Monday, February 19, 2024

MILIONI 800 KUWASAIDIA WAHANGA WA MAFURIKO MULEBA.

 


Na Alodia Babara

 Bukoba,

Walengwa wapatao 482 walioathirika na mafuriko pamoja na upepo mkali  katika wilaya za Muleba na Manispaa ya Bukoba mwaka jana wanatarajia kupata msaada wa kibinadamu wenye malengo mbalimbali utakaoghalimu zaidi ya sh. milioni 800 kutoka taasisi zisizo za kiserikali.

Msaada  huo ambao unatolewa na Kanisa la Kiinjili la Kirutheli Tanzania KKKT Dayosisi ya Kaskazini Magharibi kwa ufadhili wa taasisis inayojihusisha na shughuli za kibinadamu kwa watu wenye majanga nchini Tanzania (TCRS) na taasisi ya Actalliance Tanzania Forum utakuwa wa mwaka mmoja utawezesha kutimiza malengo sita ambayo ni msaada wa chakula, uboreshaji wa makazi, msaada wa kisaikrojia, huduma za maji, elimu na Afya na usafi wa mazingira.

Akizindua mradi huo Februari 19, mwaka huu mkuu wa mkoa wa Kagera Fatuma Mwassa alisisitiza mambo matatu ikiwemo  matumizi ya fedha za walengwa, usimamizi mzuri pamoja na  elimu ya maafa kwa walengwa.

 Mwassa alieleza kuwa, anazo taarifa kuwa mradi huo utahusisha maswala ya fedha, akaelekeza maafisa wanaohusika na maafa upande wa Serikali kama maafisa maendeleo ya jamii, watendaji wa kata, madiwani na viongozi hadi ngazi ya wilaya kushirikiana na uongozi wa kanisa la Kiinjili la Kirutheli Tanzania dayosisi ya Kaskazini Mgharibi katika uhakiki wa walengwa ambao ni harisia ili mradi usije kunufaisha ambao siyo walengwa.

“Viongozi kuanzia ngazi ya kitongoji hadi wilaya ni lazima kushiriki kikamilifu wakati wa uhakiki na kutoa huduma kwa walengwa wanaostahili na ndiyo maana nyinyi viongozi mmehudhuria uzinduzi huu” amesema Mwassa.

Amesisitiza hilo baada ya kukumbana na changamoto wakati wa kugawa chakula kwa waathirika hao kilicholetwa na kamati ya maafa kutoka ofisi ya Waziri mkuu kwani ziliingizwa siasa na likaibuka vuguvugu wakitaka watu wote wapewe msaada huo na watu waliokuwa kwenye kata zilizokumbwa na maafa wakajitokeza wakidai wote wana shida.

Amesema tathimini ilishafanyika wenye uhitaji walishatambuliwa na kuwa viongozi wasiende kuzua la kuzua kwa kulazimisha wengine kuingia kwenye hiyo risti, kaya ambazo zitahusika baada ya uchunguzi ni 482 inajullikana na ndiyo bajeti iliyopo.

“Nitumie nafasi hii kusisitiza kuwa fedha zitakazotolewa zitumike kwa matumizi yaliyokusudiwa zisiwe chanzo cha ndoa kuvunjika na kusababisha ukatili wa kijinsia katika familia za walengwa” amesema Mwassa

Aidha aliongeza kuwa, mradi ujikite sana kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kujifunza namna ya kukabiliana na maafa, mfano wananchi waelimishwe kutojenga sehemu hatarishi zinazoweza kuhatarisha maisha yao na familia zao serikali inaposema maeneo haya hayafai kujengwa makazi basi watu wote wakubaliane na waache maeneo hayo.

Kwa  upande wake Mkurugenzi wa taasisi inayojihusisha na shughuli za kibinadamu kwa watu wenye majanga nchini Tanzania TCRS Samwel Mlay amesema kuwa, mradi utakuwa wa mwaka mmoja ulianza kutekelezwa Desemba mwaka jana na utakamilika Desemba mwaka huuu, utawezesha kutimiza malengo sita ambayo ni msaada wa chakula, uboreshaji wa makazi, msaada wa kisaikrojia, huduma za maji, elimu na afya na usafi wa mazingira.

Mlay amesema, mradi utaghalimu zaidi ya shl milioni 800 walengwa wapatao 482 walioathirika na mafuriko pamoja na upepo mkali  katika wilaya za Muleba na Manispaa ya Bukoba mwaka jana watanufaika na mradi huo ambapo katika wilaya ya Muleba ni kata mbili za Kashalunga na Kalambi na Manispaa ya Bukoba ni kata nne za Rwamishenyi, Hamugembe, Bilele na Kashai  zinatarajia kupata msaada wa kibinadamu katika nyanja mbalimbali kutoka katika  taasisi zisizo za kiserikali

Diwani wa kata ya Kashai Ramadhan Kambuga amesema kuwa, kutolewa kwa misaada hiyo kutasaidia kupunguza maumivu kwa wananchi waliokumbwa na mafuriko na upepo mkali.

 

Amesema wananchi waliokumbwa na athari za mafuriko na upepo walishatambuliwa hivyo hawatakwenda kinyume na wale waliotambuliwa kikubwa viongozi wa Serikali walishawatembelea na kuwabaini na mahitaji ya kila mmoja, hawataongeza wala kupunguza mlengwa kila mmoja alishawekwa kwenye utaratibu hivyo uadilifu, busara na hekima vitaendelea kutumika.

Hata hivyo mafuriko hayo kwa wilaya ya Muleba yalitokea Octoba 15, mwaka jana na kwa manispaa ya Bukoba yalitokea Oktoba 18, mwaka jana.


DIVISHENI YA ELIMU SEKONDARI YAFANYA KIKAO KAZI CHALINZE.

 

Divisheni ya Elimu Sekondari katika Halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo, imefanya kikao kazi kufanya tathmini ya utendaji kazi ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini ya matokeo ya kidato cha pili na cha nne kwa mwaka 2023 ili kuweka mikakati mbalimbali katika kuboresha utendaji kazi ili kufikia Malengo ya utendaji kazi (Key Performance Indicators).

Kikao hicho kimefanyika leo tarehe 19 Februali 2024 katika ukumbi wa Jakaya Kikwete uliopo katika Halmashauri hiyo na kuhusisha Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule za Sekondari za Serikali na binafsi na walimu wa Taaluma katika Shule zote za Sekondari katika Halmashauri ya Chalinze.

Akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi Afisa Elimu wilaya ya Chalinze, Bi Salama Ndyetabura alieleza mafanikio na Changamoto mbalimbali zinazoikabili Divisheni ya Elimu Sekondari, huku akiishukuru Halmashauri ya Chalinze kwa kuweza kujenga maabara kwa baadhi ya Shule za Sekondari katika Halmashauri hiyo

Afisa Elimu Sekondari, ametoa pongezi kwa wakuu wa Shule kwa usimamizi bora wa miradi kwa kumpongeza Mkuu wa Shule Changalikwa Mwl Benasian Ituja kwa Kusimamia ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari ya Mbwewe kwa kuisimamia kwa weledi na maarifa hata kutotengeneza hoja yoyote ya ukaguzi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Chalinze Bwana Ramadhani Possi ametoa pongezi za dhati kwa walimu wote wa Sekondari, Maafisa Elimu na Maafisa kata kwa jinsi wanavyofanya kazi kwa weledi na uadilifu katika kutoa maarifa kwa watoto wa Taifa hili.

Possi aliwapongeza kwa kukuza taaluma na kupata matokeo mazuri ya kidato cha nne na cha pili kwa mwaka 2023.

Aidha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri amewasisitiza watendaji wa kata kushirikiana na walimu ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wote waliofaulu kuingia kidato cha kwanza kuripoti kwa wakati na kuweza kuendelea na masomo.





Saturday, February 10, 2024

MIZIGO YAONGEZEKA BANDARI YA MTWARA


 Na Albert Kawogo, Mtwara

BANDARI ya Mtwara imeongeza kiasi cha mizigo inayohudumiwa hapo kutoka kiasi cha tani laki nne hadi tani milioni 1.6 katika kipindi cha mwaka 2022/2023.

Chachu ya ongezeko hilo linatokana na hatua kubwa ya kimkakati ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania TPA kufanya maboresho yenya thamani ya shilingi bilioni 157.8 kwenye eneo la gati ya bandari hiyo sambamba na ununuzi wa mtambo wa kupakia na kushusha mizigo.

Ferdinand Nyathi meneja wa Bandari ya Mtwara amewaeleza wahariri wa habari  kutoka Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) waliotembelea bandari hiyo kuwa,  jitihada kubwa zinazofanywa na TPA kwenye uwekezaji wa miundombinu ya bandari ndio zinaongeza ufanisi katika utendaji.

"Uwekezaji  umeimarishaji  mifumo ya bandari na matunda ya kazi hii ni kwamba msimu wa korosho ambao sasa uko mwishoni tumeweza kuhudumia meli kubwa 28" Alisema Nyathi

Nyathi aliendelea kufafanua kuwa Bandari hiyo imekuwa ikisafirisha makaa ya mawe, saruji ya kiwanda Cha Dangote Cement ambapo saruji hiyo husafirishwa kupelekwa Zanzibar na Comoro.

Naye Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania Dk George Fasha alisema Bandari ya Mtwara ni Bandari ya kimkakati kwa ushoroba wa kusini.

Dk Fasha alisema mpango wa sasa ni kuanza usafirishaji wa madini ya graphite kutoka Wilaya Ruangwa Lindi,huku akisisitiza kuwa ili kuimarisha ushoroba huo TPA inaendelea kuboresha Bandari za MbambaBay ili iweze kusaidia bandari ya Mtwara kuhudumia mizigo ya Malawi na Msumbiji.

Thursday, February 8, 2024

RAIS SAMIA ASIKITISHWA NA MAUAJI YA PALESTINA.

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania inasikitishwa na vita vinavyoendelea Palestina vinavyosababisha mauaji ya watoto na raia wasio na hatia.

Rais Samia ameyasema hayo Tarehe 07 february 2024 katika sherehe za mwaka mpya 2024 (Diplomatic Sherry Party) kwa mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini pamoja na wawakilishi wa Mashirika ya kimataifa zilizofanyika Ikulu jijini Dar es salaam.

Aidha, amesema Tanzania inaunga mkono usuluhishi kati ya Palestina na Israeli kwa kutoa wito wa kusitisha mapigano na kupatiwa misaada ya kibinadamu.

Wakati huohuo Rais Samia amesema Haki, Demokrasia, Sheria na Utawala bora vitadumishwa kwa watu wote wakati wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.

Amesema ili kuhakikisha uchaguzi huru na wa haki, kikosi kazi huru cha kupitia na kushauri mageuzi muhimu katika mfumo wa siasa kiliundwa ambapo kiliwasilisha ripoti yake mwaka 2023

Rais Samia pia amesema mapendekezo mengi ya kikosi kazi yaliyopokelewa na serikali na wadau wote yalihusu kuongeza uwazi katika michakato ya uchaguzi ikiwa ni pamoja na uteuzi wa Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi.


UWT NA KIPAUMBELE CHA MAZINGIRA WEZESHI KUINUA WANAWAKE KIUCHUMI

 


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt Doto Biteko akimkabidhi Nakala ya Makubaliano kati ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC)  Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania UWT Mary Chatanda (MCC) jijini Dodoma Tarehe 07 February 2024.

.......................

DODOMA 

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt Doto Biteko  amemkabidhi Nakala ya Makubaliano kati ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC)  kwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania UWT Mary Chatanda (MCC) katika Hafla ya Utiaji Saini wa Makubaliano hayo.

Aidha, Mwenyekiti Chatanda alishiriki hafla hii kwa lengo la kuhakikisha UWT inakuwa mstari wa mbele katika kuchangia uwepo wa mazingira wezeshi ya kuwainua Wanawake Kiuchumi kuanzia katika utoaji elimu na hamasa kwa jamii.

UWT IMARA JESHI LA MAMA SAMIA KAZI IENDELEE.


Tuesday, February 6, 2024

ALIYEMKATA KIGANJA KATIBU WA BAKWATA BUKOBA AUWAWA NA WANANCHI WENYE HASIRA.

 

Na Alodia  Babara

Bukoba,

Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Abdulmalick Yahya (42) mkazi wa wilaya ya Muleba ambaye alikuwa mtunza ghala katika mradi wa ujenzi wa BAKWATA Bukoba (BAKWATA COMPLEX) amefariki baada ya kushambiliwa na wananchi wenye hasira kufuatia tukio alilofanya la kumshambulia katibu wa BAKWATA wilaya ya Bukoba na kumkata kiganja cha mkono.

Katibu wa Bakwata wilaya ya Bukoba Hamza Zakaria (43) akiwa anaendelea na matibabu katika hospital ya rufaa ya mkoa, Bukoba amesimulia alivyoshambuliwa na aliyekuwa mtunza ghala la ujenzi wa BAKWATA Complex na kuanza kumkata kwa panga kisha kutenganisha kiganja na kiwiko cha mkono wa kushoto.

"Ilikuwa ni majira ya saa 10:00 asuhuhi siku ya Tarehe 2 februali 2024 wakati nikiwa kazini kwangu nilitoka kwenda duka la jirani kuangalia viatu kwa mtu mmoja anaitwa Khalid ndipo alitokea Abdulmalick Yahya akiwa ameshika panga na kuanza kunishambulia" amesema Hamza

Ameendelea kusimulia kuwa, alipomkata panga la kwanza alikinga mkono alipotaka kumkata tena walishikana mikono na badae akajitoa kwenye mikono yake na kutaka kukimbia kutokana na kwamba  alikuwa amevaa kanzu ambayo ilimtega miguu akashindwa  kukimbia na badala yake alianguka chini.

"Kwa kuwa alikuwa anaendelea kunifukuza alinikuta hapo hapo chini akaanza kunikata mapanga huku  nikiendelea kukinga mkono wa kushoto ndipo baadaye nilijifanya nimefariki dunia alipokata mara ya mwisho akaona sijitingishi akaondoka" ameongeza Hamza.

Amesema ndani ya dakika kama tano hivi alimuona mtu anayemfahamu akamuita wakampa msaada wa kumbeba na vijana wengine na kumpeleka hospital ya rufaa ya mkoa wa Kagera, Bukoba ambapo anaendelea kupatiwa matibabu na anaendelea vizuri.

Amesema huyo aliyemkata mapanga hakuwa na visa naye labda kama vilitokana na ujenzi uliokuwa unaendelea msikitini, siku zilizopita alikuwa ni mtunza ghala na alikuwa ni miongoni mwa watu waliokamatwa wanaiba nondo na saruji akawa amesimamishwa kuendelea kusimamia ghala hilo, sasa alihisi kuwa alichongewa na Hamza na alikuwa ni mtu wa muda mrefu pale msikitini.

Kamanda wa polisi mkoani Kagera, Blasius Chatanda, amethibitisha kutokea kwa matukio hayo mawili na kusema kuwa, Abdulmalick Yahya (42) mkazi wa wilaya ya Muleba ambaye alikuwa mtunza ghala katika mradi wa ujenzi wa BAKWATA Bukoba (BAKWATA COMPLEX) kabla hajakumbwa na umauti Februari 02,2024 majira ya saa 11:30 asubuhi katika barabara ya Kawawa karibu na ofisi za Bakwata mkoa alifika na kuanza kumkata mapanga Hamza Zakaria (43) katibu wa BAKWATA wilaya ya Bukoba.

Amesema wakati akitenda tukio hilo watu waliokuwepo walimzuia asiendelee kumshambulia bila mafanikio na walipoona anataka kuwashambulia na  wao walianza kumshambulia na alibahatika kuokolewa na jeshi la polisi na kumkimbiza hospital ya rufaa ya mkoa, Bukoba ambapo wakati akiendelea kupata matibabu alifariki dunia.

Kamanda Chatanda alieleza kwamba, chanzo cha tukio hilo ni kusimamishwa kazi ya kusimamia ghala la kutunza vifaa vya ujenzi wa BAKWATA complex  kwa Abdulmalick na kamati ya ujenzi Februari mosi ,2024 ambapo Abdulmalick alimtuhumu katibu wa BAKWATA, Bukoba kwamba ndiyo chanzo cha hayo yote na akaahidi kulipiza kisasi.

Amesema kuwa, alimkata mkono wa kushoto ambao kiganja chake alikitenganisha kabisa na kiwiko na alikatwa mapanga mengine mawili kichwani japo ni kwa bahati nzuri hayakuweza kupasua fuvu.

Ametoa rai kwa wananchi wa mkoa huo kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi na badala yake kufuata sheria na taratibu za nchi.




HATUTAWAFUMBIA MACHO WANAOJIITA BOKO HARAMU NDANI YA MKOA WA PWANI - Mramba

 

Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo Mkoa wa Pwani ndg David Mramba amesema hawako tayari kuwafumbia macho wanaojiita boko haramu kwani kujiita hivyo ni kuhatarisha maisha ya Watanzania.

Mramba ameyasema hayo leo tarehe 06/02/2024 katika Ofisi za CCM Mkoa wa Pwani kuwa CCM ina macho mengi hata mtu akiwa kwenye shimo ataonekana na akibainika hataachwa salama kimaadili.

Amesema wako watu wanataka kuwatishia Wanaccm kwa kujiita wao ni boko haramu jambo ambalo si jema ndani ya CCM.

" Unapojiita boko haramu tafsiri yake wewe ni mtekaji na mbakaji hivyo lazima tuwashughulikie watu wa aina hiyo  amesema Mramba

Ameendelea kusema kuwa hakuna kikundi ndani ya CCM kitakachokuwa na uwezo wa kubadili mawazo ya Wanaccm kwa kuwatishia.

Amesema wako wanaowatishia Viongozi walioko madarakani wakidai kuanza kutengeneza safu zao huku wakijipachika majina ya aina hiyo.

Hatutawavumilia wanaokiuka taratibu za Chama na tuko tayari kuwaadhibu ili Chama na wanachama wabaki salama  amesema Mramba

Acheni vihelehele vya kuwasumbua Viongozi walioko madaraka waacheni watekeleze Ilani ya CCM kwa mioyo safi* - asema Mramba

Mramba amezungumzia usemi usemao kuwa acha haki iamue haki usitafute haki pasipo haki akimaanisha unaweza ukawa na haki ya kugombea nafasi yoyote lakini ukaipoteza haki hiyo kwa sababu ya rafu za mapema.

Amehitimisha kwa kuwataka Wanaccm kulinda heshima ya Chama na kujilinda wao ili wakati wa uchaguzi wasiwe kikwazo kwenye vikao vya mchujo.

Taarifa hii imeandaliwa na

Idara ya Siasa, Uenezi na Mafunzo CCM
Mkoa wa Pwani.


WAFANYABIASHARA WA MAFUTA ZINGATIENI MAISHA YA WANANCHI - DKT. BITEKO

 

Na Mwandishi wetu, Dodoma

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Chama cha Waagizaji na Wasambazaji wa Mafuta nchini (TAOMAC) ambapo amewataka wafanyabiashara hao pamoja na faida wanayoipata wazingatie maslahi wananchi wa hali ya chini.

Ameyasema hayo tarehe 06 Februari, 2024 jijini Dodoma katika kikao ambacho kilijadili masuala mbalimbali ikiwemo changamoto mbalimbali ambazo wanafanyabiashara hao wanazikabili.

Amesema Serikali siku zote iko tayari kutoa ushirikiano kwa wafanyabiashara na kuwekea mazingira wezeshi ya biashara zao ili waweze kuwajibika kwa mujibu wa sheria kanuni na taratibu za usimamizi katika sekta husika.

“Tunapofanya biashara hii ya mafuta lazima tuangalie mtanzania maskini ambaye anategemea sekta hii kujikwamua kimaisha, isifike mahala kila mwisho wa mwezi watu wote wanashika vichwa wakihofia kupanda kwa bei ya mafuta… Serikali inafanya kila jitihada kupunguza makali ya bei ya mafuta hivyo nanyi mlizingatie suala hili.”amesema Dkt. Biteko

Dkt. Biteko ameishukuru TAOMAC kwa ushirikiano wao kwa Serikali katika kuhakikisha kuwa nchi inakuwa na mafuta ya kutosha na kueleza kuwa Serikali inatambua na kuthamini mchango wao katika ukuaji wa Uchumi wa nchi.

Amesema uhusinao uliopo kati ya Serikali na TAOMAC unahitaji kuwa endelevu na pale zinapotokea changamoto zitafutwe njia za kukabiliana nazo kwa mstakabali wa Taifa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TAOMAC, Kalpesh Mehta ameishukuru Serikali kwa mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara wa mafuta na utayari wa Serikali kushughulikia changamoto kadhaa zinazojitokeza katika sekta hiyo.

Akizungumzia mazingira hayo, Mkurugenzi Mtendaji, Raphael Mgaya amesema ushirikiano wa TAOMAC kwa serikali hauepukiki ili kuhakikisha nchi inapata mafuta ya kutosha hivyo wapo tayari kushirikiana na Serikali.

Kikao hicho pia kimehudhuriwa na Watendaji kutoka  Taasisi mbalimbali za Serikali ikiwemo Benki Kuu  ya Tanzania (BoT) Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Shirika la Uwakala wa Meli (TASAC), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba.







TAKUKURU KAGERA YABAINI MAPUNGUFU KATIKA MIRADI 16.

 

Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Kagera Pilly Mwakasege akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za taasisi hiyo kwa kipindi cha miezi mitatu  Octoba hadi Desemba 2023

..................................

Na Alodia Babara

Bukoba

TAASISI ya kuzuia na kupamba na Rushwa mkoa wa Kagera kwa kipindi cha Oktoba-Desemba 2023, imefuatilia miradi 19 yenye thamani  zaidi ya shilingi bilioni 6.1 ambapo kati ya hiyo miradi 16 yenye thamani zaidi ya shilingi bil.4.2 imebainika kuwa na mapungufu yaliyohitaji marekebisho.

Kamanda wa taasisi hiyo mkoani humo Pilly Mwakasege amesema kuwa kiasi hicho ni sawa na asilimia 68.50 ya fedha za miradi ambapo kumekuwa na ongezeko la asilimia 18.77 ya miradi hiyo, ukilinganisha na kipindi cha Julai-Septemba mwaka jana.

Mwakasege ameeleza hayo leo Februari 06,2024 wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu yao kwa kipindi cha robo tatu ya mwisho wa mwaka 2023 ambapo,miradi iliyohusika ni ya ujenzi wa miundombinu ya shule mpya za msingi na sekondari, maji, zahanati pamoja na ujenzi wa madarasa ya msingi na sekondari ili kuhakikisha miradi yote inatekelezwa kuendana na thamani ya fedha iliyotumika.

Mwakasege amesema kuwa kwa kipindi hicho walipokea malalamiko 92 kati ya hayo 58 hayahusu rushwa ambapo 34 yanahusu rushwa na majalada yamefunguliwa ambapo 20 uchunguzi wake umekamilika na hatua stahiki zinatarajiwa kuchukuliwa kwa mujibu wa sheria.

“Idara zilizolalamikiwa ni Halmashauri ambapo idara ya fedha kesi moja, Elimu 10, Afya saba, Utawala 12, Biashara moja, Kilimo nane, Ardhi saba, Mazingira tatu na mengine yalihusu sekta binafsi ambayo ni 12, ikiwemo  Maji tatu, Ujenzi tisa, Maliasili saba, Nishati moja, Uhamiaji mbili, Polisi nne, Mahakama tatu, Uchukuzi moja na mamlaka ya mapato Tanzania moja" ameeleza Mwakasege.

 Amesema katika progaramu ya Takukuru rafiki ambayo inatekelezwa kwa kushirikisha wadau katika ngazi ya kata ambapo wananchi hupata fursa ya kuibua kero zinazowakabili katika maeneo yao ambapo kwa kipindi cha Oktoba-Desemba walitembelea kata 11 na kupokea kero kuhusu sekta za Elimu, Afya, Maji, Fedha na Nishati ambapo ufuatiliaji wake unaendelea.

Aidha amevitaja vipaumbele vya Takukuru kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Machi mwaka huu ambavyo ni kuelimisha Umma kupitia njia mbalimbali ili kuongeza ushirikishwaji wa wananchi katika kuzuia vitendo vya rushwa, kutatua kero mbalimbali katika jamii kupitia programu ya Takukuru Rafiki na kuendelea kufuatilia rasilimali za Umma kupitia ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo ili kuzuia ufujaji wa fedha za Umma.

 Nyingine ni kufanya chambuzi za mifumo kwa lengo la kuzuia rushwa zinazosababishwa na mapungufu yaliyopo kwenye mifumo ya utendaji wa sekta ya Umma na sekta binafsi ambapo amewahimiza wasimamizi wa miradi ya maendeleo kuwa waadilifu na kuhakikisha fedha zote za miradi zinatumika vizuri.


Monday, February 5, 2024

KAMATI YA BUNGE YARIDHISHWA NA UTENDAJI WA MSD

 



Na. WAF, Dodoma

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Maswala ya UKIMWI imeitaka Bohari ya Dawa (MSD) kuongeza ufanisi, ubunifu wa hali ya juu kwa kuhakikisha dawa zinanunuliwa, zinahifadhiwa sehemu sahihi, kusambaza dawa hizo kwa wakati katika sehemu zenye uhitaji na kukusanya madeni ili kuweza kuwa imara na taasisi endelevu.

Wito huo umetolewa leo Jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Afya na Maswala ya UKIMWI, Mhe. Stansilaus Nyongo baada ya kupokea taarifa ya hali ya utendaji na majukumu ya Bohari ya Dawa (MSD).

Mhe. Nyongo amesema kuwa wao kama wawakilishi wa wananchi wataendelea kuishinikiza serikali kuiwezesha MSD kupata mtaji ili kujiendesha kiufanisi katika kusambaza dawa kwa wakati.

“Bohari kuu ina majukumu ya kununua, kutengeneza, kuhifadhi dawa pamoja na kusambaza dawa katika vituo vya  vyote nchini”. Ameeleza  Mhe. Nyongo.

Mhe. Nyongo amesema kwa ujumla kamati imeridhishwa na hali ya utendaji wa Bohari ya Dawa na mipango yake ya utek


Sunday, February 4, 2024

PWANI YAHITIMISHA SHEREHE ZA MAADHIMISHO YA MIAKA 47 YA KUZALIWA KWA CCM

 


Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Pwani leo tarehe 04/02/2024 kimehitimisha sherehe za  Maadhimisho ya miaka 47 ya kuzaliwa kwa CCM katika Kata ya  FUKAYOSI Wilaya ya  Bagamoyo huku kikiwa na matumaini makubwa ya ushindi kuelekea uchaguzi Mkuu wa Serikali za Mitaa, Vijijini na Vitongoji 2024.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi katika kuhitimisha maadhimisho hayo ndg. Mwinshehe Mlao amesema ili CCM iweze kuendelea kudumu lazima Viongozi waondoe ubinafsi.

Mlao amesema unapofika wakati wa uchaguzi Kila mpiga kura ahakikishe anawachagua Viongozi wa Serikali wenye nia njema ya kuongoza na ikitokea  wakawachagua Viongozi kwa ajili ya maslahi yao binafsi basi watakuwa wamepoteza haki za wengine.

Ameendelea kusema kuwa ili kushinda chaguzi zijazo kunahitajika UMOJA huku akisisitiza kuwa kama Kuna mwanachama yeyote mwenye nia ya kugombea na anaonekana kuwa na dosari aambiwe sasa wasisubiri mpaka achukue fomu ndio waseme mabaya yake huko ni kuchafuana.

" Tusikubali kusababisha migogoro isiyo na tija tunapoelekea kwenye chaguzi zijazo na wala tusikubali watu watugawe kwa ajili ya maslahi yao" amesema Mlao

Maadhimisho hayo yameambatana na ukaguzi wa Kituo Cha afya cha Fukayosi kinachojengwa kwa gharama ya Shilingi bilioni 1, Uzinduzi wa ujenzi wa Ofisi ya CCM kata ya Fukayosi, ugawaji wa vifaa vya Shule kwa wanafunzi wanaoishi katika Mazingira magumu, ugawaji wa vyeti vya PONGEZI kwa Kata zilizofanya vizuri katika uingizaji wanachama wapya na usajili kwa mfumo wa kielektroniki sambamba na zoezi la upandaji wa miti.

Taarifa hii imeandaliwa na:

David Mramba
Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo CCM
Mkoa wa Pwani.


Friday, February 2, 2024

LIONS CLUB YAKABIDHI MATENKI YA MAJI CHALINZE.

 

MUNTAZIR Bharwan mmoja wa Wanachama wa Taasisi ya Lions Club, akielekeza jambo mbele ya Diwani wa Kata hiyo Mussa Gama mwenye Balaghashia. Picha na Omary Mngindo.

Miriam Kihiyo (Watatu kutoka kwa aliyevaa Balaghashia) akimkanidhi moja ya zawadi mtoto anayetoka kwenye Kituo cha kulelea Watoto wenye Mazingira hatarishi. Picha na Omary Mngindo.


....................................

Na Omary Mngindo, Ruvu.

TAASISI ya Lions Club ya jijini Dar es Salaam imekabidhi matenki 8 ya kuhifadhia maji katika shule za msingi na Sekondari ndani ya Kata ya Vigwaza Halmashauri ya Chalinze Mkoani Pwani.

Matanki hayo yanalenga kuwaondolea adha wanafunzi kwenye shule hizo, yamekabidhiwa kwa Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Chalinze, Ramadhani Possi, aliyewakilishwa na Miriam Kihiyo Afisa Elimu Msingi.

Muntazir Bharwan alisoma taarifa ya taasisi kwa niaba ya Mwenyekiti wa Lions Host Kaniz Naghavi, iliyoeleza kuwa kukabidhiwa kwa matenki hayo kumetokana na diwani wa Kata hiyo Mussa Gama kuelezea uwepo wa changamoto kwenye shule hizo.

Hafla hiyo iliyotumika pia kumkaribisha Gavana wa Tanzania District 411C Happiness Nkya, matenki hayo yanakwenda katika shule za Msilale, Chamakweza, Sekibwa, Ruvu, Mnindi, Kitonga na Kwazoka.

"Baada ya kupokea maombi ya diwani Gama tukawasiliana na Kampuni ya Refuelling Solutions (T) Limited na wadau wengine wakiwemo wanachama wa Lions ambao tumefanikisha upatikanaji huu," ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Gavana wa taasisi hiyo Nkya alisema kwamba kwa sasa wana wanachama 620 na Club 23, wakati Dar es Salaam zikiwa 14, na kwamba wamekuwa wakisaidia maeneo tofauti wakisaidiana na makampuni mengine.

Kwa upande wake diwani Gama ameishukuru Taasisi hiyo, huku akieleza kuwa imekuwa ikisaidia maendeleo katika nyanja mbalimbali ikiwemo vifaa katika Zahanati ya Ruvu Darajani, madaftari kwa wanafunzi ikiwemo matenki hayo.

"Club ya Lions imekuwa na msaada mkubwa sana kwetu wanaVigwaza, kwani wanasaidia kutatua matatizo kwenye kata yetu kwa kushirikiana na wadau wengine kutupatia misaada ya fedha na vitu katika sekta mbalimbali," alisema Gama.

Afisa Elimu awali na Msingi wa Halmashauri ya Chalinze, Mariam Kihiyo akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi hiyo,  aliishukuru taasisi hiyo, kwa misaada inayoendelea kuipeleka inayolenga kupunguza vikwazo kwa wanaVigwaza.

"Kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Chalinze, Alhaj Ramadhani Possi, tunawashukuru sana ndugu zetu wa Lions Club kwa namna mnavyojitoa mkishirikiana na wadau wenu, wanaChalinze tunatambua na kuthamini mchango wenu mkubwa kwetu," alisema Kihiyo.

Samwel Mjema Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Ruvu Darajani alisema matenki hayo yatasaidia kutunza maji pindi yanapokatika, huku akiahidi utunzwaji yaweze kudumu kwa muda mrefu.


Thursday, February 1, 2024

DED BAGAMOYO AZINDUA HUDUMA KITUO CHA AFYA FUKAYOSI.

 

Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo Bw. Shauri Selenda Leo tarehe 1 Februari, 2024 amezindua rasmi utoaji wa huduma katika kituo Cha Afya Fukayosi.

Akizungumza na watumishi wa Afya pamoja na Kamati ya Maendeleo ya Kata Fukayosi (WARDC) Selenda, alisisitiza kufanya kazi Kwa weledi pamoja na  kunyenyekea wagonjwa kama sehemu ya miiko ya tasnia ya utoaji wa huduma za afya.

" Mgonjwa mpaka anafika hospitali maana yake anahitaji huduma hivyo haina budi kumpokea kwa unyenyekevu na kumsikiliza shida yake na kumpatia matibabu". Alisema Bwana Selenda.           

Kituo Cha Afya Fukayosi kimejengwa kwa kutumia fedha toka Serikali Kuu na mapato ya ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo kwa lengo la kuimarisha huduma za afya ikiwemo Huduma ya Mama na Mtoto, Afya ya dharura na upasuaji wa wajawazito, Maabara, Jengo la Wagonjwa wa nje (OPD), Mionzi, na Jengo la kufulia.

Mkurugenzi Mtendaji alipanda miti kama ishara ya Uzinduzi wa huduma katika kituo hicho Cha Afya Fukayosi. Kituo Cha Afya Fukayosi kilianza Ujenzi Mwaka wa fedha 2021/2022 na kinategemea kuhudumia zaidi ya wakazi 17,000






DC. OKASH ATATUA KERO ZA BODABODA BAGAMOYO.

 

Na Daria Abdul, Hamisi Hamisi, Bagamoyo.

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Mhe. Halima Okash, akishirikiana na  viongozi mbalimbali wa Halmashauri  ya Wilaya hiyo, amefanya kikao na madereva wa pikipiki zinazobeba abiria (BODABODA)  Januari 31,2024 katika ukumbi wa flexible hall Chuo cha Sanaa Bagamoyo (TASUBA), kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili katika utendaji kazi wao wa kila siku.

 Mhe.Okash, amewasisitiza bodaboda kutii sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali, pia wajiepushe na matukio ya uhalifu wa kupora mali za wateja wao.

”Ndugu zangu lazima tutii sheria za usalama barabarani kwani tunawategemea ninyi vijana kuwa ndio Taifa la kesho hizo rizki tunazozipata kuna watu wanatutegemea tusipotii sheria za usalama barabarani, kutakuwa na ajali za mara kwa mara zitakazopelekea kupoteza maisha na kuleta ulemavu.” Amesema Okash

Akizungumza katika hafla hiyo Mkuu wa Usalama barabarani,  Wilaya ya Bagamoyo (DTO)  Azizi Zubeir, amewataka bodaboda kuhakikisha wanasajili vyombo vyao vya usafiri, leseni pamoja na bima ili wasikamatwe na vyombo vya usalama na kueleza Zaidi kuwa bima itasidia kupunguza gharama ya matengenezo ya vyombo hivyo na matibabu kwa dereva anapopata ajali.

"Ni waambie tu  bodaboda ili ufanye kazi kihalali lazima usajili vyombo vyetu, tuwe na leseni ya udereva pamoja na bima ya chombo husika ili itusaidie kupunguza gharama za matengenezo na matibabu inapotokea ajali.” Amesema Zubeir

Akitoa kero yake katika hafla hiyo Mwenyekit wa Bodaboda kata ya Dunda Ndug, James Mapunda, amesema kuwa wamekuwa wakipatiwa mafunzo ya usalama barabarani na vyuo mbalimbali vikishirikiana na Jeshi la polisi Wilayani hapo na kuahidiwa kupatiwa leseni za udereva baada ya kumalizika kwa mafunzo hayo, badala yake hawapewi leseni zao licha ya kulipia fedha kwa ajili ya leseni hizo.

Kwa upande wake Waziri Mohammed (BODABODA), ameeleza kuwa wamekuwa wakinyanyaswa na kukamatwa na Mgambo  kwa mabavu katika vituo vyao vya kazi (vijiwe) bila ya uwepo wa askari wa Jeshi la polisi kinyume na sheria hali inayopelekea kushindwa kufanya shughuli zao usafirishaji kwa amani.







WALENGWA WA TASAF WATAKIWA KUTUMIA FEDHA ZA TASAF KUJIENDELEZA KIMAISHA.

 

Mkurugenzi wa uratibu  wa shughuli za serikali ofisi ya makamu wa pili wa Rais, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Siajabu Suleiman Pandu akizumgumza na wanufaika wa mpango wa TASAF Manispaa ya Bukoba hawako pichani.

..........................................

Alodia Babara,

Bukoba.

WALENGWA wa mpango wa kunusuru kaya maskini nchini, TASAF wametakiwa kuzitumia fedha za mpango huo kama sehemu ya ukombozi, kuimarisha ndoa na familia zao kwa lengo la kuondoa umaskini.

Hayo yamesema Januari 31, mwaka huu 2024, na Mkurugenzi wa uratibu wa shughuli za serikali ofisi ya makamu wa pili wa Rais Zanzibar Siajabu Pandu wakati wadau mbalimbali wa mpango huo walipotembelea walengwa katika manispaa ya Bukoba mkoani Kagera kwa lengo la kukusanya maoni na changamoto zinazowakabili walengwa, ambazo baada ya kuzibaini zitawawezesha wadau hao kuboresha mpango unaofuata.

“Serikali tunaamini fedha hii iwe ni sehemu ya ukombozi, kwa hiyo ninawaomba muishi katika ndoa njema, familia nzuri ni sehemu ya ukombozi, fedha ni matokezeo tu sasa tuzitumie hizi fedha kuimarisha ndoa zetu, ndoa si chochote ni subira, tunapaswa kuvumiliana kuhakikisha kwamba tunaishi na watoto wetu kwa pamoja na familia zetu ili kuondoa hali hii ya umaskini” amesema Pandu

Katika ukusanyaji maoni na kusikiliza changamoto za walengwa wadau hao wamegundua kuwa, baadhi ya kaya za walengwa wametelekeza familia zao na kumuacha mzazi mmoja wapo, baba/mama, akiangalia majukumu ya kulea watoto peke yake.

Aidha baadhi ya walengwa wa mpango huo katika mtaa wa Kabale ka Ngaiza manispaa ya Bukoba wakati wakitoa hadithi zao mbele ya wadau hao imeonekana kuwa kuna baadhi ya walengwa ambao ni watoto walishindwa kuendelea katika mpango baada ya wazazi wawili mke na mme kutengana na hivyo watoto kuhamishwa eneo la mtaa husika bila kuwepo mawasiliano na mratibu wa mpango na hivyo kusababisha watoto kuondolewa katika mpango.

Esther Peter mkazi wa mtaa wa Kabale Ka Ngaiza mwenye wategemezi sita, watoto wake wanne na wadogo zake wawili amesema kuwa, yeye anakabiliwa na changamoto mbili mtaji wake kuwa mdogo tofauti na mahitaji yake pamoja na sehemu ya kuishi kwani anaishi kwenye nyumba za kupanga.

Amesema kutokana na changamoto za ndoa watoto waliingizwa kwenye mpango baadaye baba yao akawachukua kuishi nao eneo jingine na hivyo kutokana na kwamba hakuwa na mawasiliano naye watoto waliondolewa kwenye mpango na sasa baada ya kuanza kuishi nao tena anafanya utaratibu wa kuwarudisha kwenye mpango.

“Nashukuru mpango huu wa TASAF na namshukuru Rais wa nchi yetu mama Samia Suluhu Hassan mimi kabla sijaingia  katika mpango huu nilikuwa naishi kwa kuomba omba chakula na nguo kwa watu lakini baada ya kuingia kwenye mpango huu kwa sasa naweza kumudu chakula milo mitatu naweza kuvaa nguo nzuri na kuwanunulia wanangu pia na nimepata mtaji kidogo nafanya biashara ya kuuza samaki” amesema Peter

Amesema, kipindi hicho alikuwa na mdogo wake yuko kidato cha pili lakini kwa sasa amemaliza chuo cha maendeleo ya jamii ingawa bado hajapata ajira na mdogo wake yuko chuo kikuu anasomea sheria.

Aidha walengwa hao wameiomba serikali waendelee kuwa walengwa katika mpango wa kunusuru kaya maskini kwani wapo baadhi yao wamekumbwa na changamoto mbalimbali na hivyo kusababisha kutoinuka kiuchumi na kubaki wakiwa maskini.

Mwenyekiti wa mtaa wa Kabale ka Ngaiza Longino Goerge ametoa maombi kadhaa kwa wadau hao kuwa, ni pamoja na TASAF kuunda dawati la usuluhishi kwa wanandoa, kuwaingiza wazee kwenye mpango na kutoa ajira kwa vijana waliotokana na mpango.

Akijibu maswali ya mwenyekiti Kaimu mkurugenzi wa mifumo , mawasiliano na ufuatiliaji TASAF makao makuu Peter Lwanda amesema kuwa, wanaendelea kutengeneza mpango mwingine ambao utaendelea.

Kuhusu ajira ameeleza kuwa, TASAF ilikuwa inafuatilia wale wanaomaliza darasa la saba na kidato cha nne  ambao hawaendelei ofisi ya waziri mkuu inawapeleka vyuo vya ufundi na kuwa serikali bado inaangalia matatizo ya ajira na kuyafanyia kazi.

Lwanda akijibia swala la wazee kuingizwa kwenye mpango ameeleza kuwa, watalichukua na kulifanyia kazi mpango ujao.

Ikumbukwe kuwa mkoa wa Kagera una walengwa wa TASAF wapatao 80,563 ambapo tangu mpango ulipoanza mwaka 2015 hadi sasa zaidi ya shilingi bilioni 57.2 zimeishatolewa kwa walengwa hao.





Walengwa wa mpango wa kunusuru kaya masiki mtaa wa Kabale Ka Ngaiza