Thursday, July 25, 2024

MAAFISA UANDIKISHAJI DAFTARI LA MPIGA KURA KAGERA WALA KIAPO

 




Na Alodia Dominick,  Bukoba,


Maafisa uandikishaji ngazi ya wilaya na maafisa ugavi mkoani Kagera wamekula kiapo ili kwenda kutekeleza shughuli mbalimbali za tume huru ya Taifa ya uchaguzi.


Watu hao wa wameapishwa Julai 25,2024 na Hakimu mkazi mfawidhi wilaya ya Bukoba Frorah Kaijage uapisho uliofanyika katika ukumbi wa mkuu wa mkoa huo.


Akifungua mafunzo hayo ya siku mbili mgeni rasmi Jaji mstaafu Mbarouk S Mbarouk amesema kuwa mafunzo hayo yatawasaidia kufanya kazi zao kwa ueledi, bidii na moyo wa kujituma ili kufanikisha zoezi hilo na kuwaelekeza wengine ambao hawakuwahi kushiriki zoezi kama hilo.


“Wakati wa uboreshaji wa daftari mawakala wa vyama vya siasa wataruhusiwa kuwepo katika vituo vya kuandikisha wapiga kura, jambo hili ni muhimu na litasaidia kuleta uwazi wa zoezi zima pia mawakala watasaidia kuwepo uwazi ili kupunguza kuwepo kwa vurugu zisizo za lazima”


Aidha alisema kuwa, tume imetoa vibali 157  vya asasi za kiraia kwa ajili ya kutoa elimu ya mpiga kura na waangalizi wa zoezi la uboreshaji 33 watakaotazama zoezi la uboreshaji daftari la mpiga kura.


Kwa upande wake mratibu wa uandikishaji mkoa wa Kagera Mapinduzi Severian ametaja vituo vya uandikishaji mkoa wa Kagera kuwa vitakuwa  1,778 katika majimbo tisa na halmashauri 8 za mkoa huo.


 


Hadi sasa wameshafanya usaili kwa watendaji ngazi ya vituo na watakuwa na mafunzo ya siku mbili kuanzia Agosti 02 hadi Agosti tatu mwaka huu.


“Uandikisha katika mkoa wetu utaanza Agosti 05 hadi Agosti 11, mwaka huu, hivyo niwaombe wananchi uandikishaji utakapoanza basi wajitokeze kwa wingi na wakajiandikishe vituo vitakuwa karibu na wananchi”


Aidha amesema kwa upande wa wilaya ya Muleba ambapo kuna visiwa  vingi wamesha andaa boti na watendaji wa kwenda kufanya kazi huko hivyo hawatarajii changamoto yoyote katika zoezi la uandikishaji.


Naye mkurugenzi wa manispaa ya Bukoba Jacob Nkwela amesema kuwa, wao kama manispaa wamejipanga kuendesha zoezi la uandikishaji kikamilifu.


Amesema manispaa wanazo kata 16 na mitaa 66 ili  wananchi waweze kujiandikisha kwa urahisi wameweka vituo 85 ambavyo vitakuwa katika maeneo rafiki kila mmoja kujiandikisha kiurahisi na kila mmoja atawajibika kwenda kuboresha taarifa zake na wale ambao wametimiza miaka 18 wanatakiwa wakajiandikishe.


No comments:

Post a Comment