Monday, August 19, 2019

RC NDIKIRO AKABIDHI PIKIPIKI 28 KWA MAAFISA TARAFA WA MKOA WA PWANI

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo aliyekaa kwenye pikipiki akiwa na maafisa taarafa mbali mbali wa mkoa huo pamoja na baadhi ya makatibu Tawala wa Wilaya mbali mbali katika halfa ya kukabidhi pikipiki 28 kwa maafisa tarafa iliyofanyika nje ya jengo la ofisi za Mkuu wa Mkoa.
.........................................

VICTOR  MASANGU,   PWANI
   
Serikali  Mkoani   Pwani imewaagiza maafisa tarafa wote kutimiza majukumu yao bila uzembe na badala yake wahakikishe wanashughulikia na kuingilia kati  sakata la wimbi la migogoro ya ardhi ambayo inawakabili kwa kiasi kikubwa jamii ya wafugaji na wakulima kwani inapelekea kuwepo kwa uvunjifu wa amani na baadhi ya wananchi kupoteza maisha yao kutokana  na kuibuka kwa  mapigano.


Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani  Mhandisi Evarist Ndikilo wakati wa halfa ya kukabidhi pikipiki 28 kwa maafisa taarafa wa Mkoa wa Pwani zilizotolewa na serikali kuu, ambapo pia amewataka kusimamia na kumaliza  kabisa changamoto ya mimba kwa wanafunzi na kutatua tatizo la kukithiri utoro.


Aidha Ndikilo amewataka maafisa hao tarafa kuweka mikakati madhubuti katika utekelezaji wa majukumu yao hususan katika ufuatiliaji wa miradi mbali mbali ya maendeleo ili kuwaletea maendeleo chanya wananchi.


“Katika Mkoa wa Pwani katika baadhi ya maeneo kumekuwepo na changamoto kubwa ya migogoro ya ardhi kwa hivyo ili suala inatakiwa maafisa tarafa kuifuatilia wenyewe na kuimalizi sio mpaka viongozi wa ngazi za juu waende kuitafutia ufumbuzi hivo ninawaomba katika hili tujitahidi kwa hali na mali ili kuondokana na hali hii ikiwemo suala la mimba kwa wanafunzi na utoro yote myafanyie kazi,” alisema Ndikilo.


Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Theresia Mmbando amebainisha kuwa hapo awali maafisa tarafa walikuwa wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kutokuwa na usafiri wa uhakika hivyo kushindwa kutimiza majukumu yao kwa wakati katika kuwaatumikia wananchi katika suala zima la kuleta maendeleo.


Nao baadhi ya maafisa tarafa ambao wamenufaika na kupatiwa pikipiki hizo wamesema kwamba zitaweza kuwasaidia kwa kiasi kikubwa katika kufiuatilia na kusuluhisha kwa urahisi  changamoto mbali mbali  zinazowakabili wananchi kwani hapo awali walikuwa wanafanya kazi katika mazingira magumu kutokana na kutokuwa na usafiri wa uhakika.


Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Kibaha vijijini, Hamoud Juma, ambaye alihudhuria katika hafla hiyo, ametoa pongeza za dhati kwa Rais Dk John Pombe Magufuli kwa kuamua kutoa vitendea kazi hivyo vya usafiri wa pikipiki ambazo zitaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza adha ambayo walikuwa wanaipata maafisa tarafa,


Naye Katibu Tawala wa  Wilaya ya Kisarawe Mtela Mwampamba alibainisha kuwa ana imani kuwa changamoto ya awali ambayo walikuwa wanakabiliana nao maafisa hao itaweza kumalizika kutokana na kupatiwa usafiri huo wa pikipiki ambao utaweza kuwafikisha katika maeneo mbali mbali ya miradi ya maendeleo pamoja na kutekekleza kazi zao kwa urahisi.


Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo akimkabidhi pikipiki Afisa tarafa wa Msoga Juma Mgeni wakati wa halfa iliyofanyika nje ya jengo la ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani.

Mbunge wa Jimbo la Kibaha vijijini kulia Hamoud Jumaa akisalimiana na Katibu Tawala wa Wilaya ya Kisarawe  Mtela Mwampamba mara baada ya kumalizika kwa zoezi la ugawaji wa pikipiki kwa maafisa Tarafa wa Mkoa wa Pwani ambapo pikipiki 28 zimekabidhiwa,
Image may contain: 3 people, people smiling, tree, sky, motorcycle, outdoor and nature

(PICHA ZOTE NA VICTOR MASANGU)


VULU AWAASA WANA-CCM KISIJU.

Na Omary Mngindo, Mkuranga.

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Pwani, Zaynab Matitu Vulu, amewaasa wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Mkuranga mkoani hapa, kutofanya makosa katika uchaguzi wa serikali za vijiji na Vitongoji, utakaofanyika mwishoni mwa mwaka huu.

Mbunge huyo ametoa rai hiyo mwishoni mwa wiki akiwa Kisiju, akiambatana na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho (MNEC) Haji Abuu Jumaa, wakielekea Kisiwa cha Koma, ambapo akiwa huko Vulu alikabidhi kitanda na mashuka ikiwa ni ahadi yake kwa wananchi hao.

Akiwa Kisiju Vulu alipata fursa ya kuzungumza na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho na Mabaraza ya Jumuiya za Kata, kwenye kikao maalumu, mbele ya MNEC Haji, ambapo alianza kwa kuwashukuru kwa kuendelea na majukumu yao ya kukiimarisha chama hicho.

"Kwaniaba ya viongozi wa chama ngazi zote, nianze kwa kuwashukuru na kuwapongeza kutokana na umoja wetu wa kuendelee kukiimarisha chama chetu, pia niwaombe tuondokane na yale yaliyosababisha kushindwa kwenye chaguzi zilizopita, nadhani tunayatambua," alisema Vulu.

Aidha aliwataka wanachama hao kuyasena mazuri yanayotekelezwa kwa vitendo na Serikali ya CCM, inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli, ikiwemo miradi mikubwa inayoendeea kila kona ya nchi, ambapo kuna iliyokamilika na inayoendelea kutekelezwa.

"Kuna miradi mingi imefanyiwa kazi katika kila kona ya nchi, kuna iliyokamilika na inayoendelea kukamilishwa, tuwe mstari wa mbele kuyazungumzia hayo, kwani yanaonekana wazi, hivyo hatuna sababu ya kutoyasemea," alisema Vulu.

Vulu amempongeza MNEC Haji kwa ziara hiyo ya kusikiliza changamoto, kuzipokea kisha kuzifikisha kwa viongozi ngazi za juu ili kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazowagusa wananchi, huku akimpongeza Mbunge wa jimbo hilo Abdallah Ulega.

Kwa upande wake MNEC Haji aliwaambia wanachama hao wa Kisiju kuwa, ziara hiyo ya kutembelea Kata zote mkoani Pwani madhumuni yake ni kukutana na viongozi wanaokisimamia chama hicho ngazi za vijiji ambao ndio msingi imara ndani ya chama.

VIKUNDI KEREGE VYAKOPESHWA MIL. 67

Na Omary Mngindo.

Vikundi vya Ujasiriamali 12 vya vijana, wanawake ndani ya Kata ya Kerege wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani, vimepatiwa mkopo wa shilingi milioni 67 kutoka halmashauri ya wilaya ya hiyo.

Mikopo hiyo imetokana na asilimia kumi ya halmashauri hiyo ambayo ni utekelezaji wa agizo la serikali kwa halmashauri zote nchini kupitia makusanyo yake ya ndani ya kuvikopesha vikundi mikopo isiyokuwa na riba.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Diwani wa kata ya Kerege, Said Ngatipura alisema kuwa, vikundi hivyo vimepatiwa fedha hizo kulingana na maombi na kiasi cha fedha, huku akieleza kwamba vikundi hivyo vinaendelea na marejesho.

"Vikundi vilivyopatiwa mikopo ni 6 kikiwemo cha Tumaini Kilemela ambacho kimerejesha vizuri na kukopa tena, katika mikopo hiyo vikundi vya wanawake vimekopeshwa shilingi milioni 39.5 wakati vijana wakipata mkopo wa shilingi milioni 28 tu," alisema Ngatipura.

Alisema kuwa Diwani wa Viti Maalumu Tarafa ya Mwambao Shumina Sharifu, ametafuta wafadhili waliowezesha kuchimba visima viwili vya maji safi, kimoja kipo shule ya msingi Kerege na kingine shule ya Mapinga.


Akizungumzia sekta ya elimu, Ngatipula alisema kuwa Kata ina shule moja ya sekondari yenye kidato cha kwanza mpaka cha nne na wanafunzi 1,105, kati yao wavulana 540, wasichana 565 ikiwa na walimu 75.

Alisema kuwa mfuko wa jimbo umeunga mkono juhudi za wananchi katika umaliziaji wa vyumba vya madarasa sekondari ya Kerege, jengo la Utawala, vyoo shule ya msingi Mapinga, ununuzi wa bati ofisi ya Kitongoji cha Amani na mifuko 100 ujenzi wa vyumba vya madarasa.

"Pamoja na hayo, kupitia mfuko wa jimbo umeendelea na utoaji wa ruzuku kwa vikundi vya ujasiriamali vikiwemo Neema Group, Manofu Woman, Jitambue na Jitahidi ambavyo vinajihusisha na shughuli za ujasiriamali," alimalizia Ngatipura.