Friday, December 28, 2018

KIKOKOTOO KIPYA CHAMNG'OA MKURUGENZI SSRA

PROF. KABUDI ATEMBELEA SITE YA UJENZI WA OFISI ZA WIZARA DODOMA

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi ametembelea eneo linapojengwa jengo la Wizara yake na kuagiza timu maalum kupiga kambi eneo hilo ili kuhakikisha ujenzi unafanyika usiku na mchana huku wakizingatia viwango vya ubora katika ujenzi wa jengo hilo.

“Nataka ujenzi uharakishwe kama ambavyo Waziri Mkuu alivyogiza lakini viwango vya ubora katika ujenzi vizingatiwe” alisema Prof. Kabudi.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Prof. Sifuni Mchome amemtaka mkandarasi anayejenga jengo la Wizara hiyo kuhakikisha anakusanya mahitaji yote yanayotakiwa eneo la ujenzi ili kufanikisha kasi ya ujenzi inaenda kama inavyotakiwa.

Ujenzi wa Jengo la Wizara ya Katiba na Sheria unatarajiwa kukamilika mapema ifikapo tarehe 15 Januari 2019.
 

WATUMISHI 13 ULANAG HATIANI KWA UBADHILIFU WA BIL. 2.9

Nteghenjwa Hosseah, OR-TAMISEMI.

OFISI ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za mitaa (Tamisemi) imebaini matumizi mabaya ya fedha za serikali Sh. bilioni 2.98 katika halmashauri ya Ulanga mkoani Morogoro na kuagiza wakuu wa idara wote waliohusika wavuliwe nyadhifa zao huku watumishi wengine waondolewe majukumu ili vyombo vya dola viendelee na hatua kwa mujibu wa sheria dhidi yao.


Hayo yamebainishwa na Waziri wa nchi ofisi ya Rais Twala za mikoa na Serikali za mitaa Mhe. Selemani Jafo wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya uchunguzi maalum uliofanywa kwa halmashauri ya wilaya hiyo.


Jafo alisema kuwa Ofisi ya Rais Tamisemi imefanya uchunguzi maalum katika halmashari 12 nchini ambazo ni Ulanga, Same, Mbulu, Meru, Itigi, Misungwi, Nyang’hwale, Serengeti, Bahi, mpwapwa, Morogoro Dc na Kibaha Tc ambapo katika halamasahuri ya Ulanga uchuguzi ulianza Novemba 13 hadi 23 mwaka huu.


Alisema uchunguzi huo ulifanyika kufuatia malalamiko ya wanachi mbalimbali pamoja na mbunge wa jimbo la Ulanga Mhe. Goodluck Mlinga kutokana na ubadhirifu uliokuwepo.


Aidha alisema kiasi hicho kimebainika kupotea kutokana na matumizi mabaya ya fedha za serikali ambapo watumishi wasio waadilifu katika halmashauri hiyo walikiuka taratibu na kufanya manunuzi hewa na kutumia vibaya fedha kinyume na malengo yaliyopangwa.


“Halmashauri hii imekuwa ikifanya udanganyifu katika taarifa za miradi ya maendeleo taarifa za mfuko wa wanawake na vijana, kwa ujumla inausimamizi mbovu wa mapato na kuwa na udhibiti hafifu wa makusanyo na matumizi ya fedha za Umma”alisema Jafo.


Jafo alisema kuwa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Ulanga, Yusufu Daud Semguruka kwa nafasi yake ya afisa masuhuli alishindwa kusiomamia sheria ya fedha za serikali za mitaa katika kudhibiti na kuweka mifumo dhabiti ya kuhakikisha fedha ziko salama kuanzia makusanyo hadi matumizi yake.


“Hii ni pamoja na kushindwa kumsimamia mweka hazina wa halmashauri katika kutekeleza majukumu yake na kwa kushindwa kutekeleza majuku hayo amesababisha hasara halmashauri ya shilingi 2,980,172,763.60″alisema Jafo.


Alifafanua kuwa Rajabu Siriwa,ambaye alikuwa ni mweka hazina wa halmasahuri hiyo alichangia kuhujumu mapato ya serikali kwa kuweka utaratibu ambao umeisababishia hasara serikali.


Alisema kuwa mweka hazina huyo aliidhinisha malipo ya sh. 225,586,400 nje ya bajeti bila idhini ya ofisi ya Rais Tamisemi ambapo malipo hayo yalihusisha posho ya safari ya mkurugenzi mtendaji Sh. 192,000,000.


“Pia kukusanya mapato na kutoyapeleka benki, katika mfumo wa LGRCIS umeonyesha halmashauri ilikusanya fedha ambazo hazikupelekwa benki kabisa shilingi 760,686,732.43 fedha hizi hazijulikani matumizi yake halisi ni nini”alihoji Jafo.


Aidha alisema kuwa mweka hazina huyo aliandaa taarifa zenye udanganyifu kwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotumia fedha za makusanyo ya ndani.


“Halmashauri imeripoti kupeleka shilingi 301,442,686 uhalisia wamepeleka 113,406,106.34 na udanganyifu katika mfuko wa vijana na akina mama halmashauri inaripoti kupeleka shilingi 120,000,000 uhalisia wamepeleka sh. 31,500,000 kwa mwaka 2017/18 na 2018/19 hadi novemba 2018 wakati uchunguzi unakamilika”alisema.


Aidha Jafo alisema kuwa Mhandisi David Kaijage akiwa anakaimu ofisi ya mkurugenzi februari mosi mwaka huu hadi Februari nane alihusika kwenye kuihujumu halmashauri kwa mapato ya Sh. 470,000,000 yaliyopolelewa kutoka kiwanda cha kilombero Valley Teak Company kwa kuzirejesha kwa mlipaji siku hiyohiyo waliyopokea.


“Pia alisaini hati ya malipo kumlipa bahari Phamarcy kwa siku ambayo hakuwa kaimu mkurugenzi na mkurugenzi alikuwepo”alisema.

Wakati huo huo Bw. Stanley Godwil Nyange na Bw. Isaack Mwasankope Salumu ambao wote ni wahasibu wameihujumu Halmashauri kwa kutumia akaunti zao binafsi kupokea fedha za makusanyo ya Halmashauri kiasi cha sh 203.398,700 aliongeza.

 
Waziri Jafo pia alisema kuwa uchunguzi huo pia umebainisha kuwa Isaack Mwasankope, Salehe Mbogoso pamoja na Johson Mwanyombole ambao wote ni wahasibu wa halmashauri hiyo walihusika kuchukua fedha taslim za makusanyo katika kituo cha kivukoni na kisha kuzitumia bila kuzipeleka Benki sh 168,000,000.

 
Yassin Galahenga na Mohamed Majaliwa Saidi wataalam wa mifumo (TEHAMA) walishirikiana na wahasibu kurekebisha Ankara na kufuta madeni bila idhini ya Mkurugenzi alibainisha Waziri Jafo.

 
Waziri Jafo aliongeza kuwa Bw. Willy Ndabila ambaye alikua afisa manunuzi alihusika na manunuzi hewa ya madawa yenye thamani y ash.


  73,212,909.40 pamoja na kulipa fedha zaidi yaani sh 146,425,818 huku Goodluck Mbata ambaye ni muhasibu wa hospital aliandaa malipo na kusainisha mara mbili kwa watu tofauti huku akijua kufanya hivyo ni kuandaa malipo mara mbili kwa hitaji moja (double paymet).


Waziri Jafo aliagiza ofisi ya mkuu wa mkoa wa Morogoro kuhakikisha kuwa wakuu wa idara na vitengo waliohusika akiwemo Willy Ndabila ambaye amehamishiwa itilima,na Rajabu Siriwa ambaye amehamishiwa Gairo wavuliwe nyadhifa zao na mamlaka za nidhamu na vyombo vya dola viendelee na hatua kwa mujibu wa sheria.


Aliongeza kuwa watumishi wote waliohamishiwa Halmashauri ya ulanga wakiwa na makosa yaani DPMU Willy Ndabila na DT Rajabu Siriwa warejee halamashauri ya Ulanga ili kuiwezesha halmashauri na vyombo vya Dola kufanya kazi yake.

“Maelezo juu ya mkurugenzi huyu wa Ulanga yenyewe yatatolewa baadaye na serikali”alifafanua Jafo.


Hatahivyo Jafo alisema kuwa mkuu wa mkoa wa Morogoro ahakikishe kuwa Ofisi ya Rais Tamisemi imepata maelezo kwanini wataalamu hao hawakuchukuliwa hatua stahiki zenye tija dhidi ya taarifa za mkaguzi wa ndani ya robo ya tatu ya mwaka wa fedha2017/18 kabla ya januari 15 mwakani.


MAGAZETI YA LEO DESEMBA 28, 2018.

Thursday, December 27, 2018

JENERALI MABEYO ATOA WITO KWA VIONGOZI WA DINI KUHUBIRI AMANI JENERALI MABEYO ATOA WITO KWA VIONGOZI WA DINI KUHUBIRI AMANI

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini Jeneral Venance Mabeyo akipokea mkono wa Heri ya Krismasi kutoka kwa Askofu wa Jimbo Katoliki Shinyanga, Muhashamu Liberatus Sangu, katika ibada ya kubariki na kutabaruku Kanisa la Mtakatifu Petro Kigango cha Kiloleli Parokia ya Ilumya wilayani Busega mkoani Simiyu, iliyofanyika Desemba 26, 2018.

Askofu wa Jimbo Katoliki Shinyanga, Muhashamu Liberatus Sangu akimshuhudia Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini Jenerali Venance Mabeyo wakati akitia saini kama shahidi katika Hati ya kubariki na kutabaruku Kanisa la Mtakatifu Mtakatifu Petro Kigango cha Kiloleli Parokia ya Ilumya, katika ibada ya kubariki na kutabaruku  kanisa hilo, iliyofanyika Desemba 26, 2018.
.................................................


Na Stella Kalinga, Simiyu

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi hapa nchini Jenerali Venance Mabeyo ametoa wito kwa Viongozi wa Dini nchini kuendelea kuhubiri amani ili kujenga jamii iliyo bora yenye kudumisha upendo na mshikamano.


Jenerali Mabeyo ametoa wito huo wakati wa ibada ya kubariki na kutabaruku Kanisa la Mtakatifu Petro, Kigango cha Kiloleli Parokia ya Ilumya wilayani Busega ambayo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Kitaifa akiwepo Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro, Naibu Gavana wa Benki Kuu, Dkt. Benard Kibese na viongozi wengine wa Chama na Serikali, ambapo alisisitiza kuwa amani ni msingi wa maendeleo kwa Taifa lolote duniani.


“Suala la amani na utulivu ni la msingi sana katika nchi yetu, kwa vile kila mwananchi ana dini yake tunaamini kuwa viongozi wa dini zote kwa kuwa wanasikilizwa sana  na waumini  wakiweka msisitizo katika suala la amani, amani itatawala na kutakuwa na utulivu”


“Utulivu huu tunauhitaji sana ili tupate maendeleo,  kama  viongozi wetu wa kisiasa wanavyosisitiza kuwa tudumishe amani na utulivu  tupate maendeleo, bila utulivu watu wakiwa wanahaingaika hakuna maendeleo kwa sababu hakuna shughuli mtu anaweza kufanya kama hana amani na utulivu, hivyo hataweza pia kuleta maendeleo yake, familia, jamii na Taifa kwa ujumla” alisema Jenerali Mabeyo.


Kwa upande wake Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Inspekta Jenerali Simon Sirro amesema vitendo vingi vya uvunjifu wa amani na uhalifu ikiwemo ukataji wa mapanga na mauaji ya vikongwe na yanachangiwa na watu kukosa hofu ya Mungu; hivyo nyumba za ibada(makanisa na misikiti) zinapojengwa kwa wingi zitakuwa msaada mkubwa sana kwa watu kuwa na hofu ya Mungu.


Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema jamii inayoamini uwepo wa Mungu haiwezi kuwa na vitendo vya kisasi, kukatana mapanga na mauaji ya vikongwe huku akiwaasa Watanzania kukaa kwa amani na upendo bila kufanya mambo yanayoweza kuhatarisha amani.


Akibariki na kutabaruku Kanisa la Mtakatifu Petro, Kigango cha Kiloleli Parokia ya Ilumya wilayani Busega, Askofu wa Jimbo Katoliki Shinyanga, Muhashamu Liberatus Sangu amewataka Watanzania kupendana na kuacha roho ya ubinafsi na visasi.


Aidha, Askofu Sangu ametoa wito kwa viongozi na waumini kufanya nyumba za ibada zibaki nyumba za sala kama yanenavyo maandiko matakatifu na kamwe zisitumike kama majukwaa la wanasiasa.


” Palipo na msamaha pana umoja, uelewano na usawa lakini palipo na  kisasi hapana maendeleo; nyumba ya ibada isitumike kama jukwaa la Wanasiasa alisisitiza Muhashamu Askofu Sangu.
Kutoka kushoto Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga, Naibu Gavana wa Benki Kuu, Dkt. Benard Kibese, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka,Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Simon Sirro na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Venance Mabeyo wakiwa katika ibada ya kubariki na kutabaruku Kanisa la Mtakatifu Petro Kigango cha Kiloleli Parokia ya Ilumya wilayan Busega mkoani Simiyu, iliyofanyika Desemba 26, 2018.

RC NDIKILO AWAGEUKIA MAFATAKI YALIYOBEBESHA MIMBA WANAFUNZI 16 PWANI

NA MWAMVUA MWINYI, PWANI 

MKUU wa mkoa wa Pwani, mhandisi Evarist Ndikilo amewaagiza wakuu wa wilaya kuhakikisha wanawapa msukosuko na kuwakamata wanaohusika kuwapa mimba wanafunzi 16 na kusababisha kushindwa kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi  ,pasipo kuwaachia wakiendelea kutamba kitaani. 


Aidha amewataka wazazi na walezi kuacha kumalizana kesi za mimba za utotoni majumbani na kurubuniwa fedha ili kuwaachia huru wanaobainika kuwapa mimba watoto wao wakike. 


Akizungumzia changamoto zinazodaiwa kusababisha kushuka kwa ufaulu, Ndikilo alitoa maelekezo hakuna kufanya masihala kwa wanaohusika kufanya vitendo hivyo,na wanatakiwa wakamatwe na kufungwa miaka 30 jela.


Alisema wanafunzi 223 ambao ni sawa na asilimia 0.74 hawakufanya mtihani wa kumaliza darasa la saba, kutokana na utoro 149,mimba 16 ,ugonjwa 15,vifo tisa na sababu nyingine 34.
Alitaja tatizo jingine kuwa ni utoro,mdondoko suala ambalo linachangia kushusha taaluma. 


“Tunakazi ya ziada kukabiliana na mdondoko mashuleni, tunalea watoto kuacha shule, wilayani Mkuranga mdondoko ulikuwa 67,Kibiti 36,Chalinze 36,”


“Kisarawe wanne, Bagamoyo 12,Mafia wanne, Kibaha Mjini tisa na Kibaha Vijijini wanne “alifafanua Ndikilo. 


Awali katibu tawala mkoani hapo, Theresia Mbando alieleza, idadi ya wahitimu waliosajiliwa kufanya mtihani ,walikuwa 30,010 kati yao wavulana 14,304 na wasichana  15,706 ambapo waliofanya mtihani huo ni watahiniwa 29,787 wakiwemo wavulana 14,182 na wasichana 15,605 sawa na asilimia 99.26.


Nae ofisa elimu mkoa Abdul Maulid alisema, halmashauri ya Chalinze waliopata mimba ni Tisa, Mkuranga wanne ,Bagamoyo mmoja, Kisarawe mmoja na Rufiji mmoja. 


Hata hivyo,kunaonyesha kupanda kwa ufaulu kimkoa kutoka asilimia 66.9 mwaka jana hadi asilimia 77.79 mwaka huu. 

DKT JAKAYA KIKWETE AKAGUA MIRADI YA MAENDELEO KATA YA MSOGA

 Rais mstaafu wa awamu ya nne Dkt Jakaya Mrisho Kiwete hivi karibuni amekagua baadhi ya miradi ya maendeleo kwa sekta za afya na elimu na kubaini baadhi ya changamoto zinazoikabili kata ya Msoga katika sekta husika. Katika ziara hiyo Mheshimiwa Kikwete amekagua ujenzi wa miundombinu katika shule ya sekondari Mboga na kuona ujenzi wa mabweni ya shule hiyo ambapo yeye ni mlezi wa shule hiyo.


Katika ziara hiyo Kikwete aliwataka wanajamii kutambua umuhimu wa kuboresha miundombinu ya elimu katika utoaji wa elimu wenye tija kwa maana ya kuhakikisha shule zinakuwa na vyanzo vya maji vya uhakika,madarasa ya kutosha,na mabweni yanayokidhi idadi ya wanafunzi sanjari na uwepo wa nishati ya umeme mashuleni.


Aidha Mzee Kikwete aliutaka uongozi wa halmashauri ya Chalinze kushirikiana kwa ukaribu na wadau mbalimbali wa maendeleo wanaoonyesha nia ya kusaidia katika sekta za afya na elimu kwa kuweka mazingira mazuri sanjari na kuandika maandiko yenye kuwavutia kusaidia kutokana na maandishi yenye mashiko yatakayowamotisha kulingana na uhitaji wa wananchi katika huduma hizo.


Katika ziara hiyo Kikwete ametembelea hospitali ya wilaya ya Chalinze ya Msoga na kuona ujenzi unaoendelea wa jengo la upasuaji ambalo lipo katika hatua za ukamilishaji,na muda si mrefu litaanza kutoa huduma kwa wagonjwa katika halmashauri ya Chalinze,mwisho Mzee Kikwete aliwataka watumishi wa umma kufanya kazi kwa uadilifu kwa maana ya kuwahudumia wananchi na watanzania kwa ujumla pasipo kinyongo cha aina yoyote.
  
Rais mstaafu wa awamu ya nne Dkt Jakaya Mrisho Kiwete akizungumza na viongozi wa Halmashauri ya Chalinze wakiongozwa na Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Zainabu Kawawa.

WAZAZI KIBITI KUPAMBANA NA MAADILI

Na Omary Mngindo, Kibiti

JUMUIA ya Wazazi wilaya ya Kibiti Mkoa wa Pwani, imedhamilia kupambana na vitendo vya mmomonyoko wa maadili wilayani humo, vinavyoendelea kushika kasi kila kukicha.

Mwenyekiti wa Jumuia hiyo Nurdin Ugama ameyasema hayo hivi karibuni, akizungumza kwenye Kongamano lililoandaliwa na Jumuia hiyo, mbele ya mgeni rasmi Mwenyekiti wa Wazazi Mkoa Jackson Josian, Katibu Juma Gama, Mbunge Ally Ungando na Maofisa kutoka Polisi, Magereza, Walimu na TAKUKURU lililofanyika shule ya sekondari Kinyanya.

Ugama alisema kwamba, katika wilaya hiyo kuna baadhi ya vijana wanajihusisha na vitendo vinavyokinzana na sheria na taratibu, ambao hufanya fujo sanjali na kupora watu hususani wanaopita kwenye mabasi katika kituo Kikuu kilichopo Kibiti mjini.

"Kuanzia leo Jumuia ya Wazazi wilaya ya Kibiti tumekubaliana kupambana na vijana wanaojihusisha na vitendo vya mmomonyoko wa maadili, hali ikiachwa inaweza kupotosha wengine wenye maadili mema, pia tunaonya ngoma ya Kiduku," alisema Ugama.

Sanjali na hilo pia wamepiga marufuku uvaaji wa nguo fupi kwa wasichana, sanjali na kuwakemea wamiliki wa baa ambazo wasichana wanageuza maeneo ya kufanyia vitendo vya ngono, huku akiliomba jeshi la Polisi kuungana katika kukomesha vitendo hivyo.

Akizungumza kwenye kongamano hilo, Jackson alisema kuwa Jumuia inaungana na Rais Dkt. John Magufuli katika kufayanyiakazi maagizo au ushauri wote alioutoa kwa Jumuia kuhakikisha inadhibiti vitendo vinavyoendelea ambavyo havina maadili.

Jackson alisema kwamba Jumuia haitamwangusha Rais na kuwa watapambana na vitendo viovu kwani kinyume chake ni kukinzana na agizo la Serikali lililotolewa na Rais Magufuli, huku akiwataka viongozi wa vyama na serikali mkoani humo kuungana ili kukomesha vitendo viovu.

"Niwapongeze Jumuia ya Wazazi wilaya ya Rufiji kwa Kongamano hili zuri, niwakumbushe viongozi kwamba tuna ajukumu kubwa la kusimamia maadili kwa jamii kama tulivyopewa ba Rais Dkt. John Magufuli," alimalizia Jackson.

Sunday, December 23, 2018

MGALU ACHANGIA MIRADI YA MAENDELEO PWANI.

 Mbunge wa viti maalum mkoani Pwani, Subira Mgalu ameendelea kuchangia miradi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Pwani.

Mgalu ameweza kuchangia mifuko ya saruji 40 kwaajili ya ujenzi wa Ofisi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kata ya Mtongani na Mlandizi ambapo kata ya Mtongani Mifuko 20 na kata ya Mlandizi mifuko 20.

Subira alitoa mifuko hiyo ya saruji wakati alipokutana na baadhi ya viongozi wa chama ikiwa ni moja ya kazi za kichama na kusema kuwa huo ni wajibu wakena kwamba hatochoka kushiriki kusaidiana kutatua changamoto zilizopo kichama na serikali. 

Katika Ziara aliyoifanya Halmashauri ya Chalinze hapo jana, Subira mgalu alitoa Tenki la kuhifadhia maji katika zahanati ya Msata pamoja na sola itakayowasaidia pindi umeme unapokatika.

Aidha, alifika katika Zahanati ya Pongwe Kiona na kusadia mashuka 10 kwaajili ya vitanda vya wagonjwa.

Katika ziara yake kijiji cha Pongwe kiona Mbunge huyo wa Viti maalum Mkoa wa Pwani, aliweka jiwe la msingi jengo la Zahanati litakalotumika kwaajili ya kinamama kujifungulia.

Subira Mgalu ameahidi kuchangia mifuko ya Saruji katika ujenzi huo ili kuunga mkono juhudi hizo zilizoanzishwa na wananchi.


Diwani wa kata ya Mlandizi Ephrasia Kadala, alisema Hili ulilolitenda ni jambo kubwa kwa wana CCM na wananchi kijumla.

Diwani huyo aliwaomba wadau wengine kujitolea kushirikiana ili kumaliza kero zinazowakabili kichama katika kata hiyo.

Nae Katibu wa Jumuiya ya wanawake (UWT) Kibaha Vijijni Janeth Mnyaga alimshukuru mbunge huyo kuwa bega kwa bega kushiriki nao kwenye shughuli za jumuiya na chama.

Wakati huo huo Subira alitembelea kituo cha afya Mlandizi kujionea hali ya upanuzi wa majengo kwa gharama ya sh. Milioni 400 ambazo zimetolewa na serikali.

Madiwani wa kata ya Msata na Kimange Halmashauri ya Chalinze wamemtaja Subira mgalu kuwa ni mpambanaji asiyechoka na kwamba wanafarijika kuwa na muwakilishi mwenye kujali shida za wananchi katika eneo lake licha ya kuwa na jukumu la kitaifa katika wizara ya nishati.

Mganga mfawadhi wa Zahanati ya Msata Willy John amesema anamshukuru Mbunge huyo wa viti maalum mkoa wa Pwani kwa msaada wa Tenki la kuhifadhia maji na pamoja sola itakayowasaidia kwa shughuli za usiku katika Zahanati hiyo
 
 Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Pwani, Subira Mgalu akikabidhi Tenki la kuhifadhia maji katika Zahanati ya Msata Halmashauri ya Chalinze.
 
Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Pwani, Subira Mgalu, akiweka jiwe la msingi katika ujenzi wa jengo la kina mama Zahanati ya Pongwe Kiona.