Wednesday, November 7, 2018

JESHI LA POLISI MBEYA LINAWASHIKILIA WATU WAWILI KWA TUHUMA ZA KUVUNJA DUKA USIKU NA KUIBA

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kupatikana na mali ya wizi. Watuhumiwa wamefahamika kwa majina ya 1. JOSEPH DESU PARAFESTO [24] Mkazi wa Sumbawanga – Majengo 2. ENWELO SINKONDE [32] Dereva Bodaboda na Mkazi wa Chunya wakiwa na fedha taslimu Millioni kumi na saba laki tisa na kumi na sita elfu [17,916,000/=].

Watuhumiwa walikamatwa mnamo 04.11.2018 majira ya saa 22.00 usiku huko maeneo ya Kijiji cha Mwansekwa kilichopo Kata ya Mwansekwa, Tarafa ya Sisimba, Jijini Mbeya na askari waliokuwepo kwenye kizuizi cha Polisi (Barrier) kilichopo kijiji cha Mwansekwa.

Watuhumiwa hao walikuwa wanasafiri kutoka Chunya kuja Mbeya mjini wakiwa kwenye pikipiki yenye namba za usajili MC 322 CAP aina ya T.BETTER iliyokuwa ikiendeshwa na ENWELO SINKONDE [32] huku JOSEPH DESU PARAFESTO akiwa amebeba begi dogo.

Baada ya kusimamishwa na askari walipekuwa begi alilokuwa amelibeba JOSEPH DESU PARAFESTO hatimaye kukuta kiwango hicho cha pesa. Mtuhumiwa alihojiwa kuhusu pesa hizo anazipeleka wapi na amezitoa wapi alidai kuwa amekabidhiwa na kaka yake wa Makongorosi – Chunya ambaye alidai ni mfanyabiashara wa madini aina ya dhahabu na kwamba amekabidhiwa fedha hizo azipeleke Sumbawanga kwa ajili ya kununulia bidhaa za duka la jumla.

Hata hivyo kutokana na kiwango hicho cha fedha kuwa kikubwa, ufuatiliaji wa kiupelelezi ulifanyika hatimaye kugundulika kuwa watuhumiwa walihusika kwenye tukio la KUVUNJA DUKA USIKU NA KUIBA huko Wilaya ya Chunya na kupora pesa hizo, hivyo walikuwa kwenye harakati za kutoroka na pesa hizo. Upelelezi wa shauri hili unaendelea na mara baada ya kukamilika watuhumiwa watafikishwa Mahakamani.

TUKIO LA MAUAJI – MBEYA MJINI.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la THERESIA VENAS [26] Mkazi wa Mama John Jijini Mbeya kwa tuhuma kumuua kikatili VIKO BIKO, anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 60 – 65, Mkazi wa Iyela One.

Tukio hilo limetokea mnamo tarehe 05.11.2018 majira ya saa 13:00 mchana huko maeneo ya Iyela One, Kata ya Iyela, Tarafa ya Iyunga, Jijini Mbeya, ambapo wa VIKO BIKO, alikutwa akiwa ameuawa chumbani na mwili wake ukiwa chini ya kitanda.

Katika uchunguzi uliofanyika, mwili wa marehemu ulikutwa na majeraha sehemu za kichwani, mgongoni, mbavuni na tumboni karibu na kitovu, majeraha yanayoonyesha kuwa muuaji alitumia kitu chenye ncha kali.
Awali inadaiwa kuwa marehemu alikuwa akifanya biashara ya Grocery huko maeneo ya Iyela na kwa mara ya mwisho kabla hajafunga Grocery hiyo alikuwa na mwanamke mmoja aliyekuwa amevaa mavazi yaliyoficha uso wake na alikuwa hafahamiki maeneo hayo.

kufuatia tukio hilo, msako mkali ikiwemo ufuatiliaji kwa njia ya Cyber Crime ulifanyika na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa THERESIA VENAS [26] Mkazi wa Mama John Jijini Mbeya. Mtuhumiwa baada ya kuhojiwa amekiri kufanya tukio hilo akieleza kuwa chanzo cha kufanya mauaji hayo ya kikatili ni ugomvi uliotokea baina yake na marehemu wakati wakiwa chumbani kwa marehemu wakifanya mapenzi na marehemu kumlazimisha kufanya mapenzi kinyume cha maumbile. 

Mtuhumiwa ameumia bega la kulia katika ugomvi huo. Mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali ya Rufaa Mbeya kwa uchunguzi zaidi wa kitabibu.Upelelezi wa shauri hili unaendelea.

OPERESHENI NA MISAKO MBALIMBALI.

Aidha katika misako inayoendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya, Jeshi la Polisi Mkoani hapa linawashikilia jumla ya watuhumiwa 63 kutokana na kujihusisha na uhalifu hasa wizi wa mali mbalimbali.

Katika misako hiyo, mali mbalimbali zimekamatwa ikiwa ni pamoja na:-
1.   Flat Screen inchi 45 tatu aina ya LG na Hisense mbili.
2.   Flat Screen inchi 32 tatu aina ya LG na Samsung mbili
3.   Flat Screen inchi 21 aina ya LG
4.   Home Theatre aina ya Sony
5.   Betri 08 za magari aina mbalimbali.

Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea na Operesheni, Doria na Misako katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya hasa katika maeneo tete kama vile maeneo ya Mlima Nyoka, Mlima Igawilo, Mlima Mwansekwa, Mlima Iwambi ili kuhakikisha usalama kwa madereva na watumiaji wengine wa barabara unakuwepo. Pia Jeshi la Polisi linaendelea na zoezi la ukaguzi katika nyumba za kulala wageni ili kuhakikisha usalama hasa katika kipindi hiki cha kuelekea mwisho wa mwaka.

MWENYEKITI WA CCM BAGAMOYO AGAWA JEZI SEKONDARI YA KIROMO

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani Abdul Sharifu akimkabidhi jezi kwa mwalimu Mkuu wa Shule ya sekondari ya Kiromo Hosea Maganga
................................................


Na Omary Mngindo, Kiromo Bagamoyo


MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani Abdul Sharifu amekabidhi jezi kwa mwalimu Mkuu wa sekondari ya Kiromo Hosea Maganga zitumike kwa michezo mbalimbali.

Sharifu amekabidhi jezi hizo kufuatia ombi kutoka kwa Tarki Mokiwa mwanafunzi wa shule hiyo, wakati wa msafara wa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT) Mkoa wa Pwani, Farida Mgomi, alipotembelea shuleni hapo, ambapo wanafunzi walielezea changamoto ya vifaa.

Sharifu alisema kuwa baada ya kupokelewa kwa changamoto hizo, yeye aliahidi jezi, Mwanaisha Kikwete mipira wakati Mgomi akiahidi mipira, na kwamba yeye aliwasiliana na mmoja wa marafiki zake wamempatia jezi hizo, na kwamba ameambiwa na Maganga kuwa Kikwete ameshakabidhi mipira.

"Kwanza niwapongeze kwa kuwa majasiri wa kuelezea changamoto zinazowakabili, msafara wa Mwenyekiti ulipofika shuleni kwenu mlizungumza mambo mengi ikiwe vifaa vya michezo, leo nawakabidhi," alisema Sharifu.

Aliongeza kuwa kupatikana kwa jezi hizo na mipira iliyowasilishwa na Mwanaisha Kikwete itaongeza hali ya michezo shuleni hapo, huku alisema kwamba baada ya kumalizika kwa mitihani ya Kidato cha nne ataandaa michezo kati ya wahitinu na wanaobaki, ataandaa zawadi.

"Jiandaeni vizuri, baada ya kumalizika kwa mitihani nitaandaa michezo maalumu kati ya wanaomaliza Kidato cha nne, na nyie mliobaki kwa maana ya kuanzia Kidato cha kwanza mpaka cha tatu, nitaandaa zawadi nzuri," alisema Sharifu.

Akipokea zawadi hizi, mwalimu Maganga alimahukuru Mwenyekiti huyo kwa kukabidhi ahadi yake mapema, huku akiwataka wanafunzi kutumia vizuri jezi hizi, sanjali na kujiimarisha kimasomo.

"Tunaimani kubwa na Serikali iliyopo madarakani chini ya Rais Dkt. John Magufuli, tunaona dhamira yake, pia viongozi wa chama na Jumia zake mnatekeleza mnayoyaahidi, mlikuja mwishoni mwa wiki, ndani ya siku tatu tumeona mlivyoviahidi," alisema Mwalimu Maganga.

Nae Mokiwa kwaniaba ya wanafunzi wenzake wamemhaidi Sharifu kwamba watazitumia vizuri jezi hizi, sanjali na kupatikana alama A kwenye mitihani yao yote wakati wakiwa shuleni hapo.
 
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani Abdul Sharifu akishusha jezi kwenye gari kwaajilia ya kuzigawa.
    
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani Abdul Sharifu akimkabidhi jezi kwa mwalimu Mkuu wa Shule ya sekondari ya Kiromo Hosea Maganga

SERIKALI INAENDELEA KUIMARISHA USIKIVU WA TBC NCHI NZIMA:DKT.MWAKYEMBE

Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe akiwa bungeni Jijini Dodoma.
......................................


Na Shamimu Nyaki –WHUSM.

Katika kuimarisha usikivu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Serikali imeendela kuweka mikakati mizuri ya kuongeza usikivu wa shirika hilo hapa nchini kutegemea na upatikanaji wa fedha.

Hayo yamesemwa leo Bungeni Jijini Dodoma na Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt.Harrison Mwakyembe alipokuwa akijibu swali la mbunge Mhe. Zaynab Matitu Vulli (Viti Maalum) aliyeuliza Ni chanagamoto zipi zinazopelekea TBC kutosikika katika baadhi ya maeneo ya Pwani ambapo Mhe. Waziri alieleza kuwa katika Bajeti ya mwaka 2016/17 maeneo mengi ya nchi yaliongezewa usikivu.

“TBC ina mitambo ya kurushia matangazo  ya redio ya masafa ya FM katika Wilaya ya Kisarawe ambayo hufikisha matangazo kwa wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani katika masafa ya  87.8 MHz kwa idhaa ya TBC Taifa, 90.0 MHzkwa idhaa ya TBC FM na 95.3 kwa idhaa ya TBC International”.Alisema Dkt. Mwakyembe.

Aidha ameongeza kuwa katika Bajeti ya mwaka 2016/17 TBC ilitekeleza mradi wa upanuzi wa usikivu katika Wilaya tano zilizopo mpakani ambazo ni Wilaya za Longido, Rombo,Tarime,Nyasa na Kibondo.

Vilevile katika Bajeti ya mwaka 2017/18 mradi wa usikivu katika mkoa wa Mtwara na Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga ulitekelezwa ambapo hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu TBC ilikua na vituo thelathini na tatu vya kurushia matangazo katika masafa ya FM kwenye Wilaya 102 kati ya 161 nchi nzima.

Dkt. Mwakyembe ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuhakikisha kuwa TBC inapanua usikivu ambapo kwa mwaka huu wa fedha maeneo ya Unguja na Pemba,Simiyu,Njombe,Songwe,Lindi maeneo ya Nangurukuru  pamoja na Mkoa wa Morogoro maeneo ya Morogoro Vijijini,Bondwa na Mahenge yatafikiwa.