Tuesday, August 6, 2024

WATANZANIA WAHIMIZWA KULA NA KUNYWA BIDHAA ZA KOROSHO

 

NA HADIJA OMARY , LINDI.


Waziri wa Nchi ofisi ya Rais Ikulu (kazi maalum)  George Mkuchika Amewahimiza watanzania kupenda Kula na kunywa bidhaa za korosho kwani zinavirutubisho vingi vya kupambana na magonjwa pamoja na kufanya uhamasishaji wa  uongezaji wa thamani ya zao hilo.



Mkuchika ametoa Rai hiyo alipokuwa akizungumza na wananchi, Wadau na wakulima wa mikoa ya Lindi na Mtwara wakati wa maadhimisho ya siku ya Kula na Kula korosho ambayo ni mahusisi kwa ajili ya uhamasishaji wa ulaji na unywaji korosho.


Katika maadhimisho hayo Wananchi Wadau na wakulima wa korosho walijionea bidhaa mbalimbali zitokanazo na korosho kama vile chapati, maandazi, kashata , maziwa ya korosho pamoja na mvinyo.


Amesema ulaji wa  korosho licha ya kumlinda Mlaji na magonjwa lakini pia ni husaidia kukuza uchumi kwa mtu mmoja Mmoja na Soko la ndani .


" Kwa upande wa afya ya Binadamu ukila korosho zilizobanguliwa unakuwa na faida ya kuzuia ugonjwa wa moyo kwa kuzuia shindikizo la damu, ukila korosho unaongeza viini lishe vinavyozuia hatari ya kupata ugonjwa wa kansa pamoja na kuzuia Hatari ya kupata ugonjwa wa kisukari"




Kaimu mkurugenzi wa Taasisi ya utafiti wa kilimo TARI Naliendele, Dr. Rashid Kidunda  amesema licha ya Mikoa hiyo ya Lindi na Mtwara kuwa  ni wazalishaji wakubwa wa zao la korosho lakini ni asilimia 10 pekee ya kile kinachozalishwa ndicho kinachotumika kama chakula kwa wakazi wa mikoa hiyo


"Unaweza kuona ni kwa namna gani tupo chini Katika ulaji na unywaji wa korosho kwa hivyo ili kukuza Soko la ndani tuliamua  kuzifanya siku ya tarehe 5 August kila mwaka tuadhimishe siku hii" Amesema Kidunda 


Amesema Nchini Tanzania korosho imeendelea kuwa zao kubwa la kibiashara  Katika kuchangia kipato cha wakulima hasa Katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Pwani na Ruvuma 


" Kwa sasa tumeona Mikoa mingine 17 ikiingia Katika kilimo cha zao hilo na sisi kama TARI Naliendele tumepewa jukumu la  kufanya utafiti na kutatua changamoto za wakulima wa zao Hilo" alifafanua 


Kaimu mkurugenzi wa Bodi ya korosho Reveliani  Ngaiza amesema zao la korosho ni zao la kipekee tofauti na mazao mengine kwa kuwa Lina matumizi mengi kuanzia kwenye Majani, Mbegu,  Tawi , shina na hata mzizi wake


" Ukiacha ulaji wa korosho zao la korosho kwa upande wa Majani yanatumika kama Dawa kutibu minyoo tumboni, kuzuwia kuhara , kutoa Gesi tumboni pamoja na kutibu vidonda vya tumbo"


"Lakini ukichukia Jana ukachanganya na gome la mkorosho unapata Dawa ya kutibu ugonjwa wa meno, maganda ya korosho baada ya kubangua yakikamuliwa upatikana kimiminika chakutengeneza wino wa kuandikia kupitia kalamu"







Sunday, August 4, 2024

KAMPENI YA MAMA SAMIA LEGAL AID KUNUFAISHA MAELFU NANENANE.

 

Na Mwandishi Wetu, Morogoro


WANANCHI wanaopata msaada wa kisheria za mama Samia Legal Aid zinazoendelea kutolewa kwenye maonyesho ya Nane nane mkoani Morogoro wameelezea namna walivyonufaika na huduma hizo.


Wakizungumza mkoani hapa jana, wananchi hao walimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka huduma hizo kwenye maonyesho hayo ambapo wamesema zimekuwa mkombozi kwao.


Renatha Manda alimshukuru Rais Samia kwa msaada wa kisheria baada ya kusaidiwa na huduma hizo alipokwenda kwenye maonyesho hayo.


“Nilikuwa na tatizo la mirathi nikaenda wakanipa ushauri wa kisheria na kwa kweli nimeridhika na najua suala langu litafika mwisho hivi karibuni,” alisema


Luciani Mwanitu kutoka Nzuguni Dodoma alisema alifika kwenye banda la Mama Samia Legal Aid ambapo amepata elimu kuhusu namna wanavyotoa huduma hizo na alishauri huduma hizo zipanuliwe ili wananchi wengi hasa wa vijijini waweze kufikiwa.


“Namshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuamua kuanzisha huduma hii ambayo imekuwa mkombozi kwa wananchi wengi sana. Nawaomba waisogeze zaidi vijijini ili wananchi wengi zaidi waendelee kunufaika nayo,” alisema


Uwezo Maulid mkazi wa Shinyanga aliyefika kwenye banda hilo alisema amesaidiwa kwenye kesi ya mirathi ya mume wake ambaye alikuwa mtumishi wa umma kwenye manispaa ya Shinyanga Mjini.


“Nimefika hapa wamenipokea vizuri wamenipa mwanasheria wa huko Shinyanga ili aweze kunisimamia kupata haki zangu za msingi mimi mke wa merehemu Seif,” alisema na kuongeza


“Naomba mheshimiwa Rais aweze kunisaidia kwasababu kila ninapokwenda mahakamani naambiwa nirudi nyumbani mtandao umegoma kwasababu siku hizi kesi zinaendeshwa kwa mtandao. Huu ni mwaka wanne tangu mwaka 2021  nilipokonywa hadi nyumba na ndugu wa marehemu,” alisema


Alisema lakini baada ya kufika kwenye banda la mama Samia Legal Aid na kupewa mwanasheria anaamini suala lake litashughulikiwa na kufika mwisho ili aweze kupata haki zake kama mjane wa marehemu mume wake.






Wananchi wakipata huduma za msaada wa sheria bure banda la Mama Samia Legal Aid mkoani Morogoro kwenye maonyesho ya Nane Nane

WMA WATAKA WAKULIMA KUZINGATIA VIPIMO KWENYE UJAZO WA MAZAO.

 

Wakala wa Vipimo (WMA) umewataka wakulima kuzingatie sheria ya vipimo inayotaka ujazo wa mazao yao kwenye gunia yasizidi kilo 100.


Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi wa WMA, Albogast Kajungu amefafanua sheria hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika manda la WMA kwenye maonesho la wakulima nane nane.


Amesema moja ya mambo wanayowaeleza wakulima ni namna ya kuweka ujazo wa mazao yao na kuzingatia vipimo vilivyowekwa na Serikali.


Amesema katika kutafsiri neno lumbesa kwenye ujazo wa gunia sheria inasema lumbesa ni kile kilichozidi juu ya ujazo wa kilo 100.


Ameongeza kwa kusema kuwa wakulima wanapaswa kuzingatia sheria ya ujazo wa mazao kwenye gunia nayo ni kuhakikisha ujazo huo usizidi kilo 100.


Amesema sheria inataka mazao yote yanapaswa yafungashwe kwenye ujazo wa kilo 100 na si vinginevyo.


Katika kuhakikisha sheria hiyo inatekelezwa ili kulinda haki ya mkulima na mnunuzi, inashauriwa kuwe na vituo vya kuuzia mazao ambapo mizani itawekwa hapo ili kuhakiki ujazo mazao husika


Saturday, August 3, 2024

WANASHERIA WATATUA MIGOGORO ZIARA YA RAIS SAMIA MOROGORO

 


Na Mwandishi Wetu

TIMU ya wanasheria wa kampeni ya Mama Samia Legal Aid imeambatana na Rais Samia Suluhu Hassan kwenye ziara yake ya mkoani Morogoro kwaajili ya kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.

Rais Samia yuko katika ziara ya siku sita mkoani Morogoro iliyoanza tarehe mbili na inayotarajiwa kukamilika tarehe saba siku ya Jumatano mwezi huu.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii jana, Mkurugenzi Msaidizi wa Ufuatiliaji Haki wa Wizara ya Katiba na Sheria, Beatrice Mpembo alisema wameambatana na Rais Samia ili kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi wanaohitaji msaada wa kisheria.

“Tutakuwa na Rais muda wote wa ziara hapa Morogoro na tupo na Waziri wetu mheshimiwa Pindi Chana na wasaidizi wa kisheria ngazi ya wilaya na mkoa, kila anapofika mheshimiwa Rais kama kuna mtu anachangamoto ya kisheria tunaichukua na kuifanyia kazi,” alisema

“Kupitia ziara hii tumeshatoa msaada wa kisheria kwa wananchi mbalimbali na hata jamii ya wamasai tumekutana nao kwenye maeneo mbalimbali na tumewapa elimu ya sheria kuhusu migogoro yao ya mara kwa mara ya ardhi,” alisema Beatrice.

Alisema wakati wanasheria wengine wakiwa kwenye ziara  hiyo, Rais Samia ametuma wanasheria wengine kupitia Kampeni ya Mama Samia Legail Aid kutoa huduma za msaada wa kisheria kwenye maonyesho ya nane nane mkoani humo.

Beatrice alisema timu ya wanasheria hao iliwasili mkoani Morogoro juzi na inaendelea na kazi ya kuwahudumia wananchi mbalimbali ambao wanamatatizo ya kisheia kwa kuwapa msaada wa kisheria.

Tangu wanasheria hao wawasili kwenye viwanja vya nane nane mkoani Korogoro wananchi wengi wamekuwa wakifika kwenye banda la mama samia Legal Aid  katika  maonyesho hayoambapo wamekuwa wakipewa msaada wa kisheria.

Mama Samia yuko mkoani hapwa kwa ziara ya kikazi ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye wilaya za Mkoa wa Morogoro na mpaka sasa ameshatembelea Wilaya ya  Gairo, Kilosa, Mvomero,  na kesho Jumapili anatarajaiwa kuwasili wilaya ya Kilombero.

Mmoja wa wananchi aliyepata huduma ya msaada wa kisheria Jerome Kiangi,  alimpongeza Rais Samia kwa uamuzi wake wa kuwasaidia wananchi wasio na uwezo wa kutatua matatizo yao ya kisheria.

“Kwa kweli nampongeza Rais Samia kwa upendo wake kwa watanzania amegundua kwamba wengi wetu tunahitaji msaada wa kisheria nimekuja hapa nimesikilizwa na wanasheria na wamesema tatizo langu la mgogoro wa nyumba litapatiwa ufumbuzi namshukuru sana,” alisema mwananchi huyo.

Mwananchi mwingine, John Lubeja alipongeza hatua ya rais Samia kutuma wanasheria kwenye maonyesho hayo kwani wamekuwa mkombozi kwa wananchi ambao hawana uwezo wa kupata huduma za kisheria.

“Kupata wakili ni gharama sana kwa hiyo huduma kama hizi zinaposogezwa karibu na wananchi kama hapa kwenye maonyesho tena bure ni jambo la faraja sana na la kupongeza mno,” alisema Lubeja.