Friday, August 16, 2024
MPANGO WA IMASA WATUA LINDI, BILIONI 3.6 ZATENGWA.
Thursday, August 15, 2024
OMBI LA WAKILI WA UTETEZI KESI YA WANANDOA KUJERUHI LAGONGA MWAMBA MAHAKAMANI
................................................
Na Mwandishi Wetu
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imekataa ombi la wanandoa Bharat Nathwan (57) na Sangita Bharat (54) la kutaka shahidi Kiran Ratilal awasilishe kipande kifupi cha video (clip) kinachoonesha alivyotumbukizwa kwenye ndoo ya mchanganyiko wa saruji.
Nathwan na Sangita Bharat (54) wanaoishi Mtaa wa Mrima - Kisutu, jengo la Lohana Dar es Salaam wanatuhumiwa kwa mashtaka manne likiwemo la kujeruhi waliyoyatenda Julai 21,2023 kinyume cha sheria.
Ombi hilo liliwasilishwa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya na Wakili wa Utetezi Edward Chuwa kwa niaba ya wateja wake, wakati Kiran Lalit Ratilal alipokuwa akiulizwa maswali ya dodoso kutokana na ushahidi wake aliyoutoa dhidi ya washtakiwa hao.
Wakili Chuwa alimuuliza Kiran Lalit Ratilal ambae ni shahidi wa nne katika kesi hiyo, kama ni kweli kwenye ushahidi wake alidai kuwa anayo clip inayoonesha alivyotumbukizwa kwenye ndoo hiyo na upo tayari kuitoa, alidai ni kweli anayo, lakini kwa wakati huo hana.
"Kwa hiyo umeomba kuitoa mahakamani kama kielelezo kutokana na maelezo yako uliyoyatoa,"alidai Wakili Chuwa
Baada ya Chuwa kudai hivyo, Hakimu Lyamuya alimueleza kuwa shahidi hakuomba kutoa kipande hicho, lakini Wakili Chuwa aliendelea kudai kuwa wanataka itolewe kama ushahidi.
Hata hivyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Faraji Nguka alidai kuwa wao hawako tayari kutoa kielelezo hicho, lakini kama Chuwa anataka kufanya hivyo wanaweza kukitoa wao katika utetezi wao kwa kufuata utaratibu.
Wakili Chuwa alidai kuwa kama kuna hatua za kufuata yeye hazikumbuki, ndipo Hakimu Lyamuya aliwaeleza kuwa kuna taratibu za kisheria shahidi kutoa kielelezo wakati wa kipindi cha maswali ya dodoso zinatakiwa zifuatwe.
"Mahakama ya Rufaa katika uamuzi wake katika shauri la Lilian na Jesus ya mwaka 2018 ilitoa utaratibu, kwa hiyo Chuwa kama ulitaka kufanya hivyo ulitakiwa kufuata taratibu kwenye hiyo rufaa imeonesha hatua kwa hatua,"
"Ombi hili linakuja randomly, ombi hili limekataliwa,"alisema Hakimu Lyamuya
Baada ya Hakimu Lyamuya kusema hivyo, Wakili Chuwa alidai kuwa wamemaliza maswali ya dodoso kwa shahidi.
Wakili Nguka alimuuliza shahidi baadhi ya maswali ( Re-examination) kwa ajili ya kutoa ufafanuzi kwa mahakama, alidai upande wa utetezi ulimuuliza sana uhusiano wa mume wake na Hospitali ya Regency, akadai kuwa mume wake sio daktari ni Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo.
Wakili huyo, aliiomba mahakama iwapangie tarehe ya karibu ili walete mashahidi wengine katika kesi hiyo na kudai kuwa wapo tayari kuendelea hata leo.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 30, 2024 saa tatu asubuhi kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji kwa mashahidi wa upande wa mashtaka.
Wednesday, August 14, 2024
MKUTANO WA MICO HALAL WAIBUA MAMBO KUHUSU UMUHIMU WA BIDHAA ZA HALAL
Friday, August 9, 2024
MADAKTARI BINGWA KUTOKA INDIA KUFANYA UPASUAJI WA MAGOTI NA NYONGA DAR ES SALAAM.
GLOBAL EDUCATION LINK YATOA VISA 100 KWA WANAOKWENDA KUSOMA NJE YA NCHI
Na Mwandishi Wetu
WAKALA wa Elimu Nje ya Nchi, Global Education Link (GEL), imetoa Visa 100 kwa kundi la kwanza la wanafunzi wanaotarajia kuanza kwenda kwenye vyuo vikuu mbalimbali nje ya nchi kuanza masomo hayo kuanzia wiki ijayo.
Hiyo inakuja ikiwa zimepita wiki mbili tu tangu matokeo ya kidato cha sita kutoka ambapo mamia ya wanafunzi wa Tanzania wenye kuhitaji kusoma nje ya nchi kupitia GEL wameshaanza kufanya maandalizi ya kuondoka kuanzia wiki ijayo.
Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi wa Global Education Link Abdulmalik Mollel, wakati akigawa Visa 100 kwa wanafunzi wanaotarajiwa kuondoka wiki ijayo na amezungumza na wazazi na wanafunzi wanaotarajiwa kwenda nchini humo.
Mollel alisema lengo la mkutano huo ni kukabidhi Visa, kujadili na wazazi na wanafunzi kuhusu mambo mengi ya kuzingatia katika maandalizi ya safari yao, kuwakutanisha wazazi na wanafunzi na wawakilishi wa vyuo vikuu ambavyo wanafunzi hao wanatarajia kwenda kusoma pamoja na wanafunzi kujaza nyaraka mbalimbali.
“Leo tumekutana na wanafunzi hawa kuwapa viza zao ambazo zimekamilika kuwapa bima za afya kuwaeleza tarehe za kusafiri ndege watakazotumia kusafiria, kujua sehemu watakazokaa, watasafiri na nani na watapokelewa na nani,” alisema Mollel
“Wataanza kuondoka kwenda kwenye vyuo vikuu mbalimbali duniani kuanzia wiki ijayo na baada ya hapo kila wiki kundi la wanafunzi kuanzia 50 mpaka 70 watakuwa wanaondoka kwenda mataifa mbalimbali,” alisema Mollel.
Mollel aliwataka wanafunzi kuzingatia walichofuata nje ya nchi na kuachana na starehe na badala yake wazingatie masomo na kuhakikisha wanahitimu wakiwa na alama nzuri ili kuwapa moyo wazazi ambao wamejinyima kwaajili yao kuwalipia ada.
Alisema baadhi ya wanafunzi wamekuwa na kawaida ya kufanya mambo ambayo yanasababisha washindwe kumalizia masomo yao hali ambayo inawakatisha tamaa wazazi wao.
“Msiende kunywa pombe wala kwenda klabu za usiku kwasababu kule mnakwenda kufuata elimu. Malizeni masomo mpate kilichowapeleka starehe hata Tanzania zipo,” alisema Mollel
Aiman Mohamed kutoka Mwanza ambaye anatarajia kwenda masomoni nchini India wiki ijayo, alisema anashukuru uratibu uliofanywa na Global Education Link na kumwezesha kupata chuo cha Sharda cha nchini India.
“Kwa dhati kabisa niwapongeza waratibu wa safari yetu Mollel na wenzake kwa namna walivyokuwa karibu nasisi wakati wote wa kuratibu safari na hatimaye mambo yamekuwa mazuri na wiki ijayo tunasafiri kwenda masomoni kutimiza ndoto zetu,” alisema
Rita Nichalaus naye kutoka Mwanza ambaye anatarajia kujiunga na chuo kikuu cha Sharda kilichoko New Delhi India alisema amefurahi kupata elimu ya mambo ambayo wanatakiwa kufanya na ambayo hawatakiwi kuyafanya wanapokuwa masomoni.
“Mwongozo tuliopewa ni muhimu sana kwasababu mwanafunzi anapofika ugenini asipofahamu tabia na tamaduni za wenyeji anaweza kujikuta yuko matatizoni lakini tumeelezwa namna ya kuishi tukiwa huko ni jambo jema na la msingi sana kwetu,” alisema
Tuesday, August 6, 2024
KESI YA WANANDOA KUJERUHI, WAKILI WA SERIKALI AKATAA KESI KUAHIRISHWA.
Bharat Nathwani mbele na mke wake Sangita Nathwani nyuma kabisa wakiingia katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es salaam jana kusikiliza kesi inayowakabili ya kumjeruhi jirani yao inayowakabili.
....................................
Na Mwandishi Wetu
UPANDE wa Jamhuri katika kesi ya kujeruhi inayowakabili wanandoa Bharat Nathwan (57) na Sangita Bharat (54) wamekataa kuahirishwa kesi kwa madai kuwa wakili wa utetezi anataka kuchelewesha kesi hiyo kwa kudai kuwa anashida ya kiafya.
Aidha, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam iliomba pande zote mbili katika kesi hiyo kutumia lugha za kuheshimiana ndani ya chumba cha mahakama kwa sababu kuna watu wanajifunza kutoka kwao.
Ombi hilo la kukataa, liliwasilishwa jana Wakili wa Serikali Mwandamizi, Grace Mwanga mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya wa mahakama hiyo, wakati shahidi Kiran Ratilal akiulizwa maswali ya dodoso na Wakili wa Utetezi, Edward Chuwa.
Mwanga alifikia hatua hiyo, baada ya Wakili Chuwa kuomba ahirisho la maswali ya dodoso kwa shahidi Ratilal, kwa madai kuwa hawezi kuendelea kwa sababu ya afya yake na pia kuna dawa za kutumia.
Baada ya Chuwa kudai hayo, Mwanga alidai kuwa hawawezi kukubali ahirisho kwa sababu, wakili huyo alitakiwa kulisema hilo mapema kabla kesi haijaanza kusikilizwa kuwa ikifika muda fulani waahirishe.
"Jamhuri hatuwezi kukubali, wakili alitakiwa kulisema hili mapema anachokifanya ni kutaka kuchelewesha kesi hatuwezi kukubali kuahirisha tunaomba amalize maswali ya dodoso kwa shahidi,"
" Mara ya mwisho alisema anaenda Mahakama Kuu, lakini alivyotoka nje alikuwa anazungumza na vyombo vya habari na pia hakusema anaenda kwenye kesi gani,"alidai Wakili Mwanga
Hata hivyo, Chuwa alidai kuwa siku hiyo hakusema anakwenda Mahakama Kuu, alidai kuna kazi anakwenda kuifanya na pia alikuwa akizungumza na media saa ngapi?
"Naenda kuonana na daktari katika Hospitali Hindul Mandal na siku ya kesi ninaweza kuja na ushahidi hapa mimi nina umri wa miaka 60, nimeomba ahirisho kwa sababu ya ugonjwa,"alidai Wakili Chuwa
Hakimu Lyamuya alisema yeye hayuko kwenye nafasi ya kusema kama Wakili ni mgonjwa au sio mgonjwa kwani hali hiyo ni vile ambavyo mtu mwenyewe anajisikia.
"Kwa sababu umesisitiza kwa umri wako wa miaka 60, mahakama inaahirisha kesi hii kwa nafasi ya mwisho ya kufanya maswali ya dodoso ni haki yako, lakini siku ya kesi itakayotajwa inatakiwa ifike mwisho tusiipeleke hii kesi mbali sana,"alisema Hakimu Lyamuya
Pia, Hakimu Lyamuya aliwataka watumie lugha ya kuheshimiana pale wanapouliza maswali kwa sababu ni watu wengi wanasikiliza, lakini pia kuna wanafunzi washeria ambao wanajifunza kila kitu kutoka kwao.
Hakimu Lyamuya alifikia hatua hiyo, baada ya Wakili Chuwa kumtuhumu Wakili Mwanga kuwa anamsaidia shahidi, baada ya kupinga shahidi wake kuulizwa swali ambalo tayari alishalijibu.
"Mheshimiwa mimi sijamsaidia shahidi kujibu swali bali ninepinga shahidi kuulizwa swali hilohilo ambalo tayari alishalijibu,"alidai Mwanga
Kesi imeahirishwa hadi Agosti 15,2024 kwa ajili ya upande wa utetezi kuendelea kumuuliza masawali ya dodoso shahidi.
Nathwan pamoja na mke wake Sangita Bharat (54) wanaoishi Mtaa wa Mrima - Kisutu, jengo la Lohana Dar es Salaam
wanatuhumiwa kwa mashtaka manne likiwemo la kujeruhi waliyoyatenda Julai 21,2023 kinyume cha sheria.
RAIS SAMIA AACHA ALAMA YA KIPEKEE MOROGORO.
Maelfu wanufaika na msaada wa kisheria
Wamshukuru na kutaka huduma ziwe endelevu
Na Mwandishi Wetu
RAIS Samia Suluhu Hassan amehitimisha ziara yake ya siku sita mkoani Morogoro huku akiacha alama kubwa kwa uzinduzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo na timu ya wanasheria waliosaidia kutoa msaada wa sheria bure kwa maelfu ya wananchi.
Wananchi wengi walifurahia msaada wa kisheria walioupata kutoka kwa wanasheria wa mpango wa mnsaada wa sheria wa Mama Samia Legal Aid ambao bado wanaendelea kutoa msaada kwenye viwanja vya nane nane mkoani hapa.
Kulikuwa na timu ya wanasheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria waliokuwa wakisikiliza kero za kisheria kwenye ziara hiyo na kuzitatua na kulikuwa na timu ingine ya Rais Samia ambayo inaendelea kutoa huduma hiyo katika maonyesho ya nane nane yanayoendelea mkoani Morogoro.
Baadhi ya wananchi wametoa ushuhuda wa namna walivyonufaika na ziara ya Rais Samia kwa huduma za msaada wa kisheria walizopata kwenye ziara hiyo.
Mmoja wa wananchi waliopata msaada wa kisheria kutoka kwa Mama Samia Legal Aid anasema amefurahia mpango huo kwani umekuw mkombozi kwa watu ambao hawana uwezo wa kuweka mawakili.
“Mpango wa Mama Samia imekuwa msaada mkubwa kwa wananchi napendekeza kama itampendeza Rais Samia hii isiwe tu kampeni maana kampeni inaisha muda ila ikiwa Taasisi ya kudumu itawasaidia sana wananchi wanyonge ambao wanapambana sana kusaka haki zao kisheria.”
Mkazi mmoja wa mkoani Morogoro Juma Hamadi ambaye akipata msaada wa kisheria nane nane alisema alisema amepata huduma kwa ukarimu wa hali ya juu kwa watumishi wa mpango wa mama Samia na anatarajia matatizo yake ya mgogoro wa shamba yatamalizika.
Anasema wananchi wengi hawana uwezo wa kuweka mawakili kusimamia kesi zao hivyo aliomba serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria kuufanya mpango huo wa msaada wa sheriaa kuwa endelevu.
Mwanaidi Selamani alisema alitembelea banda hilo la sheria la Mama Samia na amekutana na amepata ufumbuzi wa matatizo yake ya mgogoro wa nyumba ambao ulikuwepo kwa muda mrefu Kibaigwa.
“Hapa kwa msaada wa Rais Samia tunapata msaada wa kisheria bure tunamshukuru Rais Samia huyu mama anawapenda wananchi wake kwa kweli apewe maua yake hii huduma ni mkombozi kwetu,”anasema.
Mkazi wa Morogoro Mjini, Antony Gervas, yeye anasema huduma za msaada wa sheria ziwe endelevu kwani wengi hawana uwezo na kuongeza kuwa katika maonesho ya nanenane amejifunza kupitia kampeni hiyo itasaidia wananchi wengi wasiokuwa na uelewa wa kisheria kuhusu masuala mbalimbali.
“Kwa mpango huu Rais Samia anastahili kupongezwa sana na namshukuru kwa kampeni hii ambayo imepiga kambi hapa nanenane Morogoro kwasababu itawasaidia wananchi na watanzania kwa ujumla kupata haki zao,”anasema.
Naye, Ibrahim Waso mkazi wa Arusha ambaye alihudhuria maonyesho hayo Nane Nane Morogoro anasema amepata huduma nzuri kwenye banda la kampeni hiyo na amejifunza mambo ya kisheria ya kufuata na kutoa elimu kwa wananchi wenzao wa vijijini.
“Tumepewa namba za kupiga kwa ajili ya msaada wa kisheria tutawapa watendaji wasambaze kwa wananchi ili wanufaike na huduma hii ya msaada wa kisheria ya Mama Samia, tunamshukuru sana Rais hakika mama anaupiga mwingi kwa wananchi wake,”anasema.
Mkazi wa Kihonda Morogoro , Jamila Abdalah anasema amefarijika kupata huduma nzuri ambayo hakutegemea kuipa ya elimu ya masuala ya sheria.
“Nampongeza sana Rais kwa kuona umuhimu wa kampeni hii, kweli watu wengi hapa nchini hawana uwezo wa kuweka mawakili na tunajua mawakili ni ghali lakini ameliona hilo na kuleta kampeni hii ambayo itawasaidia sana watanzania tunashukuru sana,”anasema.
Kampeni hiyo hadi sasa imewafikia wananchi zaidi ya 490,000 wa mikoa saba na kutatua migogoro iliyokuwa ikiwakabili.
Kampeni hiyo inafanyika kwa miaka mitatu na ilianza mwezi Machi, 2023 hadi mwezi Februari, 2026 kwenye mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar ikilenga kuboresha upatikanaji wa haki kwa watu wasiojiweza.
WATANZANIA WAHIMIZWA KULA NA KUNYWA BIDHAA ZA KOROSHO
NA HADIJA OMARY , LINDI.
Waziri wa Nchi ofisi ya Rais Ikulu (kazi maalum) George Mkuchika Amewahimiza watanzania kupenda Kula na kunywa bidhaa za korosho kwani zinavirutubisho vingi vya kupambana na magonjwa pamoja na kufanya uhamasishaji wa uongezaji wa thamani ya zao hilo.
Mkuchika ametoa Rai hiyo alipokuwa akizungumza na wananchi, Wadau na wakulima wa mikoa ya Lindi na Mtwara wakati wa maadhimisho ya siku ya Kula na Kula korosho ambayo ni mahusisi kwa ajili ya uhamasishaji wa ulaji na unywaji korosho.
Katika maadhimisho hayo Wananchi Wadau na wakulima wa korosho walijionea bidhaa mbalimbali zitokanazo na korosho kama vile chapati, maandazi, kashata , maziwa ya korosho pamoja na mvinyo.
Amesema ulaji wa korosho licha ya kumlinda Mlaji na magonjwa lakini pia ni husaidia kukuza uchumi kwa mtu mmoja Mmoja na Soko la ndani .
" Kwa upande wa afya ya Binadamu ukila korosho zilizobanguliwa unakuwa na faida ya kuzuia ugonjwa wa moyo kwa kuzuia shindikizo la damu, ukila korosho unaongeza viini lishe vinavyozuia hatari ya kupata ugonjwa wa kansa pamoja na kuzuia Hatari ya kupata ugonjwa wa kisukari"
Kaimu mkurugenzi wa Taasisi ya utafiti wa kilimo TARI Naliendele, Dr. Rashid Kidunda amesema licha ya Mikoa hiyo ya Lindi na Mtwara kuwa ni wazalishaji wakubwa wa zao la korosho lakini ni asilimia 10 pekee ya kile kinachozalishwa ndicho kinachotumika kama chakula kwa wakazi wa mikoa hiyo
"Unaweza kuona ni kwa namna gani tupo chini Katika ulaji na unywaji wa korosho kwa hivyo ili kukuza Soko la ndani tuliamua kuzifanya siku ya tarehe 5 August kila mwaka tuadhimishe siku hii" Amesema Kidunda
Amesema Nchini Tanzania korosho imeendelea kuwa zao kubwa la kibiashara Katika kuchangia kipato cha wakulima hasa Katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Pwani na Ruvuma
" Kwa sasa tumeona Mikoa mingine 17 ikiingia Katika kilimo cha zao hilo na sisi kama TARI Naliendele tumepewa jukumu la kufanya utafiti na kutatua changamoto za wakulima wa zao Hilo" alifafanua
Kaimu mkurugenzi wa Bodi ya korosho Reveliani Ngaiza amesema zao la korosho ni zao la kipekee tofauti na mazao mengine kwa kuwa Lina matumizi mengi kuanzia kwenye Majani, Mbegu, Tawi , shina na hata mzizi wake
" Ukiacha ulaji wa korosho zao la korosho kwa upande wa Majani yanatumika kama Dawa kutibu minyoo tumboni, kuzuwia kuhara , kutoa Gesi tumboni pamoja na kutibu vidonda vya tumbo"
"Lakini ukichukia Jana ukachanganya na gome la mkorosho unapata Dawa ya kutibu ugonjwa wa meno, maganda ya korosho baada ya kubangua yakikamuliwa upatikana kimiminika chakutengeneza wino wa kuandikia kupitia kalamu"
Sunday, August 4, 2024
KAMPENI YA MAMA SAMIA LEGAL AID KUNUFAISHA MAELFU NANENANE.
Na Mwandishi Wetu, Morogoro
WANANCHI wanaopata msaada wa kisheria za mama Samia Legal Aid zinazoendelea kutolewa kwenye maonyesho ya Nane nane mkoani Morogoro wameelezea namna walivyonufaika na huduma hizo.
Wakizungumza mkoani hapa jana, wananchi hao walimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka huduma hizo kwenye maonyesho hayo ambapo wamesema zimekuwa mkombozi kwao.
Renatha Manda alimshukuru Rais Samia kwa msaada wa kisheria baada ya kusaidiwa na huduma hizo alipokwenda kwenye maonyesho hayo.
“Nilikuwa na tatizo la mirathi nikaenda wakanipa ushauri wa kisheria na kwa kweli nimeridhika na najua suala langu litafika mwisho hivi karibuni,” alisema
Luciani Mwanitu kutoka Nzuguni Dodoma alisema alifika kwenye banda la Mama Samia Legal Aid ambapo amepata elimu kuhusu namna wanavyotoa huduma hizo na alishauri huduma hizo zipanuliwe ili wananchi wengi hasa wa vijijini waweze kufikiwa.
“Namshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuamua kuanzisha huduma hii ambayo imekuwa mkombozi kwa wananchi wengi sana. Nawaomba waisogeze zaidi vijijini ili wananchi wengi zaidi waendelee kunufaika nayo,” alisema
Uwezo Maulid mkazi wa Shinyanga aliyefika kwenye banda hilo alisema amesaidiwa kwenye kesi ya mirathi ya mume wake ambaye alikuwa mtumishi wa umma kwenye manispaa ya Shinyanga Mjini.
“Nimefika hapa wamenipokea vizuri wamenipa mwanasheria wa huko Shinyanga ili aweze kunisimamia kupata haki zangu za msingi mimi mke wa merehemu Seif,” alisema na kuongeza
“Naomba mheshimiwa Rais aweze kunisaidia kwasababu kila ninapokwenda mahakamani naambiwa nirudi nyumbani mtandao umegoma kwasababu siku hizi kesi zinaendeshwa kwa mtandao. Huu ni mwaka wanne tangu mwaka 2021 nilipokonywa hadi nyumba na ndugu wa marehemu,” alisema
Alisema lakini baada ya kufika kwenye banda la mama Samia Legal Aid na kupewa mwanasheria anaamini suala lake litashughulikiwa na kufika mwisho ili aweze kupata haki zake kama mjane wa marehemu mume wake.
WMA WATAKA WAKULIMA KUZINGATIA VIPIMO KWENYE UJAZO WA MAZAO.
Wakala wa Vipimo (WMA) umewataka wakulima kuzingatie sheria ya vipimo inayotaka ujazo wa mazao yao kwenye gunia yasizidi kilo 100.
Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi wa WMA, Albogast Kajungu amefafanua sheria hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika manda la WMA kwenye maonesho la wakulima nane nane.
Amesema moja ya mambo wanayowaeleza wakulima ni namna ya kuweka ujazo wa mazao yao na kuzingatia vipimo vilivyowekwa na Serikali.
Amesema katika kutafsiri neno lumbesa kwenye ujazo wa gunia sheria inasema lumbesa ni kile kilichozidi juu ya ujazo wa kilo 100.
Ameongeza kwa kusema kuwa wakulima wanapaswa kuzingatia sheria ya ujazo wa mazao kwenye gunia nayo ni kuhakikisha ujazo huo usizidi kilo 100.
Amesema sheria inataka mazao yote yanapaswa yafungashwe kwenye ujazo wa kilo 100 na si vinginevyo.
Katika kuhakikisha sheria hiyo inatekelezwa ili kulinda haki ya mkulima na mnunuzi, inashauriwa kuwe na vituo vya kuuzia mazao ambapo mizani itawekwa hapo ili kuhakiki ujazo mazao husika






























