Monday, May 6, 2019

TUCHANGAMKIE FURSA YA VIFUNGASHIO - MGALU

WANANCHI katika vijiji vinavyounda halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani, wametakiwa kuchangamkia fursa ya kufungiwa kwa mifuko ya plastiki, kwa kutengeneza vikapu vya asili, vitakavyochukua nafasi ya mifuko ya plastik.


Kufungiwa kwa mifuko hiyo kunakoelezwa ni hatua ya kupambana na uchafuzi wa mazingira, kunatokana na mifuko hiyo kutooza haraka iwapo ardhini, licha ya kuwa msaada kwa wananchi katika kubebea vitu mbalimbali.


Ushauri huo umetolewa na Mbunge wa viti maalum, mkoa wa Pwani, Subira Mgalu, alipozungumza na wajasiriamali katika vijiji vilivyopo Kata za Talawanda na Kiwangwa, ambao wamekopeshwa fedha za asilimia zilizotolewa na halmashauri ya Chalinze, wilayani hapa.


Alisema kwamba serikali iliyopo madarakani kupitia wizara husika ya mazingira, imefanya utafiti wa kina hivyo kubaini uwepo wa uchafuzi wa mazingira, na kufika hatua ya kufungia mifuko hiyo, inayolenga kupambana na hali hiyo.


"Tuchangamkie fursa ya kutengeneza vikapu vyetu vya asili, ukiangalia kwa haraka unaweza kusema kufungiwa kwa mifuko kutatuathiri katika uchukuzi, hii imeturejeshea fursa ya kibiashara ya kutengeneza vikapu, ambavyo wazee wetu walikuwa wanavitengeneza," alisema Mgalu.


"Miyaa, ukindu na rangi vyote tunavyo, kilichobaki sasa ni kuitumia fursa hii kutengeneza vikapu kwa wingi, kisha tuvipeleke katika maeneo mbalimbali ninaimani kubwa kwamba hatua hii imeleta neema kwetu," alisema.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa halmashauri ya Chalinze Said Zikatimu alisema kwamba, wanaendelea na ukopeshaji wa vikundi vya ujasiriamali, ikiwa ni kuunga mkono juhudi za serikali kuvikopesha vikundi mikopo isiyokuwa na riba.


"Katika halmashauri yetu fedha sio tatizo, tunazo za kutosha, tunachokiomba kutoka kwenu ni kuanziasha vikundi, kuvisajili kisha kuwasilisha kwenye ofisi ya Maendeleo ya Jamii ili muweze kunufaika na mikopo hiyo isiyo na riba," alisema Zikatimu.

KIZIMBANI KWA KUBAKA MTOTO CHINI YA MIAKA 10.

NA HADIJA HASSAN, LINDI.

MKULIMA wa Kijiji na Kata ya Rutamba, Halmashauri ya Wilaya Lindi Mkoa wa Lindi, Issa Seif Puyaye (51) amefikishwa mahakamani akikabiliwa na Shitaka la kubaka Mtoto mwenye umri chini ya miaka kumi (Jina linahifadhiwa).


Puyaye amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Lindi na kusomewa Shitaka lake mbele ya Hakimu Faudhia Jemedari, na mwanasheria wa Serikali Godfrey Mramba. 


Akimsomea Shitaka lake, Mramba alidai kuwa Aprili 14 mwaka huu, Mshitakiwa alikamatwa na askari wa Jeshi la Polisi, kufuatia wazazi wa Mtoto huyo kutoa taarifa kwenye chombo hicho. 


Mramba alidai Mahakamani hapo kuwa wazazi wa Mtoto huyo anayesoma Darasa la Pili katika Shule ya Msingi Mpilipili iliyopo Manispaa ya Lindi,walichukuwa uwamuzi huo baada ya kupewa taarifa na walipomkagua waliweza kubaini kufanyiwa kitendo hicho cha kinyama. 


Alidai kwamba kutokana na kitendo hicho mshitakiwa amefanya kosa kwa mujibu wa kifungu 130 (1) (2) (e) na 131 (1) Sheria na kanuni ya adhabu ya makosa sura ya 16/2002. 


Mwanasheria huyo aliiambia Mahakama hiyo kwamba mshiatkiwa alipata nafasi ya kumfanyia unyama huo, kutokana na Mtoto huyo kwenda likizo kwa ndugu zake wengine. 


Hata hivyo mshitakiwa amekana kosa na kesi hiyo namba 34/2019, imepangwa kusikilizwa tena Mahakamani hapo Mei 13 mwaka huu, na mshitakiwa amepelekwa rumande baada ya kukosa wadhamni.


DKT. NDUGULILE ATOA RAI KWA VIONGOZI WA KISIASA KUTOINGILIA KAZI ZA TAALUMA YA AFYA

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile (kulia ) akipokea maelezo kutoka kwa mmoja wa wakunga ya namna wanavyowahudumia wakina mama wajawazito na watoto wakati alipotembelea Banda la Chama cha Wakunga Tanzania(TAMA),  katika Maadhimisho ya Siku ya Wakunga Duniani ambayo yamefanyika Kitaifa katika Uwanja wa Bariadi Mkoani Simiyu.
......................................


Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile ametoa rai kwa viongozi wa Kisiasa hapa nchini kuacha kuingilia kazi za Kitaaluma katika sekta ya Afya na kuwaomba wawaache wataalam wafanye kazi zao kwa misingi na miiko ya Kitaaluma inayowaongoza.


Dkt. Ndugulile ameyasema hayo katika Maadhimisho ya Siku ya Wakunga Duniani yaliyofanyika Kitaifa katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, chini ya Kauli Mbiu “Wakunga Watetezi wa Haki za Wanawake”, ambapo alikuwa akimwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.


Amesema hivi karibuni kumekuwa na matamko yanayotolewa na baadhi ya viongozi wa kisiasa yanayowakatisha tamaa watumishi wa sekta ya afya na baadhi ya viongozi wameanza kuingilia masuala ya kitaalum, hivyo akawaomba ikiwa viongozi hao  watakutana na changamoto za watendaji wa afya waishirikishe wizara ya afya ili wachukuliwe  hatua kwa mujibu wa taaluma zao.


“Niwaombe sana viongozi wa Serikali na Viongozi wa vyama, masuala ya kitaaluma yanashughulikiwa kitaaluma kama kuna changamoto na wanataaluma ndiyo maana tuna mabaraza ya taaluma na ndiyo maana sisi wizara tupo mtushirikishe, nimelisema hili kwa sababu nimeona sekta imeanza kuingiliwa” alisema Dkt. Ndugulile.


Aidha, Dkt. Faustine Ndugulile amewataka wakunga hapa nchini kuendelea kuzingatia miiko na misingi ya taaluma yao katika huduma wanazotoa kwa jamii na kuahidi kuwa Serikali haitasita kuwachukulia hatua wale wote watakaokiuka misingi hiyo kwa kuwa jamii inahitaji heshimu, utu, upendo na kutiwa moyo
Katika hatua nyingine. 


Dkt. Ndugulile ametoa wito kwa  wadau mbalimbali wa maendeleo na jamii kwa ujumla kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha huduma za afya ili changamoto ya vifo vitokanavyo na uzazi vibaki kuwa historia ambapo amesema kwa sasa wanawake 11,000 wanakufa kila mwaka kutokana na uzazi.


Rais wa Chama cha Wakunga Tanzania, Bibi. Feddy Mwanga ameiomba Serikali kuongeza idadi ya wakunga ili mkunga aweze kutoa huduma kwa kiwango kinachokubalika Kitaifa na kimataifa huku akisisitiza Serikali kuona haja ya kujenga nyumba za wakunga katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya vinavyoboreshwa na vinavyojengwa.


Naye Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthoy Mtaka amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutoa shilingi bilioni saba  fedha kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa na shilingi bilioni 4.5 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali tatu za Wilaya Bariadi, Busega na Itilima ambazo ujenzi wake unaendelea vizuri.


Aidha, Kiswaga ameshukuru Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu Duniani(UNPFA) kwa namna linavyoshirikiana na Serikali mkoani Smiyu kwa kukarabati baadhi ya vituo, kununuaa vifaa mbalimmbali, kutoa mafunzo kwa wakunga jitihada ambazo zimechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.


Akitoa taarifa ya Mkoa, Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini amesema
Idadi ya wakunga katika vituo vya kutolea huduma za afya Simiyu imeongezeka hali iliyofanya wajawazito wengi kujifungulia katika vituo vya afya kutoka asilimia 62 mpaka asilimia 68, hivyo vifo vya mama wajawazito vimepungua kutoka vifo 48 mwaka 2017 mpaka vifo 40 mwaka 2018.


Naye Makamu Mwakilishi Mkaazi wa UNFPA hapa nchini, Dkt.Hashina Begum amesema kwa kushirikiana na Chama cha Wakunga nchini (TAMA) limetoa mafunzo kwa wakunga 90 kutoka katika vituo vilivyoboreshwa ili kuwasaidia wakina mama wajawazito na watoto kupata huduma za dharura na kupunguza vifo kwa mama na mtoto vitokanavyo na uzazi.

  
Grace Magengeni Mkunga kutoka Jijini Dodoma amesema” siku yetu imefana tunashukuru hotuba ya Naibu Waziri imetutia moyo katika kuwahudumia wanawake na watoto, nawashauri wenzangu tusimamie taaluma zetu tufanye kazi kwa bidii naamini hao wanaotuingilia majukumu yetu wataachaa maana ni kweli,  tunashukuru Naibu Waziri kulisemea hili suala”