Wednesday, November 28, 2018

NAIBU WAZIRI WA NISHATI ASEMA HAJARIDHISHWA NA MKANDARASI WA REA III WILAYANI KILOLO


Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akizungumza na wananchi wa kijiji cha Uwominyi wilayani Kilolo mkoani Iringa juu ya mikakati ya serikali ya kutekeleza miradi mbalimbali ya umeme.
..............................

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amebainisha kutoridhishwa na namna Kampuni ya Mkandarasi Sengerema inavyotekeleza miradi ya REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Kwanza na kuitaka hadi ifikapo Desemba 15 kuwepo na mabadiliko ya kazi walizofanya katika Wilaya ya Kilolo.

Mgalu ametoa kauli hiyo akiwa kwenye ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme katika Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa.

Alisema Serikali ilishatoa maelekezo na walikubalina na wakandarasi kuhakikisha kila wiki wanawasha umeme katika vijiji 3 na kampuni ya Sengerema imepewa kazi ya kufikisha miundombinu ya umeme katika vijiji 145 Mkoa mzima na kwa Kilolo ni vijiji zaidi ya 40.

“Muda umebaki mchache wa kukamilisha miradi hii maana inatakiwa kumalizika Juni mwakani, huku tukiwa tunashuhudia uhitaji mkubwa wa nishati ya umeme ingawa wigo wa mkandarasi ni mdogo lakini katika mkataba mkandarasi anaweza kuchepusha kwa asilimia 15.

Alisema tayari wana taarifa ya baadhi ya vijiji na vitongoji ambavyo vimerukwa na sasa wanafanya uchambuzi baada ya kupokea taarifa kutoka mikoa yote na kuwa tatizo hilo litaanza kutatuliwa mapema mwakani baada ya kuanza kutekelezwa miradi ya Ujazilizi, kufikia miji inayokuwa kwa kasi.


Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akizungumza na wananchi wa kijiji cha Uwominyi wilayani Kilolo mkoani Iringa juu ya mikakati ya Serikali ya kutekeleza miradi mbalimbali ya umeme.


WAKUU WA MIKOA, WILAYA NA WAKURUGENZI SIMAMIENI UWAJIBIKAJI-MAJALIWA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Watumishi wa Halmashauri ya Mji wa Geita  kwenye ukumbi wa Halmashauri hiyo, Novemba 27, 2018. Kulia ni Mbunge wa Chato na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani na kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Geita,  Mhandisi Robert Gabriel. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
.................................


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwaamewaagiza Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini wahakikishe wanasimamia vizuri uwajibikaji na utowaji wa huduma kwa wananchi katika maeneo yao bila ya woga. 

Kadhalika, Waziri Mkuu amemtaka kila mtumishi wa umma nchini awajibike katika kufanya kazi kwa bidii na kwamba Serikali ya Awamu ya Tano haitowavumilia watumishi ambao ni wezi, wabadhilifu, wavivu  na haitosita kuwachukulia hatua.

Waziri Mkuu aliyasema hayo jana jioni (Jumanne, Novemba 27, 2018) alipozungumza na watumishi, viongozi wa mkoa, wilaya ya Geita na taasisi za umma katika mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa Mamlaka ya Mji Geita.

 “Watumishi fanyeni kazi kwa bidii na msitarajie kuundiwa tume pale mnapofanya vibaya, ukiharibu kazi tunakushughulikia hapo hapo na huu ndio msimamo wa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli.”

 Waziri Mkuu aliwaeleza watumishi hao kuwa wanatakiwa wafanye kazi kwa kuzingatia sheria na kanuni za kazi na pia watambue dhamana kubwa waliyonayo, ambayo ni kuwahudumia wananchi wote bila ya ubaguzi wa aina yoyote.

 Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewaagiza watumishi wa umma hususani Wakuu wa Idara wahakikishe wanakuwa na kitabu cha Ilani ya Uchanguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili wapate muelekeo wa utekelezaji washughuli zao.

 Waziri Mkuu amesema kitabu cha Ilani ya uchanguzi cha CCM 2015/2020 kina maelekezo ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ambayo kila idara inatakiwa kuangalia maelekezo yaliyotolewa kuhusu idara husika na kuyafanyia kazi.

 Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel alimuhakikishia Waziri Mkuu kwamba yeye kwa kushirikiana na viongozi wenzake watayafanyia kazi maelekezo yote ambayo ameyatoa.
Baadhi ya Watumishi wa Halmashauri ya Mji wa Geita wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  wakati alipozungumza nao kwenye ukumbi wa Halmashauri hiyo, Novemba 27, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Baadhi ya Watumishi wa Halmashauri ya Mji wa Geita wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  wakati alipozungumza nao kwenye ukumbi wa Halmashauri hiyo, Novemba 27, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

DC BAGAMOYO AGAWA SUKARI YA MAGENDO KWA SHULE, MAGEREZA NA VITUO VYA KULELEA WATOTO.

 Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, ambae pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wilaya, Zainabu Kawawa, akipokea Sukari kutoka kwa Afisa Mfawidhi wa Kituo cha Forodha Bandari ya Bagamoyo, Raymond Mwanisawa.
 
Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, ambae pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wilaya, Zainabu Kawawa, akizungumza mara baada ya kupokea sukari na kuikabidhi kwa wakuu wa shule za serikali.
.........................................

Serikali wilayani Bagamoyo imekamata sukari iliyoingizwa kwa njia ya magendo na kuigawa kwa shule za sekondari na msingi, Magereza na vituo vya kulelea watoto yatima na wale wa mazingira magumu.

Akizungumza wakati wa kupokea sukari na kuigawa kwa wakuu wa shule, Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, ambae pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wilaya, Zainabu Kawawa alisema wilaya ya Bagamoyo imejipanga kikamilifu kukomesha mianya yote ya kukwepa ushuru na kwamba kila anaejaribu kutumia Bandari bubu sheria itamshughulikia.

Alisema kuwa, Serikali inahitaji kukusanya mapato kupitia vyanzo vyake ili kuendesha mambo mbalimbli ya kimaendeleo katika jamii kwahiyo anaekwepa kodi na ushuru huyo ni mpinga maendeleo na serikali itamshughulikia.

Aidha, aliwataka wakuu wa shule kuitumia sukari hiyo kwa wananfunzi kama ilivyokusudiwa na wala si vinginevyo na kuonya kuwa, atakaetumia sukari kinyume na makusudio atamshughulikia.

Kwa upande wao walimu waliopokea sukari hiyo wamesema sukari hiyo itawasaidia kwenye matumizi ya shule kwa wananfunzi.

Wameahidi kuitumia kama ilivyokusudiwa na kwamba tayari wamejipanga kuweke udhibiti wa matumizi ili kusiwe na matumizi holela.

Awali, akizungumza wakati wa kumkabidhi sukari hiyo Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Afisa Mfawidhi wa Kituo cha Forodha Bandari ya Bagamoyo, Raymond Mwanisawa, amesema wamemkabidhi Mkuu wa wilaya sukari hiyo ili agawe kwenye taasisi zenye uhitaji zikiwemo shule vituo vya kulelea watoto.

Mwanisawa alisema Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kwa bidhaa kama hizo zilizokwepa ushuru, Kamishna wa forodha na kodi ya bidhaa nchini anatoa kibali cha kugawa bidhaa hizo ili zisije kuharibika pale zilipohifadhiwa.

Alisema sukari hiyo imekamatwa kufuatia doria iliyofanywa na maafisa wa forodha kwa kushirikiana na jeshi la polisi katika kuhakikisha bidhaa zote zinazoingizwa Bagamoyo zinalipiwa ushuru halali wa serikali.

Jumla mifuko 220 ya sukari ambayo kila mmoja ukiwa na kilo 50 amekabidhiwa Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo ili kuzigawa kwa taasisi zenye uhitaji.

Sukari ikishushwa kwenye Gari na kukabidhiwa wakuu wa shule kwaajili ya shule zao.
  
Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, ambae pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wilaya, Zainabu Kawawa, akikabidhi sukari kwa shule ya Sekondari Bagamoyo.

 
Picha ya juu na chini ni Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, ambae pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wilaya, Zainabu Kawawa, akiwa katika picha ya pamoja na watoto wa mazingira magumu wanalelewa katika kituo cha MOYO MMOJA, Bagamoyo mjini.

ATUHUMIWA KUTUMIA JINA LA KIKWETE KUKWEPA KODI.


Na Shushu Joel,Chalinze.
MFANYABIASHARA mmoja mkazi wa jiji la Dar es Salaam Innocent Kimaro ambaye anajihusisha na uuzaji wa madini ya mawe aina ya Dolomite ambayo hutumika  viwandani kwa ajili ya kutengenezea Vigae katika wilaya ya Bagamoyo Halmashauri ya chalinze mkoani Pwani anatuhumiwa kutumia jina la mbunge wa jimbo hilo Ridhiwani Kikwete kwa ajili ya kukwepa kulipa kodi na kupitisha mizigo yake bure kwa kuwatishia wahusika wa kulipisha ushuru.

Akizungumza na waandishi wa habari mwenyekiti wa kijiji cha msoga Ramadhani Mrisho ambapo mawe hayo yanachimbwa  alisema kuwa mfanyabiashara huyo anayejulikana kwa jina la Innocenty Kimaro amekuwa akikataa kulipa kodi pindi anapopitisha mizigo yake kwenye mageti  kwa kudai kuwa yeye ni mtu wa karibu na mbunge wa jimbo hilo (Ridhiwani Kikwete) hivyo si sahihi yeye kulipa kodi kwenye eneo hilo.

Aliongeza kuwa magari yake yanaposimamishwa kwenye mageti ili aweze kulipa ushuru madereva wake wamekuwa wakikaidi kusimama kwa ajili ya ukaguzi wa malipo ya halmashauri ya chalinze na hivyo kusababisha hasara kubwa kutokana na kutolipa ushuru huo.

Aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo ya magari hayo kushamili kwa kupita kwenye sehemu za kulipia ushuru bila kulipa niliwashauri wale vijana wanaokatisha ushuru waende wakaombe msaada kwa matrafiki ili gari hizo ziweze kusimamishwa kwa lengo la kujua kama kwamba wanalipa ushuru kijiji cha msolwa ambako ndiko mawe hayo yanachimbwa na mfanyabiashara huyo.

“Mara baada ya kuomba msaada wa matrafiki kuzisimamisha gari hizo na kisha madereva kuulizwa ni kwanini awasimami getini walimpigia simu boss wao ambaye ni Innocent Kimaro na kufika kwenye eneo la tukio na kuweza kulipa ushuru huo huku akiwaambia hata mizigo ya Kikwete nayo inalipishwa ushuru”

Aidha mwenyekiti huyo aliongeza  kuwa mfanyabiashara huyo amekuwa akitumia jina la Ridhiwani Kikwete kwa madai ya kuwa hata mbunge wenu mnamtoza kodi huku wawekezaji amewaleta yeye kitu ambacho kinatufanya kujiuliza maswali mengi juu ya jambo hilo,kwani mbunge hajawai kuwa na biashara na asilipe kodi.

“Mara kwa mara tumekuwa tukiyasimamisha magari yake kwenye ili aweze kulipa ushuru wa maeneo ambayo anachimba madini hayo lakini mtu huyo amekuwa akikaidi na magari yake kuendelea na safari zake” Alisema Mrisho Mwenyeki wa kijiji cha msoga.

Mwandishi wa habari hizi alimtafuta mfanyabiashara huyo ili kujibu tuhuma hizo ambae alizungumza kwa njia ya simu na kusema kuwa yeye analipa kila kitu na wala hajawai kutumia jina la mtu ili kukwepa kodi. 

Akizunguza juu ya kutumiwa kwa jina lake mbunge wa chalinze Ridhiwani Kikwete alisema kuwa amesononeshwa na taarifa hizo kwa baadhi ya watu kutumia jina lake kwa ajili ya kuibia mapato serikali na hivyo ameshauri mtu huyo atafutwe ili aweze kupigiwa hesabu ili aweze kulipa madeni yote anayodaiwa.

Aliongeza kuwa simjui wala sina biashara ya mawe na hata kama ningekuwa nayo ni lazima hata mimi ningelipa ushuru ili kuliongezea pato taofa langu.

Aidha mbunge huyo alisema kuwa mpaka kipindi hiki anafanya mazungumza na wamiliki wa kiwanda ambacho mkwepa ushuru huyo anapeleka madini hayo kwa lengo la kujua amepeleka mara ngapi ili gari hizo zipigiwe hesabu yake kwa lengo la kulipa kodi za nyuma ambazo alipitisha bila kulipa ushuru wa halmashauri.

Kutokana na hali hiyo Ridhiwani Kikwete amesema kuwa hatawafumbia macho wale wote wenye lengo la kutaka kumchafulia taswira yake aliyonayo katika jamii.


MAGAZETI YA LEO NOVEMBA 28, 2018

NAIBU WAZIRI KILIMO MGUMBA ATOA ONYO KALI KWA MADALALI

Naibu waziri Omary Mgumba akiongea na wakulima wa kijiji cha ngulwe

Naibu Waziri Mgumba akikagua maghara ya kuhifadhia mbolea mkoani Iringa
........................................

Naibu waziri wa Kilimo Omari Mgumba Ametoa Onyo Kali Kwa Madalali Wanaowauzia Wakulima Wa Mazao Ya Chakula Na Biashara Mbolea Kwa Bei Ya Shilingi Elfu sabini, 70,000 Badala Ya Kufuata Bei Elekezi Ya Serikali Ya shilingi elfu sitini na nne na mia saba, 64,700  Kwa Mfuko Moja.

Akiwa Katika Ziara Mkoani Iringa Ya Ukaguzi Wa Upatikanaji Wa Mbolea Kwenye Maghara Ya Serikali Na Wawekezaji Mkoani Hapa
Naibu Omar Amewataka Madalali Hao Kuacha Mara Moja Tabia Hiyo Kwasababu Serikali Ya Awamu Ya Tano Chini Ya Rais Magufuli Aina Utani katika Kuwasaidia Watu Masikini Na Wangonge.

Onyo ilo limetolewa Baada Ya Wananchi Wa kijiji Cha Ngulwe Wilayani Kilolo Kutoa Malalamiko Yao Wakati Wa Kikao Kilichowahusisha Wakulima Na Waziri Mgumba.

“Ndugu wananchi Nimeskia Malalamiko Yenu Kuhusu Bei Ya Mbolea, Nataka Nitoe Rai Kwa Wauzaji Wa Mbolea Nchi Nzima Atakauza Mbolea Kwa Bei Tofauti Na Ile Elekezi Iliyopangwa Na Serikali Tutamchukulia Hatua Za Kisheria” Alisema Naibu Waziri Mgumba.

Aidha Naibu Waziri Aliwatoa Wasiwasi Wakulima Wote Nchini Kuhusu Upatikaji Wa Mbolea Na Pemebejio Katika Kipindi Ichi Kuelekea Msimu Wa Kilimo Serikali Imejizatiti Kikamilifu Na Mbolea Ipo Ya Kutosha Na Inauzwa Kwa Bei Elekezi Iliyotolewa Na Serikali.

Wakulima Wengi Nchini Wamekuwa Katika Changamoto Ya Upatikanaji Wa Mbolea Ambapo Hapo Awali Kulikuwa Na Waangizaji Zaidi Ya mmoja Hali Iliyopelekea Usumbufu Kwa Wakulima Na Bei Kuwa Kubwa
Jambo Lilifanya Ambalo Serikali kuingilia Kati Kwa Kuweka Wakala Maalum Wa Kuagiza Mbolea Kutoka Njee Ya Nchi Na Kutoa Bei Elekezi Kwa Wauzaji.

Msimu Wa Kilimo Unatarajia Kuanza Hivi Karibu Kutegemea Unyeshaji Wa Mvua za Masika Nchini Ambapo Mikoa Ya Nyanda Za juu Kusini Ndio Inategemewa Kwa Uzalishaji Wa Kiwango Kikubwa Cha Mazao Ya Biashara Na Chakula

Tuesday, November 27, 2018

WAZIRI JENISTA ATOA SOMO KWA WATAALAM WA MAENDELEO YA JAMII

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na wataalam wa Maendeleo ya Jamii kutoka Taasisi za serikali Sekta Binafsi, Mashirika yasiyo ya Kiserikali  waliojumuika katika uzinduzi wa Kongamano la Wataalam wa Maendeleo ya Jamii linaloendela Mkoani Arusha.
...............................


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Mhe. Jenista Mhagama amewapa somo Wataalam wa Maendeleo ya Jamii nchini kuwa mfano katika kuanzisha viwanda vidogo vidogo na kuwapa mwanga wananchi kuona mfano na kuiga na kuanzisha viwanda vidogo vidogo vitakavyowezesha kufikia azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kufikia Uchumi wa Kati ifikapo mwaka 2025.

Ameyasema hayo leo mkoani Arusha  alipokuwa akizindua Kongamano la Mwaka liliwakutanisha Wataalam wa Maendeleo kutoka Wizara husika, Taasisi za Serikali, Sekretarieti za Mikoa, Halmashauri, Sekta Binafsi na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali.

Waziri Jenista amesema kuwa katika maendeleo ya nchi yoyote Wataalam wa Maendeleo ya Jamii ni watu muhimu katika kuamsha ari ya wananchi katika kujiletea maendeleo yao na taifa kwa ujumla katika kulueta uchechembuzi katika utekelezaji wa miradi ya kimaendeleo katika maeneo yao.

Ameongeza kuwa Serikali imeweka mazingira wezeshi katika kuwawezesha wananchi kuchumi na kusema kuwa katika Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kuna jumla ya mifuko.. inayotoa mikopo kwa waananchi ili kujikwamua kiuchumi kwa kufanya biashara na kauanzisha viwanda vidogo vidogo katika maeneno yao na kuwataka Wataalam wa Maendeleo ya Jamii kuchukua mikopo hiyo na kuanzisha viwanda vidogo vidogo ili kuwa mfano kwa jamii.

“ Nataka mkutano wa mwaka 2019 kusiwe na mabanda ya maonesho tu bali kuwe na viwanda vidogo vidogo 350 zaidi katika maeneo mnayotoka ili tuiishi kauli mbiu ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kufikia Uchumi wa Kati na wa Viwanda ifikapo mwaka 2025” alisisitiza Mhe. Jenista

Aidha amempongeza Katibu Mkuu Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu kwa kusimamia Sekta ya Maendeleo ya Jamii kwa ukaribu zaidi kwani ana uzoefu katika Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kwa muda aliokuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza hilo hivyo kama atatumia uzoefu huo ataipeleka Sekta ya Maendeleo ya Jamii mbele ili iweze kuwezesha wananchi kujikwamua kiuchumi hasa wananchi waliopo vijijini.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu amesema lengo la Kongamano la Wataalam wa Maendeleo ya Jamii ni kuwakutanisha Wataalam hao kujadiliana mambo mablimbali yahusuyo Taaluma hiyo ili kuja na njia na mbinu mpya za kuiwezesha Taaluma hiyo kuendelea kuwa chachu ya mabadiliko ya kiuchumi kwa wananchi na Taifa la Tanzania kwa ujumla.

“Mhe. Mgeni rasmi Kongamano ni muhimu sana kwa ajili ya uhai wa Taalaum ya Maendeleo ya Jamii ambayo ni Njini ya Maendeleo yoyote”alisisitiza Dkt. Jingu

Naye Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mhe. Jerry Muro amesema kuwa Maafisa na Wataalam wa Maendeleo ya Jamii ni nguzi muhimu katika maendeleo na anashangaa kwanini mpaka sasa bado tupo nyuma katika taifa kwani kuna baadhi ya watu bado wanajivuta katika kujiletea maendeleo katika maeneo yao.

“Mwalimu Nyerere alisema Maendeleo yanahitaji Siasa safi  tunayo,  Ardhi tunayo, Watu tuano,na Uongozi bora tuonao chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Joseph Magufuli na kwanini mpaka sasa tuko nyuma” alisisitiza Mhe. Muro.

Pia Rais wa Mpito wa Chama cha Maendeleo ya Jamii (CODEPATA) Bw. Sunday Wambura amemuahidi mgeni rasmi kuyatekeleza yale yote ambayo amewaagiza na kuhakikisha wanatumia fursa zilizopo katika kuiwezesha jamii kuamka na kuanza kuona umuhimu wa kushiriki katika  shughuli za maendeleo yao wenyewe.

Kongamano la Wataalam wa Maendeleo Jamii kwa mwaka 2018 lina kauli Mbiu inayosema “ Wataalam wa Maendeleo ya Jamii  ni chachu katika kufikia Uchumi wa Kati 2025” na linafanyika kwa siku nne mfululizo Mkoani Arusha.

 

MHE HASUNGA ATAKA MBOLEA IWAFIKIE WAKULIMA KWA WAKATI


Waziri wa kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akizungumza jambo wakati alipotembelea kampuni ya utengenezaji na usambazaji wa Mbolea
ya Yara Tanzania Ltd ambayo kwa nchini Tanzania Makao makuu yake yapo Jijini Dar es salaam, Leo tarehe 27 Novemba 2018. (Picha zote Na Mathias Canal-Wizara ya Kilimo)
....................................................

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dar es salaam

Waziri wa kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) amewataka
wafanyabiashara kusambaza mbolea haraka iwezekanavyo ili ziwafikie kwa wakati wakulima kwani msimu wa kilimo umeanza.

Mhe Hasunga ameyasema hayo tarehe 27 Novemba 2018 wakati
alipotembelea kampuni ya utengenezaji na usambazaji wa Mbolea ya Yara Tanzania Ltd ambayo kwa nchini Tanzania Makao makuu yake yapo Jijini Dar es salaam.

Waziri Hasunga ametoa wito kwa Taasisi zinazohusika na
upakuaji wa mizigo bandarini kufanya kazi ya upakuaji kwa haraka ili mbolea ziwafikie wakulima kwani msimu wa kilimo tayari umeanza.

Alisema kuwa sio jambo jema mbolea inayotakiwa kuwa
mashambani kwa wakulima katika msimu huu wa kilimo kuendelea kukaa bandarini kwani kwa zaidi ya wiki moja.

“Kadri mbolea inavyochelewa kuwafikia wakulima
itasababisha kuongezeka kwa gharama zisizo na tija kwani atakayeumia ni mkulima jambo hili halipaswi kutazamwa kama jambo la kawaida badala yake wahusika wote watekeleze majukumu yao ipasavyo” Alikaririwa Mhe Hasunga na kuongeza kuwa

“Wakulima wengi vijijini hawajui mambo ya kukaa muda
mrefu kwa mbolea bandarini wao wanachokijua serikali inatakiwa kuwapatia mbolea msimu wa kilimo unapofika, na mbolea inahitajika haraka kwani kilimo cha Tumbaku kinaendelea na tayari malalamiko yameanza”

Pamoja na mambo mengine Mhe Hasunga ameipongeza
kampuni hiyo ya mbolea ya Yara Tanzania Ltd, ambayo imewekeza katika maabara ya kupima udongo ili kuweza kutambua virutubisho vilivyopo na vinavyokosekana kwenye udogo. 

Meneja wa kampuni hiyo nchini Tanzania na Rwanda Bw
William Ngeno, alisema “lengo kuu la kampuni ya Yara Tanzania kuweka
maabara ya udongo, ni kuweza kuwapa wateja wao huduma nzuri na mpangilio sahihi wa lishe bora na linganifu ya mimea”

Alisema mara baada ya matokeo ya udongo kampuni
hiyo kupitia wataalamu wake hutoa ushauri kwa wakulima nini cha kufanya kulingana na zao lililolimwa au linalotarajiwa kulimwa. 
Aidha, alimpongeza Waziri huyo wa Kilimo kwa kutembelea kampuni hiyo kujionea hali ya utendaji kazi.

Mbolea za YARA zimegawanyika katika makundi
makuu matano Yara Mila:  Kundi hili lina aina za mbolea zenye
madini makubwa matatu NPK  (Nitrogen, Phosphorus, Potassium), Yara
Liva:  
Kundi hili lina aina za mbolea zenye asili ya Calcium
Nitrate 
ambazo ni kama vile Nitrabor, Tropicoti na
Calicinite, Yara Bela:  Kundi hili ni Kundi lenye mbolea zenye
asili ya Ammonium Sulphate Nitrate, zina Nitrojen na Sulphur ambazo ni Sulfan,

Yara Vita:  Kundi hili ni la mbolea zile zenye madini
yanayohitajika kwa kiwango kidogo na mmea (MicroNutrients) lakini muhimu katika ukuaji wa mmea sambamba na Yara Vera:  Kundi la tano ni mbolea za UREA.

Waziri wa kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akikagua kiwanda cha kampuni ya utengenezaji na usambazaji wa Mbolea ya Yara Tanzania Ltd ambayo kwa nchini Tanzania Makao makuu yake yapo Jijini Dar es salaam, Leo tarehe 27 Novemba 2018.

Waziri wa kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akiagana na Meneja wa Kasmpuni ya utengenezaji na usambazaji wa Mbolea ya Yara Tanzania Ltd Bw William Ngeno wakati wa ziara yake ya kikazi Leo tarehe 27 Novemba 2018 Jijini Dar es salaam

NAIBU WAZIRI OMARI MGUMBA AFANYA MAZOEZI NA KUHIMIZA JAMII KUFANYA MAZOEZI KUTUNZA AFYA.

Naibu waziri wa Kilimo, Mhe Omary Mgumba pichani  akiwa Mazoezini Mkoani Morogoro kwenye Milima ya Uluguru na Kwenye uwanja mdogo wa Mpira wa Miguu katika kutunza Afya pamoja na maandalizi ya Morogoro Marathon itakayofanyika Mkoani humo tarehe 02/12/2018.

Naibu waziri huyo ambae ni Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki anafanya mazoezi hayo ikiwa ni Maandalizi ya Kuwakilisha nchi kwenye Mashindano ya Mabunge ya Afrika Mashariki nchi Burundi siku za Mbeleni, kutokana na nafasi yake ya nahodha msaidizi wa timu ya mpira wa miguu ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Ndugai Boys).

Aidha, ametoa wito kwa watanzania kuendelea kuitikia wito wa Mhe Makamu wa raisi Mama Samia Suluhu Hassani Kufanya Mazoezi kutunza afya zetu.
 
 Naibu waziri wa Kilimo, Mhe Omary Mgumba pichani  akiwa Mazoezini Mkoani Morogoro kwenye Milima ya Uluguru na Kwenye uwanja mdogo wa Mpira wa Miguu katika kutunza Afya pamoja na maandalizi ya Morogoro Marathon itakayofanyika Mkoani humo tarehe 02/12/2018.
  
Naibu waziri wa Kilimo, Mhe Omary Mgumba pichani  akiwa Mazoezini Mkoani Morogoro kwenye Milima ya Uluguru na Kwenye uwanja mdogo wa Mpira wa Miguu katika kutunza Afya pamoja na maandalizi ya Morogoro Marathon itakayofanyika Mkoani humo tarehe 02/12/2018.

MAGAZETI YA LEO NOVEMBA 26, 2018.