Monday, May 13, 2019

MBUNGE JUMAA AIKABIDHI POLISI VIFAA VYA MIL. 3

Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Mkoa wa Pwani Humoud Jumaa ( wa pili kulia) akimkabidhi vifaa hivyo Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Barnabas Mwakalukwa, kwa niaba ya Kamanda wa Mkoa, wanaoshuhudia wa kwanza kushoto ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama barabarani Josephine Protas na wa pili kushoto ni
Mkuu wa Usalama barabarani Mkoa wa Pwani, Mrakibu Msaidizi wa polisi (ASP) Mosi Ndozelo,
 .........................................

Na Omary Mngindo, Kibaha

MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Vijijini Mkoa wa Pwani Humoud Jumaa, amelikabidhi Jeshi la Polisi Usalama Barabarani mkoani hapa friji ndogo na viti kumi, kwaajili ya kuboresha utendaji kazi dawati la elimu katika jeshi hilo.

Katika hafla fupi ya makabidhiano hayo yaliyofanyika mwishoni mwa wiki kwenye ofisi za jeshi hilo mkoani Pwani, Jumaa amekabidhi friji ndogo na viti kumi kwa Kaimu Kamanda wa jeshi hilo Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Barnabas Mwakalukwa, kwa niaba ya Kamanda wa Mkoa.

Jumaa alisema kuwa, hatua hiyo imefuatia ombi alilopatiwa siku chache na Mkuu wa Usalama barabarani Mkoa wa Pwani, Mrakibu Msaidizi wa polisi (ASP) Mosi Ndozelo, ambaye alimwelezeea changamoto ya viti na friji, kwa ajili ya matumizi ya ofisi upande wa dawati katika utoaji elimu.

"Nilifika hapa siku mbili zilizopita nikakutana na Kamanda wa Kikosi cha Usalama barabarani mkoani hapa, ASP. Mosi Ndozelo, ambaye alinielezea changamoto inayohusiana na utekelezaji wa majukumu ya kazi zao"

Na kufuatia ombi hilo leo nimekabidhi friji ndogo na viti kumi vyenye thamani ya shilingi milioni 3," alisema Jumaa.

Kwa upande wake Kamanda Mwakalukwa alimshukuru Mbunge huyo, huku akitoa rai kwa wadau wengine kuungana katika kusaidia jeshi hilo, ili liweze kuendelea kutimiza majukumu yake kwa ufasaha zaidi.

"Ofisi yetu ina changamoto mbalimbali za vifaa, tunawaomba wadau wajitokeze kutuunga mkono katika kutatua mambo ambayo kwa namna moja au nyingene yanachangia kukwamisha utekelezaji wetu wa majukumu kiufasaha," alisema Kamanda Mwakalukwa.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama barabarani Josephine Protas alisema kwamba, kitendo cha Jumaa kujitolea kusaidia jeshi hilo ni cha kuigwa na wabunge wengine, huku akitoa rai kwa wadau wengine kujitokeza katika hilo.

Kamanda wa kikosi cha Usalama barabarani Ndozeli alisema kuwa walimfikishia ombi hilo mbunge huyo siku mbili zilizopita, hivyo ameonesha kujali ombi hilo, hatimae kuwapatia vifaa hivyo.
 
Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Mkoa wa Pwani Humoud Jumaa ( wa pili kulia) akimkabidhi vifaa hivyo Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Barnabas Mwakalukwa, kwa niaba ya Kamanda wa Mkoa.
Picha na Omary Mngindo.

WAUGUZI,WAKUNGA WAKUMBUSHWA KUZINGATIA MAADILI YA KAZI

Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania, Bi. Agnes Mtawa akiwaapisha wauguzi na wakunga kwenye maadhimisho ya Siku ya Uuguzi na Ukunga Duniani ambayo hufanyika Mei 12, kila mwaka. Leo wauguzi wameapishwa kukumbushwa kutoa huduma kwa kuzingatia kanuni na taratibu kama walivyojifunza.  Wengine kushoto ni viongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na viongozi wa Chama cha Uuguzi na Ukunga Tanzania (TANNA) wakishiriki katika shughuli ya kuwaapisha wauguzi jana Mei 12, 2019.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Bw. Makwaia Makani akizungumza na wauguzi jana Mei 12, 2109. katika maadhimisho ya siku ya wauguzi duniani.
...................................


Wauguzi wametakiwa kuendelea kutekeleza majukumu ya kazi kwa kuzingatia kanuni na taratibu za kitaaluma kwa lengo la kutoa huduma bora za afya kwa wagonjwa.


Wito huo umetolewa na Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania, Bi. Agnes Mtawa katika maadhimisho ya siku ya Uuguzi na Ukunga Duniani ambayo yamefanyika Hopistali ya Taifa Muhimbili (MNH) na kuudhuriwa na wauguzi na wakunga wa MNH na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
    

Maadhimisho hayo hufanyika Mei 12, kila mwaka na kauli mbiu ya mwaka huu ni “Wauguzi Sauti inayoongoza Afya kwa Wote.” Mwaka huu kitaifa maadhimisho yanafanyika mkoani Katavi.


Bi. Mtawa amewakumbusha wauguzi kuzingatia mafunzo yanayotolewa mahala pa kazi kwani ndio yanayochochea kutoa huduma bora ya afya kwa wagonjwa.


Amewataka wauguzi kutambua kwamba huduma wanayotoa kwa wagonjwa ni huduma ya kibinadamu kwani elimu inachangia kufikia malengo ya kutoa huduma bora.


“Hivi sasa mambo yetu yanakwenda vizuri. Malalamiko mengi yamepungua kwani ukifuatilia utabaini kwamba malalamiko mengi ni ya wagonjwa au mgonjwa kutaka kupewa kipaumbele kupata huduma ya afya badala ya kufuata utaratibu,” amesema Bi. Mtawa.


Pia, Msajili amewapongeza wauguzi kwa kutekeleza majukumu ya kutoa huduma za afya kwa kuzingatia taratibu za kitaaluma kwa asilimia 100.


Akisoma risala katika maadhimishisho, Katibu wa Chama cha Uuguzi na Ukunga Tanzania, tawi la Muhimbili, Bw. Seif Hamisi ameomba vitendo vya udhalilishaji kwa wauguzi vifanyiwe kazi kwa kuwa vitendo hivyo vinawapunguzia ari ya kufanya kazi.


Kupitia risala, Katibu ameishukuru Muhimbili kwa kuwapatia wauguzi mafunzo mbalimbali ambayo yamewasaidia kutoa huduma bora za afya kwa wagonjwa.


Naye, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Bw. Makwaia Makani amewataka wauguzi kutoa taarifa kwa uongozi wa MNH endapo watadhalilishwa wakati wa kutekeleza majukumu yao ya kila siku ili watakaobainika wachukuliwe hatua za kisheria.


“Mmesikia jamani nendeni mkawaeleze wenzenu kwamba endapo muuguzi atadhalilishwa, bila kuchelewa naomba atoe taarifa kwa uongozi ili wanaofanya hivyo tuwafikishe mbele  ya vyombo vya dola,” amesema Bw. Makani.

Saturday, May 11, 2019

JKT KUSHIRIKI UKARABATI WA UWANJA WA MPIRA LINDI.

NA HADIJA HASSAN, LINDI.

Jeshi la kujenga Taifa (JKT) kuongeza nguvu ya ukarabati wa Uwanja wa mpira wa Miguu wa Ilulu Stadium uliopo Manispaa ya Lindi Mkoani Lindi.


Uwanja huo wa Ilulu unatarajiwa kutumika katika fainali za Azam Federation Cup (FA) Zitakazofanyika Juni mosi mwaka huu 2019.


Akizungumza na waandishi wa Habari, Mkuu wa Wilaya ya Lindi ambae pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya uwanja huo Shaibu Ndemanga alisema kuwa wanajeshi hao wameshaanza kuwasili toka siku ya Ijumaa ya tarehe 10 mwezi huu na wataanza kufanya kazi hiyo mapema juma tatu ya Mei 13.


Alisema mpaka sasa tayari wanajeshi 13 wameshawasili na wanatarajia kuwa na wanajeshi 30 ambao watashiriki katika kukarabati uwanja huo huku akitaja fani za wanajeshi watakaofanya kazi hizo kuwa ni pamoja na Wahandisi wa Ujenzi, mafundi ujenzi pamoja na wataalamu wa ujenzi.


Ndemanga pia alitumia nafasi hiyo kumshukuru Mkuu wa Jeshi la kujenga Taifa (JKT) kwa kukubali ombi lao la kuwatumia wanajeshi hao katika shughuli za ukarabati wa uwanja huo