamba alisema kuwa kuna juhudi nyingi zinazoendelea kufanyika akiwemo Mwenyekiti wa Jumuia hiyo aliyechangia mabati 100, lengo kuhakikisha wanafunzi wanakaa shuleni. 

"Mbali ya Jumuia pia kuna wadai wengi ambao wamechagia ujenzi wa Bweni akiwemo Mbunge wa Jimbo Dkt.  Shukuru Kuwambwa aliyechanga mifuko 100 ya saruji pamoja na wadau wengi waliojitolea na wengine bado wanaendelea kujitokeza kusaidia elimu katani Dunda, " alisema Makamba.

Mwalimu Mkuu shule ya Mwambao Alpu Mwegeho akitoa shukrani kwa niaba ya walimu wenzake, alitoa kilio cha kucheleweshwa mafao ya walimu hali inayopunguza hamasa ya walimu wilayani humo. 

Mwakilishi wa wazazi Ummy Matata amepongeza juhudi za walimu, huku akisema kwamba kwa miaka mingi suala la ufaulu katani humo halikuwepo, huku akimpongeza Diwani Makamba kwa kushirikisha watu mbalimbali. 

Taarifa ya Walimu katani humo iliyosomwa na Saad Momba mwalimu shule ya Msingi Mwambao inazungumzia changamoto ya ukosefu wa kompyuta hali inayochangia kupunguza uwezo wa wanafunzi katika elimu. 
 
Mjumbe Kamati ya Utekelezaji jumuia ya wazazi Wilaya, Yahya Msonde, ambae alikuwa mgeni rasmi kumuwakilisha Mwenyekiti wa jumuiya hiyo.

 
Mjumbe Kamati ya Utekelezaji jumuia ya wazazi Wilaya, Yahya Msonde,akikabidhi zawadi kwa mwalimu Amina Ally wa shule ya msingi MWASAMA.

 
Mjumbe Kamati ya Utekelezaji jumuia ya wazazi Wilaya, Yahya Msonde,akikabidhi fedha taslimu shilingi laki moja kwa mwalimu 
 
Mjumbe Kamati ya Utekelezaji jumuia ya wazazi Wilaya, Yahya Msonde, akikabidhi zawadi kwa Mwenyekiti CCM kata ya Dunda, Mwinyi Hashim Akida.


SERIKALI IMETOA KIPAUMBELE MATUMIZI YA TEHAMA NCHINI-MAJALIWA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi Tuzo Mshindi wa Kwanza wa Mashindano ya TEHAMA ya HUAWEI, Emmanuel  Chaula wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam katika sherehe za kukabidhi Tuzo hizo kwenye hoteli ya Hayyat Regency jijini Dar es salaam, Desemba 5, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipokabidhi Tuzo za Mashindano ya TEHAMA ya HUAWEI kwenye hoteli ya Hayyat Regency jijini Dar es salaam, Desemba 5, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
............................................
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imetoa kipaumbele kwenye matumizi ya TEHAMA ili kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utendaji kazi wa shughuli za Serikali za kila siku.

Hivyo, amewataka wananchi kutumia vizuri teknolojia hiyo ya habari na mawasiliano kwenye shughuli za uzalishaji mali na utoaji huduma katika sekta mbalimbali kwa lengo la  kukuza uchumi na kuwapunguzia wananchi umaskini pamoja na kuongeza ajira.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatano, Desemba 5, 2018) katika sherehe za utoaji tuzo za mashindano ya TEHAMA ya HUAWEI yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, ambapo ametumia fursa hiyo kuwaonya watu wote wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii nchini.

“Nawaonya watu wote wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii waache. Ni vema wakatumia mitandao hiyo kwa kuhamasishana mambo mema zikiwemo shughuli mbalimbali za maendeleo. Na kwa wataokiuka sheria ipo na inaendelea kufanya kazi.”

Amsema Serikali inaamini kuwa matumizi ya TEHAMA yataongeza ufanisi katika kuwahudumia ipasavyo wananchi, mfano katika sekta ya elimu mwalimu mmoja anaweza kufundisha wanafunzi wengi kutoka katika shule tofauti kwa wakati mmoja. 

Waziri Mkuu ameongeza kuwa “Matumizi ya TEHAMA kwa kiasi kikubwa yatapunguza gharamaza za uendeshaji kwani yanaweza kufanikisha mawasiliano binafsi, warsha na maelekezo mbalimbali kuwafikia walengwa bila ya kusafiri nje ya vituo vyao vya kazi.”

Ametoa mfano Juni 2017 Rais Dkt. Magufuli alizindua mfumo wa ukusanyaji Mapato ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na Ushuru wa Bidhaa (Excise Duty) kwa njia ya kielektroniki na kudhihirisha kuwa, sekta ya teknolojia ya habari na mawasiliano ni muhimili muhimu wa maendeleo kwenye sekta zote, ikiwemo viwanda, utalii, ujenzi, elimu, afya, kilimo, uvuvi na ufugaji.

“Kwa kuzingatia hayo, mwezi Juni 2018 wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, Serikali ilizindua mifumo tisa ya TEHAMA, ambayo inalenga kuimarisha utendaji wa Serikali hususan katika kuwahudumia wananchi kwenye sekta mbalimbali ikiwemo afya, ukusanyaji mapato na utoaji wa taarifa.”

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika kutengeneza mifumo ya TEHAMA ili kutekeleza kwa vitendo azmaya kuwapatia wananchi maendeleo hususani waishio maeneo ya vijijini huduma bora na kwa wakati.

Amesema kwa sasa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) inauwezo wa kuona na kubaini makusanyo yanayoendelea kukusanywa katika halmashauri mbalimbali nchini na kiasi kinachoingizwa benki kwa kupitia TEHAMA.

Pia, Waziri Mkuu amsema Serikali imeendelea kuunganisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwenye taasisi zake ili kufanikisha azma ya kutumia Serikali mtandao, zoezi ambalo linakwenda sambamba na kuunganisha baadhi ya shule za msingi, shule za Sekondari, Ofisi za Wakuu wa Wilaya, Polisi, Hospitali za Wilaya, Vyuo Vikuu na Vituo vya Posta.

Wakati huo huo,Waziri Mkuu ameipongeza kampuni ya HUAWEI kwa uzinduzi wa program yao ya Seed of the Futureambayo inalengo la kuwajengea uwezo wa TEHAMA wanafunzi mbalimbali nchini katika hatua za awali kabisa. 

Amesema iwapo TEHAMA itatumika vizuri itatoa fursa kwa watu wote kupata elimu, kuleta usawa katika elimu, kujenga mazingira na mbinu bora za ufundishaji na kujifunza, kuongeza weledi wa walimu, kuimarisha usimamizi wa masuala ya elimu, uongozi na utawala.
  
Mashindano hayo ya TEHAMA ya HUAWEI yaliasisiwa mwaka 2015 na baadaye mwaka 2016 yakazinduliwa huko Afrika Kusini, ambapo hadi kufikia mwaka 2017 tayari wanafunzi wapatao 40,000 wameshiriki mashindano hayo. 

Kwa upande wa Tanzania, yamezinduliwa mwaka huu, ambapo wanafunzi 500 walishiriki na baadaye kubaki 50, ambapo  waliokabidhiwa tuzo ni saba na watatu kati yao na mkufunzi mmoja wamepata fursa ya kushiriki hatua inayofuata ya mashindano hayo nchini Afrika Kusini. 

Sherehe hizo zimehudhuliwa na Balozi wa China nchini Tanzania, Balozi Wang Ke, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, Naibu Wazri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye, Mkurugenzi Mtendaji wa HUAWEI Tanzania Frank Zhou na wawakilishi mbalimbali wa taasisi za Umoja wa Mataifa nchini.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Balozi wa China Nchini, Mhe. Wang Ke wakati alipowasili kwenye Hoteli ya Hayyat Regency jijini Dar es salaam, Kutoa Tuzo za Mashindano ya TEHAMA ya HUAWEI, Desemba 5, 2018.  Wapili kushoto ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Profesa  Joyce Ndalichako   na kulia ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na viongozi walioshiriki katika sherehe za Utoaji Tuzo za Mashindano ya TEHAMA ya HUAWEI kwenye hoteli ya Hayyat Regency jijini Dar es salaam, Desemba 5, 2018. Kutoka kushoto ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi, Atashasta Nditiye, Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Profesa Joyce Ndalichako, Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya HUAWEI nchini, Frank Zhou na  Balozi wa China nchini, Mhe. Wang Ke. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Viongozi wa Kitaifa na Kimataifa wakiwa katika picha ya pamoja na washindi wa Mashindano ya TEHAMA ya HUAWEI baada ya kuwakabidhi tuzo za ushindi washindi hao kwenye hoteli ya Hayyat Regency jijini Dar es salaam, Desemba 5, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).