Wednesday, November 7, 2018

WODI YA WAZAZI KATIKA KITUO CHA AFYA CHALINZE YAKABILIWA NA UFINYU WA JENGO, VITANDA NA WATUMISHI WA AFYA

 Kikundi cha Pwani generation queens walipotembelea kituo cha Afya Chalinze kutoa msaada wa vifaa vya kinamama waliojifungua.
.......................................................
NA MWAMVUA MWINYI,CHALINZE

WODI ya uzazi katika kituo  cha afya Chalinze,mkoani Pwani inakabiliwa na baadhi ya changamoto ikiwepo ufinyu wa jengo hali inayosababisha wakati mwingine akinamama wazazi kusongamana na kulazimika kulala wawili katika kitanda kimoja.

Aidha kina tatizo jingine la upungufu wa vitanda  na watumishi wa afya hasa madaktari .

Akikabidhiwa msaada wa vifaa vya akinamama waliojifungua kutoka kwa kikundi cha Pwani generation queens  ,mganga mfawidhi wa kituo hicho  Salama Masukuzi alisema kuwepo kwa mlundikano wa wagonjwa kunatokana na upungufu wa majengo ya wodi ya uzazi  pamoja na  vitanda .

Alieleza ,kwasasa  wapo maafisa tabibu wanne ,madaktari wasaidizi wawili na daktari mmoja ambao bado ni wachache kutekeleza majukumu yao ya kutoa huduma bora ya kiafya .

“Kituo hiki kinapokea wagonjwa mbalimbali na wengine wakitokea kwenye zahanati 44 zinazozunguka halmashauri ya Chalinze suala ambalo linawawia vigumu kutekeleza wajibu wao ” alifafanua Salama .

Alieleza wamepata manesi wanne kupitia ajira mpya, ameishukuru serikali lakini aliiomba kuwaboreshea zaidi huduma ya afya ili kuwahudumia wananchi.

Kwa upande wa akinamama wa Chalinze,akiwemo Demertia Milichadesi pamoja na Mariam Muhoja  walisema wanapata shida katika kununua drip,vifaa vya uzazi na kipimo cha kujua wingi wa damu ambacho hutakiwa kwenda nje wakati mjamzito akiwa tayari yupo wodini.

“Tumekuwa tukipata shida ya ukosefu wa vifaa kwa ajili ya kujifungulia  na wakati mwingine inatubidi kwenda dukani kununua na  uwezo wetu kifedha ni  mdogo ,tunqshindwa kumudu gharama za matibabu”
Demertia aliwashukuru Pwani generation queens kwa misaada waliyoipata na kuomba wadau na vikundi vingine vikumbuke kusaidia kituo cha afya Chalinze.

Akikabidhi msaada wa vifaa mbali mbali katika wodi ya uzazi kwenye kituo hicho cha afya , Mwenyekiti wa kikundi cha Pwani Generation Queens Betty Msimbe alisema wamesaidia kutokana na kubaini kuwepo kwa  upungufu wa vifaa hasa kwa wanawake  wajawazito ambao wanakwenda kupatiwa matibabu na kujifungua.

Betty alieleza,wapo wanawake ambao wamekuwa wakipata shida  pindi wanapokwenda katika zahanati, vituo vya afya na hospitali kwa ajili ya kujifungua hivyo wakaona kuna umuhimu wa kutoa msaada huo.

WALIOFARIKI AJALI YA MSATA WATAMBULIWA MAJINA YAO -RPC WANKYO

 Kamanda wa polisi mkoani Pwani, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Wankyo Nyigesa, akizungumza na waandishi wa Habari.
 ................................................
NA MWAMVUA MWINYI, PWANI.

WATU sita kati yao akiwemo mtoto mchanga jinsia ya kike ,waliofariki dunia katika ajali ,iliyotokea kijiji cha Msata, barabara kuu ya Segera /Chalinze mkoani Pwani ,wametambuliwa majina yao ili ndugu wakabidhiwe kwa ajili ya mazishi. 

Akitoa taarifa za muendelezo kuhusu ajali hiyo, kamanda wa polisi mkoani Pwani, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Wankyo Nyigesa alisema hakuna idadi ya vifo iliyoongezeka zaidi ya taarifa iliyotolewa awali.

Alitaja miili ya marehemu iliyotambuliwa kuwa ni Ibrahim Kilama (28), Mohammed Amir Shekaoneka (28 mkazi wa Korogwe na Omary Rashid (28) Tanesco Magomeni jijini Dar es salaam.

Wengine ni Lihatu Yahaya mtoto mchanga miezi mitatu mkazi wa Handeni ,Hassan Zabuni kondakta wa gari namba T. 124 DHW aina ya Toyota coaster na Emmanuel Cosmas (30) mkazi wa Chalinze .

Aidha Kamanda Wankyo alieleza, watu saba waliopata majeraha kwenye maeneo mbalimbali ya mili yao , kati yao watano wameruhusiwa baada ya kupatiwa matibabu na wengine wawili bado wapo hospital ya Tumbi Kibaha kwa ajili ya matibabu zaidi.

“Ajali hiyo ilitokea novemba 5, majira ya saa moja usiku baada ya gari namba T. 124 DHW aina ya Toyota coaster ikitokea Mkata kwenda Mbezi -Dar es salaam ,kuligonga kwa nyuma bila kuchukua tahadhari ,lori namba KBV 746C/ZE2861 FAW iliyokuwa imeegeshwa barabarani kutokana na kuharibika.”

Kamanda Wankyo alitaja chanzo cha ajali, ni uzembe wa dereva wa gari namba T. 124 DHW aina ya Toyota coaster kujaribu kulipita bila tahadhari gari jingine lililokuwa limeegeshwa baada ya kuharibika na wanaendelea kumsaka. 

Kutokana na ajali hiyo kamanda huyo alitoa wito kwa madereva, kutii sheria za usalama barabarani na kuacha tabia za kuendesha vyombo vya moto kwa mwendo kasi ili kuepuka ajali ambazo chanzo chake ni kukiuka sheria za usalama Barabarani.
 Kamanda wa polisi mkoani Pwani, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Wankyo Nyigesa, (katkati) akionesha Gari lililopata ajali, kushoto ni Mkuu wa Polisi Wilaya ya kipolisi Chalinze Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Janeti Magomi.

UJENZ WA BARABARA YA NJIA SITA UBUNGO-CHALINZE, MAANDALIZI YAANZA.

Muonekano wa barabara ya Morogoro eneo la Kimara mwisho Jijini Dar es salaam hivi leo ambapo tayari maandalizi  ya ule mradi wa ujenzi wa barabara ya njia sita kutoka Ubungo hadi Kibaha Mkoani Pwani yenye urefu wa kilometa 16 umeiva. Ujenzi wa barabara hiyo unaotarajia kuanza mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka huu utasaidia kukuza uchumi kwa kuongeza kasi ya usafirishaji wa bidhaa katika nchi jirani kupitia bandari ya Dar es Salaam.  Pia inatarajiwa utasaidia kupambana na changamoto ya msongamano wa magari na kuziwezesha barabara zote za Jiji la Dar es Salaam kupitika katika majira yote ya mwaka.  
Picha na IKULU

KILIO CHA BARABARA PANGANI HISTORIA MPYA IMEANDIKWA, MIAKA MITATU YA MAGUFULI.

Anaandika Mh.Jumaa Hamidu Aweso.
..
..
“Ndugu zangu Nina furaha sana huenda zaidi ya siku zote ukitoa siku niliopata ridhaa ya kuaminiwa na wana Pangani kua Mbunge wao.Asanteni sana.!
..
Kitu kinachoifanya siku hii ya leo kua ya kipekee sana ni BARABARA yetu ya PANGANI kupewa kibali rasmi cha matengenezo toka kwa Mh.Rais wetu Mpendwa Dk.John Pombe Magufuli na hapa nimefika ofisini kwa Katibu Mkuu Wizara ya Miundombinu Dodoma kujionea na kushukuru.
..
..
Ndugu zangu kila kilio kina mwenye ,;machozi ya furaha yamenitoka  nilipopewa habari hizi,nimekumbuka mbali sana tulivyoumia, tulivyoteseka pamoja na kwa miaka mingi sana kusubiri hili.
..
Hisia zimenipeleka mbali nilivokosa amani toka nilipopata ridhaa ya kua Mbunge namna nimekosa usingizi kila nikiwaza kulimaliza na kufanikisha hili,nilifikia hatua kila nikisimama Bungeni nasemea barabara tu,nilipiga mpaka MAGOTI kwa Waziri Mbarawa alipofika Pangani,nimeenda ofisi zote hamna sehemu sijafika kuisemea barabara hii,nimetembelea Media mbalimbali.,nimemuomba sana Mungu kila nifapo Dua.!
..
Leo ni siku ya kihistoria ninaomba kuwajulisha rasmi kua tunaenda kupata barabara ya kiwango cha lami na zoezi hili litaanza muda si mrefu.
Tumesema sana,tumepaza sauti kila kona,tumezungumza na kila aliehusika na sasa faraja kubwa hii hapa Mbele yetu.!
..
Nichukue nafasi hii kuwashukuru sana wana Pangani kwa uvumilivu wenu kipindi chote nilipowaambia naipambania barabara hii,na niwaombe tuendelee kua na subira mpaka mchakato unapoanza,nawashukuru sana kwa Dua zenu na nawaomba uzidi kuniombea nina mengi ya kufanya kwa ajili yenu.
..
Mwisho nikiri nimeupokea utendaji wa Mh.Raisi wetu wa Miaka mitatu kwa moyo wa furaha sana na Mungu ampe nguvu na Afya na maisha marefu tokana na hiki kilio cha muda mrefu kinachokwenda kufutika ikiwa ni kama Pangani tulikua pangoni sasa tunaenda kupaa angani.!


MAGAZETI YA LEO NOVEMBA 07, 2018.