Thursday, April 25, 2019

BAGAMOYO WAADHIMISHA SIKU YA MALARIA DUNIANI.



 Wahudumu wakitoa huduma ya vipimo vya malaria kwa wananchi waliofika uwanja wa majengo mjini Bagamoyo leo Aprili 25, 2019 katika maadhimisho ya siku ya Malaria duniani.
 
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Bagamoyo, Athumani Stili akimuakilisha Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo.
.................................
 
Wananchi wilayani Bagamoyo wametakiwa kuwa na tabia ya kufika hospitali kupata pindi wanapohisi dalili za homa ili kujua kama ni Malaria au la.


Wito huo umetolewa na Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Bi Zainabu Kawawa katika maadhimisho ya siku ya Malaria duniani kupitia hutuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Bagamoyo, Athumani Stili.


Amesema baadhi ya wananchi wamekuwa na tabia ya kutumia dawa bila ya kupima hali inayopelekea kupata madhara pale ugonjwa unaposhika kasi.


Alisema sio kila homa ni Malaria hivyo ni vyema unapojisikia maumivu ya mwili kufika kwa wataalamu wa afya ili ujue kitu gani kinakusumbua.


Awali akisoma Taarifa mbele ya Mgeni rasmi Mratibu wa Malaria wilaya ya Bagamoyo Dkt. Zena Mtajuka amesema miongoni mwa magonjwa yanayosababisha vifo wilayani humo ni pamoja na Malaria.


Alisema katika kipindi cha mwaka 2018 asilimia tano ya wagonjwa waliohudhuria kitengo cha nje (OPD) wamekutwa na Malaria huku wagonjwa waliolazwa ni asilimia 7.9 ndio waliokutwa na Malaria.


Alisema ugonjwa wa Malaria huleta athari kwenye jamii na taifa kwa ujumla kwakua kipato kinashuka kutokana na watu kuugua malaria.


Aidha, alisema ili kufikia lengo la taifa katika kudhibiti Malaria, Halmashauri ya Bagamoyo imejipanga katika kutekeleza kazi mbalimbali za kupambana na ugonjwa huo.


Alisema miongoni mwa kazi hizo ni upatikanaji wa matibabu sahihi ya ugonjwa wa malaria katika vituo vyote 27 vilivyopo katika Halmashauri hiyo, kupatikana kwa Vyandarua vyenye viuatilifu kwa wajawazito na watoto chini ya mwaka mmoja wakati wa chanjo ya kwanza ya surua.


Taasisi ya Utafiti wa afya ifakara (ihi) tawi la Bagamoyo ndio waliodhamini maadhimisho hayo na kutoa elimu mbalimbali kwa jamii kuhusu ugonjwa wa Malaria.


Katika maadhimisho hayo ambayo kwa Bagamoyo yamefanyika uwanja wa Majengo ambapo wananchi walipata huduma ya kupima malaria pamoja Virusi vya Ukumwi bila ya malipo.


Siku ya Malaria duniani huadhimishwa kila mwaka ifikapo Aprili 25 ambapo ujumbe wa mwaka huu "Ziro Malaria huanza na mimi" 
 Mwenyekiti wa Bodi ya Afya Halmashauri ya Bagamoyo, Roswita F. Kasikila akizungumz katika maadhimisho hayo yaliyofanyika uwanja wa majengo mjini Bagamoyo.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bagamoyo, Ally Ally issa akizungumza  katika maadhimisho hayo yaliyofanyika uwanja wa majengo mjini Bagamoyo.

 Kiongozi wa wanasayansi kutoka Taasisi ya Utafiti wa afya ifakara (ihi) Dkt. Ally Olotu akizungumza  katika maadhimisho hayo yaliyofanyika uwanja wa majengo mjini Bagamoyo.
 
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Bagamoyo, Athumani Stili akimuakilisha Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, ( wa pili kushoto, wa kwanza kushoto ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bagamoyo, Ally Ally issa, wa tatu kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Afya Halmashauri ya Bagamoyo, Roswita F. Kasikila na wa kwanza kulia ni Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa afya ifakara (ihi) tawi la Bagamoyo Dkt. Aseline Charles.


Kaimu Mganga Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Dkt. Salvio Wikes kizungumza  katika maadhimisho hayo yaliyofanyika uwanja wa majengo mjini Bagamoyo.
 
 Mratibu wa Malaria wilaya ya Bagamoyo Dkt. Zena Mtajuka (kulia) akimkabidhi risala Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Bagamoyo, Athumani Stili akimuakilisha Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo.


NIDA, TCRA NA MAKAMPUNI YA SIMU NCHINI KUWEZESHA ZOEZI LA USAJILI WA LAINI ZA SIMU KWA KUTUMIA ALAMA ZA VIDOLE.

Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Makampuni ya Simu nchini, itawezesha zoezi la uandikishaji wa watumiaji wa simu nchini kwa kutumia Namba za Utambulisho wa Taifa au Kitambulisho cha Taifa.  Zoezi la Uandikishaji wa laini za simu linatarajia kufanyika kuanzia tarehe 01-Mei-2019. 


Mazoezi ya majaribio ya zoezi hili yamefanyika katika baadhi ya Mikoa na Taasisi na kuonyesha mafanikio.


NIDA tayari imesajili asilimia 88 ya watu wote wanaostahili kusajiliwa kwa ajili ya vitambulisho vya Taifa nchi nzima. 

Zoezi la Utambuzi na usajili ni endelevu, hivyo asilimia 12 ya lengo la usajili lililobaki linaendelea kutekelezwa katika wilaya zote nchini kwa kusajili watu ambao hawakusajiliwa kwenye zoezi la usajili wa umma (Mass Registration) na ambao wamekisha umri wa miaka 18, ambacho ni kigezo cha kisheria kinachoruhusu mwananchi kusajiliwa kwa ajili ya Utambulisho wa Taifa.  


Vile vile usajili wa umma unafanywa tena katika mikoa ambayo watu wengi hawakusajiliwa katika usajili wa awali. Mikoa hiyo ni pamoja na Dar es salaam, Tanga, Pwani na Kigoma.


NIDA tayari imetengeneza Namba za Utambulisho wa Taifa Milioni 12, sawa na asilimia na 59 ya usajili uliofanyika. Zoezi la uhakiki, kuchakata na kutengeneza Namba za Utambulisho wa Taifa linaendelea kutekelezwa kwa kasi usiku na mchana. 


Aidha tunatoa rai kwa wale wote ambao wamejulishwa kuwa vitambulisho vyao vipo tayari wafike Ofisi za NIDA au Ofisi za Serikali za Mitaa walipo jiandikishia kuvichukua. Vitambulisho vya Taifa vinaendelea kuzalishwa na kusambazwa kwa wananchi. 


Namba za Utambulisho wa Taifa zitatumika katika usajili wa Namba za simu na matumizi mengine. Hivyo wale ambao tayari wana Namba za Utambulisho wa Taifa wazitumie kujisajili wakati vitambulisho vinazalishwa.


Wananchi mnaweza kupata Namba ya Utambulisho wa Taifa na huduma zingine zitolewazo na NIDA kwa njia zifuatazo:-


a. Kupiga namba * 152 *00#; chagua Ajira na Utambuzi; Chagua NIDA


b. Kupakua nakala ya Kitambulisho cha Taifa kwa kutembelea tovuti: https://services.nida.go.tz/nidportal/NID_Copy.aspx au tovuti ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa.


c. Kupiga simu huduma wateja; 0673 333444, 0743 202020, 0743 201020, 


d. 0759 102010, 0765 201020. 


e. Kufika ofisi za NIDA ya Wilaya ilyopo karibu.


Ni Muhimu kwa Wananchi wote wenye sifa za kusajiliwa kwa ajili ya Utambulisho wa Taifa kufanya hivyo sasa pasipo kusubiri mpaka wanapokuwa na hitaji la haraka kwani uhakiki wa taarifa zako lazima ufanyike kabla ya utoaji wa Namba ya Utambulisho wa Taifa na baadae kitambulisho cha Taifa.

“Utambulisho wa Taifa kwa Maendeleo na Ustawi wa Nchi Yetu”


Imetolewa na

MAMLAKA YA VITAMBULISHO VYA TAIFA
23 APRILI, 2019.

WAANDISHI WATAKIWA KUFUATA MAADILI NA SHERIA ZA UANDISHI KATIKA VYOMBO VYA HABARI

Baraza la Habari Tanzania (MCT)  limewataka waandishi pamoja na wahariri hapa nchini waweze kuwa makini katika uandaaji wa taarifa ambazo zinakidhi kiwango na zenye maadili ya uandishi na pia zisiegemee upande mmoja kwani kunaweza kumsababishia kuingia kwenye wakati mgumu.


Hayo yamesemwa leo katika uzinduzi wa machapisho ya vitabu ambavyo vimetoa ripoti mbalimbali juu ya uhuru wa wanahabari katika vyombo vya habari hapa nchini hasa kutokana na matukio mbalimbali yaliyojitokeza hivi karibu ikiwemo kupotea kwa waandishi na wengine kutishiwa.


Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Jaji Mstaafu Juxon Mlay amesema kuwa tunalinda na kutetea uhuru wa wanahabari kwaajili ya wananchi kupata habari na si kwaajili ya wanahabari pekee.


“Mazingira ya sasa ni magumu katika tasnia ya uandishi wa habari, sasa yale ambayo yameandikwa kwa kutuonya, kutuelekeza na kutukumbusha humu ni muhimu kwetu ili tuweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi katika mazingira ya sasa wakati huohuo tukiwa tukijalibu kupambana na kushirikiana na wale wenye mamlaka ili kuboresha haya mazingira ya kufanya kazi zetu”. Amesema Bw.Mlay.


Kwa upande wa mwandishi wa chapisho la taarifa inayomhusu mwandishi wa Channel Ten Geofrey Nilahi ambaye alikuwa Ruvuma, Bw. Attilio Tagalile amesema kuwa mwaka jana mwandishi huyo aliwaandikia viongozi wa MCT ya kuwa maisha yake yapo hatarini kutokana na kazi ambayo anaifanya hasa kutokana na kutoa taarifa ambayo ilikuwa inamkwaruzano baina ya wananchi na serikali.


“Alikuwa ameandika taarifa za kichunguzi zilikuwa zinaonyesha matatizo yaliyokuwa katika maeneo yale ambapo matatizo hayo ni pamoja na matatizo ya shule kutokana na wanafunzi kusoma katika mazingira magumu ikiwa jimbo hilo lina viongozi wakubwa”. Amesema Tagalile.


“Yeye anavyodai ni kwamba baada ya kupata stori zake alijaribu kupata wahusika ili aweze kubalansi stori zake kwamaana ya wabunge pamoja na wakuu wa wilaya na vilevile. Mbuge wa jimbo la Peramiho Jenista Mhagama alitumiwa ujumbe mara mbili lakini hakujibiwa”. Ameongeza Tagalile.


Hata hivyo Bw. Tagalile amesema kuwa waandishi walishiriki kufuta ile taarifa ambayo ameiandika mwandishi Nilahi, waandishi ambao walikuwa wanatakiwa kumuunga mkono kwa harakati zake lakini chakushangaza wao ndo wanakuwa chanzo cha kumkandamiza mwenzao.


Kwa upande wa Bi. Pili Mtambalike amesema ripoti ambayo ameia imelandaa imelenga kuangalia changamoto mbalimbali ambazo vyombo vya habari vimepitia ikiwemo masuala ya sheria,masuala ya sera za nchi pamoja na changamoto mbalimbali zitokanazo na sheria za vyombo vya habari.


“Hivi karibuni gazeti la Citizen lilifungiwa baada ya kuandika masuala ya uchumi, masuala ya uchumi si rahisi kukosewakosewa kwasababu kuna wachumi waliobobea ambao unaweza kuwauliza pia kuna takwimu zinatolewa na benki kuu pamoja na wizara husika na kama ni mwandishi mzuri ukiziandika zile huwezi kuwa na mashaka na taarifa yako”. Ameongeza Bi. Pili.


Aidha kwa upande wa Bw. Absalom Kibanda amesema kuwa katika chapisho la ripoti ambalo ameliandaa limelenga kuwakumbusha wanahabari wajibu wao kitaaluma pamoja na kimaadili ambapo hali ya vyombo vya habari kwasasa kuna wasomi wengi kuliko zamani.


“Kwanini kuna kuwa na ukiukwaji wa kitaaluma pamoja na misingi ya kimaadili kuliko ilivyokuwa zamani ambapo wasomi walikuwa wachache na pengine hili kwasisi katika vyombo vya habari tunatakiwa tujitathimini kama tutatimiza wajibu wetu kitaaluma na vilevile kimaadili”. Amesema Kibanda.

MAGAZETI YA LEO APRILI 25, 2019.