Saturday, November 10, 2018

MAKAMU WA RAIS AZINDUA BARABARA MPYA YA BONITE MOSHI MANISPAA

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiweka jiwe la msingi la ufunguzi wa barabara Bonite yenye urefu wa kilomita 2.93 iliyojengwa kwa kiwango cha lami wengine pichani ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Anna Mghwira(katikati), Meya wa Manispaa ya Moshi Ndugu Raymond Mboya (kulia)  Mkuu wa Wilaya ya Moshi Ndugu Kippi Warioba na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo (kushoto).Makamu wa Rais yupo mkoani Kilimanjaro kwenye ziara ya kukagua na kuhamasisha shughuli za maendeleo. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akikata utepe kuashiria uzinduzi wa barabara ya Bonite yenye urefu wa kilomita 2.93 iliyopo Moshi Manispaa. Makamu wa Rais yupo mkoani Kilimanjaro kwenye ziara ya kukagua na kuhamasisha shughuli za maendeleo. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Meya wa Manispaa ya Moshi Ndugu Raymond Mboya wakati wa kuweka jiwe la msingi la ufunguzi wa barabara ya Bonite yenye urefu wa kilomita 2.93, wengine pichani ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Anna Mghwira(katikati),Mkuu wa Wilaya ya Moshi Ndugu Kippi Warioba na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo (kushoto).
Makamu wa Rais yupo mkoani Kilimanjaro kwenye ziara ya kukagua na kuhamasisha shughuli za maendeleo. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)

MAGAZETI YA LEO NOVEMBA 10, 2018.

RATIBA YA KOMBE LA SHIRIKISHO HII HAPA.

TAZAMA RATIBA YA LIGI YA MABINGWA AFRIKA HAPA

SIMBA KUANZA NA MBABANE SWALLOWS YA SWAZILAND LIGI YA MABINGWA AFRIKA


KLABU ya Simba ya Dar es Salaam itaanza na Mbabane Swallows Swaziland katika Raundi ya Awali ya mchujo wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2019.
 
Ikifanikiwa kuvuka mtihani huo, Simba SC itakwenda hatua ya mwisho ya mchujo kuwania kuingia hatua ya makundi ya michuano hiyo.
 
Na huko itamenyana na mshindi kati ya Uniao Desportiva Do Songo ya Msumbiji na Nkana FC ya Zambia, anayochezea beki wake wa zamani, Mtanzania, Hassan Kessy aliyewahi kucheza na Yanga pia.
 
Wawakilishi wa Zanzibar, JKU watamenyana na Al Hilal ya Sudan na mshindi baina yao atakutanana mshindi kati ya APR FC ya Rwanda na Club Africain ya Tunisia.

Mechi za kwanza za raundi ya kwanza ya mchujo zitachezwa kati ya Novemba 27 na 28 na marudiano Desemba 4 na 5, mwaka huu, wakati mechi za kwanza za raundi ya pili ya pili na ya mwisho ya mchujo zitachezwa kati ya Desemba 14 na 16 na marudiano Desemba 21 na 23, mwaka huu.

Katika Kombe la Shirikisho, Mtibwa Sugar itaanza na Northern Dynamo ya Shelisheli na ikivuka mtihani huo itakutana na K.C.C.A ya Uganda.
 
Wawakilishi wa Zanzibar, Zimamoto wamepewa kigongo, Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini na mshindi baina yao atakutana na mshindi kati ya El Geco ya Madagascar na Deportivo Unidad ya Equatorial Guinea.


YANGA YAKUBALI KUFANYA UCHAGUZI JANUARI 13 FOMU ZAANZA KUTOLEWA

KLABU ya Yanga imekubali kufanya uchaguzi, kwa ajili ya kujaza nafasi zilizo wazi, Januari 13, mwakani huu.

Wiki mbili zilizopita Baraza la Michezo la Taifa (BMT), iliwataka Yanga kuitisha uchaguzi wake kwa ajili ya kujaza nafasi za viongozi waliojiuzuru huku ikiwemo ya mwenyekiti wao wa zamani Yussuf Manji.
 
Yanga kwa sasa imebaki na wajumbe wanne kati ya wajumbe  13 waliochaguliwa katika uchaguzi wa juni 12, mwaka 2016 Dar es Salaam.
 
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo mjini Dar es Salaam, Kaimu Mwenyekiti wa Yanga, Thobias Lingalangala amesema kwamba wanatarajia kufanya uchaguzi  mapema mwakani na fomu za kugombea tayari zimeshaanza kutolewa.

Lingalangala amesema uchaguzi utafanyika kama ulivyotangazwa na kamati ya uchaguzi ya  Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na fomu zimeanza kutolewa rasmi leo ofisi za TFF na klabuni.

Alisema kuwa kuna baadhi ya wanachama  walikuwa wanazuia uchaguzi huo ameomba wapuuzwe na wanachama wote w anaruhusiwa kuja kuchukua fomu kama anaona anafaa kuweza kuongoza klabu yao.
 
“Tumeanza kutoa fomu leo hivyo tunawaomba wanachama wenye nia ya kugombea waje kuchukua fomu na hata mwanachama pia kama  unaona kuna mtu anafaa kugombea katika nafasi yeyote basi amshawishi ili aweze kuchukua  fomu mapema,” alisema Lingalangala.
 
Hata hivyo Lingalangala alisisitiza kuwa kama itatokea wanachama au mwanachama yeyote ambaye atapinga uchaguzi huo basi watampeleka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ili waweze kumpa adhabu inayostahili.
 
Hata hivyo Lingalangala alisema kuwa garama za fumu hizo nafasi ya Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti ni Sh. 200,000 na wajumbe wake ni sh.100,000. 
 
Wakati huo huo kamati ya utendaji ya klabu ya Yanga imemteua Lingalangala kuwa Kaimu Mwenyekiti wa klabu hadi uchaguzi wa kujaza nafasi utakapofanyika.
 
Klabu ya Yanga imekuwa ikihairisha mara kwa mara kufanya uchaguzi wake, licha ya Juni 10 mwaka huu Waziri Mwakyembe kuwataka wafanye uchaguzi kuziba mapengo ambayo yapo wazi.
 
Kati ya viongozi wa klabu hiyo ambao waliingia madarakani Julai mwaka juzi, viongozi sita wamejiuzulu nafasi hizo wakidai kuwa na majukumu mengi.
 
Viongozi waliojiuzulu ndani ya klabu hiyo pamoja na Manji, wengine ni Makamu Mwenyekiti, Clement Sanga na wajumbe Inspekta Hashim Abdallah, Salum Mkemi, Omary Said, Ayoub Nyenzi na huku waliobaki ni wajumbe Thobias Lingalangala,
Samuel Lukumay, Siza Lyimo na Hussein Nyika.

Friday, November 9, 2018

SERIKALI YATOA SIKU NNE KWA WANUNUZI WA KOROSHO

SERIKALI imetoa siku nne kwa wanunuzi wote 35 waliojiandikisha kununua korosho wawe wamepeleka barua katika Ofisi ya Waziri Mkuu wakionesha  kiasi cha tani wanazohitaji na lini watazichukua.

“Hivyo wanunuzi waliojiandikisha wakiwemo na wale wote ambao wamekuwa wananunua kwenye minada lakini kwa kiasi kidogo, wahakikishe ndani ya siku hizo nne kuanzia leo Ijumaa hadi Jumatatu saa 10 alasiri wawe wameleta barua na ofisi yangu ipo wazi saa 24.”

Hayo yamesemwa leo (Ijumaa, Novemba 9, 2018) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akitoa tamko la Serikali kuhusu ununuzi wa zao la korosho, ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma.Baada ya kupita siku hizo Serikali italazimika kufuta usajili kwa wote waliojisajili kununua zao hilo kwa sababu walikubaliana kwenda kununua lakini hali inayoonekana sasa ni kama kumkomoa mkulima kitu ambacho imesema haitakubaliana nacho.

“Mwenye nia ahakikishe katika siku hizo nne iwe ndio mwisho wa kununua korosho na waandike barua kwani ofisi yangu ipo wazi saa 24 wana nafasi ya kuleta barua wakati wowote wakionesha nia yao na kiwango wanachokihitaji. Zaidi ya hapo Serikali haitoruhusu kampuni yoyote kununua korosho tena.”

Waziri Mkuu amesema kwenye msimu wa ununuzi wa korosho wa mwaka huu, walishuhudia kusuasua kwa minada, ambapo Serikali ilikutana na wanunuzi wa korosho katika kikao kilichoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli ambapo walikubaliana kununua kwa bei inayoanzia sh 3,000 na kuendelea.

“Mjadala ulikuwa wa wazi na wafanyabiashara wenyewe walipendekeza bei ambayo ilikuwa inaanzia sh. 3,000, hata hivyo baada ya kikao hicho ununuzi katika minada imeendelea kusuasua na hata tani zilizokuwa zikinunuliwa zilikuwa kidogo sana. Sisi tunaiona hali hii kama mgomo baridi ambao si sawa sawa sana kwani malengo yetu sisi na sekta binafsi ni kumfanya mkulima apate bei nzuri.

Hali hii haifurahishi kwa sababu Serikali imedhamiria kuboresha mazao yanayolimwa na wakulima kwa kuwasaidia kuanzia katika hatua za utayarishaji wa mashamba, upatikanaji wa pembejeo na masoko ili waweze kunufaika na kilimo na kupata tija katika mazao hayo.”Waziri Mkuu amesema baada ya kugundua bei imekuwa tatizo Serikali ilifanya jitihada za kupeleka wataalamu wake katika masoko makuu duniani na kupata bei halisi ambayo bado  inatosha kumlipa mkulima sh 3,000.

Hatua hiyo imekuja baada ya zao la korosho kuendelea kununuliwa kwa bei ya chini na idadi ya wanunuzi kuwa ya chini licha ya uzalishaji wa mwaka huu kuwa mdogo ukilinganisha na msimu wa mwaka jana.Amesema msimu wa mwaka jana uzalishaji ulikuwa zaidi ya tani 300,000 na mwaka huu zinatarajiwa tani zaidi ya 200,000 hivyo wafanyabiashara wanao uwezo kununua korosho zilizopo.

Hata hivyo Serikali imewataka wananchi hususani wakulima wa korosho nchini kuendelea kuwa wavumilivu na watulivu wakati ikiendelea kushughulikia suala hilo.