Saturday, May 11, 2019

SERIKALI YASISITIZA KATAZO LA MIFUKO YA PLASTIKI.

Mtakumbuka kuwa 9 Aprili 2019 Serikali ilitoa Tamko la kusitisha matumizi ya Mifuko ya plastiki hapa nchini ifikapo Juni Mosi 2019.

Katazo hili linalenga kuepusha athari za kiafya na mazingira zinazoendelea kujitokeza kutokana na matumizi ya mifuko hiyo.

Katazo hilo lililotolewa na Waziri Mkuu Mhe. Kasssim Majaliwa linahusu kupiga marufuku uzalishaji, uingizaji, usafirishaji nje ya nchi, usambazaji, uuzaji na matumizi ya mifuko ya plastiki ya aina zote.

Ofisi ya Makamu wa Rais imekuwa ikitoa taarifa mbalimbali ili kuwaelimisha wananchi kuhusu katazo hilo kupitia Vyombo vya Habari ikiwa ni pamoja na magazeti, Runinga na Redio, Mitandao ya Kijamii, Mikutano ya wadau na kupitia mikusanyiko ya watu ikiwa ni pamoja na taarifa kusomwa katika nyumba za ibaada.

Mpaka sasa Serikali imetekeleza yafuatayo:
Ofisi ya Makamu wa Rais imeandaa Kanuni kuhusu Katazo hili.

Kanuni hizi zitaanza kutumika tarehe 1 Juni 2019. Kwa mujibu wa Kanuni hizi, itakuwa ni marufuku kuzalisha, kuingiza nchini, kusambaza na kutumia mifuko ya plastiki iliyotajwa katika Katazo hili.

Kiwanda, Kikundi cha Watu au Mtu Binafsi atakayebainika kukiuka matakwa ya Kanuni hizi atakuwa ametenda kosa la jinai na hivyo sheria itachukua mkondo wake.
 
Tumetoa maelekezo Mahsusi kwa Sekretariet za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhusu utekelezaji wa katazo hii ambapo baadhi yao wameanza kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya uhifadhi wa shehena ya mifuko itakayosalimishwa.
 
Kwa kushirikiana na Makampuni ya Simu ya Vodacom, Tigo, Airtel na Halotel tumefanikiwa kutuma ujumbe mfupi kwa njia ya simu kwa watumiaji wa mitandao hiyo ambapo watumiaji milioni 11 wa Tigo, Milioni 15.5 wa Vodacom wameshapata ujumbe huu, hii itakuwa endelevu kila wiki.
 
Tumeandaa na kusambaza taarifa kwenye taasisi za dini ili nao watusaidie kufikisha ujumbe huu kwa waumini wao, tunawashukuru sana wameitikia wito vizuri.

Tumekutana na wazalishaji wa mifuko mbadala wa plastiki na wamepanga kuongeza kasi zaidi uzalishaji wa bidhaa hii na baadhi wameshaagiza mitambo ya kuzalisha mifuko mbadala.

Tunaendelea kutoa matangazo kwa kutumia vipaza sauti katika ngazi ya Kata, Mitaa na Vijiji kila wiki
Tumeendelea kutoa elimu kupitia Vyombo vya Habari ikiwa ni pamoja na kufanya Media Tour, kutoa ‘Count down’ kwenye magazeti, kutumia redio za kijamii na redio za mikoani kutoa matangazo juu ya katazo hili.

Pia tumetumia mitandao ya kijamii (Tovuti, blogs, facebook, twitter na istagram) bila kusahau katuni ili kuhakikisha ujumbe unafika kote.

Tumetengeneza Bronchure, fliers, Banners na stickers na tunahakikisha tunawasambazia watu wote ili wapate uelewa ikiwa ni pamoja na wasafiri katika Vyombo vya usafiri

Tunaendelea na utoaji wa Makala maalumu katika magazeti na kutumia redio kurusha matangazo yetu.
Jitihada zote hizi zinapaswa kuungwa mkono na si kubezwa, pia nitoe rai kwa watanzania wote kutopotosha jambo hili kama ilivyofanywa juzi katika kipande cha video (Clip) iliyosambazwa katika mitandao ya kijamii.

Na kipande hiko ni cha mwaka jana 2018 wakati wa kikao kilichoandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kuzungumza na Wadau wa mifuko.
 
Ikumbukwe kuwa ifikapo tarehe 1 Juni 2019, Serikali itaendesha operesheni kabambe nchi nzima ya kusaka mifuko hii.

Operesheni hii itahusisha Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya, Mamlaka za Serikali za Mitaa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Shirika la Viwango la Taifa (TBS), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, pamoja na Mamlaka za Viwanja vya Ndege, Bandari, Forodha, Uhamiaji, na Usafiri wa Nchi Kavu.
 
Kwa wale ambao watakuwa tayari kusalimisha kwa hiari shehena ya mifuko watakayokuwa nayo, utaratibu utatolewa wa mahali rasmi wanapotakiwa kuisalimisha kwenye maeneo yao.
 
Kwa taarifa zaidi kuhusu utekelezaji wa katazo hili Wananchi kwa ujumla mnashauriwa kutembelea Ofisi za Kanda za Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) zilizopo Dar es Salaam, Mtwara, Dodoma, Mbeya, Mwanza, Kigoma na Arusha.

Aidha, wanaweza pia kuwasiliana na Wakurugenzi wa Halmashauri za Majiji, Manispaa Miji na Wilaya.
 
Nirudie tena kutoa rai kwa Watanzania wote kuzingatia maelekezo haya ya Serikali pamoja na matakwa ya Kanuni za kupiga marufuku matumizi na biashara ya mifuko ya plastiki nchini kwa mustakabali wa uhifadhi wa mazingira ya nchi yetu.
 
Asanteni kwa kunisikiliza,
Imetolewa na:
Balozi Joseph E. Sokoine
NAIBU KATIBU MKUU, OFISI YA MAKAMU WA RAIS
11 MEI, 2019

MANISPAA YA LINDI KUANDAA MPANGO WA USAFIRI KWA WANAFUNZI.

 NA HADIJA HASSAN, LINDI.

Manispaa ya Lindi Mkoani humo imesema inaanda mpango maalumu wa kuwasaidia Usafiri wanafunzi wanaoishi mbali na maeneo ya shule.


Hayo yamesemwa jana Mei 10, 2019 na mkuu wa Wilaya ya Lindi Shaibu Ndemanga mbele ya Mkuu wa Mkoa huo alipokuwa ametembelea katika shule ya Sekondari ya Mingoyo iliyopo kata ya Mnazi mmoja manispaa ya Lindi.


Ndemanga alisema kama Halmashauri imeamua kuandaa mpango huo kwa kuwa wamebaini kuwepo kwa wanafuzi ambao hutembea umbali mrefu kutoka maeneo wanayoishi na kuja shuleni.


Ndemanga alisema wapo baadhi ya wanafunzi wanaosoma katika baadhi ya Shule za Sekondari katika Manispaa hiyo ambao hutembea umbali wa zaidi ya kilomita 16 wakati wa kwenda na kurudi shuleni.


Elody Osward (14) ni miongoni mwa wanafunzi wanaosoma katika shule ya Mingoyo iliyopo halmashauri ya Manispaa ya Lindi anaishi katika mtaa wa mayani ambae hulazimika kutembea umbali wa kilomita 16 wakati wa kwenda na kurudi shuleni.


Osward alisema kuwa Changamoto anayokabiliana nayo wakati anakwenda shuleni ni kukutana na wanyama wakati akiwa njiani ambao analazimika kuwafukuza ama kujificha ili kuwaacha wapite wanyama hao ndipo yeye aendelee na safari yake ya kwenda shuleni ama kurudi nyumbani.


Hata hivyo Osward alisema kitendo hicho cha yeye kutembea umbali mrefu kunamfanya ajihisi kuchoka anapokuwa darasani ambapo aliiomba serikali kumsaidia chombo cha usafiri ambacho kitaweza kumuwezesha kufika kwa wakati shuleni hapo.


Nae mkuu wa Shule ya Sekondari Mingoyo, Mwichande Lihoma, alimuelezea Osward kuwa ni mwanafunzi hodari na anaeonakana kupenda masomo kwani pamoja na kwamba anaishi mbali na Shule hiyo lakini hajawahi kukosa kufika shuleni na kwamba anapofika kwa kuchelewa huwa anafidia muda wake kwa kuchelewa kutoka Shuleni.


Alisema kitendo hicho cha kuchelewa kuondoka ni hatari kwake kwani hufika usiku sana nyumbani kwao.


Nae mkurugenzi wa Manispaa ya Lindi Jomary Satura, alisema kuwa katika kutekeleza mpango huo tayari wameshaagiza gari ndongo aina ya hice ambayo itakuwa inatumika kwa wanafunzi hao ambao wanaishi mbali na maeneo ya Shule.


Alisema gari hizo zitakapoanza kufanya kazi , zitaanzia katika Stendi kuu ya Mabasi ya Halmashauri hiyo na majira ya saa 12 Asubuh kuelekea Mto Mkavu na nyingine kuelekea Mkwaya

RIDHIWANI AWATAKA WANAFUNZI KUSOMA MASOMO YA SAYANSI.

MBUNGE wa jimbo la chalinze wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani Ridhiwani Kikwete, akifungua kitambaa kama ishara ya uzinduzi wa Hosteli ya wasichana katika shule ya sekondari Mboga iliyopo katika Jimbo lake.


Wanafunzi wa shule ya sekondari Mboga Halmashauri ya Chalinze wakisalimiana na Mbunge wa jimbo hilo, Ridhiwani Kikwete wakati wa uzinduzi wa Hosteli ya wasichana katika shule hiyo.

...............................................
 
Na Shushu Joel, chalinze.


MBUNGE wa jimbo la chalinze wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani Ridhiwani Kikwete amewataka wanafunzi wa sekondari katika jimbo lake kusoma kwa bidii masomo ya sayansi kutokana na uharaka wa upatikanaji wa ajira kwenye fani hiyo.


Rai hiyo ameitoa alipokuwa akizungumza na wanafunzi wa shule ya sekondari Mboga mara baada ya uzinduzi wa majengo ya hostel kwa wasichana shuleni hapo .


"Masomo ya sayansi yana nafasi kubwa katika ajira na hasa katika serikali ya viwanda kutokana na uzalishaji mwingi ni wa kisayansi hivyo tuchangamkie nafasi ya kusoma masomo hayo " Alisema Kikwete.


Aliongeza kuwa kutokana na kukua kwa technologia duniani wanasayansi wamekuwa wakihitajika kila siku hivyo juhudi za ufundishaji wa masomo hayo iongezeke ili kuwafungulia fursa watoto wetu wa chalinze.


Mbali na hilo Kikwete amewataka wanafunzi kuzingatia masomo kwani wazazi na walezi wamekuwa wakijibana katika matumizi yao ya kila siku ili kuhakikisha wanasomo na kuja kuwakomboa baadae hivyo muda wautumie ipasavyo ili kufanikisha malengo yao ya baadae.


"Ni aibu msichana kukatisha masomo yako kwa ujauzito na pia aibu kwetu wazazi hivyo nawataka msidanganyike na wavulana katika kipindi hiki cha masomo yenu, pia hata wavulana kuwekwa ndani na kinamama wenye uwezo ingawa kesi hii ni ndogo kuliko ya wasichana kukatishwa masomo yao na wanaume".


Aidha amewataka wavulana kuwa na subra kwani bado anakusanya nguvu za kumalizia majengo yao matatu ya hostel ili nao waweze kuhamia shuleni hapo kwa kusudi la kuendelea kupiga kitabu.


Omary Adam ni mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule hiyo amempongeza Mbunge huyo kwa juhudi zake za kupambana na elimu katika jimbo hilo ili uzalishaji wa wasomi jimboni humo uweze kuwa mkubwa.


Aliongeza kuwa kwa upande wa wasichana wao tayari majengo yao yamekamilika na wamesha anza kutumia lakini yetu wavulana bado kupauliwa hivyo kama ukipata wafadhili na sie utukumbuke ili kupunguza nafasi za kwenda na kurudi nyumbani nasi tuwe tunabaki kama wasichana.


Naye Amina Ally amemshukuru Mbunge huyo kwa kutambua thamani ya watoto wa kike na kuona changamoto zao zilizokuwa zikiwakabili na kuzitatua kwa haraka.


Hivyo kutokana na wasichana Kulala shuleni ufaulu utaongezeka kwa asilimia kubwa kwani vishawishi tulivyokuwa tukivipata njiani havitakuwepo tena.

MAGAZETI YA LEO MEI 11, 2019.

Friday, May 10, 2019

RC. ZAMBI ABAINI MAKOSA KWA MADEREVA WA BODABODA LINDI.

Mkuu wa Mkoa huo wa Lindi Godfrey Zambi akizungumza na madereva wa bodaboda katika kata ya mnazi mmoja Halmashauri ya Manispaa ya Lindi Mkoani humo.
..............................................

NA HADIJA HASSAN, LIND.


Zaidi asilimia 98 ya madereva Boda boda wa kata ya mnazi mmoja Halmashauri ya Manispaa ya Lindi Mkoani humo hutumia vyombo hivyo vya usafiri bila kuzingatia sheria za usalama barabarani jambo ambalo huchangia kuwepo kwa Ajali za mara kwa mara.


Hayo yamebainika baada ya Mkuu wa Mkoa huo wa Lindi Godfrey Zambi kufanya Ziara katika Manispaa hiyo na kulazimika kuteremka kwa muda katika kituo kimoja cha Boda boda Mjini humo ili kuzungumza na madereva hao.


Wakati Mkuu huyo wa Mkoa akizungumza na Madereva wa Bodaboda hao alimuamuru ofisa wa polisi kutoka ofisi ya Mkuu wa jeshi la Polisi Wilaya ya Lindi inspekta Mohamedi kamada, kufanya ukaguzi wa madereva hao pamoja na pikipiki zao Ambapo Baada ya kufanya ukaguzi huo kwa zaidi ya bodaboda 15 zilizopo katika kituo hicho afisa huyo alibaini mapungufu kadhaa kutoka kwa madereva pamoja na pikipiki zao


Moingoni mwa dosari hizo ni pamoja na asilimia 98 ya piki piki hizo zilizokaguliwa zimekutwa hazijakatiwa bima, pikipiki hizo hazina kofia mbili ngumu (helmet) ambazo ni muhimu kwa abiria na dereva kwa ajili ya kujilinda pindi ikitokea ajali.


Dosali nyingine ni madaereva hao kutokuwa na leseni inayowaruhusu kuendesha chombo chochote cha moto pamoja na mavazi waliyovaa kuonekana sio salama kwa shughuli wanayoifanya.


Akielezea makosa aliyobaini yanayotokana na mavazi, mkaguzi huyo wa Polisi alisema ni pamoja kutokuvaa koti linalizuia upepo pamoja na uvaaji wa kandambili ( marapa au ndara)


Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Lindi Godfrey Zambi alitoa Wiki moja kwa Madereva Boda Boda hao kuhakikisha wanalipia bima katika pikipiki zao, wawe na leseni zinazowaruhusu kuendesha vyombo vya moto kuwa na kofia ngumu (helmet) mbili pamoja na koti la kuzuia upepo huku akimuagiza ofisa wa Mkuu wa Jeshi la Polisi Wa Wilaya hiyo kufanya ukaguzi baada ya muda huo.


Zambi alisema endapo kutakuwa na madereva wa Boda boda watakaokaidi agizo hilo atawachukulia hatua kali za Kisheria.


Pamoja na mambo mengine pia Zambi alitumia fursa hiyo kupiga marufuku kwa madereva Boda boda wa Mkoa huo kuacha tabia ya kupakia abiria zaidi ya mmoja (mishikaki) pamoja na kuacha kutumia boda bada zao kama chombo cha kubebea mizigo.
 
Askari wa usalama barabarani, inspekta Mohamedi kamada, akifanya ukaguzi kwa madereva pamoja na pikipiki zao kata ya mnazi mmoja Halmashauri ya Manispaa ya Lindi Mkoani humo.

Picha na Hadija Hassan.