Monday, May 20, 2019

PROF. DOS SANTOS SILAYO AELEZA MIKAKATI YA KUONGEZA MAPATO KATIKA SEKTA YA MISITU

Image may contain: 1 person, suit
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ( TFS) imeweka mikakati kadhaa katika kuhakikisha misitu yake inaingiza mapato ya kutosha kupitia huduma za utalii sambamba na kuuza mazao ya misitu.


Mtendaji Mkuu wa TFS Profesa Dos Santos Silayo amesema miongoni mwa mikakati hiyo ni kuvitangaza vivutio vya utalii ekolojia vilivyopo kwenye misitu ya mazingira asilia iliyo chini ya taasisi hiyo.


Akizungumza wakati akifungua mkutano wa nane wa baraza la wafanyakazi wa TFS lililofanyika Morogoro, Profesa Silayo alisema aina hiyo ya utalii na biashara ya mazao ya misitu na nyuki ni nguzo ya utendaji kazi wa taasisi hiyo.


Akitolea mfano wa uvunaji wa utomvu wa miti inayokaribia kuvunwa katika shamba la Sao Hill amesema bidhaa hiyo inahitaji kufanyiwa utafiti na kuangalia uwezekano wa kuongeza uzalishaji wake.


Alisema katika eneo hilo pia upo uwezekano wa kuongeza uzalishaji wa gundi kutoka katika miti ya migunga, zao linalotarajiwa kuingiza fedha nyingi siku za usoni.


Amesema ni jukumu la watumishi kuongeza jitihada katika utendaji wao ili kuhakikisha lengo hilo hilo linatimia na kuleta matokeo chanya.


Profesa Silayo amegusia pia suala la udhibiti wa usafirishaji wa mazao ya misitu na nyuki pamoja na kushindwa kuimarisha huduma katika vivutio vya utalii.


“Haya ni maeneo ambayo inabidi tujipange vizuri zaidi kuyatekeleza katika kipindi cha miaka mitano ijayo ili kuondoa kero na kutoa huduma bora kwa umma.


“Endapo tutaimarisha maeneo haya, itasaidia kuongeza tija katika jukumu letu la ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali, kuongeza mauzo ya nje na fedha za kigeni kupitia huduma za utalii na uuzaji wa mazao ya nyuki,” alisema.





Pia alisisitiza kuhusu nidhamu kwa watumishi wa taasisi hiyo na kuwataka kila mmoja kutimiza wajibu wake na kujiepusha na vitendo vya ukiukwaji wa maadili ya kazi, na kusisitiza kuchukua hatua kali kwa watabainika kukiuka.



Kwa upande wake Mwenyekiti wa TUGHE wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Francis Kiondo alisisitiza umuhimu wa kuzungatia sheria na kanuni za utumishi wa umma kwa kila mtumishi pindi anapotekeleza majukumu yake.


MBUNGE WA CHALINZE ACHANGIA MILIONI TANO UBENA.

Mbunge wa Jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo, Mh. Ridhiwani Kikwete, akizungumza wakati wa kukabidhi Saruji mifuko 20 kwaajili ya uanzishwaji wa shule ya Msingi Kitongoji cha Choza.
....................................
 
Na Shushu Joel, Chalinze.



Mbunge wa Jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo, Mh. Ridhiwani Kikwete amekabidhi msaada wa vifaa mbalimbali ikiwemo mifuko ya saruji 20 kwa ajili ya uanzishwaji ujenzi wa shule ya Msingi katika kitongoji cha Choza, Matofali Elfu tatu, fimbo nne maalum kwa ajili ya walemavu wa macho, Kadi 23 za Afya kwa ajili ya matibabu ya wazee, vyote vikiwa na thamani zaidi ya shilingi Milioni tano.



Akizungumza na viongozi mbalimbali wa kata, vijiji na vitongoji wa kata hiyo alisema kuwa amefanya maamuzi hayo ya kuanzisha ujenzi wa shule hiyo kutokana na changamoto zinazowakabili wazazi/walezi na wanafunzi kwa kutembea umbali mrefu kwa ajili ya kupata elimu ya shule ya msingi huku wazazi kwa ajili ya masuala ya kimaendeleo.


Aliongeza kuwa kuongezeka kwa watu katika eneo hilo la choza kumepelekea kuhitajika kwa haraka kwa huduma za kijamii ili kuendana na mahitaji ya wakazi wa eneo hilo. 


"Saruji niliyotoa ni uanzilishaji wa ujenzi wa shule hiyo lakini si kwamba ndio mwisho wa utoaji wangu wa mahitaji katika ujenzi huo bali ni kama kiongozi wa mfano ili hata wananchi wanapoambiwa wachangie wasisite" Alisema Ridhiwani Kikwete.


Aidha aliongeza kuwa wananchi ndio nguzo ya maendeleo hivyo wanapoamua jambo lolote lile la kimaendeleo ni lazima lifanyike kutokana na umoja, nguvu na mshikamano wao katika ufanikishaji wa maendeleo katika eneo husika. 


Mara baada kutoa saruji hiyo Ridhiwani aliwataka viongozi wa eneo hilo kutafuta eneo lingine kubwa lenye kufaa ujenzi wa zahanati ili pia choza pajengwe zahanati. 


Alitumia nafasi hiyo kuwataka wananchi wa choza kujitokeza kwa wingi katika kuhamasishana juu ya maendeleo kwani serikali inatambua makusudi yao. 



Kuhusu misaada aliyoitoa, Mh Mbunge alisema kuwa ilikuwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi za Ilani ya Uchaguzi na maombi mbalimbali ya wananchi.Katika shughuli hiyo pia Mhe.Mbunge alikutana na wanachama mbalimbali wa vikundi vya Maendeleo katika kata hiyo .
  

Kwa upande wake diwani wa kata hiyo ya ubena zomozi Nicholaus Muyuwa amempongeza Mbunge huyo kwa uanzilishi wake wa kutoa saruji kwa lengo la ujenzi wa shule katika eneo hilo ili kuwaondolea changamoto watoto wa maeneo hayo. 


Aidha amemhakikishia Ridhiwani kuwa mifuko hiyo itatumika kama ilivyokusudiwa kufanyika kwani hata wao walikuwa wakilifikiria tu lakini Mbunge wetu kafanya kweli juu ya hilo hivyo utoaji wake wa hiyo mifuko kwa wananchi kweli Ridhiwani Kikwete ni kiongozi wa mfano. 


Naye Cosmos Alphonce ni Mwenyekiti wa kijiji cha kaloleni ameshukuru kwa mchango uliotolewa na Mbunge na kumtaka aendelee na moyo huo wa kujitolea kwa wananchi wake. 


Aliongeza kuwa kujengwa kwa shule katika eneo hilo kutaondoa changamoto ya watoto wa eneo hilo kutembea kilometa nyingi.
 
 Mbunge wa Jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo, Mh. Ridhiwani Kikwete, akiwakabidhi fimbo maalum za kuwaongoza kutembea walemavu wa kata ya Ubena.

Mbunge wa Jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo, Mh. Ridhiwani Kikwete akimkabidhi msaada wa Baiskeli ya Miguu mitatu (Wheel Chair), Mkazi wa Zomozi-Ubena Mzee Cosmas Alphonce Chongwe ambaye ni mlemavu wa miguu.
  
Mbunge wa Jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo, Mh. Ridhiwani Kikwete, akiwa anarekebisha Baiskeli inayomsadia kutembea mlemavu wa miguu Mkazi wa Zomozi-Ubena Mzee Cosmas Alphonce Chongwe wakati alipokabidhi vifaa mbalimbali kwa walemavu wa kata ya Ubena.

SERIKALI KUHAMASISHA UFUGAJI NYUKI

Serikali ya Tanzania imesema ipo mbioni kuja na mpango mkakati wa kitaifa wa kutoa hamasa kwa wananchi kutambua umuhimu wa kufuga nyuki na faida ya asali kiuchumi na kiafya.


Kauli hiyo imetolewa leo Jumatatu Mei 20, 2019 na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla katika maadhimisho ya siku ya nyuki duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dodoma.


Dk Kigwangalla amesema lengo ni kuwasaidia wananchi wanaojishughulisha na ufugaji wa nyuki kuchakata na kusindika asali kwa pamoja ili kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje.


“Lengo la kuanzisha mpango huo wa kitaifa ni kuwaenzi nyuki kwa kuwekeza fedha ya Serikali na ujuzi kutoka kwa wataalam. Kwa wananchi ni kuunda ushirika kwa mikoa kumi ya Tanzania Bara, na kila wilaya kuwapa mizinga ambayo wataitumia kwa ajili kufuga nyuki,” amesema Dk Kigwangalla.


Amebainisha kuwa baada ya hapo kila wilaya itakuwa na ushirika na kiwanda kimoja kitakachokuwa kinachakata na kusindika asali.