Friday, May 18, 2018

YANGA YAPATA KOCHA MPYA, ASAINI MIAKA MIWILI

Kocha Mkongomani wa Yanga, Mwinyi Zahera, amesaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia klabu ya Yanga.

Zahera amechukua rasmi mikoba ya Mzambia aliyekuwa kocha mkuu wa kikosi cha Yanga baada ya kuondoka kimyakimya kurejea kwao Zambia katika klabu yake ya zamani, Zesco United.

Zahera alichelewa kusaini mkataba na Yanga kutokana na majadiliano baina yake na uongozi wa klabu hiyo, lakini sasa wamefikia mwafaka na ameamua kuweka kandarasi hiyo itakayomalizika mwaka 2020.

Licha ya kusaini mkataba huo, Katibu Mkuu wa Yanga, Biniface Mkwasa, mapema leo asubuhi alieleza kuwa Zahera ameondoka nchini kwenda kwao Congo kwa majukumu ya kukitumikia kikosi cha timu ya Taifa ya Congo.

Aidha, mkanganyiko umekuja mara baada ya kusema kuwa Zahera ameondoka akiwa bado hajasaini mkataba kutokana na makubaliano kutofikia mwafaka baina ya pande mbili kati ya Zahera na uongozi.

MAJID MWANGA AFUNGA MAFUNZO YA SUMA JKT GUARD LTD KIBAHA.


Kaimu Mkuu wa wilaya ya Kibaha Alhaj, Majid Mwanga alipokuwa akifunga Mafunzo ya vijana wa SUMA JKT GUARD LTD kundi la 08 katika kikosi cha 832 KJ kilichopo Mlandizi.
 
Kaimu Mkuu wa wilaya ya Kibaha Alhaj, Majid Mwanga, akizungumza wakati wa kufunga  Mafunzo ya vijana wa SUMA JKT GUARD LTD kundi la 08 katika kikosi cha 832 KJ kilichopo Mlandizi.
....................................

Taasisi za Serikali na zile za Binafsi wilayani Kibaha,  zimetakiwa kutumia walinzi waliopata mafunzo ya kitaalamu katika kukabiliana na majanga mbalimbali ili kuepuka usumbufu.

Wito huo umetolewa na Kaimu Mkuu wa wilaya ya Kibaha Alhaj, Majid Mwanga alipokuwa akifunga Mafunzo ya vijana wa SUMA JKT GUARD LTD kundi la 08 katika kikosi cha 832 KJ kilichopo Mlandizi.

Alisema vijana hao wamepata mafunzo mbalimbali ya kujihami na kupambana na uhalifu hivyo kuwatumia ni kuwa na uhakika wa ulinzi lakini pia ni kuonyesha uzalendo na imani kubwa kwa vijana hao ambao wamezalishwa na vikosi vya jeshi vyenye uzalendo.

Kaimu Mkuu huyo wa wilaya ya Kibaha ambae pia ni Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo alisema kufuatia kuwatumia vijana wanaotoka JKT hali ya hifadhi za misitu katika wilaya ya za Bagamoyo na Kibaha zimeimarika kwakuwa sasa hakuna mtu aneweza kuvamia kutokana na ulinzi wa SUMA JKT GUARD LTD.

Aidha, alitumia nafasi hiyo kuwaasa vijana wahitimu wa Shirika la Uzalishaji Mali la JKT (SUMA JKT GUARD LTD.) kuwa waadilifu, waaminifu na watiifu kwa viongozi wao ili kujenga nidhamu ya Jeshi na kulinda heshima ya kiapo walichokula kwa mujibu wa sheria.

Wakati huo huo Majid alitoa rai kwa Viongozi wa SUMA JKT GUARD LTD kuangalia uwezekano wa kuboresha maslahi ya  walinzi wao ili kuwapa moyo wa kufanya kazi hasa ukizingatia umuhimu wa sehemu wanazolinda na familia walizonazo.

Kaimu Mkurugenzi wa SUMA JKT, Kanali Endrew Mkinga aliwataka vijana hao wahitimu wa SUMA JKT GUARD LTD kuwa na nidhamu heshima na uadilifu ikiwa ni pamoja na kuepuka vitendo vya rushwa.

Askari ni mpinga rushwa namba moja hivyo ni wakawa wazalendo katika kuhakikisha kuwa wanakataa na kupambana na rushwa ndani na nje ya kazi.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa kikosi cha 832 KJ, Meja James Michael alisema vijana hao wamejifunza masomo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ulinzi binafsi kwa askari.

Aliongeza kuwa kutokana na mafunzo hayo vijana hao wako imara kupambana na aina yoyote ya uhalifu ikiwa ni pamoa na kujilinda wenyewe.

Awali wakisoma Risala mbele ya Mgeni Rasmi wahitimu hao walisema mafunzo wayoyapata yamewajengea uwezo katika nyanja mbalimbali ambapo watayatumia kuimarisha ulinzi na kujiongezea kipato kutokana na kazi watakazopata kwa taluma hizo.

Aidha waliongeza kuwa muda wote watakuwa watiifu kwa viongozi wao na kupokea maelekezo yatakayopelekea kuwajibika katika maeneo mbalimbali watakayopangiwa.
 
 Kaimu Mkuu wa wilaya ya Kibaha Alhaj, Majid Mwanga, (katikati) kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa SUMA JKT, Kanali Endrew Mkinga na kushoto Kaimu Mkuu wa kikosi cha 832 KJ, Meja James Michael
wakati wa kufunga  Mafunzo ya vijana wa SUMA JKT GUARD LTD kundi la 08 katika kikosi cha 832 KJ kilichopo Mlandizi.
 
wahitimu wakiwa wametulia kwa nidhamu kusikiliza hutuba za viongozi wakati kufunga mafunzo ya vijana wa SUMA JKT GUARD LTD kundi la 08 katika kikosi cha 832 KJ kilichopo Mlandizi.


JAFO ATOA SIKU TANO KWA HALMASHAURI 10 KUJIELEZA KUHUSU MATUMIZI YA FEDHA ZA MIRADI YA AFYA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Selemani Jafo akifungua kikao kazi juu ya utekelezaji wa miradi ya afya inayotekelezwa chini ya Mamlaka za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kilichowajumuisha Makatibu Tawala kutoka mikoa yote
nchini.
 .............................................
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI) Seleman Jafo ametoa siku tano
kwa wakurugenzi na waganga wakuu wa halmashauri 10 nchini kutoa
maelezo ya kina kwa nini halmashari hizo hazijafika asilimia kumi ya
matumizi ya fedha za miradi ya afya.


Jafo ameyasema hayo leo wakati akifungua kikao kazi juu ya utekelezaji
wa miradi ya afya inayotekelezwa chini ya Mamlaka za Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa kilichowajumuisha Makatibu Tawala kutoka mikoa yote
nchini.


Amesema halmashauri hizo zimeshindwa kutumia fedha zilizotolewa kwa
ajili ya miradi ya afya kama inavyotakiwa ambapo matumizi yake
yanaonekana kuwa chini ya kiwango, huku akizitaja halmashauri hizo kuwa
ni halmashauri ya wilaya ya Karatu, Mpimbwe, Mbulu Dc, Songwe,
Simanjiro, Mkinga, Mkuranga, Namtumbo, Nzega TC pamoja na Kilindi.


“Halmasharu hizi zina kila dalili ya kupata hati chafu, naagiza hadi kufika
siku ya Jumatano niwe nimepata majibu ya kuridhisha ni kwanini
hawajatumia fedha walizopewa kama maelezo yanavyotaka, tukiacha
kufanya kazi kwa mazoea tutapata matokeo mazuri, lakini kwa hali hii
tusitegemee matokeo mazuri kwa baadhi ya maeneo” Alisema Jafo


Kuwa upande mwingine Waziri Jafo aliwaagiza Makatibu Tawala hao
kuwaelekeza wakurugenzi wa halmashauri nchini kuwekeana malengo na
watumishi wao kwa kuwafanya tathmini ya uwajibikaji kila mwaka ili
kuongeza ufanisi na uwajibikaji kazini kwani bado wapo baadhi ya
watumishi wanafanya kazi kwa mazoea.


Amesema kuwa iwapo mtumishi wataonekana amefanya kazi chini ya
kiwango cha alama 50 kama ni mkuu wa idara atawajibishwa kwa
kushushwa cheo, na yule ambaye ataonekana kufanya vizuri zaidi alishauri
anastahili kupewa zawadi ya mfanyakazi bora wakati wa maadhimisho ya
siku ya wafanyakazi Duniani-Mei Mosi.


Aidha Waziri Jafo amesema kwa sasa kipaumbele cha utoaji wa fedha
kwa ajili ya miradi ya maendeleo zitatolewa kwa kuzingatia kipimo cha
matokeo mazuri kwa halmashauri husika, kwani kwa kufanya hivyo
itasaidia kuongeza uwajibikaji.


Wakati huo huo Waziri huyo aliagiza halmashauri zote nchini kuweka
mfumo wa matumizi ya mfuko wa afya ya jamii wa CHF iliyoboreshwa
sambamba ya kuhimiza matumizi ya ukusanyaji wa mapato wa njia ya
kimtandao ili kuepuka upotevu wa fedha za serikali.


Akizungumzia mafanikio ya mfuko huo Mratibu wa mfuko wa afya ya jamii
TAMISEMI, Nkinda Shekalaghe amesema kuwa hadi sasa mfuko huo
haujafikia lengo lililowekwa na serikali la kuunganisha wananchi kwa
asilimia 30 hadi kufikia mwaka 2015, kwani kwa mwaka 2016/2017
wamefikia asilimia 24.


Alitaja baadhi ya changamoto zinazoukabili mfuko huo kuwa ni pamoja na
utayari wa wananchi kujiunga na mfuko, huduma duni za afya, kutokuwepo
kwa mfumo rasmi wa utoaji wa taarifa pamoja na kiwango kidogo cha
uchangiaji ambapo amesema tayai wameshachukua hatua mbalimba
katika kukabiliana na changamoto hizo.
 

Wednesday, May 16, 2018

CCM BAGAMOYO YAIKAMUA CHALIWASA ITOE MAJI.

Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Bagamoyo, Abdu Rashidi Zahoro akiongoza Mkutano Maalu wa Halmashauri kuu ya CCM wilaya ya Bagamoyo.
.....................................
Halmashauri kuu ya CCM wilaya ya Bagamoyo katika kikao chake maalum kimetaka ufafanuzi wa kina kuhusu tatizo la maji linaloikabili Halmashauri ya Chalinze.

Wakizungumza katika Mkutano huo wajumbe wa Halmashauri kuu ya CCM wilayani humo walisema kwa muda mrefu sasa Chalinze kumekuwa na tatizo la Maji bila ya kupatiwa ufumbuzi wowote licha ya kuwepo Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Chalinze, (CHALIWASA)

Aidha wajumbe hao walimtaka Mkurugenzi wa Mamlaka ya maji safi na Usafi wa Mazingira Chalinze (CHALIWASA)  kutoa ufafanuzi wa kutosha ili wajumbe hao waweze kuwaelimisha wananchi juu ya tatizo hilo la maji.

Akijibu hoja ya za wajumbe mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Chalinze (CHALIWASA) Mhandisi Christer Mchomba alianza kwa kutoa historia ya mradi jambo ambalo wajumbe hawakulizika na kutaka majibu ya kwanini maji hayapatikani.

Aidha Mhandisi Mchomba alisema maji hayatoshi kusambaza eneo lote linalohudumiwa na CHALIWASA na hivyo huduma hiyo hutolewa kwa mgao jambo linalopelekea baadhi ya maeneo kukosa maji kwa siku kadhaa.

Akizungumzia uzalishaji wa maji katika mradi huo Mhandisi Mchomba alisema kwa siku wanan uwezo wa kuzalisha lita laki tatu tu ambapo katika Halmashauri ya Chalinze peke Mradi huo unahudumia vijiji 55 kati ya vijiji 58 vya Halmashauri hiyo.

Aliongeza kuwa, licha ya kuhudumia Halmashauri ya Chalinze mradi huo unahudumia wilaya tano zikiwemo Kibaha, Bagamoyo, Morogoro vijijini ambapo ukilinganisha ukubwa wa eneo la kutoa huduma na uwezo wa kuzalisha maji ni wazi kuwa kuna changamoto ya upatikanaji wa maji.

Kufuatia maelezo hayo wajumbe wa mkutano huo maalu wa CCM hawakuridhika na majibu hayo na kuomba taarifa kwa Mwenyekiti ambapo wajumbe walitaka kuelezwa kwa kifupi ni si kuleta historia ambayo wasingeweza kuwasilisha kwa wananchi ili wawaelewe.

Baada ya mjadala kuendelea Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Bagamoyo, Abdu Rashidi Zahoro amemtaka Mhandisi huyo kuwa na majibu ya uhakika ili wajumbe waridhike na kuwafahamisha wananchi.

Miongoni mwa mambo yaliyowachukiza wananchi ni pamoja ni pamoja na kuwa maji hayatoki siku zote lakini siku ya kufika kiongozi wa kitaifa maji yanatoka.

Mwandishi wa habari hizi alishuhudia baadhi ya vizimba vya CHALIWASA vikitumika kama duka badala ya sehemu ya kupatia maji.

Tatizo la maji katika Halmashauri ya chalinze limekuwa la muda mrefu ambapo mpaka sasa halijapatiwa ufumbuzi.

Awali akiwasilisha Taarifa ya utekelezaji wa ilani kwa mwaka 2017 kwa miradi mbalimbali, Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo ambae ni mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM wilaya, Alhaj Majid Mwanga alisema Serikali ya wilaya imeweka mikakati ya upatikanaji wa maji ikiwa ni pamoja na kutengeneza miundombinu ya maji kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.

Alisema wadau hao wakiongozwa na DAWASA ambao ndio wanaoshughulikia ujenzi wa miundombinu, DAWSC pamoja CHALIWASA ambazo zote ni taasisi za serikali zinazoshughulikia huduma ya maji.

Aidha, alisema pamoja na taasisi hizo za serikali, Serikali ya wilaya imeweza kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha huduma ya maji inapatikana ipasavyo wilayani humo.

Aliwataja wadau ambao waliweza kushirikiana na serikali ya wilaya katika kufanikisha huduma ya maji ni Pamoja na The Islamic Foundation yenye makao yake makuu mjini Morogoro ambayo iliweza kuchimba visima virefu na vifupi 50, katika kipindi cha mwaka 2017 tu, Dhi Nureyn Islamic Foundation yenye makao yake makuu mjini Iringa ilichimba visima 14 pamoja na jenereta katika maeneo ambayo hayakuwa na umeme, wengine ni taasisi ya waturuki ya REHEMA visima 40 na  Jumuiya ya watu wa Korea kusini walichimba visima 15.

Mkuu huyo wa wilaya alisema kufuatia uchimbaji wa visima hivyo hali ya upatikananji wa maji Halmashauri ya Bagamoyo imefikia asilimia 66 kwa mjini na asilimia na 74 kwa vijijini huku Halmashauri ya Chalinze ikiwa ni asilimia 56 mjini  na asilimia 58 vijijini.
Moja kati ya vizimba vya maji vya CHALIWASA katika Halmashauri ya Chalinze ambacho kimegeuzwa duka baada ya huduma ya maji kukosekana kwa muda mrefu kama kilivyokutwa na mpiga picha wetu.

 
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani Ramadhani Maneno ambae ni Mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM wilaya akizungumza katika Mkutano huo.
Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Alhaj, Majid Mwanga akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa ilani katika kipindi cha mwaka 2017.

Wajumbe wa Halmashauri kuu ya CCM wilaya ya Bagamoyo wakiwa katika Mkutano maalum ambao ulifanyika ukumbi wa Sekondari ya Lugoba.

Wakuu wa idara wa Halmashauri ya Chalinze wakiongozwa na Mkurugenzi wa Halmashauri hiy, Edes Lukoa, (mwenye suti) katika mkutano maalumwa Halmashauri kuu ya CCM.


Wakuu wa idara wa Halmashauri ya Chalinze wakiongozwa na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Fatuma Latu (wa tatu kushoto) katika mkutano maalumwa Halmashauri kuu ya CCM.

 Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Chalinze (CHALIWASA) Mhandisi Christer Mchombaakitoa maelezo kuhusu CHALIWASA.

Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Bagamoyo, Abdul Rashidi Zahoro (katikati) akiongoza mkutano maalum wa Halmashauri kuu ya CCM wilaya, Kulia ni Katibu wa CCM wilaya Kombo Kamote na kushoto ni Katibu mwenezi John Francis (Bolizozo). 

 Wajumbe wa Halmashauri kuu ya CCM wilaya ya Bagamoyo wakiwa katika Mkutano maalum ambao ulifanyika ukumbi wa Sekondari ya Lugoba.

RC NDIKILO AWAHAKIKISHIA WANANCHI KUSHUKA KWA BEI YA MAFUTA PWANI.

Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama mkoani Pwani,mhandisi Evarist Ndikilo(aliyeinama) wakati alipotembelea maduka ya bidhaa ya mafuta ya kupikia na sukari ,Loliondo ,Mailmoja ,Mjini Kibaha,(Wa pili kutoka kulia) ni kamanda wa polisi wa mkoa huo , (ACP) Jonathan Shanna na wa kwanza kushoto mwenyekiti wa wafanyabiashara Mkoani Pwani ,Abdallah Ndauka.
..........................................

Na Mwamvua Mwinyi,Pwani

SERIKALI mkoani Pwani,imewahakikishia wananchi kuwa inawasimamia wafanyabiashara wa mafuta ya kupikia ,washushe bei ya bidhaa hiyo ambayo kwasasa inauzwa lita moja sh.5,000 kutoka sh.3,200 iliyokuwa ikiuzwa kipindi cha nyuma.

Aidha imetoa onyo kwa wafanyabiashara wa sukari na mafuta hayo, ambao watajaribu kuficha bidhaa hizo kwa lengo la kujitajirisha haraka haraka baadae kwa kupandisha bei na kudai atakaefanya hivyo atakiona.

Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama mkoani Pwani,mhandisi Evarist Ndikilo aliyasema hayo wakati alipotembelea maduka ya bidhaa hizo ,Loliondo ,Mailmoja ,Mjini Kibaha huku akiwa ameambatana na kamanda wa polisi wa mkoa huo , (ACP) Jonathan Shanna .

Alisema Mei 16 mwaka huu,waliamua kutembelea baadhi ya magodauni na maduka ya bidhaa hizo ambapo wamejiridhisha kwa kukuta sukari ikiuzwa bei nzuri na maeneo mengine wakishusha madumu ya mafuta kwa ajili ya kuuzia walaji.

Ndikilo alieleza kwamba ,hategemei kuona wala kusikia kuna mfanyabiashara atakaefanya kitendo hicho ili bidhaa hizo ziwe adimu .
“Kama yupo mfanyabishara atakaejaribu kuficha mafuta na sukari kwa uroho wa fedha ,atakumbana na mkono wa sheria na hatutosita kumchukulia hatua za kisheria”

“Serikali inachunguza wote watakaoficha bidhaa hizo ,na jeshi la polisi mkoani hapa chini ya kamanda Shanna linaendelea na misako mbalimbali na kusimamia suala hili na wamejipanga”alisisitiza Ndikilo.

Akizungumzia sukari ,Ndikilo ambae pia ni mkuu wa mkoa huo,alisema bidhaa hiyo ilikuwa ikiuzwa 2,600 kwa kilo lakini imeshuka hadi 2,400/2,300 .
Mwenyekiti wa wafanyabiashara mkoani Pwani, Abdallah Ndauka aliwataka wafanyabiashara watoe huduma kama inavyostahili na kwa wakati.
Aliwaomba wazalishaji wa bidhaa  viwanda kuzalisha na kusambaza kwa wingi bila kuwakwaza wananchi.

Ndauka alisema kuwa,kama chama watawashughulikia wafanyabiashara watakaokwamisha jambo hilo na kuwaasa wawe sehemu ya kutoa huduma stahiki hasa mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.

Nae kamanda wa polisi mkoa wa Pwani ,Shanna alisema wameyabeba maagizo yaliyotolewa na kusema wanajua magodauni,store na maduka yote yanayouza bidhaa hizo hivyo asithubutu mfanyabiashara kulijaribu jeshi hilo.
Shanna alielezea,ameshayapokea maelekezo kazi yake kubwa ni utekelezaji wa vitendo kwani wanaintelijensia ya kutosha.

Kwa upande wao wafanyabiashara akiwemo Kassim Haji ,alisema mafuta ya kupikia yalipotea lakini kwasasa kuanzia Mei 16 yameanza kuingia na kwa yeye anatarajia kupokea madumu 600.

Alisema wanatarajia kushusha bei baada ya kuanza kupelekewa mafuta kwani awali kulikuwa na shida bandarini na anaahidi kushusha gharama ya bidhaa hiyo.

Nao baadhi ya wananchi waliokuwepo soko la Loliondo kwa ajili ya kujinunulia vyakula na bidhaa mbalimbali akiwemo Zulfa Rashid ,alisema bidhaa inayowaumiza ni mafuta ya kupikia.

Aliomba mafuta hayo yashushwe bei kwani yanauzwa kwa sh,5,000 kwa lita moja fedha ambayo ni kubwa na maisha ni magumu hasa kuelekea kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani.

“Tunaomba gharama zishushwe ,serikali isimamie suala hilo,na tunashukuru mkuu wa mkoa kuja kuzungumza na sisi ,pamoja na kutuhakikishia bidhaa hizo zitashushwa bei.

Zulfa alisema, wengi wao wanatumia nazi na kuacha kununua mafuta kutokana na gharama kupanda tofauti na zamani.

Tuesday, May 15, 2018

MAKAMU WA RAIS APOKEA VIFAA VYA UPASUAJI KUTOKA UBALOZI WA KUWAIT

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimsalimia mtoto Daniella Wilfred Pallangyo mwenye umri wa miaka 8 ambaye ana matatizo ya kichwa kikubwa wakati wa hafla ya kupokea vifaa vya chumba cha upasuaji wa watoto vilivyotolewa na Ubalozi wa Kuwait kwa Taasisi ya Mifupa (MOI).
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Balozi wa kuwait nchini Mhe. Jasem Al Najem wakati wa hafla ya kupokea vifaa vya chumba cha upasuaji wa watoto vilivyotolewa na Ubalozi wa Kuwait kwa Taasisi ya Mifupa (MOI).
............................

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema uboreshaji wa huduma katika hospitali zetu za kibingwa kama MOI, zitaipunguzia Serikali mzigo wa kupeleka wagonjwa nje ya nchi na hivyo kutekeleza azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuboresha huduma za afya kwa wananchi.

Makamu wa Rais ameyasema hayo wakati wa kupokea vifaa vya Chumba Cha Upasuaji wa Watoto vilivyotolewa na Ubalozi wa Kuwait kwa Taasisi ya Mifupa (MOI) leo tarehe 15 Mei, 2018.

“ Aidha kwa namna ya kipekee nakushukuru Mheshimiwa Balozi wewe binafsi na Serikali ya Kuwait kwa ushirikiano ambao mnaendelea kuipatia Serikali yetu ya awamu ya Tano katika Sekta mbalimbali za maendeleo lakini hasa hasa katika sekta ya afya” alishukuru Makamu wa Rais.

Makamu wa Rais amesema kuwa Balozi wa Kuwait Mhe. Jasem Al Najem amekuwa mstari wa mbele katika kuendeleza sekta ya Afya hapa nchini ambapo leo wamesaidia vifaa vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 258 ambavyo vitaiwezesha Taasisi kuimarisha utoaji wa huduma ya upasuaji hasa kwa watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi.

Makamu wa Rais amesema msaada huo utaiwezesha Taasisi kuwa na chumba cha upasuaji ambacho kitakuwa maalum kwa watoto tu, hivyo idadi ya wagonjwa watakaopata huduma ya upasuaji itaongezeka kutoka 500-700 kwa mwezi, kufikia zaidi ya wagonjwa 1000 kwa mwezi na watahudumiwa kwa haraka zaidi.

Wakati huo huo Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Faustine Ndugulile  amesema Tanzania iatendelea kuimarisha uhusiano na nchi ya Kuwait kwani wamekuwa mstari wa mbele katika kutoa msaada haswa msaada inayohusu sekta ya afya.

Balozi wa Kuwait hapa nchini Mhe. Jasem Al Najem amesema kuwa Wananchi wa Kuwait wana mapenzi makubwa na Watanzania na kuahidi wataendelea kutoa msaada.

Tuesday, May 8, 2018

SERIKALI KUFUTA LESENI 587 ZA MADINI.

Serikali imesema itazifuta leseni za madini 587 ambazo hazijaendelezwa ili kukomesha tabia ya ulanguzi wa leseni hizo.

Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni Wilayani Bagamoyo na Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko alipokuwa akizungumza katika kikao cha pamoja kati ya wamiliki wa migodi ya madini wa Halmashauri ya Chalinze na wajumbe serikali za vijiji.

Biteko alisema wapo watu ambao wamechukua leseni za madini lakini mpaka sasa hawajaziendeleza na hivyo kukwamisha juhudi za mandeleo ya vijiji husika na Taifa kwa ujumla.

Aidha alibainisha kuwa wapo ambao wamechukua leseni lakini hawana mpango wa kuanza kazi na badala yake wanasubiri mwenye kuhitaji ili wamuuzie na kuonya kuwa watazifuta.

Alisema tayari mchakato umeshaanza wa kufuta leseni za madini 587 ambazo hazijaendelezwa.

Katika hatua nyingine aliwataka wawekezaji wote walioahidi kutekeleza miradi ya maendeleo kwenye vijiji kutekeleza haraka iwezekanavyo na kwamba amemuagiza Mkuu wa wilaya kushughulikia hilo na kwamba taarifa yake aipate baada ya siku saba tu.

Alisema wawekezaji wengi wameingia makubaliano na serikali za vijiji na kisha hawatekelezi makubaliano hayo na hatimae kuzorotesha shughuli za maendeleo.

Awali akizungumza mbele ya Naibu waziri wa Madini, Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete alisema mgongaano wa sheria ni miongoni mwa changamoto zinazoikabili sekta ya madini kwa serikali za vijiji ukilinganisha mamlaka iliyonayo wizara ya madini na serikali za vijiji.

Alisema wakati mchakato wa kijiji unaendelea ili kujiridhisha na muwekezaji tayari muwekezaji ameshapewa leseni na wizara au kibali kutoka kamishna wa madini wa kanda jambo ambalo linaleta mkanganyiko
 

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko akizungumza na wamiliki wa Migodi ya madini pamoa na waumbe wa serikali za vijiji katika Halmashauri ya Chalinze.

 
  Wamiliki wa Migodi ya madini pamoa na waumbe wa serikali za vijiji katika Halmashauri ya Chalinze wakimsikiliza Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko (hayupo pichani)

Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Alha, Maid Mwanga akimkaribisha Naibu Waziri wa Madini.

Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete akizungumza kwenye Mkutano huo.