Thursday, November 8, 2018

SERIKALI YAPIGA MARUFUKU WATUMISHI WA UMMA WALIOHAMIA DODOMA KUOMBA UHAMISHO KUREJEA DAR ES SALAAM

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro akizungumza katika mahojiano maalum na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) ofisini kwake jijini Dodoma kuhusiana na zoezi zima la uhamisho wa watumishi wa umma kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma.
.......................................


Serikali imepiga marufuku Watumishi wa Umma waliohamia Makao Makuu ya Nchi Dodoma kwa gharama za Serikali kuomba uhamisho wa kurejea jijini Dar es Salaam.

Hayo yamesemwa leo na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro alipokuwa akifanya mahojiano maalum na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kuhusiana na zoezi zima la uhamisho wa watumishi wa umma kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma.

Dkt. Ndumbaro amesema kuwa,  Ofisi yake imekuwa ikipokea barua mbili au tatu kwa siku za watumishi waliohamia Dodoma kuomba uhamisho wa kurejea Dar es Salaam kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na za kiafya wakati hospitali ya Rufaa ya Benjamin Mkapa ina vifaa vya kisasa na uwezo mkubwa wa kutoa huduma za matibabu kwa watumishi hao.

Dkt. Ndumbaro amefafanua kwamba,  kabla ya watumishi kuhamia Dodoma, Serikali ilitoa maelekezo kwa waajiri kuwasilisha orodha ya watumishi wenye matatizo ya kimsingi ili wabaki kwenye vituo vya kazi vilivyopo Dar es Salaam wakiendelea kutekeleza majukumu yao.

Dkt. Ndumbaro ameongeza kuwa, baadhi ya watumishi waliohamia Dodoma, wamegeuza uhamisho huo kuwa mradi  wa kuwaingizia kipato kwani mara baada ya kuripoti Dodoma, ndani ya kipindi kifupi wanaomba uhamisho wa kurejea Dar es Salaam.

Dkt. Ndumbaro amesisitiza kuwa, kutokana na suala hilo, Serikali imetoa Waraka wa Barua wenye Kumb. Na. CAC 228/257/01/A/53 wa tarehe 25 Septemba, 2018 kuhusu Uhamisho wa Watumishi Waliohamia Dodoma Kutekeleza Uamuzi wa Serikali Kuhamishia Makao Makuu ya Nchi Dodoma ambao unazuia mtumishi aliyehamishiwa Dodoma kwa gharama za Serikali kuomba uhamisho wa kurejea Dar es Salaam mpaka atimize miaka mitatu katika kituo cha Dodoma.

Watumishi wa Umma kuhamia Dodoma ni utekelezaji wa agizo la Serikali lililotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 25 Julai, 2016 wakati wa maadhimisho ya Kumbukumbu ya Siku ya Mashujaa.

KAWAMBWA APONGEZWA JIMBONI KWAKE.

 Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, Dkt. Shukuru Kawambwa.

Na Omary Mngindo, Bagamoyo

Mbunge wa jimbo la Bagamoyo Dkt. Shukuru Kawambwa amepongezwa kwa kitendo cha kutoa ardhi ekari 6 na nusu kwaajili ya ujenzi wa shule ya msingi.
Pongezi hizo zimetolewa na WAKAZI wa Kitongoji cha Kitopeni Jimbo la Bagamoyo Mkoa wa Pwani, na kuongeza kuwa kitendo hicho ni cha kizalendo na wanamshukuru kwa hatua hiyo.

Wakizungumza katika mkutano ulioandaliwa na Mbunge huyo mbele ya Mwenyekiti wao Bushir Kitumboi, wakazi Sapi Ibrahimu na Lumpa Rajabu kwa niaba ya wenzao walisema kuwa, wamefurahishwa na hatua ya Mbunge huyo kwa kujitolea ardhi hiyo kwa ajili ya shule.

Sapi alisema kwamba hatua ya mbunge wao kuwapatia ardhi eneo la mjini, ni kitendo cha kiubinadamu na kujali elimu kwa watoto na kwamba angetaka kuiuza angepata mamilioni ya shilingi.

"Binafsi nimegushwa na juhudi hizi za Mbunge, ameamua mwenyewe kutupatia eneo, umeamza ujenzi, kwa mapenzi yake akatuongezea nguvu ya trekta kwa ajili ya kufanikisha ujenzi, binafsi namshukuru kwa ubinadamu aliouonesha," alisema Sapi.

Nae Lumpa alisema kwamba kabla ya kupatikana kwa eneo hilo na ujenzi huo, wanafunzi walikuwa wanatembea umbali mrefu kufuata huduma ya kielimu, lakini kwa sasa wanashukuru kwa shule kuwa karibu.

Mwenyekiti Kitumboi alisema kuwa wananchi wanatambua juhudi zinazofanywa na mbunge wao, sanjali na viongozi wote ngazi mbalimbali katika kuiletea maendeleo Kitopeni, na Jimbo kwa ujumla, huku akiwaomba kuendelea kuwapatia ushirikiano viongozi hao.

"Kwa hili la ardhi ambayo tumeshaanza ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa, wana- Kitopeni tuna kila sababu ya kutembea kifua mbele kupitia Mbunge wetu, ameonesha kutujali kwenye sektq muhimu ya elimu kwa watoto wetu," alisema Kitumboi.

Akizungumza na wananchi hao, Dkt. Kawambwa alisema kuwa ameshawishika kuwakabidhi ardhi hiyo baada ya kuona uwepo wa umuhimu wa shule kwenye eneo hilo, ili kuwakomboa watoto waliokuwa wanateembea umbali mrefu kufuata masomo.

"Nimeona watoto wetu wanavyotembea umbali mrefu kwenda kusoma, nimetoa ardhi ile kwa moyo mmoja ili tujenge shule itayosaidia vizazi vyetu, pia nimetoa trekta kwa ajili ya shughuli mbalimbi za ujenzi wa shule," alisema Dkt. Kawambwa.

MAGAZETI YA LEO NOVEMA 08, 2018.

Wednesday, November 7, 2018

PROF.MBARAWA ATOA ONYO KWA MAMLAKA ZA MAJI

Waziri wa maji Prof. Makame Mbarawa, ametoa onyo kwa mamlaka za maji na usafi wa mazingira nchini kuacha tabia ya kuwabambikizia bei za ankara za maji wateja.

Mbarawa ameyasema hayo leo jijini Dodoma alipokuwa akifungua kikao kazi cha siku mbili kwa watendaji wa mamlaka za maji za mikoa na wilaya

Aidha ametoa onyo kwa wakuu wa mamlaka hizo ambao bado wanatoza gharama za huduma kwa wateja (Services Charges) kuacha mara moja kwani atakaye bainika mshahara wake utakatwa ili kurejesha fedha za wateja.

Prof.Mbarawa amesema  kuwa amekuwa akipokea malalamiko mengi kutoka kwa wateja kubambikiziwa ankara za maji na mamlaka za maji katika maeneo mbalimbali nchini.

“Tusiwabambikizie wateja wetu bill za maji kiasi ambacho hawajatumia, wananchi wamekuwa wakilalamika  katika maeneo ambayo nimekuwa nikipita kuzungumza nao nawataka watendaji wote kuacha mara moja tabia hii”amesema Prof. Mbarawa.

Hata hivyo amezungumzia  juu ya malipo ya gharama za huduma alizitaka mamlaka zote za maji nchini kuacha kutoza wanachi na atakae bainika hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.

Mbarawa amesema kuwa mpaka sasa anashamgaa sana kuwa Services Charge tulishaziondoa lakini bado nasikia kuna baadhi ya mamlaka watu  bado wanatozwa fedha hizi ambazo tulikubaliana kwa pamoja kuziondoa sasa naagiza kuwa atakaye bainika hivi sasa kuwa bado anaendelea kutoza wanachi mshahara wake utakatwa ili kufidia kiasi ambacho wateja wamelipa

Prof. Mbarawa ameziagiza mamlaka zote za maji nchini kuongeza udhibiti wa maeneo yanayotumika kutibu maji kwa kuweka ulinzi ikiwemo kufungwa mifumo ya kielekitroniki.

“Kwa jambo hili naomba mfanye haraka bila kuchelewa uwepo ulinzi wa askari pamoja na mifumo ya cctv camera ili hata kama likiharibika lolote tunakwenda kurejea katika video na kuona nini kilitokea nini ili muweze kutibu maji ni eneo nyeti sana leo hii ukienda nchi kama Misri kuingia katika eneo hili lazima uwe na kibari maalum”alifafanua Prof. Mbarawa.

Prof.Mbarawa ameitaka mamlaka ya udhibiti wa maji na nisahti kwa  kushirikiana na wizara kuona namna gani ambavyo wanaweza kuweka utaratibu wa bei moja kwa huduma ya maji vijijini.

“Leo hii ukienda vijiji unakuta baadhi ya maeneo ndoo ya lita 20 wananunua kwa sh. 500, wengine 200 na wengine 100 hivyo lazima tuwe na bei ambayo itafahamika kwa kila eneo ili tuweze kuwasaidia wananchi wanyonge”amesema Mbarawa

Aidha Mbarawa ametoa onyo kwa mamlaka ambazo zimekuwa na tabia ya kushindwa kulipa ankara za umeme pamoja na madawa ya kutibu maji.

Prof.Mbarawa amesema kuwa katika utawala wangu mimi kama waziri wa maji sitakubaliana na mamlaka ambazo zimekuwa zikishindwa kulipa umeme na kutaka wizara iwalipie kutoka katika mfuko wa maji wakati wanatoa huduma na wanalipwa

Katika kikao hicho Prof. Mbarawa amesema  wizara yake   itaweka mfumo sahihi wa kuwapima wakuu wa mamlaka za maji kwa kila baada ya miezi mitatu na atakayeshidwa ataondolewa katika nafasi yake.

BALOZI MPYA WA KUWAIT NCHINI AJITAMBULISHA KWA MAKAMU WA RAIS LEO JIJINI DODOMA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Balozi mpya wa Kuwait nchini Mhe. Mubarak Mohammed Faleh ALSEHAIJAN aliyefika ofisini kwa Makamu wa Rais Kilimani jijini Dodoma kwa lengo la kujitambulisha.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Balozi mpya wa Kuwait nchini Mhe. Mubarak Mohammed Faleh ALSEHAIJAN aliyefika ofisini kwa Makamu wa Rais Kilimani jijini Dodoma kwa lengo la kujitambulisha. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
…………………
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan leo amekutana na kuzungumza na Balozi mpya wa Kuwait nchini Mhe. Mubarak Mohammed Faleh ALSEHAIJAN aliyefika ofisini kwa Makamu wa Rais Kilimani jijini Dodoma kwa lengo la kujitambulisha