SWEETBERT NKUBA AAHIDI KULETA MABADILIKO TLS.
Na Mwandishi Wetu Mgombea wa urais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Sweetbert Nkuba ameelezea namna ambavyo amejipanga kuleta mabadiliko ndani ya chama hicho endapo atachaguliwa kushika nafasi hiyo. Moja ya mipango yake amesema ni kuboresha miundombinu ya TLS, uimarishaji wa miundombinu ya kisheria na kiteknolojia ili kuwezesha huduma bora kwa wanachama na jamii hususani kuongeza uwekezaji katika mifumo ya kidijitali ya kurahisisha upatikanaji wa taarifa na huduma za kisheria na kuboresha ofisi za TLS katika mikoa mbalimbali kwa vifaa vya kisasa na miundombinu bora. Jambo la pili anasema atasisitiza mafunzo endelevu kwa wanachama wa TLS ili kuhakikisha kuwa wanasheria wanakuwa na ujuzi wa kisasa na uwezo wa kushindana kimataifa ikijumuisha kuanzisha programu za mafunzo ya mara kwa mara kuhusu sheria mpya na mabadiliko ya sheria pamoja na kushirikiana na taasisi za kimataifa kwa mafunzo na kubadilishana uzoefu. La tatu anasema atahakikisha TLS inakuwa na sauti yenye nguvu...