Friday, March 20, 2020

MGALU- VIWANDA 50 PWANI, MTWARA NA DAR KUUNGANISHWA NA NISHATI YA UMEME WA GESI ASILIA

Naibu Waziri wa Nishati Mh. Subira Mgalu akizungumza jambo kuhusiana na mikakati ya serikali ya awamu ya tano ya kuweka mipango ya kuunganisha nishati ya umeme wa gesi asilia katika viwanda vipya 50 wakati wa ziara ya Kamati ya kudumu ya bunge ya nishati na madini ambayo ilifanya ziara yake ya kikazi ya kutembelea baadhi ya viwanda vilivyopo katika Wilaya ya Mkuaranga. (Picha na Victor Masangu).
.....................................


VICTOR MASANGU, MKURANGA.
 Naibu Waziri wa nishati Subira Mgalu amesema katika kutimiza azma ya Tanzania kuwa na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 serikali imedhamiria kusambaza na kuwaunganishia  nishati ya umeme wa gesi asilia  katika viwanda vipya vipatavyo 50  ambavyo vimepitiwa na bomba la gesi ikiwemo Mkoa wa Dar es Salaam Pwani pamoja na Mtwarana.

Mgalu  aliyasema hayo wakati wa ziara ya kikazi ya kamati ya kudumu ya bunge ya nishati na Madini ambayo wameifanya  kwa lengo la kutembelea baadhi ya viwanda vilivyopo Wilayani Mkuranga Mkoa wa Pwani  ambavyo vinajiendesha kwa kutumia nishati ya umeme ikiwa ni pamoja na kuzungumza na wawekezaji ili kubaini changamoto wanazokabiliana nazo na kuzitafutia ufumbuzi.

Naibu Waziri huyo alibainisha kwamba kwa sasa serikali ya awamu ya tano mpango wake mkubwa ni kuhakikisha inasambaza na kuviunganishia viwanda mbali mbali nishati ya umeme ili viweze kutimiza malengo ya azma ya serikali ya kuwa na uchumi wa kati pamoja na kutoa fursa  mbali mbali za ajira kwa vijana  ambao ni wazalendo  lengo ikiwa waweze kujikwamua na wimbi la umasikini.

“Mpango wetu wa serikali licha ya kuwa bado kuna baadhi ya maeneo ya viwanda hayajafikiwa na nishati ya umeme lakini kwa sasa kupitia nishati ya gesi asilia tuna mpango wa kuviunganishia viwanda vipya vipatavyo 50 ambavyo vipo katika Mikio ya Dar es Salaam, Mtwara pamoja na Mkoa wa Pwani hivyo juhudi za makusudi bado zinaendelea kwa hiyo viwanda ambavyo vinapitiwa na bomba kubwa la gesi vitaweza kunufaika.

Aidha Naibu Waziri huyo alifafanya kwamba pindi mradi wa umeme wa bwawa la Mwalimu Nyerere uliopo Wilayani Rufiji utakapokamilika utaweza kuwa ni mkombozi mkubwa kwa wawekezaji wa viwanda vidogo, vya kati na vile vikubwa kutoka maeneo mbali mbali sambamba na kuwaunganishia wananchi wengine pamoja na taasisi za serikali na sizozo  za serikali.

Katika hatua nyingine Mgalu ameipongeza kamati ya kudumu ya bunge ya nishati na madini kwa kuweza kwenda kutembelea katika kiwanda cha kuzalisha chuma pamoja na mabomba ya maji ili kuweza kubaini changamoto mbali mbali ambazo zinawakabili wawekezaji na hatimaye kuweza kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu ambao utasaidia kutimiza azma ya serikali ya kuwa na uchumi wa kati kupitia viwanda hivyo.
Kwa upande wake  Kaimu mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya bunge ya nishati na Madini Vedastus Matayo alibainisha kwamba ujenzi wa kiwanda hicho utaweza  kuipunguzia serikali gharama kubwa ambazo zimekuwa zikitumia kwa ajili ya kuagiza baadhi ya Nondo kutoka nje ya nchi hivyo amempongeza mwekezaji huyo kwa  kuwekeza katika  Wilaya ya Mkuranga kwani kumesaidia vijana zaidi ya 1,300 kupata fursa ya ajira.

“Sisi kama kamati kwa kweli tunapenda kumpongeza mwekezaji huyo kwa kuweza kuwekeza katika Wilaya ya Mkuranga ambayo ipo katika Taifa letu ya Tanzania hii ni hatua nzuri ambayo ameifanya na kwa sasa anazalisha bidhaa mbali mbali kwa kutumia nishati ya umeme wa gesi asilia hivyo kutaweza kuleta mabadiliko chanya ya kimaendeleo kwa wananchi wenyewe pamoja na wale wawekezaji wa ndani na nje ya nchi,”alibainisha  Matayo.

Aidha Matayo katika hatua nyingine alibainisha kuwa Kamati ya bunge ya nishati ya kudumu ya nishati na  madini  ilibaini kuwepo kwa urasimu na ucheleweshaji wa vibali kutoka kwa baaadhi ya mamlaka zinazohusika kwa wawekezaji wa sekta ya viwanda pamoja na gharama ya nishati ya umeme kuwa ni kubwa hivyo hivyo watayachukua mapendekezo hayo kwa ajili ya kuyawasilisha bungeni ili serikali iweze kuyatafutia ufumbuzi wa kudumu.

Pia alisema kuwa mapendekezo pamoja na changamoto mbali mbali ambazo wamekutana nazo katika kiwanda hicho ikiwemo na maeneo mengine ambayo tayari wameshayapitia watayawasilisha serikalini ili yaweze kufanyiwa kazi ikiwemo na kutilia mkazo katika suala la usumbufu mkubwa wanaoupata wawekezaji pindi wanapohitaji kuagiza matilio mbali mbali kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kutengeneza bidhaa zao.

Awali  akitoa taarifa mbele ya Kamati ya nishati na madini Mkurugenzi mtendajiwa wa kiwanda hicho cha kuzalisha chuma, Haruni Lodhia amebainisha kwamba hapo awali walikuwa wanakabilia na changamoto kubwa ya ukosefu wa nishati ya umeme wa uhakika pamoja na miundombinu ya barabara,ambapo ameipongeza serikali ya awamu ya tano kupitia Shirika la maendeleo ya  Petroli Tanzania (TPDC) kwa litafutia ufumbuzi suala hilo na hatimaye kuanza utekelezaji wa kuzalisha bidhaa mbali mbali, ikiwemo Nondo, mabomba ya maji na bodi za jasi.
Mmoja wa wakurugenzi wa kiwanda cha Lodhia ambacho kinajishighulisha na uzalishaji wa bidhaa mbali mbali ikiwemo chuma, akiwaonyesha wajumbe wa kamati ya bunge ya nishati na madini jinsi ya kiwanda hicho kinavyofanya kazi pamoja na kuwaelezea changamoto mbali mbali zinazowakabili ili kuziwasilisha kwa serikali zifanyiwe kazi. (Picha na Victor Masangu).
Badhi ya wabunge wanaounda kamati ya nishati na madini wakati wanaingia katika kiwanda cha kuzalishia chuma cha Lodhia ikiwa ni moja ya ziara yao ya kikazi kwa ajili ya kuijionea shughuli mbali mbali zinazofanywa na wawekezaji pamoja na kubaini changamoto zao, wa kati kati ni Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa. (Picha na Victor Masangu).
Baadhi ya wajumbe wa kamati ya bunge ya nishati na madini wakiwa na viongozi mbali mbali wa kiwanda hicho wakitembezwa katika maeneo mbali mbali ili kuweza kujionea mwenendo mzima wa vyuma chakavu vinavyoyayushwa na kutengenezwa Nondo mpya kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbali mbali ikiwemo ile ya serikali. (Picha na Victor Masangu)
 Kaimu mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya bunge ya nishati na Madini Vedastus Matayo akipokea maelekezo kutoka kwa mmoja wa viongozi wa kiwanda cha kuzalishia chuma cha Lodhia kilichopo kata ya Kisemvule wakati wa ziara ya kamati hiyo ilipokwenda kwa ajili ya kujionea shughuli mbali mbali za uzalishaji kiwandani hapo (Picha na Victor Masangu).

Mwonekano wa mtambo maalumu wa kuzalishia nishati ya umeme wa gesi asilia ambao umefunngwa na  shirika la TPDC katika kiwanda hicho cha kuzalishia chuma pamoja na kutengenezea  mabomba ya maj wakati wa ziara hiyo ya kamati ya bunge ya nishati na madin.(Picha na Victor Masangu)
 Mkurugenzi mtendaji wa kiwanda cha Lodhia  Haruni Lodhia ambacho kinajihusisha na uzalishaji wa kutengeneza Nondo pamoja bidhaa zingine mbali mbali akizungumza mbele ya wajumbe  kamati ya bunge ya nishati na madini  hawapo pichani ilipofanya ziara ya kikazi ya kutembelea kiwanda hicho. (Picha na Victor Masangu)
 

WAHAMIAJI HARAMU 49 WAKAMATWA BAGAMOYO.

Wahamiaji haramu 49 wamekamatwa  Wilayani Bagamoyo usiku wa kuamkia tarehe 19/03/2020 Wahamiaji hao haramu wamekamatwa na raia wema wakishirikiana na Jeshi la Polisi Wilayani Bagamoyo katika Kijiji cha Kidomole Kata ya Fukayosi.

Raia hao 49 wa Ethiopia wamekiri kuingia nchini kinyume cha sheria kwa kupitia pwani ya Bagamoyo wakitumia majahazi ikiwa lengo lao ni kuelekea Afrika kusini.

Akizungumzia tukio hilo Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ambae pia ni Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Mhe. Zainab Kawawa amesema kuwa walipokea taarifa toka kwa raia wema juu wa uwepo wa kundi la watu wasiofahamika katika Kijiji cha Kidomole kilichopo Kata ya Fukayosi, na baada ya taarifa hiyo hatua za haraka zilichukuliwa na Jeshi la Polisi Wilayani humo kufika eneo la tukio na kufanikiwa kuwakamata wahamiaji hao haramu 49.

Mhe. Zainab ameongeza kwa kusema kuwa, kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Corona ulioingia Nchini, tumeona ni vyema kuwafanyia vipimo vya awali vya kiafya wahamiaji hawa ili kujiridhisha kuwa wako salama kabla hawajaendelea na taratibu zingine za kimahakama.

"Hivyo tumewaleta hapa katika Kituo cha Afya Matimbwa ili kuwaangalia Afya zao kwanza hasa joto la mwili kuwaangalia kama wana homa kali, kama wana dalili zozote za kikohozi, au mafua makali, kisha wataendelea na taratibu zingine za kisheria, Alisema Kawawa.

 “Niwapongeze Wananchi wema waliosaidia kukamatwa kwa wahamiaji hawa haramu, lakini pia nitoe rai kwa Wananchi wote wa Bagamoyo kuwa wazalendo na kuacha kabisa vitendo vya kuwasaidia wahamiaji haramu na kufanya Bagamoyo kuwa uchochoro wa kupita kuelekea Nchi jirani, kuwasaidia wahamiaji haramu kupita Bagamoyo na kokote Nchini kunahatarisha usalama wa Nchi yetu hasa kipindi hiki ambacho Nchi nzima inapambana na mlipuko wa ugonjwa huu wa Corona” Alisema Mhe. Zainab Kawaw.

Jeshi la Polisi Wilayani Bagamoyo limekuwa likiwakamata wahamiaji haramu hasa wanaotoka Nchini Ethiopia na kuingia Nchini kwa kutumia pwani ya Bahari ya Hindi, wakiwa njiani kuelekea Nchi jirani na kuwafikisha katika vyombo vya Sheria ikiwa ni katika kupambana na uingiaji wa makundi haya ya wahamiaji haramu.

Tuesday, March 17, 2020

KITUO CHA WATOTO YATIMA MSANAGANI CHAPATIWA MSAADA NA WANAWAKE WA PWANI GENERATION

Mwenyekiti wa kikundi cha Pwani Generation  mwanamke sahihi wa kushoto akimkabidhi msaada wa vyakula mbali mbali Lilian Mbise ambaye ni Mlezi wa kituo cha kulelea watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu cha Sharom kilichopo katika eneo la Kwa mathiasi  kata ya Msangani Wilayabi Kibaha,katika halfa iliyofanyika katika kituo hicho.(PICHA NA VICTOR MASANGU).
...............................................

NA VICTOR MASANGU, KIBAHA
Watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu katika kituo cha Sharom  kilichopo kata ya Msangani Wilayani Kibaha Mkoani Pwani wamemuomba Rais Dk. John Pombe Magufuli kuwasaidia kwa hali na mali kuwatatulia changamoto mbali mbali zinazowakabili ikiwemo  ukosefu wa mahitaji ya chakulai,nguo, huduma za matibabu pamoja na ujenzi wa jengo la nyumba kwa ajili ya kuweza kuishi.

Baadhi ya watoto  hao akiwemo Sara Yendemba Dickson Michael  wakizungumza wakati wa halfa ya kupokea msaada wa mahitaji mbali mbali ikiwemo chakula kutoka kwa kikundi cha Pwani Generation mwanamke sahihi, walisema kwamba baada ya kuondokewa na wazazi wao wamekuwa wanaishi katika mazingira magumu  na wakati mwingine walikuwa wanakwenda kutafuta chakula majalalani hivyo wanahitaji msaada wa hali na mali kutoka serikalini na wadau wengine wa maendeleo ili waweze kujikimu kimasiha kama watoto wengine.


“Tunashukuru sana kwa msaada wa vyakula mbali mbali ambavyo tumepatiwa na  uongozi wa  wanawake wa Pwani Generation kwani msaad huu utaweza kutusaidia, kwakuwa  sisi hapa ni watoto yatima na wengine tunaishi katika mazingira magumu, lakini tu bado tunamuomba Rais wetu aweze kutusaidia zaidi ujenzi wa nyumba ya kulala kwani idadi yetu ni kubwa kuliko vitanda vilivyopo”walisema watoto hao kwa masikitiko makubwa.


Pia waliongeza kwamba kabla ya kufikishwa katika kituo hicho walikuwa wanaishi mitaani kwa shida kubwa sana kutokana na kukabiliwa na changamoto mbali mbali ya kukosa mavazi, chakula sambamba na mambo mengine muhimu lakini kutokana na kituo hicho angalau wameweza kupatiwa hata fursa ya kwenda shule kwaajili ya kupata elimu.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa kikundi cha Pwani Generation mwanamke sahihi,  Betty Msimbe amesema kwamba wameamua kutoa msaada huo wa mchele, mafuta, unga, sukari, pamoja na maharage katika kituo hicho kutokana na kubaini kuwepo kwa changamoto nyingi ambazo zinawakabili watoto hao ambao wanahitaji kusaidiwa mahitaji mbali mbali ili waweze kujikimu kimaisha.


Mwenyekiti huyo alisema kwamba katika kikundi chao wamekuwa na utaratibu wa mara kwa mara kwenda kutoa misaada katika vituo mbali mbali vya kulelea watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu vilivyopo katika Mkoa wa Pwani  lengo ni kuwapatia mahitaji muhimu ambayo wanastahili pamoja kwenda kuwafariji.


“Sisi kama Pwani Generation mwanamke sahihi, tumeweza kubaini kuwa kituo hiki cha Sharom ambacho kipo katika Wilaya ya Kibaha bado kinakabiliwa na changamoto mbali mbali na ndio maana tukaamua kukusanya fedha na kuamua kununua mahitaji mbali mbali ambayo wanastahili kupatiwa watoto hao kwani kutoa ni moyo na wala sio utajiri hivyo ni moja ya kuunga mkoni juhudi za serikali katika kuwasaidia watoto,”alisema Msimbe.


Naye mlezi wa Kituo hicho Lilian Mbise ambaye pia na yeye  ni yatima  amesema kwamba kituo hicho ambacho kilianzshiwa tangu mnamo mwaka 2016 kina watoto wapatao 18 ambao wanaishi katika nyumba ya kupanga hivyo kunahitajika msaada zaidi  kutoka serikalini kwa lengo la kuweza kuzitatua changamoto hizo zinazowakabili kwani mahitaji yao  ni mengi.


Kikundi hicho cha Pwani Generation mwanamke sahihi, kilitoa msaada wa vitu mbali mbali, ikiwemo unga wa sembe, sukari, mafuta ya kula, mchele,maji pamoja na mahitaji mengine ya msingi kwa ajili ya watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu katika kituo cha Sharoom ambavyo  vimegharimua kiasi cha zaidi ya shilingi milioni moja.
Baadhi ya wanawake wanaounda kikundi cha Pwani Generationi mwanamke sahihi wakiwa katika picha ya pamoja na watoto wanaoishi katika mazingira magumu na yatima mara baada ya sherehe za kukabidhi vyakula mbali mbali pamoja na mahitaji mengine ya msingvi katika kituo cha Sharom kilichopo kata ya Msangani Wilayani Kibaha.(PICHA NA VICTOR MASANGU)


 Baadhi ya watoto yatima na wale amabo wanaishi katika mazingira magumu katika kituo cha Sharom kilichopo kata ya Msangani wakiimba wimbo maalumu wakati wa halfa ya kukabidhiwa msaada wa vvyakula mbali mbali kutoka na kikundi cha Pwani Generation mwanamke sahihi kwa lengo la kuwasaidia watoto hao waweze kupata mahitaji muhimu.(PICHA NA VICTOR MASANGU)