Wednesday, April 24, 2019

TUGHE PWANI YAHIMIZA MIRADI

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) Mkoa wa Pwani, Catherine John Katele, akimkabidhi fulana katibu wa chama hicho tawi la Chuo Cha Maendeleo Wilaya ya Kisarawe, Regina Mpashobirwa, kulia ni Mratibu wa TUGHE Muharami Juma, katikati ni Mwenyekiti wa Tawi hilo

..............................

Na Omary Mngindo, Kisarawe


April 24 CHAMA Cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) Mkoa wa Pwani, kimewataka wanachama wake kuanzisha miradi, itayowawezesha kujiendesha kupitia asilimia zinazorudishwa katika vyama vyao.


Aidha wameshauliwa kufungua akaunti benki zitazotumika kwa ajili ya kuingiziwa fedha hizo, ambazo wanaweza kuzitumia kwa kujikopesha kisha kurejesha kwa faida kidogo, hatua itayoviwezesha vyama vyao kujitegemea katika mambo mbalimbali.


Ushauri huo umetolewa na Mwenyekiti wa TUGHE mkoani hapa Catherine Katele, alipozungumza na wanachama wa chama hicho wilayani Kisarawe, akiwa kwenye ziara ya siku mbili ya kukutana na kusikiliza changamoto zinazowakabili.


"Kuna asilimia yenu 20 katika kila tawi, lakini kama hamna akaunti itakuwa vigumu kuwekewa, sababu siwezi kuziingiza katika akaunti ya Mwenyekiti, ni jambo la muhimu kuwa na akaunti ili mnufaike nazo kwa semina na miradi mbalimbali," alisema Mwenyekiti huyo.


Akizungumzia upandishwaji vyeo na maslahi yao, Catherine alisema kwamba, hilo limetokana na kazi nzuri inayofanywa na Rais Dkt. John Magufuli, ya kuwabaini watumishi hewa, na kwamba serikali inafanyiakazi, huku akiwataka waandike barua kwa viongozi wao kukumbushia masuala yao.


Kwa upande wao Mwambusa Juma ametaka kujua asilimia zao 20 ambazo hawajarudishiwa muda mrefu, Mwanana Msumi Afisa Tawala ametaka taarifa za vikao ziwafikie mapema, huku Mratibu wa TUGHE Wilaya Mwarami Juma akiwahimiza kujitokeza kwa wingi siku ya Mei Mosi ambayo Kimkoa inafanyika wilayani hapa.


Nae Ramadhani Maguo kwaniaba ya watumishi wanachama wa TUGHE ameelezea kilio cha kutolipwa malipo ya likizo kwa miaka zaidi ya mitano, hali inayowaweka katika mazingira magumu wakati wakiwa katika napumziko hayo. 


Akitoa shukrani kwa niaba ya wanachama wa chama hicho, Zuberi Pendeza kwanza alimpongeza Mwenyekiti huyo kwa ziara hiyo, huku akiomba watembelee maeneo ya kazi kwani wanakabiliwa na changamoto nyingi.


 "Kwaniaba ya wenzangu leo ndio tumepata elimu na faida ya TUGHE, tunakushukuru sana kwa elimu hii, tunawaomba mtutembelee maeneo ya kazi tunakabilwa na changamoto nyingi," alimalizia Pendeza.
 
 Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) Mkoa wa Pwani, Catherine John Katele, akiwa katika picha ya pamoja na wanachama wa TUGHE wanaofanya kazi katika Chuo cha Maendeleo ya FDC Wilaya ya Kisarawe Mkoani Pwani.
 
 Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) Mkoa wa Pwani, Catherine John Katele, akiwa katika picha ya pamoja na wanachama wa TUGHE wanaofanya kazi katika Chuo cha Maendeleo ya FDC Wilaya ya Kisarawe Mkoani Pwani. 
PICHA ZOTE NA OMARY MNGINDO. 

RAIS DK MAGUFULI AANZA ZIARA YA KIKAZI NCHINI MALAWI

MAGAZETI YA LEO APRILI 24, 2019.

DC KASESELA: AKANUSHA UWEPO WA KIWANDA CHA KUTENGENEZA UUME BANDIA

Mkuu wa wilaya ya Iringa Richard Kasesela akiongea na waandishi wa vyombo mbalimbali ofisini kwake juu ya kusambaa kwa habari inayohusu uwepo wa kiwanda cha kutengeneza uume bandia.
..................................


Siku chache baada ya kusambaa kwa picha zinazomuonesha Mkuu wa Wilaya ya Iringa Richard Kasesela akiwa ameshika viungo bandia vya kiume na kuzua Taharuki katika jamii, Mkuu huyo wa Wilaya ametolea ufafanuzi.


Akizungumza na Wandishi wa habari ofisini kwake  Kasesela amesema kuwa taarifa zilizosambaa mtandaoni juu ya uzalishaji wa viungo bandia vya kiume, zimeleta changamoto huku akiwataka wananchi  kuondokana na dhana potofu za kuchukua habari za mitandaoni na kuupotosha umma.


“Naomba niende kuwaomba radhi watanzania kwa ajili ya jambo ambalo lilileta taharuki kwenye mitandao ya kijamii hasa nchi ya jirani zetu hapo Kenya" alisema Kasesela. 


Kasesela aliwataka watanzania kuacha kufuatia mambo ya ajabu na kuyapa nafasi kwenye mitandao ya kijamii kuliko kupata mambo ya kujenga nchi na yenye tija kwa maslahi ya Taifa.


“Jamani ile habari ilitungwa na ni habari ya hovyo sana kwa kuwa nililishwa habari ambayo mimi sijaisema kwenye chombo chochote kile kwenye vyombo vya habari hivyo hiyo habari ni ya

kupuuza tu” alisema Kasesela.


Kasesela amewashauri watanzania kuhakikisha wanafatilia taarifa zenye kuleta maendeleo na zenye

kujenga katika jamii inayomzunguka.


“Kwa sasa habari nyingi ambazo zinazungumzwa ni habari ambazo ni za hovyo hovyo mno ndio

maana leo wamesema kuwa wilaya ya Iringa kuna kiwanda hicho kitu ambacho sio kweli” alisema Kasesela.


Katika hatua nyingine Mkuu wa Wilaya ya Iringa Richard Kasesela amelaani kitendo cha Dawson Kagine   kusambaza taarifa zisizo za kweli na kuongeza kuwa mkoani Iringa kuna kiwanda cha kuzalisha vifaa vya elimu ya mapambano

dhidi ya Ukimwi.

MBUNGE VULLU NA DAU WATOA MSAADA WA VIFAA MAFIA

NA MWAMVUA MWINYI,  Mafia

MBUNGE wa viti maalum Mkoa wa Pwani ,Zaynabu Vullu, ametoa kitanda na vifaa tiba katika zahanati ya Kijiji cha Malimbani ,wilayani Mafia.

Aidha mbunge wa Jimbo la Mafia Mbaraka Dau nae amekabidhi mashine ya kusambazia maji, kata ya Kiegeani ili kuwarahishia wakazi hao kupata huduma hiyo kupitia kisima kilichochimbwa eneo hilo.

Vullu alikabidhi vifaa hivyo ,wakati alipokuwa kwenye ziara ya siku mbili wilayani Mafia, kwa lengo la kutimiza ahadi yake ya kukabidhi vifaa hivyo vinavyolenga kuboresha upatikanaji wa huduma kwa wakazi hao, ambapo alipokelewa na mwenyeji wake Dau.

Alisema , anaunga mkono juhudi za serikali  kwa kununua kitanda, na vifaa tiba vitavyosaidia wagonjwa wataokwenda kupatiwa huduma kwenye zahanati hiyo
“Niwapongeze kwa umoja, upendo na mshikamano ambao mnaendelea kuuonyesha katika kujiletea maendeleo, nami leo nimekuja kuunga mkono juhudi za serikali kwa kuelekeza nguvu katika kuboresha sekta ya afya” alisema Zaynab.

Nae Dau alielezea kwamba ,amenunua mashine hiyo inayolenga kuboresha upatikanaji wa maji katika kisima kilichopo, ambacho kwa sasa ni cha mdundiko.

Alielezea, baada ya kufungwa mashine maji yatakuwa yanasambazwa umbali wa mita 1,000. Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mwajupi Abdallah Sharifu aliwashukuru wabunge hao kwa namna walivyojitoa katika sekta hizo.