Sunday, May 12, 2024

JUMUIYA YA WAZAZI BAGAMOYO YASIMAMISHA UPIMAJI ARDHI CHALINZE.

 

Na Omary Mngindo, Chalinze.

JUMUIA ya Wazazi Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani, imeitaka Idara ya Ardhi halmashauri ya Chalinze wilaya ya Bagamoyo mkoani hapa kusitisha upimaji wa ardhi katika eneo linalomilikiwa na Jumuia hiyo.


Agizo hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Jumuia hiyo Aboubakary Mlawa, katika kikao kilichojumuisha wanachama wa Jumuia kwenye kuelekea sherehe za Wazazi Kitaifa, itayotanguliwa na ya Mkoa ambapo kiwilaya imefanyika Kata ya Bwilingu.


Alisema kuwa eneo hilo lenye ukubwa wa  ekari 50, Jumuiya hiyo ilipewa na uongozi wa Kijiji mwaka 2000 kwaajili ya kujenga shule ya wazazi, lakini wavamizi wametoa alama za mipaka ya eneo hilo na kujenga na sasa wanarasimisha  rasmi ili wapatiwe hati.


"Ardhi ni yetu hivyo kuwabana wale ambao wameingia watalazimika kutulipa hela yetu kulingana na thamani ya ardhi ya sasa, hatutawanyang'anya ila watafidia maeneo yetu kulingana na thamani ya sasa," alisema Mlawa.


Aliongeza kwamba "Mimi msimammo wangu ni huo zoezi lisimame kwa wale waliochukua mali zetu waturudishie, uzuri ni kwamba tunajua eneo letu lina ukubwa gani na linaanzia wapi," alisema Mwenyekiti huyo.


Kwa upande wake Diwani Wa Kata ya Bwililingu Nasser Karama alithibitisha kuwepo kwa eneo hilo ambalo kwa kiasi kikubwa limevamiwa na watu baadhi huku baadhi yao wakiwa wamejenga na wengine kuuza.


"Leo itanibidi niongee ukweli, moja ya vitu vinavyofanya nichukiwe na baadhi ya  wananchi ni namna ninavyotetea mali za chama na serikali, ninapofanya hivyo naambiwa naleta wawekezaji, lakini nashukuru wengi wameelewa sasa baada ya watu kuona ukweli," alisema Karama.


Mwenyekiti Mstaafu wa Jumuia hiyo wakati huo ikitambulika Kata ya Chalinze Mzee Kibindu ameelezea namna ardhi hiyo ilivyogawanywa kwa viongozi, huku nae akipatiwa kwa ajili ya shughuli za kilimo.


"Baada ya zoezi hilo kulikuwepo na hatua mbalimbali za kesi, na katika mchakato huo kila tulipokuwa tunakwenda tulikuwa tunashindwa, hivyo ninachojua pale hatuna eneo," alisema Kibindu huku wajumbe wakionesha kushangazwa kutokana na kauli hiyo.


Anold Mtumuyu aliyewahi kushika wadhifa mbalimbali wakati huo aliwaambia wanaJumuia hiyo kwamba akiwa kiongozi katika Kata amewahi kutembelea eneo hilo mara kadhaa, huku akisikitishwa na kauli ya Mzee Kibindu ya kwamba Jumuia haina ardhi katika eneo hilo.


"Mwenyekiti binafsi nimesikitishwa na kauli ya mzee wetu, kumbe wakati akiwa kiongozi kumbe nae alijimegea eneo lake, mimi nashauri tuanze na yeye kwani kuna mengi tutayafahamu zaidi," alisema Mtumuyu.


Wakichangia mada Alhaj Abdallah Sakasa na Amir Mramba wameelezea masikitiko yao kuhusiana na kuchukuliwa kiholela kwa ardhi ya Jumuia, huku wakishauri hatua za kisheria zichukuliwe kuwabaini wote ambao wamehusika na kuhujumu ardhi hiyo.






Saturday, May 11, 2024

RUNALI WAGAWA VITENDEA KAZI KWA WAKULIMA KUELEKEA MSIMU WA UFUTA NA MBAAZI

 

CHAMA kikuu cha ushirika (RUNALI) kinachounganisha wakulima wa Wilaya za Ruangwa,  Nachingwea na Liwale Mkoani Lindi kimegawa jumla ya viroba laki 800,000, vitabu pamoja na kamba kwa wakulima wa wilaya ya Nachingwea, Ruangwa na Liwale kuelekea msimu wa mauzo ya mazao ya ufuta,Mbazi na Korosho.


 uzinduzi wa ugawaji wa vifungashio hivyo ulioenda sambamba na utoaji wa mafunzo wa matumizi mfumo wa TMX kwa watendaji wakuu wa vyama vya msingi (AMCOS) yaliyofanyika huko Wilayani Nachingwea.


Akizungumza wakati wa zoezi hilo meneja wa chama hicho Jahida Hassan alisema kuwa wamegawa vifungashio hivyo kwa lengo la kuwawezesha wakulima kuhifadhi mazao kwenye ubora unaotakiwa sokoni.


Bi. Jahida  alisema kuwa RUNALI wamekuwa wanatoa elimu mara kwa mara kwa wakulima ili waweze kulima kilimo kilicho bora na kufanikiwa kupeleka mazao yaliyo bora sokoni.


" tupo  tayari kwa kuanza msimu mpya wa Mbaazi na ufuta na lengo la mafunzo haya ni kuwajengea utayari wa kwenda kwenye msimu mpya pia wametoka kufahamishana umuhimu wa kufanya ukaguzi.


  mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Nachingwea Adinan Mpyagila amewasihi wakulima kutouza mazao kiholela na kuweka vituo kwenye mipaka ya wilaya ili mazao yasiuzwe nje ya wilaya kwa kuwa itapelekea kupoteza mapato ya Halmashauri kwenye mazao ya mbaazi na ufuta.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama cha ushirika (RUNALI) Odas Mpunga amewapongeza vyama vya Ushirika kwa kazi kubwa waliyofanya na kuingiza mapato makubwa. Pia, amewataka kuyatumia vyema mafunzo haya kwa vitendo ili kuleta Matokeo chanya.






MLAO AWAASA MADIWANI MKOA WA PWANI.

 

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani Mwishehe Mlao akizungumza na Madiwani hao (Hawapo pichani) Picha na Omary Mngindo.

...................................

Na Omary Mngindo, Pwani.

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani Mwinshehe Mlao, amekutana na Madiwani kutoka katika Halmashauri zote zinazounda mkoa wa Pwani, lengo ni kutathmini kuelekea uchaguzi ujao.


Katika kikao hicho kilichofanyika wilayani Mkuranga, Mlao amewaagiza madiwani hao  kuhakikisha chama hicho kinashinda kwa kishindo katika chaguzi za Serikali za mitaa, Vijiji na Vitongoji kwa mwaka 2024.


Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti huyo akiwakumbusha kuzingatia maadili, kuepuka udini, kutumia mitandao ya kijamii kwa tija, ukaribu na wananchi wakiwemo wana CCM kuelezea mazuri yanayofanywa na Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu.


"Yeyote atakaye kiuka maadili ya chama chetu kwa kutukana mitandaoni, ninaagiza kuanzia sasa aitwe katika vikao husika na kujadiliwa sanjali na kuchukuliwa hatua za kinidhamu" alisema Mlao.


Aidha amewasisitizia madiwani hao pamoja na wanaCCM kuacha mara moja kujichukulia dhamana ya kuwa wasemaji katika mitandao au vijiwe bila kuwa na uhalali huo.


Kwa upande wake Katibu wa chama hicho mkoani hapa Bernard Ghaty alitumia nafasi hiyo kuwatahadharisha madiwani hao, akiwataka kuhakikisha hawapotezi  mitaa, viijiji wala vitongoji katika kata zao.


"Lengo la chama chetu ni kuhakikisha mitaa, vijiji na vitongoji vyote vinarudi CCM, mkumbuke Mwenyekiti wetu alipokea kijiti hiki nafasi zote za uongozi zikiwa CCM, ndoto yake ni kuona vijiji vyote vinarudi,' alisema Ghaty.


"Madiwani wa viti maalum fanyeni ziara kwenye Halmashauri zenu na si katika kata mnazoishi, nendeni mkakiimarishe chama, shughulikieni masuala yote pia kuzisimamia kwa mujibu wa sheria na kanuni katika majukumu yenu," alisisitiza Ghaty.


Aidha Katibu huyo amehitimisha kwa kuwataka Madiwani hao kujiandaa na uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka 2024, kwa kuhakikisha wanatatua changamoto zinazowakabili wananchi ili chama hicho kiweze kushinda kwa asilimia zote.


Katika kikao hicho Madiwani hao wameahidi kwenda kutekeleza maagizo yaliyotolewa, na kwamba watafanya kazi kwa bidii na uzalendo ikiwa ni kuendelea kumuunga mkono Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Taifa.





DIBIBI AGAWA VITENDEAKAZI KISARAWE

 

Na Omary Mngindo, Kisarawe

MWENYEKITI wa Jumuia ya Wazazi Wilaya ya Kisarawe Mkoa wa Pwani Khamis Dibibi, mwishoni mwa wiki amegawa vitendeakazi kwa viongozi wa matawi 119 yaliyopo Kata zote 17 wilayani hapa.


Katika hafla hiyo chini ya mgeni mualikwa Kaimu Katibu wa Jumuia hiyo mkoani hapa Sophia Abdul, Dibibi alikabidhi vifaa hivyo lengo  ni kuwawezesha viongozi kutekeleza shughuli za kuwatumikia wanachama.


Vifaa alivyokabidhi ni pamoja na mihuri, reja za kusajiria wanachama wapya katika matawi, vidau vya mihuri (Stap Pad), kadi za Jumuiya ya wazazi 300 kila tawi sanjali na bips (Reflector).


"WanaJumuia wenzangu nimeamua kununua vitendeakazi hivi, lengo kubwa kuwawezesha katika kutekeleza majukumu yetu ya Jumuia, pia niwaombe tuhamasishe wanachama wapya wajiunge," alisema Dibibi.


Akizungumza na wanaJumuia hao, mgeni mualikwa amehimiza umoja, mshikamano na upendo huku akiwataka kujitokeza kuwania nafasi ya Wenyeviti wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji.


"Tumpongeze Mwenyekiti wetu Khamis Dibibi kwa kutuwezesha vitendeakazi hivi, niwaombe tukavitumie katika kuhakikisha vinatusaidia kuwatumikia wanaJumuia," alisema Sophia.


Aidha aliongeza kwamba "Twendeni tukahamasishe wanachama wapya wajiunge katika Jumuia yetu, pia tugombee uenyekiti wa serikali katika uchaguzi ujao," alimalizia Kaimu Katibu huyo.





MTU MMOJA AFARIKI KWA KUSOMBWA NA MAJI BUKOBA.

 

Na Alodia Babara, Bukoba

Mvua zinazoendelea kunyesha zimesababisha kifo cha mtu mmoja katika kata ya Bakoba manispaa ya Bukoba mkoani Kagera huku barabara zikifungwa kwa muda kutokana na baadhi ya madaraja katika barabara hizo kufunikwa na maji.


Kamanda wa jeshi la zimamoto na uokoaji mkoani Kagera Zabron Muhumha akizungumza leo ametaja aliyefariki kwa jina moja la Lea anayekadiliwa kuwa na umri wa miaka 19 ambaye wakati anachota maji mtoni aliteleza na kusombwa na maji ya mvua.


"Mei 09,2024 majira ya saa 4:00 jioni binti huyo akiwa anachota maji katika mto aliteleza na kusombwa na maji na mwili wake ulipatikana  na kupelekwa kuhifadhiwa hospitali ya Rufaa ya mkoa, Bukoba" alisema Muhumha.


Ametaja madhara mengine yaliyopatikana na mvua hizo kuwa zimesababisha nyumba nyingi ambazo ziko mwambao wa mto Kanoni na ziwa Victoria kuzingirwa na maji na baadhi ya barabara kufungwa kwa muda.


Ametaja maeneo ambayo yamezingirwa na maji kuwa ni Kiwanja cha Jymkana kata ya Miembeni, baadhi ya nyumba Kasalani na Nyakanyasi kata ya Bakoba, Nyamkazi kata ya Miembeni na  Omukigusha  kata ya Bilele.


Aidha amesema jeshi hilo linaendelea kutoa elimu na linazungukia maeneo ambayo ni hatarishi na kuwajuza wananchi wahame maeneo hayo, kila mwaka yamekuwa yakijaa maji kwa kuwa mvua zinaendelea kunyesha ardhi imejaa maji hata ikinyesha mvua ya wastani maji yanajaa mengi sana hivyo wahamie maeneo salama.


Kwa upande wake Diwani wa kata ya Bakoba Shaaban Rashid amesema kuwa, katika kata yake mtaa wa Nyakanyasi eneo la Mwizinga mvua iliyonyesha usiku wa kuamkia Mei 10,2024 ilisababisha eneo hilo kujaa maji na walikuwa wanaendelea na zoezi la kutoa watu ndani ya nyumba na kuwapeleka maeneo salama.


Amewaomba wananchi ambao maeneo yao huwa yanajaa maji hata kama bado hayajawafikia kuhama maeneo hayo kwa ajili ya kulinda usalama wao.


Aidha diwani wa kata ya Miembeni
Richard Gaspal amesema kuwa katika mtaa wa Nyamkazi eneo hilo limejaa maji kwani ni eneo ambalo liko mwambao wa ziwa Victoria na hata barabara hazipitiki zimejaa maji  na daraja lililojengwa hivi karibuni limefunikwa na  maji hivyo wananchi wanapita kwenye vichochoro wanapanga mawe wanapita ili kuhama katika maeneo yao na kwenda maeneo salama.


Amesema, baadhi ya waathirika wamehamia kata ya Kashai na wengine wamewawekwa sehemu moja katika shule ya msingi Nyamkazi.


Ikumbukwe kuwa, mji wa Bukoba ni mji ambao uko katika mwambao wa ziwa Victoria na kuna mito inapita katika mji huo ikimwaga maji yake katika ziwa hilo na nyumba zaidi ya 70 zimeathiriwa na maji.


Wednesday, May 8, 2024

MADAKTARI BINGWA WA RAIS SAMIA WAFIKA LINIDI

 


Na Mwandishi wetu

Lindi

Zaidi ya Madaktari 50 ambao ni Bingwa na Wabobezi wa Rais Samia Suluhu  wameweka kambi maalumu ya matibabu ya Afya katika Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Lindi Sokoine kwa siku 5 kuanzia tarehe 6 mai hadi 10.

Akizindua utoaji wa  matibabu hayo mkuu wa wilaya ya Lindi Shaibu Ndemanga kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Lindi  amesema huduma hizo za kibingwa zitarahisisha kwa kiasi kikubwa huduma kwa kuwafikia wananchi na hivyo kupunguza gharama ya kusafiri kwenda nje ya mkoa huo kufuata huduma hizo.

'Tunatoa shukrani za dhati kwa Rais wetu Dkt samia kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya utoaji wa huduma za Afya kwa kuhakikisha anapeleka fedha za ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za Afya pamoja na manunuzi ya vifaa tiba” alisema Ndemanga

Aidha, Ndemanga amewaomba Wananchi wote wenye matatizo ya kiafya kuhudhuria katika kambi hiyo ili kuonana na kutibiwa na Madaktari Bingwa na Bingwa bobezi ambapo itasaidia kuwapunguzia gharama za kusafiri umbali mrefu nje ya mkoa kufuata huduma.

Dkt.Alexander Makalla ambaye ni mganga mfawidhi wa hospitali ya Rufaa Sokoine amesema ili kuwafikia wananchi wengi zaidi huduma za kumuona daktari zitatolewa bure isipokiwa kwa wagongwa waliokuwa na Bima za Afya huku mgonjwa akitakiwa asilimia 70 kwa huduma za vipimo, upasuaji na dawa.

Amesema huduma zitakazotolewa ni pamoja na Magonjwa ya wanawake na uzazi, Magonjwa ya Watoto, Magonjwa ya mfumo wa mkojo, magonjwa ya ngozi, Magonjwa ya kinywa na meno.

Huduma zingine ni Magonjwa ya macho, Magonjwa ya Afya ya akili pamoja na magonjwa ya pua, koo na Masikio pia huduma za mazoezi Tiba na viungo, upimaji wa saratani ya mlango wa kizazi na matiti pamoja na huduma za vipimo vya maabara, mionzi na upasuaji

Naye Meneja wa mfuko wa taifa wa bima ya afya Irine Katarahiya ametumia fursa hiyo kuwahasa wananchi kujiunga na mfuko wa Bima ya Afya ili waweze kunufaika na huduma lukuki.

" Kwa Mkoa wa Lindi hii ni fursa hasa kwa wale wenye kadi ya mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya  kwa sababu kadi yake inamuwezesha kumuona daktari yeyote Madaktari zaidi ya  hamsini wako hapa Mkoani Lindi hivyo nitumie fursa hii kuwahasa wananchi amabo bado hawajakata kadi za Bima za Afya kufanya hivyo ili kuweza kunufaika na fursa zijazo"Alisema

Nao baadhi ya wananchi waliofika kupata matibabu hayo wakamshukuru Rais Samia kwa kuwasogezea huma hizo karibu yao.



WAUZA MLIMA MILLIONI 20 KILOSA.

 

Na Mwandishi Wetu

Jeshi la Polisi wilayani kilosa limewatia mbaroni watu wawili akiwemo Mwenyekiti wa Kitongoji cha Msowero A, Petro Sanga (Paroko) na mwenzake, Awadh Ngajime kwa tuhuma za kuuza eneo la mlima, mali ya kijiji cha Msowero wilayni Kilosa.


Pia, inaendelea kuwatafuta watu wengine 48 ambao wanaosadikiwa kuwa sehemu ya mtandao huo, uliohusika kuuza mlima  wenye ukubwa wa jumla ya ekari 1158 za Kijiji zilizopo katika mlima huo kinyume na utaratibu.


Hayo yalibainika wakati wa mkutano wa hadhara wa kusikiliza kero za wanachi katika Kata ya Msowero ulioitishwa na Mkuu wa Wilaya ya KIlosa Shaka Hamdu Shaka mwishoni mwa wiki kijjijini hapo.


Shaka alisema kumekuwa na wimbi la uvamizi wa maeneo ya ardhi unaoonekana kukithiri siku hadi siku na baadhi ya maeneo wananchi wamekuwa wakihusika kuyauza kinyume na sheria.


"Tuna kata saba ndani ya wilaya hii zinaongoza kwa migogoro ya ardhi ikiwemo hii ya Msowero, mnaongoza mnavamia maeneo ya serikali, viongozi wapo mnashirikiana nao wengine kisha mnageuka mnasingizia viongozi wa wilaya mkoa na taifa kuwa wanakuja kupora ardhi yenu kumbe ni uongo kabisa.


"Mmeuza mlima kinyume na utaratibu ekari 1,158 zote mmevamia na kuuza hii ni mali ya serikali ya kijiji kisha mnageuka kushutumu wengine kumbe ninyi  wenyewe ndio wahusika, OCD. Huyu mwenyekiti aliyeshiriki kuratibu mauziano na kulipwa 500,000 na huyu aliuza eneo la mlima kwa sh 20,000,000 naondoka nao, pia naagiza watu wengine 48 waliohusika kwenye kuuza wajisalimishe polisi,  vinginevyo watafutwe popote walipo na wafikishwa kwenye vyombo vya sheria," alisema.


Hata hivyo, Shaka alipiga marufuku na kuweka zuwio la kuendeleza shuhuli yoyote katika eneo la mlima unaodaiwa kuuzwa huku akisisitiza kuwa waliouziwa maeneo hayo wametapeliwa na bado ni mali ya Serikali.


"Viongozi mpo mnayaona kitongoji, kijiji, kata wote mnajua lakini mnalea uovu huu, haiwezekani kila aliyehusika kwenye hili hatabaki salama ili iwe fundisho kwa wengine, naomba wajuilisheni wote walionunua eneo lile wametapeliwa na hatutasita kuchukua hatua kwa yoyote atakaekaidi maelekezo ya serikali.


"Kibaya zaidi baada kufanya uovu mnatafuta watetezi ambao na wao kwa kukosa busara na sababu wanatafuta umaarufu wa kisiasa,  wanalibeba jambo bila kulifanyia utafiti na kujridhisha kumbe mnawaingiza mkenge.


"Nilishangaa sana viongozi wa chama kimoja cha siasa wakilibeba jambo hili wakidai wananchi wananyang'anywa ardhi wanapigwa na kuondoshwa katika maeneo yao, kumbe mumewalisha matango pori mnaficha uovu wenu na wao kwa vile maarifa yao madogo wakaona ndio ajenda ya kuibeba limebuma sasa warudi kukanusha uongo waliouaminisha umma wa watanzania. Alifafanua Shaka.


Mwenyekiti wa Kijiji cha Msowero Abdalla Machera alimueleza mkuu wa wilaya kuwa katika siku za karibuni viongpzi wa kisiasa wamekuwa wakifika katika maeneo yao huku wakilazimisha wananchi kupigwa picha na kutoa malalamiko ama shutuma za uongo  dhidi ya serikali jambo ambalo amesema sio la kiungwana na kistarabu.


" Mhe DC unayoyasikia huko ni kutaka kuchafua kata yetu na viongozi wetu ninyi ili wao kutafuta kuungwa mkono kwa mambo ya uongo na uzushi, yaliopo hapa ni baadhi ya wananchi kujihusisha katika matendo maovu sasa wakiona mnataka kuwachukulia hatua wanakimbilia kwa viongozi wa kisiasa ili wapaze sauti wakidhania wanaweza kuzima uovu wao wasichukuliwe hatua kwa makosa  yao, haiwezekani, wameuza mlima wetu ekari 1158" Alisema Abdallah mKweche  mkti wa kijiji Msowero


Jumla ya wananchi 50 wanadaiwa kuhusika katika kuuza Mlima Gongwe wenye ukubwa wa ekari 1128 kwa watu mbali mbali kutoka nje ya wilaya kwa ajili ya shuhuli za kilimo na ujenzi wa makaazi na wengine kuvamia kuweka maakazi na kilomo ambapo imebainika kuna uharibifu mkubwa wa mazingira.






WAHITIMU MAFUNZO YA AWALI YA KIJESHI KWA KUJITOLEA WAASWA KUWA WAZALENDO. 

 

Na Mwandishi wetu,
Lindi.

 Brigedia Jenerali Charles Peter Feruzi amewataka vijana waliohitmimu  mafunzo ya awali ya kijeshi ya jeshi la kujenga Taifa (JKT)  kuwa wazalendo waaminifu  katika kusimamia na kuijenga  nchi yao.

Brigedia Jenerali Charles Feruzi ametoa rai hiyo wakati akifunga mafunzo ya awali ya kijeshi kwa kujitolea  oparesheni ya miaka 60 ya Jeshi la kujenga Taifa (JKT) Kikosi cha 843 huko Wilayani Nachingwea 

Amewataka wahitimu hao kutumia Mafunzo waliyoyapata katika kuijenga na kuilinda Nchi  kwa kuzingatia kiapo chao.

Pia amewataka kujiepusha na matumizi yasiyofaa katika mitandao ya kijamii na  badala yake waitumie mitandao katika kujifunza na kwa manufaa bila kuvunja sheria na Taratibu za Nchi yao.

Luteni Kanali Nyagalu  Malecela ni mkuu wa kikosi cha 843 Nachingwea amesema vijana hao wakiwa kambini hapo kwa majuma 16  wameweza kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo mafunzo ya awali ya kijeshi na kuwajenga vijana hao kuwa wakakamavu pamoja na wazalendo

Awali akitoa salamu za Wilaya katibu tawala wa wilaya ya Nachingwea Haji Mabruck Balozi, aliwasihi wahitimu hao  kuendelea kujiendeleza kimasomo.

" ni kwa kupitia Elimu kijana unaweza kuwa Meneja wa Benk, Mkuu wa kikosi, Mbunge , Waziri na Hata Rais hivyo niwasihi vijana kujiendeleza kimasomo ili mfikie malengo yenu" alisema Balozi.

Nao baadhi ya wahitimu  wakaeleza umuhimu wa mafunzo hayo sambamba na kuwasihi vijana wengine kujiunga na jeshi hilo








Thursday, May 2, 2024

MAHAKAMA YAELEZWA NATHWANI ALIVYOMJERUHI JIRANI YAKE.

 

Bharat Nathwani katikati na mke wake Sangita Bharat anayeshuka ngazi wakishuka kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam jana kusikiliza kesi yao ya kumjeruhi jirani yao.

.....................

Na Mwandishi Wetu

MSIMAMIZI wa Msikiti wa Wahindi Lohana aitwae, Ankit Dawda (32) ameileza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jinsi wanandoa Bharat Nathwan (57) na Sangita Bharat (54) walivyomshambulia jirani yao Lalit Ratilal na kutoa matusi ya nguoni kwa lugha ya kihindi.


Wanandoa hao ambao ni raia wa Tanzania wenye asili ya kihindi wanaoishi Mtaa wa Mrima - Kisutu, jengo la Lohana Dar es Salaam wanaotuhumiwa kwa mashitaka manne likiwemo la kujeruhi waliyoyatenda Julai 21,2023 kinyume cha sheria.


Dawda alidai hayo jana mbele Hakimu ya Hakimu Mkazi Mkuu,  Aaron Lyamuya wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa kwa mashahidi wa upande wa mashtaka.


Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Grace Mwanga akisiadiana na Frank Rimoy, Dawda alidai kuwa kazi yake anasafisha mazingira ya msikiti, kupamba na kutoa mapambo pia kukusanya vitu vya msikiti huo, na kusimamia usafi na ukarabati jengo nzima yenye nyumba za makaazi ambapo msikiti huo upo katika na jengo hilo.


Alidai kuwa Julai 21,2023 alikuwa ofisini kwake akiendelea na majukumu yake ya kazi, ghafla alifuatwa na watu ambao hakuwafahamu wakimueleza kwamba aende akaangalie  juu ya ghorofa kuna makelele.


Alidai kuwa alivyofika juu alikuta Sangita Bharat akilalamika na kuwafokea mafundi waliokuwa wakifanya ujenzi katika eneo hilo watoe viroba vya vigae vilivyokuwa katika kibaraza wakati vitu vyote vilikuwa katika eneo la Lalit Ratilal na hakuna kitu kilichopo katika eneo la Sangita Bharat.


Dawda alidai kuwa kwa wakati huo kulikuwa na kelele nyingi zinaendelea, ndipo Sangita Bharat akaendelea kupaza sauti yake kwamba uchafu uliyokuwa katika kibaraza chao utoke.


"Kwa sababu hao mafundi hawakutoa hivyo vigae, Sangita Bharat akaanza kurusha matusi kwa lugha ya kihindi, na hapo hapo waume zao wakawasili na Sangita akawa anaendelea kutoa matusi ambapo Kiran Lalit akapigwa na Bharat Nathwani - mume wa Sangita, hadi kuzamisha kichwa chake kwenye ndoo  ya saruji akatumbukia huko na mume wake naye akapigwa kifuani, kichwani na mguuni akadondoka chini akazimia".


"Waliita ambulance wakamshusha chini wakapelekwa hospitali lakini sikujua ni hospitali gani wamepelekwa,"alidai Dawda


Kesi imeahirishwa hadi Juni 3,2024 kwa ajili ya kuendelea kwa mashahidi wa upande wa mashitaka.


Awali, Fundi Seremala, Dominic Mpakani (43) aliileza mahakama jinsi mshitakiwa Bharat Nathwan allivyomshambulia jirani wake, Lalit Ratilal kwa kumpiga kichwa kifuani kisha akadondoka chini na nakupoteza fahamu kwa muda.


Aidha, alidai kuwa kulikuwa na ugomvi kati ya mke wa Bharat (Sangita Bharat) na mke wa Lalit, (Kiran) ambao walikuwa wakirushiana maneno kwa ukali kwa lugha ya kihindi huku, baada ya muda kidogo waume zao walifika kwa pamoja na kuingilia ugomvi huo.


Alidai kuwa Julai 21,2023 alikuwa nyumbani kwa Lalit Ratilal maeneo ya mtaa wa Mrima katika jingo la Lohana, alimuita kwa ajili ya kuifanyia kazi zinazohusiana na mbao na kazi zingine ndogo ndogo.


Alidai kuwa alifika katika jengo hilo saa tatu asubuhi ambapo bosi wake huyo anakaa floor ya tatu, wakati anaendelea na kazi alidai kuwa Sangita alikuwa amesimama kwenye dirisha lake na Kiran alikuwa amesimama kwenye mlango wake, kila mmoja alianza kuzungumza kwa ukali na kwa jaziba wakitumia lugha ya kihindi.


"Lakini nilimsikia mke wa Bharat, Sangita akimwambia mke wa Lalit kwamba uchafu wake apeleke huko ambapo vitu vyote vilikuwa vimewekwa katika eneo la Lalit na hakuna kitu chochote kilichokuwa katika eneo la Sangita. Baada ya dakika kadhaa sijui walipiga simu au vipi waume zao walikuja kwa wakati mmoja na malumbano yakaendelea kwa wote wanne," alidai Fundi Mpakani


Shahidi huyo alidai kuwa, wakati malumbano hayo yanaendelea wote walikuwa wamesimama kwenye mlango wa Lalit, baada ya muda Bharat akampiga kichwa Lalit na Lalit akadondoka chini na kupoteza fahamu.


Shahidi mwingine ambae ni Dk Lucia Augustino (52) wa Hospitali ya Mnanzi Mmoja alidai kuwa Julai 21,2023 alikuwa Idara ya Dharura chumba namba  20 muda wa mchana alipokea wateja wawili wenye asili ya kiashia walikuwa wamechafuka kuanzia kichwani hadi miguuni , mama alichafuka sana kuliko baba.


Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, washitakiwa hao ambao ni raia wa Tanzania jinsia ya kihindi wanaoishi Mtaa wa Mrima - Kisutu, jingo la Lohana Dar es Salaam wanaotuhumiwa kwa mashitaka manne waliyoyatenda Julai 21,2023.


Katika shitaka la kwanza la kujeruhi linalomkabili Nathwani peke yake, ambapo anatuhumiwa Julai 21,2023 akiwa eneo la mtaa wa Mrima-Kisutu, jingo la Lohana, ndani ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam kinyume cha sheria alimsababishia madhara makubwa Kiran Lalit kwa kuzamisha kichwa chake kwenye ndoo la saruji iliyochanganywa.


Pia, katika shitaka la pili la shambulio la mwili linalomkabili Nathwani peke yake, ambapo tarehe hiyo na eneo hilo alimsababishia madhara Lalit Ratilal katika mwili wake kwa kumpiga kichwa, ngumi na mateke kichwani.


Ilidaiwa kuwa katika shitaka la tatu na la nne linalomkabili Sangita peke yake, ambapo anatuhumiwa kutoa matusi makubwa dhidi ya Lalit na Kiran kitendo ambacho kilileta fujo kwa namna ambayo inaweza kuleta uvunjifu wa amani.



Wednesday, May 1, 2024

NEMC YAPIGA KAMBI KANDA YA ZIWA KUELIMISHA MATUMIZI YA ZEBAKI.

 





Na Mwandishi Wetu

BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kushirikiana na ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali wameanza kampeni ya kutoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya zebaki kwa migodi ya dhahabu kanda ya ziwa.


Akitoa elimu hiyo kwa wachimbaji wa migodi ya Wilaya ya Misungwi Mwanza, Meneja wa usajili wa kemikali na maabara za kemia, kutoka Ofisi ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Musa Kazumila, alisema elimu hiyo inatokana na matakwa ya mkataba wa Minamata (Minamata convention).


Alisema mkataba huo unataka kutekeleza matakwa yake ambapo moja likiwa la kudhibiti matumizi ya zebaki kwa wachimbaji wadogo na kuongeza kuwa wameanza na wachimbaji wa migodi ya Chata, Shokeraera, Shilalo na luhala zilizopo Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza.


Alisema katika mradi huo unaofadhiliwa na Benki ya  Dunia na  kuratibiwa na (NEMC), Mkemia Mkuu amepewa jukumu la kutoa elimu ya usimamizi salama pamoja na matumizi salama ya zebaki kwani ndiye anayesimamia utekelezaji wa Sheria Na.3 ya mwaka 2003 inayohusu usimamizi na udhibiti wa kemikali za viwandani na majumbani ikiwemo zebaki.


Aidha, alisema  lengo la utoaji wa elimu hiyo pia ni kuwajengea uwezo wachimbaji na watumiaji wa zebaki ili waweze kutambua jinsi zebaki inavyoingia mwilini, madhara yake namna ya kujikinga.


Naye Dereki Masako kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Dodoma, aliainisha maeneo ambapo madhara ya zebaki yanatokea kuwa ni wakati wa usagaji wa mawe na kudondosha matope ili zebaki ikamate na wakati wa uchukuaji wa kusanyiko anapokamua na kitambaa kwani matone hudondoka chini na kusambaa ardhini na hewani na kuleta madhara.


Alisema ni vyema wachimbaji wakatumia vifaa Kinga ili kujilinda dhidi ya athari za zebaki na kubainisha madhara yake kuwa ni kuharibu mfumo wa fahamu na kuleta athari ya kushindwa kuhisi, kukakamaa kwa mwili, macho na kuharibika kwa Figo.


Alisema zebaki huathiri ukuaji wa mtoto kwa mama mjamzito kupita kwenye kondo la mama, kupoteza nguvu za kiume kwa wanaume, msongo wa mawazo na mwili kuwasha na kupungua.


Mmoja wa wachimbaji, Haji Nasri, alikiri kutokuwa na uelewa wa madhara ya zebaki na kwamba wamefurahishwa  na elimu hiyo kwani wengi wao wamekuwa wakijishughulisha na uchimbaji wa dhahabu bila kuzingatia madhara ya kiafya yanayoweza kutokea.