Thursday, January 3, 2019

DC BAGAMOYO ATAKA KASI YA KUKUSANYA MAPATO IONGEZEKE.

Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Zainabu Kawawa, akizungumza na katika kikao cha Kamati ya ushauri ya wilaya (DCC).
................................. 

Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Zainabu Kawawa, amewataka wahasibu wa Halmashauri za Chalinze na Bagamoyo, kuacha kukaa ofisini muda mrefu na badala yake wafike kwenye vyanzo vya mapato ili kujionea hali halisi ya mapato halisi katika maeneo husika.

Agizo hilo amelitoa wakati akizungumza kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) kilichofanyika Ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Bagamoyo.

Amesema kazi ya kukusanya fedha inahitaji ufuatiliaji hivyo ni wajibu wa wakuu wa idara kuhakikisha mnafuatilia walipa ushuru kwenye vyanzo ili kujiridhisha endapo malipo wanayolipa yanalingana na kile walichobeba au kuzalisha.

Amesisitiza swala kuongeza mapato ndani Halmashauri zote mbili kwakuwa fedha hizo zinaweza kutatua baadhi ya changamoto zilizopo ikiwemo upungufu wa vyumba vya madarasa.

Awali Afisa Mipango wa Halmashauri ya Chalinze, Shabani Milao, akisoma taarifa ya utendaji kazi shughuli za Halmashauri hiyo, alisema mapato yameendelea kukua mwezi hadi mwezi na kufikia milioni 600, kwa mwezi wa Oktoba na Novemba 2018 kutoka milioni 400 mwezi Julai 2018.

Milao alisema ongezeko hilo limetokana na juhudi za Mkuu wa wilaya kufuatilia kwa karibu vyanzo vya mapato na namna watumishi wa Halmashauri wanavyokusanya hali iliyoleta msukumo na kuongezeka kwa mapato.

Aidha, Milao alitaja changamoto zinazowakabili katika kufikia lengo ikiwa ni pamoja uelewa mdogo wa wafanya biashara juu ya ulipaji kodi ya huduma za mji pamoja na uhaba wa vyombo vya usafiri.

Hata hivyo, Afisa mipango huyo amesema Halmashauri imejiwekea mikakati ya kuhakikisha inaendelea kuwahamasisha wananchi juu ya umuihmu wa kulipa kodi ya huduma na kuwachukulia hatua wale wote wenye madeni sugu.

Katika hali hiyo, Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, ameonyesha kutoridhishwa na mapato hayo na kutaka kasi iongezwe katika ukusanyaji ili kufikia milioni mia tisa kutoka mia sita za sasa.

Alisema tayari ameshafanya uchunguzi na kubaini fedha nyingi zinazopotelea kwenye mifuko ya watu na kwamba hatokubali mapato ya Halmashauri yapotee.

Aliwaagiza wakurugenzi wa Halmashauri zote mbili za Chalinze na Bagamoyo kuhakikisha wanasimamia ukusnyaji wa mapato na kwamba ikitokea mkuu wa idara husika anazembea katika kufuatilia na kukusnaya mapato atahakikisha anamuwajibisha.
 
 Wajumbe wa kikao cha Kamati ya Ushauri ya wilaya ya Bagamoyo wakiendelea na kikao. 


 Afisa Mipango Halmashauri ya Chalinze, Shabani Milao akisoma Taarifa ya utendaji kazi wa Halmashauri hiyo kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC).
 
Afisa Mipango Halmashauri ya Bagamoyo, Malboard M. Kapinga akisoma Taarifa ya utendaji kazi wa Halmashauri hiyo kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC).

JAFO APONGEZA UJENZI OFISI ZA HALMASHAURI KIBITI.

Muonekano wa Jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti linaloendelea kujengwa.
...................................

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Selemani Jafo amewapongeza viongozi wa Wilaya ya Kibiti kwa Ujenzi mzuri wa Ofisi za Halmashauri ya Wilaya Kibiti mradi unao tarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi bilioni tatu. 

Waziri Jafo alitoa pongezi hizo Leo hii alipokuwa katika ziara ya kikazi Wilayani Kibiti Mkoani Pwani.  

Ujenzi huo unaojengwa na mkandarasi SUMAJKT chini ya Mshauri Chuo Kikuu cha Ardhi umemridhisha sana Waziri Jafo kutokana na kuzingatiwa kwa viwango vya ubora katika ujenzi huo. 

Hata hivyo Jafo ameagiza kuongezwa kwa kasi ya ujenzi ili mradi huo ukamilike kabla ya mwezi Julai, 2019.

Katika ziara hiyo ya kikazi wilayani Kibiti Waziri Jafo alifanikiwa kutembelea mradi huo pamoja na mradi wa ujenzi wa kituo cha Afya Kivinja “A” ambao unagharimu shilingi milioni 400.

Katika kuhitimisha ziara yake wilayani humo waziri Jafo ameutaka uongozi wa wilaya hiyo kutumia fursa waliyonayo ya tofali nzuri zenye ubora zinazo zalishwa na SUMAJKT katika ujenzi wa hospitali ya wilaya ambayo wameshapokea shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo. 

Aidha, Mbunge wa Jimbo la Kibiti Mhe. Seif Ungando ameishukuru sana Serikali ya DKT. John Pombe Joseph Magufuli kwa msaada mkubwa wa miradi ya maendeleo inayo elekezwa wilayani Kibiti.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa Na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo(katikati) akitoa maelekezo wakati akikagua ujenzi wa Ofisi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo aKiwa na viongozi wa Wilaya ya Kibiti wakati wa ziara yake Wilayani humo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa Na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo(katikati) akitoa maelekezo wakati akikagua ujenzi wa Ofisi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti.

MAKOSA YA UBAKAJI NA KUPATIKANA NA SILAHA YALIONGEZEKA MKOANI PWANI 2018.

NA MWAMVUA MWINYI, PWANI 

MAKOSA ya ubakaji yametajwa kuongezeka kutoka 206 kwa mwaka 2017 na kufikia 271 mwaka 2018, mkoani Pwani .

Aidha kupatikana na silaha mwaka 2017 yalikuwa makosa tisa ambapo mwaka uliopita 2018, yameongezeka na kufikia 26 .

Akielezea tathmini ya hali ya uhalifu katika kipindi cha mwaka 2018 ikilinganisha na mwaka 2017, kamanda wa polisi mkoani Pwani Kamishna Msaidizi wa Polisi, (ACP)  Wankyo Nyigesa alisema tathmini ya kijumla inaonyesha wamepunguza matukio 151 makubwa .

Alisema, makosa ya ubakaji yameonekana kupanda kutokana na uelewa kwa jamii na mwamko wa kuripoti matukio hayo polisi. 

Wankyo alieleza, matukio ya mauaji yalikuwa 61 ikilinganisha na matukio 70 yaliyoripotiwa mwaka 2017 .

“Makosa ya kufanya biashara ya kusafirisha binadamu mwaka 2018, yalikuwa 03 ikilinganishwa na makosa 05 yaliyorekodiwa mwaka 2017″alifafanua Wankyo. 
Kamanda huyo alisema kuwa, makosa ya unyang ‘anyi wa kutumia silaha mwaka 2017 yalikuwa 21 na mwaka 2018 makosa hayo ni 13.

Unyang’anyi wa kutumia nguvu mwaka 2017 yaliriporiwa makosa 126 ,wakati mwaka 2018 makosa ya namna hiyo yameripotiwa makosa 52 .

Alisema, jeshi hilo pia limefanikiwa kudhibiti uingizaji bidhaa kupitia bandari bubu wilayani Bagamoyo kwa kukamata makosa 27,watuhumiwa 31 pamoja na madumu 5,435 ya mafuta ya kula aina mbalimbali .
“Sukari kutoka nchi za nje mifuko 78, mabello 20 ya nguo za mitumba aina mbalimbali ikiwemo manne ya khanga na vyombo vya moto vilikamatwa ikiwa ni pamoja na pikipiki sita na magari matatu. “alieleza Wankyo.  

RPC MOROGORO AIPONGEZA TIF.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, (SACP) Wilbroad Mutafungwa, (kushoto) akisalimiana na Mwenyekiti wa The Islamic Foundation (TIF).
..................................... 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, (SACP) Wilbroad Mutafungwa,  ameipongeza Taasisi ya The Islamic Foundation yenye makao yake makuu Mkoani humo kwa kazi inayofanya katika kuihudumia jamii.

Kamanda Mutafungwa amesema Taasisi hiyo imekuwa mfano wa kuigwa katika shughuli zake ambazo zinafanywa na kusimamiwa kwa weledi huku huduma zake zikiwa hazibagui dini, rangi wala kabila.

Akizungumzia vyombo vya habari vinavyomilikiwa na Taasisi hiyo  Kamanda Mutafungwa amesema vyombo hivyo vimekuwa msaada mkubwa kwa jeshi la polisi mkoani humo kutokana na vipindi vyake vya kuelimisha jamii kuhusu amani, na usalama barabarani hali iliyopelekea kupungua kwa kiasi kikubwa kwa ajali za barabarani.

Aliongeza kwa kusema kuwa, vyombo vya habari vinaweza kuwa chanzo cha uvunjifu wa amani mahali popote pale na kwamba vikitumika vizuri vinakuwa msaada mkubwa kwa serikali katika kulinda amani ya sehemu husika.

Alisema jeshi la polisi linahitaji ushirikiano katika kutekeleza majukumu yake hivyo kinachofanywa na Taasisi ya The Islamic Foundation ni kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo ili kurahisisha utendaji kazi wa polisi.

Alifafanua kuwa, jeshi la polisi kazi yake ni kulinda usalama wa raia na mali zao huku wajibu wa raia ni kutii sheria bila ya shuruti na kwamba anaevunja sheria anachukuliwa hatua kwa mujibu wa kosa alilotenda.

Alisema katika hali hiyo, raia wakielewa kazi ya polisi, na wajibu wao wa kutii sheria kama raia, hakutakuwa na uhasama miongoni mwao na kwamba uendeshaji wa shughuli mbalimbali za kijamii utafanywa kwa ushirikiano.

Akizungumzia ajali za barabarani, Kamanda Mutafungwa amesema kwa sasa ajali zimepungua kwa kiasi kikubwa na kwamba utii wa sheria hasa kwa madereva wa bodaboda upo kwa kiwango kikubwa mkoani humo.

Alimalizia kwa kuwataka wananchi wote mkoani humo kutoa ushirikiano kwa jeshi la Polisi ili kukomesha vitendo vyote vya uvunjifu wa sheria, ikiwemo zile za barabarani na uhalifu wa aina zote.

Nae Mwenyekiti wa Taasisi ya The Islamic Foundation, Aref  Nahd amelipongeza Jeshi la polisi mkoani humo kwa kutoa ushirikiano wao na Taasisi hiyo hali inayaopelekea kuendesha vipindi vya usalama barabarani kupitia Tvimmaa na Redio imaan ambapo elimu hiyo imewasaidia sio tu wakazi wa mkoa wa Morogoro, bali kila sehemu vinaposikika vyombo vya habari vya imaan.

Alisema Taasisi hiyo pamoja na kujishughulisha na huduma za kiroho lakini pia inatekeleza miradi mbalimbali ya kijamii kwa lengo la kuisaidia serikali katika kuleta maendeleo.

Aidha, Mwenyekiti Aref Nahdi,  alimueleza Kamanda Mutafungwa kuwa, Taasisi hiyo imekuwa ikitoa elimu mbalimbali kuhusiana na kulinda amani na kwamba katika hilo inashirikiana na wahadhiri mbalimbali wa ndani na nje ya nchi kwa lengo la kudumisha amani.

Aliongeza kuwa, wamefanikiwa kuandaa makongamano ya kuelimisha jamii umuhimu wa amani ndani ya mkoa wa Morogoro na nje ya mkoa huo na kwamba muitkio unakuwa mkubwa hali inayoashiria kuwa elimu iliyokusudiwa inafika ipasavyo.

Kamanda wa  Polisi Mkoa wa Morogoro, alitembelea ofisi za The Islamic Foundation (TIF) zilizopo msamvu mjini Morogoro kwa kutambuana na viongozi wa Taasisi hiyo ambapo aliweza kukutana na Mwenyekiti wa The Islamic Foundation, Aref Nahd, Mkurugenzi Mtendaji wa Taassi hiyo, Sheikh Ibrahim Twaha, na Katibu Mkuu Haroun Rajab.

Akiwa katika ofisi za The Islamic Foundatio, Kamanda Mutafungwa alijionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na taasisi hiyo huku kumbukumbu zikiwa makao makuu ya ofisi.

Miongoni mwa shughuli alizoweza kuona kumbukumbu zake ni pamoja na ujenzi wa Misikiti, uchimbaji wa visima, utoaji wa misaada mbalimbali, vituo vya kulelea watoto yatima na uendeshaji wa shule za msingi na sekondari.

Kamanda Mutafungwa ameipongeza The Islamic Foundation kwa miradi mbalimbali ya maendeleo na kuahidi kushirikiana nao katika kipindi chake chote atakachokuwepo Mkoani Morogoro.

  Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, (SACP) Wilbroad Mutafungwa, akimsikiliza Mwenyekiti wa Taasisi ya The Islamic Foudation (TIF), Aref Nahdi, alipotembelea Makao ya Taasisi hiyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, (SACP) Wilbroad Mutafungwa, akiwa anazungumza na Tvimaan nje ya ofisi mara baada ya kumaliza kuzungumza na viongozi wa Taasisi ya The Islamic Foundation (TIF) Makao makuu ya Taasisi hiyo iliyopo Msamvu Mkoani Morogoro.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya The Islamic Foundation (TIF) Sheikh Ibrahim Twaha, (Kulia) Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, (SACP) Wilbroad Mutafungwa (katikati) Mwenyekiti wa The Islamic Foundation, Aref Nahdi, (kushoto) wakiangalia kitabu cha utekelezaji wa miradi ya TIF.

 Mwenyekiti wa The Islamic Foundation, Aref Nahdi, (kulia) akimkabidhi zawadi ya ngao, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, (SACP) Wilbroad Mutafungwa (katikati) anaeshuhudia kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya The Islamic Foundation (TIF) Sheikh Ibrahim Twaha.
Katibu Mkuu wa The Islamic Foundation, Haroun Rajab (kulia) Mwenyekiti, Aref Nahd, (katikati) wakifurahia jambo na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, (SACP) Wilbroad Mutafungwa.

WAZIRI LUGOLA APIGA MARUFUKU POLISI KUWAKAMATA WAENDESHA BODABODA WAKIWA HAWAJAVAA SARE

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (kushoto) akitoka Kituo Kikuu cha Polisi cha mjini Bukoba mara baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika Kituo hicho, leo, kwa kufuatilia utendaji kazi wao. Katikati ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Revocatus Malimi, na kulia ni Mkuu wa Jeshi la Magereza Mkoani humo, ACP Raymond Mwampashe. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola akizungumza na mamia ya wananchi mjini Bukoba Mkoani Kagera, katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Uhuru, Mayunga mjini humo, leo. Lugola licha ya kuwa amewataka waendesha bodaboda wafuate sheria za usalama barabarani, lakini ametoa onyo kwa Polisi mjini humo kuacha  kuwakamata waendesha bodaboda wakiwa hawajavaa sare.
............................................

Na Felix Mwagara, MOHA-Bukoba.

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amepiga marufuku tabia ya baadhi ya Askari Polisi nchini kukamata pikipiki wakiwa hawana sare za Jeshi.

Akizungumza na mamia ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa uhuru, Mayunga, mjini Bukoba Mkoani Kagera, leo, Lugola alisema polisi wanapaswa kufuata utaratibu wa kijeshi hasa wanapokamata vyombo vya moto na siyo kuvunja utaratibu.

Lugola aliongeza kuwa, bodaboda zinazovunja sheria za usalama barabarani zinapaswa kukamatwa bila kuwaonea huruma, ila ni kosa Polisi kuwanyanyasa vijana hao ambao wanapata ridhiki kupitia biasahara hiyo.

“Mnapaswa kukamata hizi bodaboda zinapofanya makosa, tabia ya kukurupuka huku mkitafuta fedha zisizo halali, huko ni kuwaonea waendesha bodaboda,” alisema Lugola.

Pia Lugola aliwataka waendesha bodaboda mjini Bukoba na Tanzania kwa ujumla wafuate sharia za usalama barabarani zikiwemo kuvaa kofia ngumu, kutokubeba abiria zaidi ya mmoja na pia wakiendesha wanapaswa kuwasha taa.

Lugola ameanza ziara yake ya siku nane mkoani humo akitembelea Wilaya zote za Mkoa huo akisikiliza kero za wananchi pamoja na kufuatilia maagizo yake aliyoyatoa kwa vyombo vya ulinzi na usalama vilivyopo ndani ya Wizara yake.

Lugola mwaka jana alitoa maagizo kwa makamanda wa mikoa nchini ambayo ni dhamana zitolewe saa 24 katika vituo vyote vya polisi nchini, na pia kupiga marufuku tabia ya baadhi ya Polisi kubambikizia kesi wananchi, na pamoja na agizo la pikipiki zote zilizopo vituoni ziondolewe.

Waziri Lugola tayari amemaliza ziara yake kwa Wilaya ya Bukoba na Kesho ataanza ziara Wilaya za Misenyi, baadaye Karagwe, Kyerwa, Ngara, Biharamulo na Januari 8, 2019 atamalizia ziara yake Wilaya ya Muleba ambapo katika Wilaya hizo pia atazungumza na wananchi pamoja na watumishi waliopo ndani ya Wizara yake ambao ni Jeshi la Polisi, Idara ya Uhamiaji, Jeshi la Magereza, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, pamoja na Idara ya Probesheni ambayo jukumu lake kuu ni kupunguza msongamano gerezani na kusimamia wafungwa waliopewa adhabu mbadala na Mahakama au wafungwa waliopata msamaha kupitia sheria ya huduma kwa jamii na kutumikia kifungo chao nje ya Gereza.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (kushoto) akimsikiliza Mkazi wa mjini Bukoba alipokuwa anaeleza kero yake mara baada ya Waziri huyo kuwaita wananchi hao mbele waweze kutoa kero zao, mara baada ya kumaliza kuzungumza na wananchi hao katika mkutano wa hadhara  uliofanyika Uwanja wa Uhuru, Mayunga mjini humo, leo. Lugola licha ya kuwa amewataka waendesha bodaboda wafuate sheria za usalama barabarani, lakini ametoa onyo kwa Polisi mjini humo kuacha kuwakamata waendesha bodaboda wakiwa hawajavaa sare.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (kushoto) akimsalimia Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt Bashiru Ally, wakati alipoonana naye Uwanja wa Ndege wa Bukoba, leo. Lugola yupo Mkoani Kagera kwa ziara ya kikazi akitembelea Wilaya zote, akisikiliza kero mbalimbali za watumishi wa Wizara yake pamoja na wananchi mkoani humo.

Wednesday, January 2, 2019

TAARIFA KUTOKA JESHI LA POLISI MKOANI MWANZA LEO

Jeshi la Poliisi Mkoa wa Mwanza kwa kutumia kikosi chake kabambe chenye uweledi uliotukuka tumefanikiwa kuwakamata watu watatu kwa kosa la kupatikana na dawa za kulevya aina ya bhangi kiasi cha kilogramu 110, huko mtaa wa Ngumo “A”, Wilayani Kwimba.

Tukio hilo limetokea tarehe 01.01.2019 majira ya saa 21:00hrs, hii ni baada ya kikosi hicho mahiri cha askari wakati kikiwa doria na misako kilipokea taarifa toka kwa wasiri kwamba katika mtaa wa Ngumo ”A” na Safari club wapo watu wanaojihusisha na utumiaji na uuzaji wa dawa za kulevya. 

Ndipo askari walifanya ufuatiliaji na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao watatu wakiwa na kiasi hicho cha dawa za kulevya aina ya bhangi.

Watuhumiwa waliokamatwa na dawa hizo za kulevya aina ya bhangi ni;

Consolatha Elias, miaka 52, mkazi Ngumo “A”, huyu amekamatwa na dawa za kulevya aina ya bhangi kiasi cha kilogramu 100.

Emmanuel Lucas, miaka 21, mkazi wa kijiji cha Manguluma, na
Rehema Joseph, miaka 27, mkazi wa Chato, hawa wawili wamekamatwa na dawa za kulevya aina ya bhangi kiasi cha kilogramu 10.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza tunaendelea na mahojiano na watuhumiwa wote watatu ili kuweza kubaini watu wanaoshirikiana nao katika uuzaji, utumiaji na usafirishaji wa dawa hizo za kulevya aina ya bhangi. Aidha pindi uchunguzi ukikamilika watuhumiwa wote watatu watafikishwa mahakamani ili hatua stahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, tunatoa onyo kwa baadhi ya wananchi waojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya kuwa waache kwani ni kinyume na sheria na endapo mtu atabainika hatua stahiki za kisheria zitachukuliwa dhidi yake. 

Vilevile tunawaomba wananchi waendelee kutupa ushirikiano kwa kutupa mapema taarifa za uhalifu na wahalifu ili waweze kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Imetolewa na;

Jonathan Shanna – ACP
Kamanda wa Polisi (M) Mwanza.
02 January, 2019.

MAGAZETI YA LEO JANUARI 02, 2019.

Tuesday, January 1, 2019

MWENYEKITI WA CCM BAGAMOYO ATOA SALAM ZA MWAKA MPYA.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Bagamoyo, Abduli Sharifu, ametoa salamu za mwaka mpya 2019 huku akisema kuwa anathamini michango ya watu wa vyama vyote.

Katika salamu zake hizo, Sharifu amewataka wa CCM na wanachama wa vyama vingine kuishi kwa umoja na kushirikiana katika mambo mbalimbali ya maendeleo.

Alisema maendeleo hayana chama hivyo kila mtanzania bila ya kujali chama chake anapaswa kushiri shughuli za maendeleo katika eneo lake.

Alisema katika uongozi wake ndani ya CCM wilaya ya Bagamoyo, atahakikisha wana siasa wote wanaishi kwa amani na utulivu na kuthamini mawazo ya watu wote.

Aliongeza kuwa, kukosolewa ni miongoni mwa chaangamoto kuona wapi panahitaji marekebisho ili kuboresha zaidi.

Katika hatua nyingine Mwenyekiti huyo wa CCM wilaya ya Bagamoyo alisema katika kipindi hiki ambacho anatimiza mwaka mmoja katika uongozi wake ameweza kusimamia vyema utekelezaji wa ilani ya uchaguzi pamoja na kusimamia katiba ya CCM.

Alisema miongoni mwa mambo ambayo ameyafanya katika kipindi cha mwaka mmoja ni pamoja na kujenga mahusiano mema kati ya chama na serikali na kuamsha ari kwa wanachama wa CCM.


DC BAGAMOYO AKABIDHI VITAMBULISHO KWA WAJASILIAMALI.

 Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Zainabu Kawawa, akimkabidhi kitambulisho mmoja wa wafanyabiashara ndogo ndogo, zoezi ambalo lilifanyika katika ofisi ya Mkuu wa wilaya.
 
Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Zainabu Kawawa, akizungumza na wafanyabiashara ndogo ndogo.
................................................ 

Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Zainabu Kawawa, amezindua rasmi zoezi la ugawaji wa vitambulisho kwa wafanya biasahara ndogo ndogo kama alivyoelekeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkuu huyo wa wilaya aliwataka wafanyabiashara hao kuzingatia vigezo villivyowekwa kwa mfanyabiashara anaestahiki kupata kitambulisho hicho.

Alisisitiza kuwa, mfanyabiashara atakaekiuka masharti yaliyowekwa na kusema uongo atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Aidha, amewaagiza maafisa biashara na wale wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kutoa elimu kwa wafanyabiashara ili wale wanokidhi vigezo waweze kupatiwa vitambulishi hivyo.

Katika hatua hiyo ya uzinduzi, Mkuu huyo wa wilaya amewakabidhi wafanyabiashara ndogo ndogo 10 wa awali ambapo baada ya hapo zoezi litaendelea kwa kushirikiana kati ya Maafisa wa biashara na wale wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) pamoja na watendaji wa kata kwaajili ya kuwatambua wafanyabiashara ndogo ndogo wenye sifa ya kupata vitambulisho hivyo.

Tayari zoezi la awali limeshafanyika la kuwatambua wafanyabiashara ndogo ndogo ambapo mitaji yao haizidi milioni 4.

Katika hatua ya awali kwa Halmashauri ya Bagamoyo jumla ya wafanyabiashara ndogo ndogo 4,400 wamekidhi vigezo na kustahiki kupewa vitambulisho hivyo.

Kwa upande wao wafanyabiashara ndogo ndogo, wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli kwa hatua hiyo ambayo itawaondolea kero wafanyabiashara wadogo wadogo.

Walisema awali walikuwa wakisumbuliwa na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) hata kama biashara ikiwa ndogo unatakiwa kukadiriwa kodi hali iliyopelekea watu wengi kushindwa kuendesha biashara zao.

Waliongeza kwa kusema kuwa, utaratibu huu wa sasa ni mzuri kwa upande wao kwani kila mmoja ataweza kuiingizia serikali mapato kulingana na uwezo wake.

Hivi karibuni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa vitambulisho kwa wafanyabiashara ndogo ndogo nchini wenye mitaji isiozidi shilingi milioni nne 4,000,000/= ili waepukane na usumbufu wanaoupata kutoka TRA na mgambo wa jiji.

Jumla ya vitambulisho laki sita na sabini elfu 670,000 vilitolewa na kugawanywa kwa wakuu wa mikoa nchi nzima ambapo kila mkuu wa mkoa alipewa vitambulisho 25,000 avigawanye kwenye wilaya zake.
Baadhi ya wafanyabiashara ndogo ndogo waliokabidhiwa vitambulisho vyao na Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo.
Sehemu ya wafanyabiashara ndogo ndogo waliofika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo kupata vitambulisho vyao.