Wednesday, January 9, 2019

MFUMUKO WA BEI KWA MWAKA 2018 WASHUKA, WAVUNJA REKODI MIAKA YA 40.

Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Bw. Ephraim Kwesigabo akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya Mfumuko wa Bei kwa mwezi Desemba 2018 leo jijini Dodoma.
..........................................

Na: Beatrice Lyimo-MAELEZO, Dodoma

Wastani wa Mfumuko wa Bei wa Taifa kutoka Januari hadi Desemba Mwaka 2018 umepungua hadi asilimia 3.5 kutoka wastani wa asilimia 5.3 kama ilivyokuwa mwaka 2017.

Hayo yamesemwa leo jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Bw. Ephraim Kwesigabo wakati akitoa taarifa kuhusu mfumuko wa bei wa mwezi Desemba 2018 pamoja na wastani wa mfumuko huo kwa mwaka mzima.


“Wastani huu wa mfumuko wa bei wa mwaka wa asilimia 3.5 ndiyo wastani mdogo kabisa kwa kipindi cha zaidi ya miaka 40 iliyopita ambapo tangu mwaka 1970 mfumuko huo ulikuwa 3.6,” ameongeza Kwesigabo.


Aidha, akizungumzia kuhusu mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwezi Desemba ,2018, Kwesigabo amesema kuwa mfumuko huo umeongezeka hadi kufikia asilimia 3.3 kutoka asilimia 3.0 kwa mwezi Novemba 2018.


“Kuongezeka kwa Mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwaka ulioishia mwezi Desemba, 2018 kumechangiwa hasa na kuongezeka kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula kwa kipindi kilichoishia mwezi Desemba, 2018 zikilinganishwa na bei za mwezi Desemba, 2017, mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwezi Desemba, 2018 umeongezeka hadi asilimia 1.0 kutoka asilimia 0.4 ilivyokuwa mwezi Novemba, 2018,” amefafanua Kwesigabo.


Aidha amesema kuwa, baadhi ya bidhaa ya chakula zilizochangia kuongezeka kwa mfumuko wa bei ni pamoja na nyama kwa asilimia 4.6, samaki wabichi asilimia 8.2, dagaa asilimia 26.2, matunda kwa asilimia 4.3 na mbogamboga asilimia 8.5 baadhi ya bidhaa zisizo za chakula zilizochangia mfumuko wa bei ni pamoja na vitambaa vya kushonea nguo kwa asilimia 2.1, nguo za kiume na za kike kwa asilimia 6.1, nguo za watoto kwa asilimia 3.0, sare za shule kwa asilimia 3.1, dizeli kwa asilimia 27.6, petroli asilimia 10.8 na huduma za malazi kwa asilimia 6.8.


Kwa upande wa nchi za Afrika Mashariki, mfumuko wa bei kwa mwaka unaoishia mwezi Desemba, 2018 nchini Kenya umeongezeka hadi kufika asilimia 5.71 kutoka asilimia 5.58 kwa mwaka ulioishia mwezi Novemba, 2018 na mfumuko wa bei kwa mwaka unaoishia mwezi Desemba, 2018 nchini Uganda umepungua hadi kufika asilimia 2.2 kutoka asilimia 3.0 kwa mwaka ulioishia mwezi Novemba, 2018.

RC NDIKILO AAGIZA WANANCHI WALIOVAMIA ENEO KATA YA PANGANI KUONDOKA MARA MOJA

NA MWAMVUA MWINYI, PWANI 

WAKALA wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoani Pwani ,unatarajia kutumia kiasi cha sh.bilioni 25.4 kwa ajili ya kufanya matengenezo mbalimbali ya barabara kwa bajeti ya mwaka 2018-2019.

Hayo yalisemwa mjini Kibaha na meneja wa TANROADS mkoani hapo, mhandisi Yudas Msangi,  wakati wa kikao cha bodi ya barabara cha mkoa huo .

Alieleza, hadi kufikia septemba 2018 zimepokelewa kiasi cha sh. milioni 958.7  kwa ajili ya matengenezo mbalimbali.

“Katika kipindi hicho kiasi cha shilingi bilioni 2 zimetumika kufanya matengenezo mbalimbali kwenye barabara kuu”, 

“Kazi za matengenezo zilichelewa kuanza kutokana na taratibu za manunuzi na uhakiki wa mikataba ambavyo huchukua muda mrefu kukamilika hasa mikataba inayohakikiwa kwa mwanasheria mkuu wa serikali”alisema Msangi. 

Aidha Msangi alibainisha, mkoa umepanga kufanya miradi ya maendeleo ya barabara zenye urefu wa kilometa 32.5 zenye thamani ya sh.bilioni 2.3.
Alisema,meneja huyo alisema kwenye miradi hiyo ya maendeleo sh. bilioni 1.3 ni bajeti ambapo sh.milioni 969 ni kutoka mfuko wa barabara vilevile bilioni 7.5 ni kutoka serikali zitafanya ukarabati kwa kiwango cha changarawe/udongo.

Nae mkuu wa  mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo alieleza, ili kuboresha barabara za mkoa huo watendaji wanapaswa kuwa waadilifu.

“Kutokana na mkoa kuwa na viwanda vingi uboreshaji wa miundombinu ya barabara utasaidia kuinua uchumi wa wananchi na Taifa”:” Pia Muwe makini na baadhi ya watu wanaoharibu miundombinu ya barabara ,” alisema Ndikilo.
 

WAGONJWA 45 KUFANYIWA UPASUAJI WA MOYO WA KUFUNGUA NA BILA KUFUNGUA KIFUA KATIKA KAMBI MAALUM YA MATIBABU YA MOYO INAYOFANYIKA KATIKA TAASISI YA MOYO JAKAYA KIKWETE KUANZIA TAREHE 7/01/2019 HADI 18/01/2019

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kupitia madaktari wake bingwa wa magonjwa ya moyo kwa kushirikiana na Madaktari Afrika na Shirika la Cardio Start wote kutoka nchini Marekani  wameanza  kambi maalum ya matibabu ya moyo  ya siku 12 kuanzia tarehe 07/01/2019 hadi 18/01/2019 kwa watu wazima .

Matibabu yanayofanyika  katika kambi hiyo ni upasuaji wa kufungua kifua na bila kufungua kifua. 

Upasuaji wa bila kufungua kifua unafanyika kupitia tundu dogo linalotobolewa kwenye paja kwa wagonjwa kuzibuliwa mishipa ya moyo iliyoziba (Percutaneous Coronary Intervention – PCI) na kuwekewa vifaa  vinavyosaidia kurekebisha mapigo ya moyo ambavyo ni (Permanent Pacemaker na High powered devices CRT-P, CRT –D) .

Wagonjwa watakaofanyiwa upasuaji ni wale wenye matatizo ya moyo ambayo ni  valve, mishipa ya moyo iliyoziba, moyo kushindwa kufanya kazi vizuri, matibabu kwa watu wazima waliozaliwa na matatizo ya moyo na wale wenye matatizo ya moyo yaliyotokana  na ugonjwa wa Kisukari.

Kambi hii inaenda  sambamba na utoaji wa elimu kwa madaktari na wauguzi pamoja na kubadilishana ujuzi wa kazi kwa wageni na wataalamu wetu. Katika kambi hii tunatarajia kufanya upasuaji wa kufungua kifua kwa wagonjwa  20 na bila kufungua kifua kwa wagonjwa 25. 

Hadi jana tarehe 8/1/2019 jumla ya wagonjwa nane wamefanyiwa upasuaji wa bila kufungua kifua na wagonjwa wanne wamefanyiwa upasuaji wa kufungua kifua.

Hii ni kambi ya kwanza ya matibabu ya moyo tangu kuanza kwa mwaka huu wa 2019 na ni mara ya kwanza kwa shirika Cardio Start  kuja  hapa nchini kufanya kazi na sisi.

UCHAGUZI WA YANGA KUFANYIKA BWALO LA MAAFISA WA POLISI OYSTERBAY JUMAPILI JANUARI 13,2019

Uchaguzi wa kugombea nafasi za Uongozi ndani ya Klabu ya Young Africans utafanyika kwenye Bwalo la Maafisa wa Polisi Oysterbay Jumapili Januari 13,2019.

Kadi zitakazotumika katika Uchaguzi ni kadi za Kitabu na kadi za Benki zilizohakikiwa.

Kampeni za kuelekea Uchaguzi huo zimefunguliwa rasmi leo.

Akitangaza kufunguliwa kwa kampeni hizo Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF Malangwe Mchungahela amewataka wagombea kufanya kampeni kwa amani bila kumchafua mwingine.

Mchungahela ameongeza kuwa kila mgombea anaruhusiwa kujinadi kokote ikiwemo katika tawi lolote la Young Africans.

Naye Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Young Africans ambaye pia ni Msaidizi wa Kaimu Mwenyekiti Siza Lyimo amewataka Wanachama kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi huo utakaokuwa wa amani na utulivu.

Amewataka Wanachama kupita mapema kwenye matawi yao kuhakiki kadi zao za Uwanachama ili kupunguza usumbufu siku ya Uchaguzi.