Monday, November 12, 2018

WANAFUNZI 600 S/M VIKAWE KATA YA PANGANI, KIBAHA MJINI WASOMEA KATIKA MADARASA MANNE

NA MWAMVUA MWINYI,KIBAHA

SHULE ya msingi Vikawe ,kata ya Pangani ,Mjini Kibaha ,Mkoani Pwani  ina upungufu wa vyumba vya madarasa hali inayosababisha ,wanafunzi 600 kusomea kwenye vyumba vinne vinavyotumika shuleni hapo .

Aidha wakazi wa Vikawe ,wanakabiliwa na adha ya ukosefu wa maji safi na salama hali inayosababisha kutumia maji ya visima ambayo sio salama kwao.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika mkutano wa hadhara wa wakazi wa Vikawe Bondeni, Vikawe Shule na Mtaa wa Miwale, ulioitishwa na mbunge wa jimbo la Kibaha Mjini ,Silvestry Koka , mkazi Amina Seif alisikitishwa kuona baadhi ya vyumba vya madarasa vina majani ya miba badala ya wanafunzi.

Akizungumzia suala la ukosefu wa maji , Majawa Mtwana alisema ,hawapaswi kuwa na tatizo la maji kwakuwa bomba limepita kwenye eneo lao .

Alisema wangefaidika na mradi huo ulioanzia Ruvu Chini -Vikawe Shuleni hadi Miwale .

“Tunaomba utusaidie mbunge ,hatupaswi kuishi mjini wakati tunashida ya maji ,ndoa za watu zipo matatani kwa kukosa maji ,tunaoga maji ya visimani,tunataka ushughulikie suala hili ili tuondokane na kero hii” alielezea.

Kaimu afisa elimu msingi ,Ramadhani Lawoga alisema,shule ya msingi Vikawe ina jumla ya vyumba vya madarasa saba,kati ya vyumba hivyo viwili na ofisi ya mwalimu ni jengo la zamani ambalo limechakaa.

Hata hivyo alisema ,nalo jengo jipya lililojengwa shuleni hapo nalo ni bovu .

Lawoga alieleza, kutokana na hali hiyo ,vyumba vitatu kati ya saba vilivyopo ni vibovu na hivyo vinatakiwa kujengwa upya ,ambapo wanatarajia kuanza kujenga vyumba viwili kwa bajeti ya mwaka 2018/2019. 

Akijibu juu ya upungufu wa madarasa ,aliahidi kwenda kushauriana na mkurugenzi wa halmashauri ya Mji wa Kibaha Jennifer Omolo ili kuangalia namna ya kukarabati baadhi ya madarasa .

Kuhusu changamoto ya maji ,halmashauri ya mji huo imekiri kuwepo deni la bili walilokuwa wakidaiwa na DAWASA ya sh.milioni 4.8 ambapo imeshalipa kiasi cha sh.milioni 3.4 na imebakia deni la milioni 1.4 .

Kutokana na ubovu pamoja na wataalamu kutofanya kazi ya usambazaji ipasavyo ya mradi huo ,Koka alisema kinachofuata ni hatua ya uchunguzi na mradi kurudishwa chini ya DAWASA ili kuondoa tatizo hilo .
Mbunge huyo alilazimika kuunda kamati ya watu sita akiwemo injinia wa DAWASA Kibaha, Injinia wa maji Halmashauri ya Mji Kibaha, Diwani wa Pangani ,katibu wa nbunge na wananchi wawili kwa ajili ya kwenda Bagamoyo ili kufuatilia jambo hilo na kutoa mrejesho ndani ya wiki moja .

WAZIRI KALEMANI AIVUNJA BODI YA WAKURUGENZI YA WAKALA WA NISHATI VIJIJINI (REA)

Waziri wa Nishati Dk Medard Kalemani leo (Novemba 12.2018) amevunja Bodi ya Wakurugenzi ya Wakala wa Nishati Vijiji REA kutokana na kutoridhishwa na utendaji kazi wake.

Waziri Kalemani amewaambia waandishi wa habari leo jijini hapa  kuwa bodi hiyo iliundwa mwaka 2017 kwa mujibu wa sheria ya wakala vijijini No.8 ya mwaka 2005.

“Kwa mujibu wa mamlaka niliyopewa chini ya kifungu 9 (3)(b) cha sheria No. 8 ya nishati vijijini ya 2005 nimeamua kuivunja bodi kwa kutengua uteuzi wa mwenyejuti pamoja na wajumbe wa bodi ya wakurugenzi ya wakala wa nishati vijijini kuanzia leo tarehe 12 novemba 2018″amesema Kalemani.

Aidha amesema kuwa bodi nyingine itaundwa baadae kwa mujibu wa sheria ya nishati vijijini ya mwaka 2005 Bodi hiyo iliyokuwa ikiongozwa na mwenyekiti wake Gigion Kaunda ilidumu kwa muda wa mwaka mmoja baada ya mwaka jana.

Dk, Kalemani amesema kuwa Bodi mpya itaundwa badaye kwa mujibu wa sheria ya Nishati Vijijini ya mwaka 2005.

Wajumbe wa Bodi ambao wametenguliwa ni pamoja na Mhandisi Innoceent Lwogwa,Happiness Mhina,Stella Mandago, Scholastica Jullu,Amina Chinja,Teobard Sabi na Michael Nyagoga.

Sunday, November 11, 2018

TFS KUANZISHA BUSTANI ZA MICHE YA MITI NCHI NZIMA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan (mwenye kilemba) akifuatiwa na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Profesa Dos Santos Silayo akikagua kitalu cha miche wakati alipotembelea shamba la miti la Rongai linalomilikiwa na TFS Rongai Rombo. 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akikagua kitalu cha miche wakati alipotembelea shamba la miti la Serikali lililopo Rongai Rombo. Makamu wa Rais yupo kwenye ziara ya kukagua na kuhamasisha shughuli za maendeleo mkoani Kilimanjaro. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
..........................

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan yupo kwenye ziara ya kukagua na kuhamasisha shughuli za maendeleo mkoani Kilimanjaro.

Desemba 21, 2017 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiongoza wakazi wa mji wa Dodoma katika Uzinduzi wa Kampeni ya Kuifanya Dodoma iwe ya kijani kwa kupanda mti kwenye chanzo cha maji Bonde la Makutupora - Dodoma.

 Aliagiza kila shule, chuo na familia na hata taasisi kuanzisha kupanda miti na kuanzisha bustani ndogo za miti itakayoduma mazingira yaliopo.

 “ itapendeza zaidi katika majumba yetu tukahakikisha kila mtu ana mti mmoja wa matunda anayoyapenda na mmoja wa kivuli, mamlaka zetu za tawala za mikoa na serikali za mitaa lazima zihakikishe kuna sheria ndogo ndogo zinazosimami mambo haya,” alisema Makamu wa Rais.

Awali Serikali kupitia Ilani ya Uchaguzi ya 2015-2020, inaelekeza kupanga na kuendelea kutekeleza miradi ya upandaji miti ili kuondokana na hatari ya Taifa kugeuka kuwa jangwa kwa kuhakikisha kila Halmashauri inapanda na kutunza miti isiyopungua milioni 1.5 kila mwaka na kuongeza eneo la kupanda miti kutoka hekta 60,000 mwaka 2015 hadi hekta 130,000 mwaka 2020.

Katika kutekeleza maagizo hayo; Prof. Silayo aliagiza kanda zote za TFS kuanzisha bustani za miche ya miti ambayo huipanda katika maeneo mbalimbali ya nchi pamoja na kugawa kwa taasisi mbalimbali zenye uhitaji pale inapobidi. 

“Ofisi zetu za kanda zinajukumu kubwa la kutoa elimu na ushauri juu ya upandaji miti pamoja na kuotesha miche ya miti ya aina mbalimbali, iwe matunda, kivuli, mbao laini, mbao ngumu na hata miti ya asili na ikibidi miti huyo huigawa kwa taasisi zenye uhitaji,” alisema Prof. Silayo.

LUGOLA ASAFISHA JESHI LA POLISI, KIGOMA.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amemuagiza Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro kuwaondoa katika madaraka Mkuu wa Utawala wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma ambaye alikuwa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa, Mkuu wa Operesheni  wa Mkoa huo, Mkuu wa Polisi  Wilaya ya Uvinza na Mkuu wa Intelejinsia wa wilaya hiyo.

Pia Lugola ameagiza askari wote wa kituo cha polisi Mpeta na Nguruka wilayani Uvinza wahamishwe haraka iwezekanavyo katika vituo hivyo.

Lugola ametoa kauli nzito kwa kuwaondoa katika nyadhifa zao maafisa wa juu wa jeshi hilo, kutokana na mapungufu aliyoyaona katika operesheni iliyofanyika mwezi uliopita ya kuwaondoa wakulima na wafugaji waliovamia ranchi za Taasisi ya NARCO ambao ipo chini ya Wizra ya Mifugo, ambayo katika operesheni hiyo askari polisi wawili na raia wawili waliuawa.

Akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika  Kitongoji cha Mwanduhubandu, Kijiji cha Mpeta Wilayani Uvinza, leo, Waziri Lugola alisema viongozi hao wa Polisi wameshindwa kuifanya kazi hiyo kwa umakini ndio mana kulikua upungufu mkubwa katika operesheni hiyo, hivyo damu za waliouawa zinakua juu ya hao viongozi wa polisi mkoa na wilaya.

“Kutokana na hali hiyo, namuagiza IGP Sirro kuwaondoa kwenye madaraka hao wote niliowataja ifikapo kesho, na kesho Jumatatu nitakapo kuwa Dodoma nitakutana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ili kuona hatua nyingine za kinidhamu zitakazochukulia kwa hao niliowataja,” alisema Lugola.

Waziri Lugola aliongeza kuwa, Jeshi la Polisi halina nia ya kuua mtu, kumuonea mtu, kudhulumu  mtu lakini pale inapotokea jeshi hilo limeshindwa kutekeleza wajibu wake vizuri, lazima yeye Waziri achukue hatua.

Hata hivyo, Lugola alisema Jeshi la Polisi halipaswi kuvunjika moyo, litaendelea kufanya operesheni za mara kwa mara katika kuhakikisha linapambana na uhalifu, kwa hayo ambayo yanayojitokeza hayana nafasi ya kuwakatisha tamaa wala kuwavunja moyo.

“Mimi Waziri wa Wizara hii, dhamana yangu na haya ninayoyafanya, vyombo vyangu vya ulinzi na usalama ninavyovisimamia msinione mimi kama mwanasiasa, msichukulie maagizo yangu na matamko yangu kama ya mwanasiasa, atyakaye jidanganya hivyo, itakula kwake,” alisema Lugola.

Lugola alioagiza waondolewe madaraka ni Mkuu wa Utawala wa Jeshi l aPolisi Mkoa wa Kigoma ambaye alikuwa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wakati operesheni hiyo ilipotokea, ACP Simon Ngowi, Mkuu wa Operesheni  wa Mkoa huo, SP Msembele, Mkuu wa Polisi  Wilaya ya Uvinza, SSP Mwakisambwe, na Mkuu wa Intelejinsia wa wilaya hiyo, InspektaDotto Daudi.

CHANZO FULL SHANGWE BLOG.