Na Alodia Dominick Bukoba,
Wadau mbalimbali wa uchaguzi hapa nchini wameombwa kuhamasisha jamii kujitokeza wakati wa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura.
Wito huo umetolewa Julai 24, 2024 na mwenyekiti wa tume huru ya taifa ya uchaguzi Jaji Mbarouk S Mbarouk katika mkutano wa tume na wadau wa uchaguzi mkoani Kagera ambao ulilenga kutoa taarifa mbalimbali za maandalizi ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura.
Amesema kuwa, uzinduzi la daftari la kudumu ulifanyika mkoani Kigoma na Waziri mkuu wa Tanzania Kasimu Majaliwa na kuwa uzinduzi awamu ya pili utafanyika kuanzia Agosti 05, mwaka huu hadi Agosti 11, mwaka huu katika mikoa ya Kagera na Geita.
Amewaomba viongozi wa dini, makundi mbalimbali ya wenye ulemavu na wanawake kuhamasisha wananchi kujitokeza kupiga kura na akasema mama wajawazito, wenye watoto wachanga, wazee na wenye ulemavu watapewa kipaumbele wakati wa kupiga kura.
Wakati huo huo, Kaimu mkurugenzi wa tume huru ya Taifa ya uchaguzi Giveness Aswile amesema kuwa, tume ya taifa ya uchaguzi inatarajia kuandikisha wapiga kura wapya mkoani Kagera katika daftari la kudumu wapatao 219,321.
Ameeleza kuwa, kuandikishwa kwa wapiga kura wapya zaidi ya laki 200 mkoani Kagera ni ongezeko la asilimia 15.5 ya wapiga kura milioni 1.4 waliopo kwenye daftari la kudumu la wapiga kura hivyo tume baada ya uandikishaji inatarajia mkoa wa Kagera utakuwa na wapiga kura milioni 1.6.
Aidha amevitaja vituo vya kuandikisha wapiga kura kuwa idadi yake ni zaidi ya vituo elfu 40 ambavyo vitatumika katika uboreshaji wa daftari mwaka 2024, vituo elfu 39 vipo Tanzania Bara na vituo 417 vipo Zanzibar, hili ni ongezeko la vituo zaidi ya 2,000 ikilinganishwa na vituo zaidi ya elfu 37 vilivyotumika mwaka 2019/2020.
Ameongeza kuwa, Kagera vituo vya uandikishaji vitakuwa 1,778 vilivyoongezeka ni vituo 101.
Aidha, ameongeza kwamba zoezi la uboreshaji daftari la kudumu litakuwa la siku saba, kwa Tanzania waligawa zoezi hilo katika mizunguko13 na sasa wako mzunguko wa pili Kagera na Geita na shughuli za uandikishaji zitakuwa zinaanza saa mbili asubuhi hadi saa 12 jioni wahusika ni kuanzia miaka 18 na kuendelea.
Mmoja wa washiriki wa mkutano huo, katibu wa chama cha watu wenye ulemavu mkoa wa Kagera (CHAWATA) Sweatbert Bishanga ameiomba tume huru ya taifa ya uchaguzi kuandaa vitabu maalum vya kupigia kura kwa ajili ya wasioona katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika mwaka huu.
Amesema katika uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na Rais mwaka 2020 wasioona walipewa vitabu ambavyo viliwawezesha kupiga kura wenyewe bila kupigiwa na mtu ili kukwepa kupigiwa kura kwa kiongozi wasiyemuhitaji.
Hata hivyo, baadhi ya wadau wameomba tume huru ya taifa ya uchaguzi kutumia vyombo vya habari kuelimisha jamii faida za kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura.
No comments:
Post a Comment