Sunday, February 23, 2020

NMB LINDI YATOA MSAADA WA MILIONI 20 KWA SHULE ZA SEKONDARI.

 Meneja wa Bank ya NMB kanda ya kusini Bi, Janeth Shango kulia akikabidhi Meza na Viti kwa Mkuu wa Wilaya ya Lindi Mkoani humo Shaibu Ndemanga jana katika viwanja vya Shule ya Sekondari Mnolela Halmashauri ya Mtama.
..................................................


NA HADIJA HASSAN, LINDI

BANK ya NMB yatoa Msaada wa Meza, Viti , Mabati pamoja na Kofia zake kwa Shule za Sekondari za Wilaya ya Lindi Mkoani humo vyote vikiwa na thamani ya Shilingi Mlioni 20.

Msaada huo ni Meza150, Viti 150, Bati136 pamoja na kofia zake 26 ambazo zitagawiwa kwa Shule Nne za Sekondari za Wilaya hiyo.

Msaada huo umekabidhiwa na Meneja wa kanda wa Bank hiyo Janeth Shango kwa Mkuu wa Wilaya hiyo Shaibu Ndemanga jana katika viwanja vya shule ya Sekondari Mnolela Halmashauri ya Mtama.

Miongoni mwa shule zilizonufaika na mgao huo ni pamoja na shule ya Sekondari Ng’apa, iliyopo Manispaa ya Lindi ambayo imepatiwa viti 50 na meza 50, shule ya Sekondari kitomanga Halmashauri ya Mtama meza 50 na viti 50, Mnolela Sekondari halmashauri ya Mtama viti 50 na meza 50 pamoja na Shule ya Sekondari Kiwalala Mtama ambayo imepatiwa mabati 136 pamoja na kofia zake 26.

Akizungumza kabla ya kukabidhi msaada huo Meneja wa NMB Benk kanda ya kusini Janeth Shango alisema kuwa hatua ya Bank yao kutoa msaada huo ni kutaka kuunga jitihada zinazofanywa na Serikali ya awamu ya nne ya kuboresha sekta ya Elimu hapa Nchini.

Shango alisema kuwa kwa NMB changamoto za sekta ya Elimu na Afya Hapa Tanzania ni jambo la kipaumbele kutokana na umuhimu wa sekta hizo kuwa ndio nguzo kuu ya maendeleo kwa Taifa.

“sisi kama NMB tumekuwa msitari wa mbele kuchangia huduma za kijamii kwa lengo la kurejesha sehemu ya faida yetu kwa jamii ,ambapo kwa zaidi ya miaka saba mfululizo tumeweza kuchangia 1% ya faida yetu kama sehemu ya uwajibikaji kwa jamii inayotuzunguka” alisema Shango.

Hata hivyo shango aliongeza kuwa mwaka 2020 Benk yao imetenga kiasi cha Tsh. Bilioni 1 kwa ajili ya kuchangia maendeleo ya jamii ikiwemo kusaidia sekta ya Elimu na Afya . Kwa upande wake Rahma Athumani mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Ng’apa aliishukuru Bank ya NMB kwa kuwatatulia changamoto iliyokuwa inawakabili Shuleni hapo ya Meza na Viti.

Alisema kuwa kwa Darasa lao walikuwa wanalazimika kutumia Maabara kama Darasa kutokana na changamoto hiyo ya meza na viti jambo ambalo lilikuwa linawaletea usumbufu pale ambapo madarasa mengine wakitaka kujifunza kwa vitendo.

Akizungumza baada ya kupokea msaada huo Mkuu wa Wilaya ya Lindi Shaibu Ndemanga aliishukuru Bank hiyo kwa kuunga mkono jitihada za Serikali ya awamu ya tano katika kuboresha Sekta ya Elimu.

Ndemanga alisema kuwa uboreshwaji wa vifaa vya kujifunzia pamoja na mazingira wezeshi ya kufundishia ni miongoni mwa mpango mkakati kuinua ubora wa Elimu katika Mikoa huo wa Lindi hivyo sehemu ya Meza na Viti ni hatua moja wapo ya kutekeleza mpango huo mkakati.

Hata hivyo Ndemanga aliongeza kuwa Serikali inatambua mchango mkubwa unaotolewa na Bank hivyo katika shughuli mbali mbali za maendeleo pamoja na majanga yanapotokea huku akitoa wito kwa Taasisi zingine kuendelea kuunga mkono jitihada hizo.
Meneja wa Bank ya NMB kanda ya kusini Bi, Janeth Shango kulia akikabidhi Mabati Mkuu wa Wilaya ya Lindi Mkoani humo Shaibu Ndemanga jana katika viwanja vya Shule ya Sekondari Mnolela Halmashauri ya Mtama.

Saturday, February 22, 2020

WAJASIRIAMALI LINDI WANUFAIKA NA MIKOPO

NA HADIJA HASSAN, LINDI.

Vitambulisho vya wajasiriamali (machinga) vyapandisha huduma za mikopo zinazotolewa na shirika la kuhudumia viwanda vidogo vidogo (SIDO) Mkoa wa Lindi kwa zaidi ya asilimia 124%.

Ongezeko hilo la kiwango cha pesa zilizokopeshwa kwa wajasiriamali limepanda kutoka shilingi ML.79 Desemba mwaka 2015 mpaka kufikia shilingi ML.224 Desemba mwaka 2019.

Hayo yameelezwa na meneja wa Shirika hilo jana Mwita Kasisi alipokuwa akitoa taarifa ya huduma za mikopo katika khafla ya utowaji wa mafunzo ya ujasiriamali na usimamizi wa mikopo kwa wajasiriamali.

Kasisi alisema miongoni mwa sababu zilizofanya huduma hizo za mikopo kwa wajasiriamali na wafanya biashara wa kati wa mkoa huo ni kutokana na mazingira wezeshi yaliyowekwa na serikali kwa wajasiriamali hasa ya kutoa vitambulisho.

Alisema tokea vitambulisho hivyo vimeanza kutolewa shirika limeweza kuwatambua kwa urahisi wajasiriamali ambao wanakidhi vigezo vya kupatiwa mikopo.

Kasisi alieleza sababu nyingine ya upandaji huo wa huduma za mikopo ni uwelewa wa kutosha walionao wajasiriamali kupitia Elimu mbali mbli inayotolewa na shirika hilo juu ya faida za mikopo katika kukuza na kueneleza biashara zao.

Kasisi alisema kuwa ongezeko hilo pia limepanda kwa wastani wa uchukuwaji wa mikopo kwa mtu mmoja mmoja kutoka wastani wa milioni 1 kwa kila mjasiriamali mpaka wastani wa milioni 2.1 kwa mjasiriamali mmoja kwa mwaka.

Kasisi aliongeza kuwa kwa kipindi hicho cha miaka minne jumala ya pesa shilingi milioni 895.9 zimetolewa kwa wajasiliamali 414 kwa wastani wa shilingi milioni 2.1 kwa kila mjasiliamali mmoja.

Akifungua mafunzo hayo Mkuu wa Wilaya ya Lindi Shaibu Ndemanga aliwataka wajasiliamali hao kuyatumia mafunzo hayo kwa kuonyesha mabadiliko katika shughuli zao kwa kujitofautisha kati yao na wafanya biashara.

"Lengo la kuwaweka hapa tofauti na kuwapatia mikopo lakini pia mnafundishwa kuziongezea thamani bidhaa zenu, uwezi kununua magauni na vitenge kariakoo ukaja kuuza Lindi ukajiita wewe ni mjasiliamali tunatamani baada ya mafunzo haya tuone tofauti katika shughuli zenu kabla ya mafunzo na baada ya mafunzo " alisisitiza Ndemanga.

Ndemanga pia alisisitiza nidhamu ya fedha za mikopo walizokopeshwa wajasiliamai hao kutumia kwa malengo waliyokusudia ili waweze kurejesha kwa wakati.

Kwa upande wake Amina Khalphani Mjasiliamali Manispaa ya Lindi Mkoani humo aliishukuru Serikali kupitia Shirika hilo la SIDO kwa kuwawezesha kuwapa mafunzo ya ujasiliamali na usimamizi wa mikopo itakayowawezesha kukuza na kuendelezabiasharazao.

DC KAWAWA AAGIZA CHANZO CHA MACHIMBO YA MCHANGA KISIMAMIWE KUINUA MAPATO BAGAMOYO

NA MWAMVUA MWINYI,BAGAMOYO 

MKUU Wa Wilaya Ya Bagamoyo ,Zainab Kawawa ameiagiza halmashauri ya Bagamoyo kutumikia wananchi kwa maslahi mapana ya jamii pamoja na kusimamia chanzo kikuu cha machimbo ya mchanga ambacho kinalegalega na kusababisha kushuka kwa mapato. 

Aidha mkuu huyo wa wilaya, ameelekeza kupatiwa maelezo ya kina ni kwanini mashine za makusanyo (posi) zinazimwa na kushindwa kukusanya mapato kwa muda mrefu na hivyo kuhitaji maelezo ofisini kwake. 

Akizungumza na watumishi na madiwani wa halmashauri hiyo, Zainab alisema , wabadilike ,wasimamie na kufuatilia mapato pasipo kujenga uongo na udanganyifu kwa maslahi ya matumbo yao. 

“Haiwezekani mapato ya mchanga yanashuka ,licha ya vyombo vya ulinzi na usalama kubaini mianya na udanganyifu, hasa katika eneo hili la mchanga, mmefikia hatua ya kuidanganya hadi TAKUKURU mnapotosha taarifa na takwimu sahihi za makusanyo ili kujinufaisha”” 

“Ninahitaji maelezo pia kwanini mnazima posi ,hizi mashine mnazima kwa kipi?!nahitaji maelezo na nakala nyingine ielekezwe kwa mkuu wa mkoa na nyingine TAMISEMI”alisema Zainab.

Zainab alieleza, kuzimwa kwa posi ni kukiukwa maelekezo ya TAMISEMI ,halmashauri ni eneo lenye heshima na hadhi yake, ambapo inapaswa kuendeshwa kwa kuzingatia sheria,kanuni na taratibu hivyo pasifanyiwe mchezo ama kuendeshwa kiholela (kihuni). 

Nae mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Ally Ally Issa alisema, hali ya mapato hairidhishi kutokana na chanzo mama cha mchanga kuyumba ambapo makusanyo yamefikia asilimia 43 wakati walitakiwa kufikia asilimia 50 kwa kipindi hiki cha miezi sita. 

Alifafanua kwamba, kutokana na hilo wamebaini machimbo holela ya mchanga 23 na sasa wapo katika mkakati wa kuyafunga baadhi ya machimbo na mengine kuyarasimisha na kuongeza usimamizi ili kunusuru utoroshaji na kuongeza mapato. 

Alieleza kwamba, machimbo ambayo yamesharasimishwa ni pamoja na Nzole,Fukayose na Mapinga. Kuhusu posi, Ally alieleza tatizo kubwa kuna nyingine zimeharibika na nyingine hazifanyikazi hivyo pia wamenunua posi mpya 43 ili kupunguza changamoto iliyojitokeza. 

Kwa upande wake ofisa mazingira Bagamoyo, Cleophace Murugwa aliwataka wachimbaji kufuata taratibu za kupata kibali na leseni .
Alibainisha ,kwasasa wanapambana na wale wanaofanya uchimbaji wa maeneo yasio rasmi, na atakaeenda kinyume na taratibu sheria inachukua nafasi yake. 

Murugwa alitaja maeneo yaliyo rasmi ni Kilomo eneo la Buma, Yombo -Chasimba na Fukayose huko

Friday, February 21, 2020

WANAFUNZI KILWA HUTEMBEA UMBALI MREFU KUFUATA SHULE.

NA HADIJA HASSAN, LINDI.

ZAIDI ya wanafunzi 260 wanaosoma katika Shule ya msingi Hotel tatu katika kata ya Hoteli tatu Wilayani Kilwa Mkoani Lindi hulazimika kutembea umbali mrefu kwa zaidi ya masaa matatu ili kufuata huduma hiyo ya shule jambo ambalo ni hatari kwa usalama wao.

Hayo yameelezwa na mkuu wa Shule hiyo ya Hotel tatu Iddy Manonji hivi karibuni alipokuwa anazungumza na bagamoyo blog ofisini kwake

Kwa mujibu wa mkuu wa shule huyo wa shule wanafunzi hao ni kutoka kitongoji cha kalashi, kibaoni na Manyuli Mnonji alisema kutembea umbali mrefu kwa wanafunzi hao kunafanya hali ya kitaaluma kwao iwe inashuka kutokana na kufika shuleni wakiwa wamechelewa huku wakiwa wamechoka sana hali inayopelekea kutosoma vizuri

Alisema kutokana na umbali huo pia wazazi wa maeneo hayo wanashindwa kuwapeleka watoto wao wadogo kwa ajili ya kuanza madarasa ya awali kwa kuhofia usalama wao njiani ukizingatia hali ya mapoli na vichaka vilivyomo.

Kwa upande wake Hamida Saidi (11) mwanafunzi wa Darasa la tatu anaishi kitongoji cha mayuli alisema kuwa yeye na wenzake hulazimika kutembea alfajili licha ya kuwa na msitu na vichaka njiani ili waweze kuwahi vipindi darasani

“tukitoka saa 11 asubuhi nyumbani kwetu, tunafika shuleni saa mbili tukiwa tumechoka wakati mwingine tunasinzia darasani kwa sababu ya kukatisha katisha usingizi lakini hata tunaporudi tunafika nyumbani usiku sana kama ukiwa peke yako wakati mwingine unaogopa kutembea pekeyako” alisema Halima

Nae Fatuma mavumbi kutoka kitongoji cha kalashi alieleza changamoto nyingine wanayokabiliana nayo ni pale wanapofika shuleni wakiwa wamechelewa na kukuta mwalimu ameshaanza kufundisha hulazimika kuanzima dafutari za wanafunzi wenzao ili kuandika ambapo wakati mwingine unanakili na makosa ambayo aliyafanya mwanafunzi mwezio.

Mavumbi pia alitumia fursa hiyo kuiomba serikali kujenga shule karibu na maeneo yao ili kuwapunguzia adha ya kutembea umbli mrefu kufuata huduma hiyo.

Nae mtendaji wa kijiji hicho abdalah shante alisema kuwa Kutokana na kutembea kwa muda mrefu pamoja na njia wanazotumia watoto hao wanajikuta hali ya ulinzi na usalama sio rafiki kwani jambo lolote linaweza kutokea kati kati bila ya mzazi au mwalimu kufahamu kwa haraka.

Kwa upande wake ofisa Elimu Msingi wa Halmashauri hiyo Husen Kitingi amekili kuwepo kwa changamoto hiyo huku akieleza kuwa jitihada zinazochukuliwa kwa sasa ni kuanzisha shule shikizi katika vitongoji ambavyo vipo mbali na huduma hiyo ya shule

"Kama Halmashauri tunatarajia kuanzisha shule shikizi zaidi ya 20 katika vitongoji ambavyo vipo mbali na huduma ya shule ambapo tunashirikiana na wanajamii husika wa maeneo hayo"