Friday, September 29, 2023

RAIS WA ZANZIBAR KATIKA SWALA YA IJUMAA,MASJID JAMIUU

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi (wa tatu kulia) leo ameshiriki ibada ya swala ya ijumaa katika Masjid Jamiuu Zinjibar pamoja na Waumini wengine kama wanavyoonekana katika picha wakiitikia Dua iliyosomwa na  Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi  (katikati)  baada ya Ibada ya   Swala hiyo ya ijumaa, Mazizini  Mkoa wa Mjini Magharibi. [Picha na Ikulu] 29/09/2023

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi (kushoto) akisalimiana na Balozi Mdogo wa Oman hapa Zanzibar Mhe.Said Salim Al Sinawi pamoja na Viongozi wengine wakati alipowasili katika Masjid Jamiuu Zinjibar Mkoa wa Mjini Magharibi  leo kushiriki katika Swala ya Ijumaa. [Picha na Ikulu] 29/09/2023.

Waumini wa Dini ya Kiislamu waliohudhuria Ibada ya Swala ya Ijumaa leo, Masjid Jamiuu Zinjibar,Mkoa wa Mjini Magharibi wakiitikia Dua Iliyoombwa baada ya  ibada hiyo, iliyowajumuisha  Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi na Viongozi mbali mbali. [Picha na Ikulu] 29/09/2023.
 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi (kulia) akisalimiana na Sheikh Salum Mardhia baada ya kumalizika kwa ibada ya Sala ya Ijumaa Leo katika masjid Jamiuu Zinjibar Mazizini  Mkoa wa Mjini Magharibi. [Picha na Ikulu] 29/09/2023.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi (kushoto) akiteta na Mkurugenzi wa Mkuu wa Kituo cha Ahmed Al Faatih  cha Kiislamu -Bahrain Bw.Nawaf Rasshid Al Rashid (katikati) baada ya Ibada ya   Swala ya Ijumaa katika  Masjid Jamiuu Zinjibar Mazizini  Mkoa wa Mjini Magharibi.[Picha na Ikulu] 29/09/2023.


TANZANIA YATANGAZA UTAJIRI WA MADINI MKAKATI UFARANSA

 

Dkt. Kiruswa asema Tanzania mdau muhimu kuokoa Dunia na uchafuzi wa mazingira.

Atumia jukwaa hilo kunadi fursa za uwekezaji nchini

......................

Paris, Ufaransa.

Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye rasilimali madini kwa wingi yakiwemo Madini Mkakati ambayo mahitaji yake yanazidi kuongezeka kutokana na kutumika kuzalisha aina tofauti za vyanzo vya nishati na teknolojia zinazohitaji aina mbalimbali za madini mkakati kama vile Lithiamu, Nikeli, Kobalti, Manganese na Grafiti.


Ameyasema hayo Septemba 28, 2023, jijini Paris nchini Ufaransa wakati akihutubia Mkutano wa Kilele wa Usalama wa Madini Mkakati ambao umejadili masuala muhimu kuhusu madini hayo, kubadilishana uzoefu pamoja na kujadili namna ya kushiriki katika kuchochea usimamizi na usambazaji endelevu wa madini hayo.


Alisema kuwa kutokana na mwelekeo wa sasa teknolojia, zinahitaji aina mbalimbali za madini mkakati na kwamba, nchini Tanzania madini hayo yanapatikana kwa wingi.


“Ndugu Washiriki, mengi ya madini mkakati yanayohitajika kwa mabadiliko ya nishati safi yanapatikana kwa kiasi kikubwa nchini Tanzania. Hizi ni pamoja na rasilimali muhimu ya Grafiti, Nikeli, Kobalti, Lithiamu, Vipengee Adimu vya Dunia (Rare Earth Elements [REE]), Shaba, Manganese, Zinki na Alumini.” alisema Dkt. Kiruswa.


Aidha, Dkt. Kiruswa alisema kuwa kutokana na uwepo wa rasilimali hizo Tanzania ni miongoni mwa wadau muhimu katika Mkakati wa Mpito wa Nishati Safi kutokana na kuwa na Rasilimali Madini muhimu na Mkakati ya aina mbalimbali kwa kiasi kikubwa.


Sambamba na hilo, Dkt. Kiruswa aliueleza mkutano huo kuwa, miongoni mwa masuala yanayohitaji mkakati wa pamoja wa kimataifa, ni pamoja na namna bora ya ugavi wa madini hayo, uboreshaji wa uwazi wa masoko, kuongeza kasi ya teknolojia za uvumbuzi na uchakataji na kukuza mazoea ya maendeleo endelevu na yenye uwajibikaji.


Aidha, alitumia jukwaa hilo kuwakaribisha wawekezaji kuwekeza nchini na kuongeza kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi barani Afrika ambazo zina amani na utulivu mkubwa kisiasa.


“Tanzania imeunganishwa vyema na mitandao mizuri ya barabara inayofanya mikoa na wilaya zote kufikika. Faida nyingine kubwa ya kuwekeza nchini Tanzania ni uwepo wa mfumo ujao wa reli ya kisasa ya Standard Gauge (SGR) ambao unaendelea kujengwa kuanzia Bandari ya Dar es salaam hadi katika nchi jirani zisizo na bandari zikiwemo Rwanda, Zambia, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC)” aliongeza Dkt. Kiruswa.


Mbali na Naibu Waziri, wengine walioshiriki kutoka Wizara ya Madini ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo, Kamishna Msaidizi wa Madini sehemu ya Uendelezaji Migodi kutoka Wizara ya Madini, Terence Ngole, Kaimu Mkurugenzi wa Kanzidata kutoka Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania ( GST) Hafsa Seif.


Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Mawaziri, Wafanyabiashara, Wawekezaji, taasisi za kimataifa na taasisi za kiraia kutoka nchi tofauti Ulimwenguni.


Katika hatua nyingine Ujumbe huo wa Tanzania ulipata nafasi ya kuzungumza na wadau wengine wa Sekta ya Madini kutoka mataifa mbalimbali ikiwemo India ambapo ulizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Kabir ambayo ni sehemu ya Shirika la Madini la Taifa Nchini India, lengo likiwa ni kuona namna nzuri ya kuanzisha ushirikiano wa kikazi na kubadilishana ujuzi kwenye Sekta ya Madini.





CP. WAKULYAMBA ATOA SOMO LA MIONGOZO YA JESHI LA UHIFADHI.

 

Na Sixmund Begashe


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Kamishna Benedict Wakulyamba amewataka askari wa Jeshi la Uhifadhi kufanya kazi kwa kufuata Miongozo, Kanuni na kuzingatia sheria zilizopo ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Uhifadhi.

CP. Wakulyamba ametoa kauli hiyo Jijini Arusha kwenye Warsha maalum aliyoianda kwa Maafisa wa Jeshi la Uhifadhi chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa lengo la kukumbushana masuala mbalimbali ya uhifadhi pamoja na haki za binadamu kama sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan la kumtaka arejeshe nidhamu ya Jeshi hilo.


Katika somo alilotoa kwa Maafisa hao wa Jeshi la Uhifadhi, CP. Wakulyamba alisisitiza nidhamu katika matumizi sahihi ya sare za Jeshi hilo pamoja na matumizi ya nguvu katika kukabiliana na uhalifu hususani kwenye matumizi ya Silaha.



Aidha CP. Wakulyamba amelitaka Jeshi hilo kuimarisha mahusiano mema na Vyombo vingine vya ulinzi na Usalama, taasisi za Serikali na wananchi kwa ujumla kuwa kazi ya uhifadhi ni jukumu la kila Mtanzania kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kinachokuja.












CHATANDA AFURAHISHWA NA UTEKELEZAJI WA ILANI YA CCM WILAYANI CHATO. 

 


Mwenyekiti wa Umoja wa wanawake Tanzania UWT, Mary Chatanda, amefurahishwa na Utekelezaji wa Ilani ya CCM wilayani Chato Mkoani Geita alipotembelea Miradi mbalimbali ya Maendeleo katika wilaya hiyo .

Akizungumza leo  katika Mradi  wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Chato Mwenyekiti Chatanda amewapongeza viongozi wa Serikali chini ya Mkuu wa wilaya ya Chato Deusdedith Katwale ambaye ameshirikia na Mkurugenzi wake wa Halmashauri kwa usimamizi na Ufanisi wa hali ya Juu .

" Fedha ya Serikali zaidi ya Bilion 31 imejenga Hospitali hii ya Kanda ya Chato niwaombe wauguzi wa Hospitali hii muwahudumie wagonjwa vinzuri kwa kuwa wananchi mbalimbali watakuja kutibiwa hapa hivyo Uadilifu, upendo na hekima ili wananchi wafurahie matunda ya Rais Samia kwa upande wa  afya katika kupata huduma bora kwa wauguzi wao."

 

TUSIKIMBIE KUFANYA KAZI VIJIJINI - KIKWETE

 

Watumishi wa Serikali wametakiwa kuacha tabia ya kukimbia kufanya kazi sehemu wanazopangiwa na kuchagua sehemu wanazotaka wao.



Maneno hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora Ndg. Ridhiwani Kikwete alipokuwa anazungumza na watumishi wa Halmashauri ya Chalinze katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri hiyo.


Ndg. Kikwete alitumia mkutano huo kuwakumbusha watumishi umuhimu wa kufanya kazi kuzingatia misingi ya kazi ikiwemo kujitambua na kutambua tunaowahudumia. 


Katika kusistiza utumishi wenye tija na weledi, Naibu Waziri huyo aliwakumbusha watumishi kuendelea kuwahudumia wananchi wote sawa na hakuna sababu ya kuchagua na kuweka madaraja katika utoaji wa huduma. 


Katika mkutano huo , Ndg. Kikwete alitumia nafasi hiyo pia kuwakumbusha umuhimu wa kutochagua vituo vya kazi huku akiwakumbusha kuwa uchaguzi wa Vituo vya kazi unalenga sio tu kuwasaidia baadhi lakini unatengeneza madaraja katika utumishi wa umma. 


Aidha, Kikwete alitumia nafasi hiyo kuwaasa watumishi wa umma kutochagua vituo vya kazi na badala yake mtumishi kila mtumishi anapopangiwa sehemu fulani ya kazi anapaswa kutekeleza kwa mujibu wa maelekezo.


Popote ambapo utapelekwa pana hadhi ya mtumishi kufanya kazi na kuwakumbusha hasa wazazi kuacha utaratibu wa kupiga simu za kuwaombea watoto wao vibali vya kuhamishwa vituo wapelekwe mijini. 


Katika kikao hicho Ndg. Kikwete pia aliwapongeza watumishi wa halmashauri hiyo kwa kazi nzuri wanayoifanya. 



MAGAZETI YA LEO IJUMAA TAREHE 29 SEPTEMBA 2023.

 


























Thursday, September 28, 2023

MAJALIWA: VIONGOZI WA DINI TUSHIRIKIANE KUPIGA VITA DAWA ZA KULEVYA

 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewasihi viongozi wa madhehebu ya mbalimbali ya dini nchini waendelee kushirikiana na Serikali katika kupiga vita biashara na matumizi ya dawa za kulevya . 


 


"Tushirikiane kupambana na biashara na matumizi ya dawa za kulevya ambayo yameathiri zaidi vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa." 


 


Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo leo (Alhamisi, Septemba 28, 2023), alipomuwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Baraza la Maulid lililofanyika Kitaifa jijini Dodoma kwenye kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete.


 


“Matumizi ya dawa za kulevya yana madhara mengi kwa Taifa yakiwemo ya kiuchumi, kiafya na kimazingira pamoja na kuathiri uwezo wa mtu kufikiri”


 


Pia, Waziri Mkuu ametoa rai kwa viongozi wa dini waendelee kukemea vitendo vya mmomonyoko wa maadili katika jamii na wawahamasishe waumini kushiriki katika shughuli zitakazowaongezea kipato. 


 


Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka wananchi waendelee kudumisha amani nchini kwa kuwa amani ni jambo la msingi katika maendeleo ya Taifa. "Tuendelee kuishi kwa amani na upendo pamoja na kuliombea dua Taifa na viongozi wakuu. " 


 


Wakati huo huo, Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwahakikishia wananchi kuwa Serikali itaendelea kuwachukulia hatua wale wote watakaobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa pamoja na matumizi mabaya ya madaraka, hivyo waendelee kuiamini Serikali yao. 


 


Awali, Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Alhaj Nuhu Jabir Mruma amesema kuwa Baraza hizo linaridhishwa na utendaji kazi wa Rais Dkt. Samia za kuwaletea watanzania maendeleo katika Sekta za Uchumi, Siasa, Kijamii pamoja na kuboresha mfumo wa demokrasia nchini.


 


Aidha, Alhaj Mruma ametumia fursa hiyo kuiomba Serikali iongeze wigo wa kutoa elimu ya uraia kwa kushirikiana na viongozi wa dini ili kuwawezesha wananchi kupata uelewa na washiriki katika chaguzi zijazo ukiwemo wa Serikali za Mitaa inayotarajiwa kufanyika 2024.