Friday, February 21, 2020

MGALU AITAKA EWURA KUHARAKISHA UANDAAJI KANUNI KWA WAWEKEZAJI BINAFSI WA UMEME

Naibu Waziri wa Nishati,Subira Mgalu akiongea na wananchi wa kijiji cha Matipwili kilichopo kata ya Mkange, Wilaya ya bagamoyo, Mkoa wa Pwani alipokuwa kwenye ziara ya kazi ya ukaguzi wa kazi ya usambazaji umeme.
..............................................


Hafsa Omar-Pwani.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, ameitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma  ya Nishati na Maji (EWURA) kuharakisha uandaaji wa kanuni ambazo zitatumika kudhibiti bei za umeme ambazo zitatumiwa na wawekezaji binafsi wa umeme nchini.


Ameyasema hayo, Februari 20,2020 wakati alipokuwa akijibu maswali mbalimbali ya wananchi ambao walikuwa wakilalamikia bei kubwa ya umeme wanaotozwa na Mkandarasi wa kampuni ya Husk Power iliyopo katika kijiji cha Matipwili kata Mkange, Wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani.


Alisema, Ewura inatakiwa kuyafanyia kazi maelekezo hayo kwa haraka ili wawekezaji hao wadogo, wapate muongozo huo ambao utawasaidia kufanya kazi kwa kufuata sharia za nchi bila ya kujichukulia maamuzi ya kujiwekea bei za juu ambazo zinawaumiza Watanzania wa kipato cha chini.


Alifafanua kuwa, Serikali ilitoa fursa kwa wawekezaji hao kuwapelekea umeme Watanzania ambao wapo katika maeneo ambayo yapo mbali na gridi ya Taifa na Serikali iliamua kutoa ruzuku ili wawekezaji hao watoe bei nafuu ya umeme kwa Watanzania wa kipato cha chini.


“Ni kweli wao wamewekeza miundombinu yao hapo lakini haiwezekani 5000 itumike kwa siku, haiwezekani kabisa, pia haiwezekani laki tatu na nusu iwe bei ya mtumiaji wa kioski kweli hiyo hapana, laki tatu na nusu ni umeme unaotumika kwenye kiwanda cha saizi ya kati lakini sio kioski” alisema Mgalu 


Alieleza kuwa, Serikali inajukumu la kuwalinda watumiaji wa Nishati nchini, kwa kuzingatia jukumu hilo, inawakumbusha wawekezaji nchini kuwa bei ya kunganisha umeme vijijini ni 27000 na kuwataka wawekezaji hao kupunguza gharama za undeshaji wa kampuni zao ili waweze kujiendeshe kwa kupata faida kwenye kampuni zao.


“Tunataka wapunguze gharama za uendeshaji watumie wataalamu wa ndani, watumie vifaa vya ndani ili gharama za uendeshaji zishuke ili watanzania hawa wapate nafuu vyenginevyo  gharama za umeme zisiposhuka sisi tutakwenda hata maeneo ambayo tulisema waende wao watakosa hii fursa kwasababu sisi hatutakubali bei kama hizo”alisema


Aidha,alimtaka mkandarasi huyo kukutana na Meneja wa TANESCO mkoa wa Pwani ili kujadiliana na kuzipitia tena bei za umeme  ambazo zinatumiwa na mkandarasi huyo, ili kupatikane uwiano wa bei  za umeme vijijini  ambazo zinatawanufaisha Watanzani wote ili waweze kujiletea maendeleo.
 Naibu Waziri wa Nishati,Subira Mgalu akiwasikiliza wananchi wa kijiji cha Matipwili kata ya Mkange, wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa pwani alikuwa kwenye ziara ya kazi ya ukaguzi wa kazi ya usambazaji umeme.

 Mwanakijiji wa kijiji cha Matipwila kilichopo kata ya Mkange, Wilaya ya bagamoyo, Mkoa wa Pwani akiuliza mwaswali kwa Naibu Waziri wa Nishati,Subira Mgalu wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini humo.




 

NEC YATAJA SABABU ZA KUONGEZA SIKU ZA UANDIKISHAJI WA DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA DAR

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)imetaja sababu za kuongeza siku za   uandikishaji katika zoezi la uboreshaji wa Daftari la kudumu la Wapiga Kura kwa mkoa ya Dar es Salaam, sababu kubwa ikiwa ni maombi mbalimbali katika vituo vya uandikishaji..
Nec imeongeza siku tatu, kuanzia feb 21 hadi Februari 23, 2020, na kuwataka watu kuhudhuria kwa wingi katika vituo mbalimbali vilivyopo katika jiji la Dar es salaam..

Akizungumza na waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Uchanguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Dkt Wilson Charles alisema hawakuongeza muda kwa sababu watu walikuwa hawajitokezi katika kujiandikisha ila tumeongeza kwa sababu kuna uhitaji, watu wengi wanataka huduma, tunataka kuwa na watu wengi katika uchaguzi huu.
Dkt.Charles amesema baada ya maombi hayo walifanya kikao cha Februari 19 kwa ajili ya kutathmini zoezi hilo na kuamua kuongeza muda wa kujiandikisha. 
Amesema vituo vyote vitafunguliwa kama kawaida kuanzia saa mbili hadi saa 12 jioni.

Monday, February 17, 2020

Rais Magufuli Amtaka Makonda Arudishe Fedha za TASAF alizosema alitumia kwenda Dodoma wakati sio masikini

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam, Paul Makonda kuzirudisha fedha za TASAF ambazo alizitumia vibaya kwa safari ya kwenda Dodoma ili hali sio Masikini.

Rais Magufuli ameyasema hayo hii leo tarehe 17, Febuari, 2020 wakati akizindua kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya mpango wa Maendelo wa kunusuru Kaya masikini wa TASAF. Hafla imefanyika katika Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dsm.

”Kwenye mpango huu wa TASAF zilijitokeza baadhi ya changamoto, kupitia zoezi la uhakiki wa Kaya Masikini, lililofanyika kuanzia mwezi Novemba 2015 hadi mwezi Juni 2017. Tuliweza kubaini uwepo wa Kaya hewa 73,561.”

”Ambapo Kaya 2234 zilithibitika kuwa wanakaya wake sio Masikini na hapa nafikiri wakina Makonda ambao walizitumia hizi fedha kwenda safari ya Dodoma wakati sio Masikini naomba kama hili ni kweli Makonda azirudishe hizi fedha. Kama ni kweli alitumia fedha za TASAF akaenda nazo huko alipokuwa anaeleza, na yeye hausiki kwenye Kaya Masikini mkae muziangalie hizo fedha lazima azirudishe.”

Kabla ya Rais kutoa kauli hiyo, Makonda alisema mwaka 2012 alipewa nauli na Rais mstaafu, Benjamin Mkapa kwenda mkoani Dodoma kugombea makamu mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM). Amesema fedha hizo zilikuwa sehemu ya mfuko

“Namshukuru sana mzee Mkapa kuona bado anaendelea kufanya kazi yake, naomba Rais Magufuli niseme mbele yako mfuko huu wa Tasaf nami nimenufaika nao, haikuwa moja kwa moja.”

“Lakini wakati naomba nafasi ya  makamu mwenyekiti wa vijana (UVCCM) Mkapa ndio aliyenipa nauli ya kwenda kuomba kura Dodoma. Kwa hiyo naimani ilikuwa sehemu ya huu mfuko, alikuwa na moyo,” alisema Makonda.

Waziri mkuu Kassim Majaliwa atumia jukwaa la Maulid ya Mtume Muhammad (S.A.W) kuwataka Watanzania kudumisha amani


    

By Selemani BETA, Dar es salaam.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa rai kwa viongozi wa dini zote na jamii kwa ujumla kuendelea kuvumiliana na kustahamiliana hususan pale zinapotokea tofauti miongoni mwao, lengo likiwa ni kudumisha amani na ulivu uliopo nchini
Pia Waziri Mkuu, amesema Serikali inatambua na kuheshimu dini zote nchini na itaendelea kutoa ushirikiano kwa madhehebu yote katika kutunza na kulinda amani.
Ametoa kauli hizo, Jumapili Februari 16, 2020 kwenye Kumbukumbu ya Mazazi ya Mtume Muhammad Swalla Allahu Alayh Wasallam iliyoandaliwa na Nida Textile Mills (T) Ltd, na kufanyika katika mtaa wa Indira Ghandi jijini Dar-es-Salaam.
Alisema amani ndiyo msingi wa kila binadamu kufurahia maisha ya dunia na kufanya ibada zake kulingana na imani yake. “Kwa hiyo,tunapoazimisha mazazi ya Mtume Muhammad Swalla Allahu Alayh Wasallam, tuna kila sababu ya kumuenzi kwa kufuata mafundisho yake.“
Waziri Mkuu amesisitiza kwamba Serikali kwa upande wake inatambua na itaendelea kuthamini, mchango wa dini, taasisi mbalimbali zisizo za kiserikali na hata mtu mmoja mmoja katika kutunza na kulinda amani ya nchi yetu.
 “Kuvumiliana na kustahamiliana ndiko kulikotufanya tuendelee kuwa wamoja na kuitunza neema hii kubwa ya amani katika nchi yetu. Kila mmoja wetu anapaswa kutambua kuwa anao mchango mkubwa katika kutunza na kuimarika kwa amani ya nchi yetu.”
Akizungumzia kuhusu maadhimisho hayo ya Mazazi ya Mtume Muhammad (S. A. W), Waziri Mkuu amesema kwamba hiyo ni fursa muhimu kwa waislamu wote kuyasoma na kuyatafsiri kwa kivitendo maisha ya Bwana Mtume katika mfumo wao wa maisha ya kila siku ili kuyafanya maisha yao hapa duniani yawe bora zaidi.
“Tukio hili la leo ambalo nimefahamishwa kuwa linafanyika kwa mwaka wa 25 sasa, ni kielelezo cha umoja, mapenzi na undugu miongoni mwetu. Katika Quran Surah ya 49 (Al-Hujurat) ayah ya 10, Mwenyezi Mungu anatufahamisha kuwa ’hakika waumini ni ndugu.......’ Kwa msingi huo, tukiwa Waislamu suala la kuimarisha umoja, undugu na ushirikiano katika nyanja zote ni wajibu wa kila mmoja wetu.“
Kadhalika, Waziri Mkuu ameongeza kuwa Mtume Muhammad (S.A.W) naye katika kusisitiza suala hilo la umoja, kwenye hotuba yake ya kuaga alihimiza kuwa mtu yeyote yule hawezi kuwa bora dhidi ya mwingine kwa sababu tu ya rangi yake au kabila lake lakini kitu pekee kitakachompa yeye daraja hilo la kuwa bora ni kutenda haki na kumuogopa Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Nayei, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Aboubakari Bin Zuberi alisema katika kuadhimisha Mazazi ya Mtume Muhammad (S.A.W) waislamu nchini wanapaswa waendelee kuwa watulivu na wasikivu wa kila jambo linalotolewa kwao na viongozi.
Maadhimisho hayo yamehudhuliwa na masheikh na viongozi wa Serikali kutoka maeneo mbalimbali nchini. Pia yamehudhuriwa na masheikh kutoka nchi za Paksani, Iraq na Misri ambao kwa ujumla wao wameisifu Serikali ya Tanzania kwa kudumisha amani, utulivu pamoja na umoja.

    

Thursday, February 13, 2020

WAZIRI KALEMANI AWASHA UMEME KIJIJI CHA MPENDA HALMASHAURI YA MTAMA LINDI.

 Waziri wa nishati, Dkt. Medard Kalemani, akikata utepe kuashiria kuwasha umeme katika kijiji cha Mpenda Halmashauri ya Mtama mkoani Lindi.
....................................................
 
NA HADIJA HASSAN, LINDI.

Huwenda Ndoa za wakaazi wa kijiji cha Mpenda halmashauri ya Mtama Mkoani Lindi zikanusurika kuvunjika baada ya Waziri wa Nishati, Dkt. Medard kalemani kuwasha umeme katika kijiji hicho ambao pamoja na mambo mengine utasaidia kuzalisha maji.

Akitoa salamu za Mkoa pamoja na kuwasalimu Wananchi wa Mpenda Mkuu wa Wilaya ya Lindi Shaibu Ndemanga kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo Godfrey Zambi alisema kuwa kwa muda mrefu Wananchi wa Kijiji hicho walikuwa wakiikosa huduma hiyo ya Maji kutokana na kukosa nishati ya Umeme ya uhakika.

Ndemanga alisema baada ya kuwashwa kwa umeme huo sasa ni muda wa Mamlaka ya Maji safi na maji taka Mkoani humo Luwasa kuanza mikakati ya kufikisha maji katika kijiji hicho.

“hapa mpenda Mh, Waziri, baada ya leo kuwa umewasha umeme, tayari watu wa maji Luwasa wamesema na wao wanakuja kwa sababu wanauhakika sasa wa umeme, kwa hivyo umeme huu maana yake pamoja na matumizi mengine ya kibinaadamu lakini pia utavuta maji” alisema Ndemanga.

Akizungumzia changamoto hiyo ya maji diwani wa kata ya Mtama Hassan kunyong’onyea alisema kuwa changamoto hiyo imedumu kwa zaidi ya miaka 15 ambapo zaidi ya wakazi 1,280 wa kijiji hicho hutegemea kisima kimoja kupata huduma hiyo.

Hata hivyo Kunyong’onyea alisema Kisima kinapatikana umbali wa kilomita mbili kutoka kijijini hapo ambapo hata hivyo wananchi wanaokwenda kufuata maji wanalazimika kusubiri kwa zaidi ya masaa matatu mpaka manne ili kupata huduma hiyo.

Alisema hali hiyo ya kusubiri maji kwa muda mrefu inapelekea shughuli nyingi za kiuchumi za wananchi hao kudolola na mahali pengine hata kupelekea migogoro inayopelekea kuvunjika kwa Ndoa.

Kunyong’onyea aliongeza kuwa sasa yupo muwekezaji ambae amechimba kisima chake ambapo anauza maji kwa wananchi hao kwa shilingi 150 /= kwa ndoo yenye ujazo wa lita 10 na shilingi 250/= kwa dumu la lita 20 ambapo hata hivyo kulingana na kipato cha wananchi hao wengi wao wanashindwa kumudu ghalama hiyo.

Nae Amina Dadi Mkazi wa kijiji cha Mpenda Alisema Ndoa nyingi zinaingia kwenye migogoro kwa kile kinachodaiwa kuwa wanawake wanasingizia kigezo cha kufuata maji wakati wanaenda kufanya mambo yao kwa wanaume wa pembeni.

“licha ya kuwa wanaume zetu wanafahamu changamoto hii ya upatikanaji wa maji lakini bado tukirudi nyumbani kwa kuchelewa wakati mwingine tunapigwa au tunapewa taraka hivi juzi tuu kiangazi cha mwaka uliopita wapo wanawake waliopewa talaka na waume zao kwa kuchelewa kurudi nyumbani walipokwenda kufuata maji” Aliongeza Amina.

“kama kweli shida ilikuwa ni umeme sasa umeme umeshafika tunaiomba Serikali utufikirie sisi wanawake wa Mpenda tunateseka sana jamani, wakati mwingine tunakutana na chui simba huko tunakofuata maji” Alisema amina.
 
 Waziri wa nishati, Dkt. Medard Kalemani, akikabidhi kifaa cha Umeme Tayari (UMETA) kwa wananchi wa kijiji cha Ng'au Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa.

 Waziri wa nishati, Dkt. Medard Kalemani, akisalimiana na wananchhi mbalimbali katika kijiji cha Ng'au Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa.