Wednesday, June 29, 2016

RAIS, DKT JOHN MAGUFULI AWAAPISHA WAKUU WA MIKOA WATATU.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli akizungumza na wakuu wa mikoa aliowaapisha leo na wakuu wa wilaya, ikulu jijini Dar es Salaam.




Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 29 Juni, 2016 amewaapisha wakuu wa Mikoa watatu aliowateua Jumapili iliyopita tarehe 26 Juni, 2016.

Wakuu wa Mikoa walioapishwa leo Ikulu Jijini Dar es salaam ni Dkt. Binilith Satano Mahenge ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Dkt. Charles Ogesa Mlingwa ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Mara na Bi. Zainab Rajab Telack ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.

Hafla ya kuapishwa kwa wakuu hao wa Mikoa imehudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama na wakuu wa wilaya wateule ambao waliteuliwa na Rais Magufuli Jumapili iliyopita tarehe 26 Juni, 2016.

Aidha, miongoni mwa wakuu wa wilaya 139 walioteuliwa, Rais Dkt. John Pombe Magufuli amefanya mabadiliko madogo katika wilaya tatu ambapo ametengua uteuzi wa Mkuu wa Wilaya ya Rombo Mteule Mhe. Fatma Hassan Toufiq na badala yake amemteua Bi. Agness Elias Hokororo kuwa Mkuu wa Wilaya hiyo, ametengua uteuzi wa Mkuu wa wilaya ya Serengeti Mteule Bw. Emile Yotham Ntakamulenga na badala yake amemteua Bw. Nurdin Hassan Babu kuwa Mkuu wa Wilaya hiyo na ametengua uteuzi wa Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mteule Bw. Fikiri Avias Said na badala yake amemteua Bw. Miraji Mtaturu kuwa Mkuu wa wilaya hiyo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewataka wakuu wa wilaya wateule kwenda kuchapa kazi na kutatua kero za wananchi katika wilaya zao huku wakizingatia kufanya kazi kwa uadilifu na uaminifu.

Rais Magufuli pia amewataka kusimamia ukusanyaji mapato ya serikali na matumizi ya fedha na rasilimali nyingine za umma, kuhakikisha wananchi wapo salama na pia kuhakikisha wananchi wanafanya kazi za uzalishaji mali.

"Katika kazi hizi wapo watakaowakejeli, katika kazi hizi wapo watakaowadhihaki, nyinyi kavumilieni na mmuweke Mungu mbele na mkawaweke watanzania mbele, mkafanye kazi kadiri Mungu atakavyokuwa amewaongoza.

"Nataka kuwahakikishia tunawaunga mkono kwa nguvu zote, mkafanye kazi bila uwoga wowote, katembeeni kifua mbele, kwa sababu tumewaamini wala msiwe na wasiwasi, ukifanya kitu kizuri kwa dhamira yako iliyo njema kitazaa matunda mazuri, ukifanya kitu kwa unafiki hakitafanikiwa" Amesema Rais Magufuli

Katika hafla hiyo, wakuu wa mikoa walioapishwa na wakuu wa wilaya wateule wamekula kiapo cha ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma, zoezi ambalo limeongozwa na Kamishna wa Maadili Jaji Mstaafu Salome Kaganda.

Katika hatua nyingine, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amekutana na kufanya Mazungumzo na mwenyekiti mwenza wa taasisi ya Bill and Melinda Gates ya Marekani Bi. Melinda Gates ambapo Rais Magufuli amemuhakikishia mwenyekiti mwenza huyo kuwa serikali ya awamu ya tano itaendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano wake na taasisi hiyo ambayo imekuwa ikishirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Afya, Uongozi na Kilimo.

Kwa upande wake Bi. Melinda Gate amempongeza Rais Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya katika kukabiliana na rushwa na kuongeza ukusanyaji wa mapato ya serikali, na pia kwa nia yake thabiti ya kuinua sekta ya kilimo inayotegemewa na idadi kubwa ya watanzania na ameahidi kuwa taasisi ya Bill and Melinda Gates itaendelea kushirikiana na Serikali ya awamu ya tano katika kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao ya kilimo.


Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
29 Juni, 2016 .

Tuesday, June 28, 2016

TASUBA, YAPATA MKURUGENZI MPYA.



Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) imepata mkurugenzi mtendaji mpya atakae ongoza chuo hicho kikongwe katika fani ya sanaa na utamaduni hapa nchini.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya Habari leo, juni 28, 2016, ilisema kuwa, waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape mnauye, amemteua  Dkt. Herbert  F. Makoye, kuwa Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa).

Uteuzi huo umefanywa chini ya kifungu namba  9. (1) cha sheria ya wakala wa serikali,  (Executive Agencies Act) iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2009 ambacho kinampa mamlaka waziri, ya kufanya uteuzi huo.

Dkt. Makoye anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Bw. Juma Bakari aliyestaafu kwa mujibu wa sheria ya Utumishi wa uma.

Dkt. Makoye ana shahada ya Uzamivu (PhD) kutoka chuo kikuu cha Ghana na shahada ya Umahiri- (M. A. in Theatre Arts) kutoka chuo kikuu cha Dar es Salaam.

Kabla ya uteuzi huo Dkt. Makoye alikuwa Mhadhiri mwandamizi wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam, idara ya sanaa na maonesho.

Uteuzi huo utaanza rasmi Tarehe 01/07/2016.                 

Monday, June 27, 2016

BUNGE LAPITISHA MUSWADA WA MAREKEBISHO YA SHERIA YA ELIMU.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. George Masaju akijibu hoja za Wabunge mapema leo June 27, 2016 Bungeni  Mjini Dodoma wakati akihitimisha hoja kuhusu muswaada wa sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali  wa mwaka 2016.



Bunge la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania leo, Mjini Dodoma limepitisha muswada wa marekebisho ya sheria ya Elimu kifungu kinachoeleza kuwa mtu anayempatia ujauzito mwanafunzi wa shule ya msingi au sekondari kuwa adhabu yake ni faini isiyozidi shilingi laki tano au kifungo kisichozidi  miaka mitatu.

“Muswada unapendekeza kuwa kifungu hicho kifutwe na badala yake kitungwe kifungu kipya cha 60A ili kuweka masharti yanayojitosheleza kuhusu zuio la kuoa au kumpatia ujauzito mwanafunzi wa shule ya msingi au sekondari, kinapendekeza adhabu yake iwe kifungo cha miaka 30 gerezani,” alifafanua Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. George Masaju.

Vile vile mtu atakayebainika kusaidia, kushawishi au kuacha mwanafunzi wa shule ya msingi au sekondari kuolewa au kuoa anatenda kosa la jinai ambalo adhabu yake ni faini isiyopungua shilingi milioni tano au kifungo cha miaka mitano gerezani au vyote kwa pamoja.

Mhe. Masaju aliendelea kwa kufafanua kuwa, sheria hiyo imependekeza kuwa pale ambapo kosa hilo litafanywa na mtoto basi adhabu yake itakuwa kwa mujibu wa masharti ya sheria ya motto,

Alifafanua kuwa, kwa sababu sheria ya mtoto inakataza mtoto anayetiwa hatiani kufungwa gerezani.

Aidha marekebisho hayo katika sheria ya Elimu yanalenga kumjengea mwanafunzi wa shule ya msingi au sekondari mazingira mazuri ya kumaliza ipasavyo elimu yake kwa ngazi hiyo.Hivyo basi kila Mkuu wa shule au Mwalimu Mkuu atawasilisha kwa Kamishna wa Elimu taarifa ya robo mwaka kuhusu matukio ya ndoa na mimba kwa wanafunzi katika shule yake na hatua zilizochukuliwa.

Sheria ya Elimu inamruhusu mwanafunzi aliyepewa ujauzito kuendelea na masomo mara tu anapojifungua. Sheria hiyo inasubiri kuwekwa saini na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli ili ianze kutumika.

MECHI YA TP MAZEMBE NA YANGA WASHIBIKI WOTE KUINGIA BURE UWANJANI.


Sunday, June 26, 2016

MAJID HEMED MWANGA, ABAKI BAGAMOYO.

Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Alhaji, Majid Hemed Mwanga.


Kufuatia uteuzi mpya alioufanya na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Maguful, Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Majid Hemed Mwanga, ameendelea kubaki wilayani Bagamoyo.
Katika uteuzi huo wakuu wa wilaya za mkoa wa Pwani ni hawa wafuatao

1.      Bagamoyo       -           Alhaji Majid Hemed Mwanga
2.      Mkuranga       -           Filberto H. Sanga
3.      Rufiji           -           Juma Abdallah Njwayo
4.      Mafia            -           Shaibu Ahamed Nunduma
5.      Kibaha           -           Asumpter Nsunju Mshama
6.      Kisarawe        -           Happyness Seneda William
7.      Kibiti            -           Gulamu Hussein Shaban Kifu


bagamoyokwanza.blogspot.com  inawatakia mafanikio mema katika majukumu yao wakuu wa wilaya wote walioteuliwa na Mh. Rais Dkt. John Magufuli wa mkoa wa Pwani na Tanzania kwa ujumla


MUNGU IBARIKI TANZANIA.