Saturday, August 3, 2024

WANASHERIA WATATUA MIGOGORO ZIARA YA RAIS SAMIA MOROGORO

 


Na Mwandishi Wetu

TIMU ya wanasheria wa kampeni ya Mama Samia Legal Aid imeambatana na Rais Samia Suluhu Hassan kwenye ziara yake ya mkoani Morogoro kwaajili ya kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.

Rais Samia yuko katika ziara ya siku sita mkoani Morogoro iliyoanza tarehe mbili na inayotarajiwa kukamilika tarehe saba siku ya Jumatano mwezi huu.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii jana, Mkurugenzi Msaidizi wa Ufuatiliaji Haki wa Wizara ya Katiba na Sheria, Beatrice Mpembo alisema wameambatana na Rais Samia ili kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi wanaohitaji msaada wa kisheria.

“Tutakuwa na Rais muda wote wa ziara hapa Morogoro na tupo na Waziri wetu mheshimiwa Pindi Chana na wasaidizi wa kisheria ngazi ya wilaya na mkoa, kila anapofika mheshimiwa Rais kama kuna mtu anachangamoto ya kisheria tunaichukua na kuifanyia kazi,” alisema

“Kupitia ziara hii tumeshatoa msaada wa kisheria kwa wananchi mbalimbali na hata jamii ya wamasai tumekutana nao kwenye maeneo mbalimbali na tumewapa elimu ya sheria kuhusu migogoro yao ya mara kwa mara ya ardhi,” alisema Beatrice.

Alisema wakati wanasheria wengine wakiwa kwenye ziara  hiyo, Rais Samia ametuma wanasheria wengine kupitia Kampeni ya Mama Samia Legail Aid kutoa huduma za msaada wa kisheria kwenye maonyesho ya nane nane mkoani humo.

Beatrice alisema timu ya wanasheria hao iliwasili mkoani Morogoro juzi na inaendelea na kazi ya kuwahudumia wananchi mbalimbali ambao wanamatatizo ya kisheia kwa kuwapa msaada wa kisheria.

Tangu wanasheria hao wawasili kwenye viwanja vya nane nane mkoani Korogoro wananchi wengi wamekuwa wakifika kwenye banda la mama samia Legal Aid  katika  maonyesho hayoambapo wamekuwa wakipewa msaada wa kisheria.

Mama Samia yuko mkoani hapwa kwa ziara ya kikazi ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye wilaya za Mkoa wa Morogoro na mpaka sasa ameshatembelea Wilaya ya  Gairo, Kilosa, Mvomero,  na kesho Jumapili anatarajaiwa kuwasili wilaya ya Kilombero.

Mmoja wa wananchi aliyepata huduma ya msaada wa kisheria Jerome Kiangi,  alimpongeza Rais Samia kwa uamuzi wake wa kuwasaidia wananchi wasio na uwezo wa kutatua matatizo yao ya kisheria.

“Kwa kweli nampongeza Rais Samia kwa upendo wake kwa watanzania amegundua kwamba wengi wetu tunahitaji msaada wa kisheria nimekuja hapa nimesikilizwa na wanasheria na wamesema tatizo langu la mgogoro wa nyumba litapatiwa ufumbuzi namshukuru sana,” alisema mwananchi huyo.

Mwananchi mwingine, John Lubeja alipongeza hatua ya rais Samia kutuma wanasheria kwenye maonyesho hayo kwani wamekuwa mkombozi kwa wananchi ambao hawana uwezo wa kupata huduma za kisheria.

“Kupata wakili ni gharama sana kwa hiyo huduma kama hizi zinaposogezwa karibu na wananchi kama hapa kwenye maonyesho tena bure ni jambo la faraja sana na la kupongeza mno,” alisema Lubeja.










No comments:

Post a Comment