Monday, March 19, 2018

MAGARI 50 YA WAGONJWA YAGAIWA KWA HALMASHAURI.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe. Selemani Jafo (Mb) akimkabidhi moja ya gari la wagonjwa aina ya Suzuki Maruti, Ashura Nkya ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Babati katika bandari ya Dar es Salaam jana.
Baadhi ya magari aina ya Suzuki Maruti ambayo Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliamuru yagawiwe katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuhudumia Sekta ya Afya nchini.
.......................................

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Selemani Jafo, ameendesha zoezi la kugawa magari 50 ya wagonjwa aina ya Suzuki Maruti (Ambulances) kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini Jijini Dar es Salaam.

Magari hayo ambayo awali Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliagiza yafanyiwe utaratibu wa kisheria wa kiforodha na yagawanywe kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa ili yatumike kwa kuwahudumia wananchi katika vituo mbalimbali vya afya nchini.

“Hii ni agenda ya Mhe. Rais ya kutaka kuhakikisha watanzania wanapata huduma bora, ambulance hizi ulaji wake wa mafuta ni mdogo sana na zitatusaidia katika halmashauri nyingi,”amesema Jafo.

Aidha, Mhe. Jafo amemshukuru sana Rais wa John Magufuli kwa kuonyesha mapenzi makubwa lakini pia amependezwa na Watumishi wa Wizara, Mikoa na Halmashauri zote kuweza kuhudhuria hafla hiyo muhimu iliyofanyika bandarini Jijini Dar es Salaam.
 
Naye Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Afya Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt. Zainabu Chaula amemshukuru Waziri wa Nchi TAMISEMI na Waheshimiwa Wabunge wote kwa utendaji wao na kuwataka wabunge kuwa na lugha ya ufahamu mmoja ili kuboresha utendaji Serikalini.

“Kwa niaba ya watendaji nawashukuru sana waheshimiwa Wabunge, nilitamani tutembee pamoja kwa maana ya kuwa na uelewa wa pamoja na ndio maana Mhe.Waziri amewakabidhi wabunge magari nao watukabidhi sisi,”Amesema.

Charles Kichere Kamishna Mkuu wa Mapato Tanzania, amesema awali magari hayo aliyaona Mhe. Rais alipofanya ziara bandarini na kwamba magari hayo yalikuwa yameteleekezwa na mmiliki wake kutofahamika na ndipo rai, aliagiza kufuata utaratibu wa forodha na kuyataifisha magari hayo na kasha yagawiwe kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini.

Kwa upande wake Mhe. Prof Norman Sigalla King, Mbunge wa Makete, amemshukuru Mhe. Rais kwa kutoa ambulance hizo kwa ajili ya kuimarisha huduma za mama wajawazito.

“kwanza nitoe shukrani za pekee kabisa kwa kupewa ambulance kwa ajili ya wilaya yangu ya Makete nakumbuka niliomba kwa ajili ya tarafa za Ukutama, Matamba, Magomba, Tulongwa na Niwaho”amsema.

Amebainisha umbali wa kata ya Ukutama hadi Makete mjini ni kilomita 70 na hivyo itawanusuru wakina mama dhidi ya vifo vya uzazi visivyotarajiwa.

Kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya Kigoma, Hakimu Ndatama amemshukuru Mhe. Rais kwa kuwapatia ambulance ambayo itaokoa vifo vya akina mama na watoto kwa kiasi kikubwa.

MAGAZETI YA LEO TAREHE 19 MARCH 2018.

Sunday, March 18, 2018

MOTO WATEKETEZA NYUMBA BAGAMOYO.


Nyumba moja imeteketea kwa moto baada ya mota huo kutokea ndani ya nyumba hiyo majira ya saa sita mchana kitongoji cha Bong'wa kata ya Magomeni wilaya ya Bagamoyo.

Tukio hilo la ilimesababisha taharuki kwa wakazi wa mitaa ya jirani baada ya mitungi ya gesi iliykuwemo ndani ya nyumba hiyo kulipuka kwa sauti nzito na kuruka umbali kutoka ndani nyumba hiyo.

kufuatia hali hiyo wananchi wameweza kutoa ushirikiano ili kuudhibiti moto huo usiingie nyumba nyingine ambazo zimejengwa kwa karibiana.

Aidha Jeshi la zimamoto na uokoaji Bagamoyo limeweza kufika eneo la tukio na kuwahi kuudhibiti moto usende nyumba nyingine nyumba iliyoshika moto ikiwa tayari imeshika mota kwa kasi kutokana na mitungi ya gesi iliyokwemo ndani ya nymba hiyo.

Afisa wa zamu wa zima moto, ambae ni  Mkaguzi Msaidizi wa Zimamoto, A/INSP. Samweli Ponela alisema toka kupata taarifa hiyo imewachukua dakika tano kufika eneo la tukio na kuanza kupambana na moto huo.

Aidha, Ponela alitoa wito kwa wananchi kutoa taarifa za majanga ya moto kupitia namba 114 na sio namba za watu binafsi ambao huwenda hawapo kazini.

Alisema taarifa ya tukio hilo wameipata kupitia askari wa zimamoto ambae hakuwa zamu jambo ambalo husababisha pia kuchelewa kupata taarifa za moto.

Chanzo cha moto huo hakijafahamika ingawa inaaminika ni kulipuka kwa mtungi wa gesi ambapo jumla mitungi ya gesi kumi na sita 16 imekutwa ndani huku mitungi sita ikiwa imeripuka yenyewe kabla ya kulipuliwa na jeshi la zimamoto.

Miongoni mwa watu waliokimbilia tukio hilo mama mmoja ambae hakufahamika jina lake alijeruhiwa na mtungi wa gesi baada ya mtungi wa gesi kulipuka na kuruka umbali wa mita mita 15 ambapo mama huyo ulimjeruhi kwenye miguu.

MBEGU YA MAHINDI YA W. 21 09 YAZINDULIWA BAGAMOYO.

Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Majid Mwanga ( wa pili kushoto mwenye miwani) akizindua rasmi Mbegu ya mahindi ya W. 21 09 katika msimu wa kilimo 2018. pamoja nae kulia ni Mkurugenzi wa fedha na utawala, Shabani Hussein kutoka Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) na wapili kulia ni
mtafiti wa mbegu hiyo ya mahindi ya  W. 21 09 kutoka kituo cha utafiti Ilonga wilayani Kilosa, Mikidadi Hamidu.

Na Athumani Shomari
......................................

Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Majid Mwanga amezindua Mbegu bora ya Mahindi ya W. 21 09 katika msimu wa kilimo 2018 itakayotumika na wakulima wa mahindi kwaajili ya kuzalisha mahindi mengi na yenye ubora.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Mkuu huyo wa wilaya alisema mbegu hiyo itawapa fursa wananchi wa Bagamoyo kuvuna mazao mengi na yenye ubora hali itakayowasaidia kukabiliana na soko la ajira wilayani humo.

Alisema wilaya ya Bagamoyo ipo katika ujenzi wa viwanda hivyo ili mwananchi aingie kwenye ushindani wa ajira anahitaji kuwa na chakula kitakachomuwezesha kuwa na utulivu wa akili na mwili.

Akizungumzia utafiti mkurugenzi wa fedha na utawala, Shabani Hussein kutoka Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) alisema tume hiyo inafadhili tafiti mbalimbali ikiwemo mbegu za mahindi na muhogo ili wakulima wapate matokeo mazuri ya kile wanachopanda.

Afisa mipango wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Bestina Daniel alisema mbegu hiyo ambayo imefanyiwa utafiti katika kituo cha Ilonga kilichopo Kilosa imetia michakato yote ya kuthibitishwa na kuidhinishwa kwaajili ya kuingia sokoni kwa matumizi.

Nae mtafiti wa mbegu hiyo ya mahindi ya  W. 21 09 kutoka kituo cha utafiti Ilonga wilayani Kilosa, Mikidadi Hamidu alisema Mbegu hiyo ya mahindi ina uwezo wa kutoa gunia 35 kwa ekari moja endapo mkulima atazingztia kanuni za kilimo cha mahindi.

Kwa upande wake, Afisa kilimo wa Mkoa wa Pwani George Kapilima alisema wilaya ya Bagamoyo inaongoza kwa kilimo cha mahindi Mkoani wa Pwani, huku zao la mahindi likishika nafasi ya pili baada ya zao la muhogo mkoani humo.

Alisema katika msimu wa kilimo wa mwaka 2016/2017 Mkoa wa Pwani ulizalisha tani laki moja na kumi 110,000 ambapo Halmashauri ya Chalinze iliyopo ndani ya wilaya ya Bagamoyo ilizalisha tani elfu sitini na tano 65,000 za mahindi.

Alisema mazao yanayoongoza mkoani Pwani ni Muhogo, Mahindi na Mpunga ambapo alisema mbegu hiyo ya W. 21 09 itasaidia kuongeza uzalishaji wa zao la mahindi wilaya ya Bagamoyo na Mkoa wa Pwani kwa ujumla.

 Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Majid Mwanga, akipanda mahindi ikiwa ni ishara ya kuzindua rasmi mbegu ya W. 21 09 katika kitongoji cha Kilemela kata ya Kerege wilayani Bagamoyo.

Afisa kilimo wa Mkoa wa Pwani George Kapilima kushoto
akipanda mahindi ikiwa ni ishara ya kuzindua rasmi mbegu ya W. 21 09 katika kitongoji cha Kilemela kata ya Kerege wilayani Bagamoyo.
 mkurugenzi wa fedha na utawala, Shabani Hussein kutoka Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) akizungumza katika uzinduzi wa mbegu mpya ya mahindi ya W. 21 09.

Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Majid Mwanga ( wa pili kushoto mwenye miwani) akizindua rasmi Mbegu ya mahindi ya W. 21 09 katika msimu wa kilimo 2018. pamoja nae kulia ni Mkurugenzi wa fedha na utawala, Shabani Hussein kutoka Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) na wapili kulia ni

mtafiti wa mbegu hiyo ya mahindi ya  W. 21 09 kutoka kituo cha utafiti Ilonga wilayani Kilosa, Mikidadi Hamidu, anaekabidhiwa ni Anna Macha kutoka kikundi cha Tupendane kijiji cha Kongo.

MWALIMU JOHN MPONDA WA TaSUBa AFARIKI.


Mwalimu wa sanaa Bagamoyo, kutoka Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) JOHN MPONDA, amefariki dunia leo Tarehe 18 Mach 2018, TaSUBa zamani ilijulikana kama Chuo Cha Sanaa Bagamoyo

Mwalimu Mponda ambaye ni Mtaalam wa Dance Theory na Dance Choreography Chuoni hapo ndiye pia alikuwa Mwenyekiti wa Tamasha la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo amefariki mapema hii leo katika Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Aidha, amekuwa akiigiza katika matangazo ya TV ya Taasisi mbalimbali kuhusu ujumbe wa kujikinga na Malaria na pia HAKI ELIMU.


Mwalimu John Mponda atakumbukwa kwa ucheshi wake akiwa kazini hata nje ya kazi kwa watu wa rika zote.

Taratibu za mazishi zinafanyika nyumbani kwake Blok P Bagamoyo na baadae kutolewa maamuzi ya lini atazikwa na wapi.
 Mwalimu John Mponda kushoto enzi za uhai wake akiwa katika majukumu yake ya kikazi.

Friday, March 16, 2018

YANGA YAAPA KUPINDUA MATOKEO BOTSWANA HAPO KESHO LIGI YA MABINGWA AFRIKA



Yanga inaendelea na maandalizi yake ikiwa ugenini kwa ajili ya mchezo wao wa marudiano wa klabu bingwa Afrika dhidi ya Township Rollers ya Botswana utakaochezwa siku ya Jumamosi machi 17, 2018.

Mjumbe wa kamati ya utendaji na Katibu wa Kamati ya Mashindano Yanga Samuel Lukumay amesema kambi inaendelea vizuri kila kitu kipo sawa na wachezaji wote waliosafiri na timu wako salama kwa ajili ya mchezo wa Jumamosi.

“Maandalizi yanaendelea vizuri hatukupata shida yoyote tangu tunakuja hadi tumefika, tulitembelewa na balozi wa Tanzania nchini Afrika kusini ambaye ndio anasimamia pia Botswana akapata muda wa kuzungumza na vijana na kuwatia hamasa na kuwaambia katika mpira kilakitu kinawezekana kwa hiyo tunaweza kugeuza matokeo.”

“Hakuna majeruhi yoyote kiujumla kambi inaendelea vizuri bila tatizo lolote”
Mchezo wa awali uliozikutanisha yanga na Township Rollers kwenye uwanja wa Taifa, yanga ilipoteza kwa kufungwa 2-1 hivyo inahitaji kushinda kuanzia 2-0 ili kukata tiketi ya moja kwa moja kufuzu hatua ya makundi ya vilabu bingwa Afrika.

TAIFA STARS YASHIKA MKIA AFRIKA MASHARIKI KATIKA VIWANGO VYA UBORA WA SOKA DUNIANI



Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA), limetoa orodha ya Viwango Vya Ubora wa Soka ambapo Tanzania imeshika nafasi ya mwisho ukanda wa Afrika Mashariki.

Uganda inaongoza kwa Afrika Mashariki ikiwa nafasi ya 78 huku Kenya ikiwa nafasi ya pili kwa kushika namba 105, Rwanda ya tatu ikiwa nafasi ya 112 na Tanzania ikiwa mkiani katika nafasi ya 146.

Kwa upande wa Afrika, Tunisia inaongoza kwa kushika nafasi ya 23 huku Germany wakisalia nafasi ya kwanza Duniani na Brazili ikiwa nafasi ya pili.
Kumi bora ya FIFA ipo namna hii

1: GERMANY
2: BRAZIL
3: PORTUGAL
4: ARGENTINA
5: BELGIUM
6 :POLAND
7: SPAIN
8: SWITZERLAND
9: FRANCE
10: CHILE

WANAVYUO WAFUNDISHE KUJIAJIRI- KASSIM MAJALIWA.



Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Profesa William Anangisye, ofisini kwa Waziri Mkuu Mjini Dodoma, Machi 16, 2018.
...........................................


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema ni umuhimu mfumo wa ufundishwaji wa wanafunzi wa vyuo vikuu nchini ukaboreshwa ili wanapomaliza waweze kujiajiri.

“Kumekuwa na tatizo kubwa la wasomi wetu kuwa na mtazamo kwamba wanapomaliza masomo yao lazima waajiriwe. Upo umuhimu wa kubadili mtazamo huo kwa kuwapa mbinu zitakazowawezesha kujiajiri.”

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Machi 16, 2018) alipokutana na kufanya mazungumzo na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Prof. William Anangisye, ofisini kwake mjini Dodoma.

Amesema wanafunzi hao wanapomaliza wanatarajiwa wawe na uwezo wa kubuni mbinu mbalimbali za kujiajiri na kuondokana na mtazao wa kusubiri ajira za kuajiriwa maofisini.

Waziri Mkuu amesema wasomi hao wanaweza kuchukua kauli mbiu ya Rais Dkt. John Magufuli ya uchumi wa viwanda kwa kuanzisha kilimo cha mazao mbalimbali yatakayotoa malighafi za viwandani.

Pia Waziri Mkuu amesema wasomi hao wanaweza kujikita katika shughuli za uchimbaji wa madini au usindikaji wa mazao mbalimbali, hivyo tayari watakuwa wamejiajiri kwa sababu ajira si za ofisini pekee.

Aidha, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kumpongeza Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam aliyestaafu Profesa Rwekaza Mukandara kwa kazi nzuri aliyoifanya kipindi cha uongozi wake.

Kwa upande wake, Profesa Anangisye amesema mzigo aliopewa wa kuiongoza taasisi hiyo si mwepesi, hivyo ameahidi kufanya kazi kwa bidii na hatokwenda kinyume na matarajio ya Serikali ya Awamu ya Tano.

Kiongozi huyo amesema katika kuhakikisha wanaboresha masomo chuo hapo wameanzisha skuli ya kilimo na uvuvi, hivyo wanatarajia kuanzisha mashamba ya mfano kwa ajili ya mazao mbalimbali.


FEDHA ZETU ZINALETA MAENDELEO- RAIS DKT. MAGUFULI .



Uzinduzi wa tawi la CRDB Chato uliofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli unadhihirisha Tanzania ya maendeleo ni lazima.

“Kujenga standard gauge kwa shilingi trilioni 7.6 fedha za ndani, msifikiri watu wanafurahi” “Tunapoamua kujenga Stigler’s Gorge ambayo itazalisha umeme zaidi ya megawati 2100 usifikiri wanaweza kufurahi” ”Tunapoweza kununua ndege kwa fedha zetu, kitu ambacho tulishindwa kwa miaka 50 usifikiri watu wanafurahi” “Tunapoweza kulipa mishahara tarehe 21 usifikiri wengine wanafurahi”. Rais Magufuli.

Maneno hayo ya Rais yametokana na utekelezaji wa miradi mikubwa kadhaa ya maendeleo, kupiga vita rushwa, uboreshaji wa huduma za jamii hususan elimu bure, afya, usambazaji wa umeme, maji na matumizi sahihi ya fedha za Umma zimeipaisha Tanzania kiuchumi.

Nina hakika sio rahisi kumshawishi Mwingereza au nchi yeyote iliyobobea kwenye uchumi mkubwa iwapo unafanya hovyo hovyo, eti akushabikie kuwa nchi yako uchumi wake unamuelekeo mzuri na itafika mbali. 

Lakini leo sio ajabu maana imetokea Tanzania ambayo ina muelekeo mzuri wa uchumi na inatabiriwa kufika mbali kimaendeleo.

Penye ukweli uongo hujitenga, Waziri anayeshughulikia masuala ya Afrika nchini Uingereza Stewart Rory ameeleza namna alivyovutiwa na mabadiliko yanayofanywa kwenye sekta ya elimu, kupitia sera ya elimu bure ambayo imewezesha kuwepo kwa ongezeko kubwa la udahili wa wanafunzi.

Kufuatia mabadiliko hayo Uingereza imetoa Paundi milioni 140 kusaidia maboresho katika miundombinu ya utoaji wa elimu hususan ujenzi wa madarasa na nyenzo za ufundishaji.

 “Nimetembelea shule za msingi na kushuhudia mabadiliko makubwa yaliyofanyika, ikiwemo utoaji elimu bure. Tutatoa zaidi misaada kusaidia masuala ya kitaaluma, ikiwemo ujenzi wa madarasa”. Amesema Rory.

Aidha, Balozi wa ufaransa nchini Friederic Clavier alipokwenda kumtembelea Mhe. Samia Suluhu Hassan Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ofisini kwake Jijini Dar-es-salaam, alisema kuwa, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, anaunga mkono juhudi za dhati zinazochukuliwa kuhakikisha uchumi wa Tanzania unaimarika.

“Rais wa Ufaransa anauhakika na Tanzania ijayo na anaunga mkono jitihada za maendeleo zinazofanywa na Rais Magufuli” amesema Clavier.

Naye, Muwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, kwenye masuala ya Watoto Profesa Virginia Gamba amesema kuwa anaipongeza Tanzania kwa jitihada za kudumisha amani ndani na nje ya nchi.

Aidha, amesema;“Tanzania ni miongoni mwa nchi ya kuigwa Afrika zinazopiga hatua kubwa ya maendeleo zinazopaswa kutiliwa mfano lakini yote hiyo inatokana na umadhubuti wa serikali yake na Jeshi la Wananchi wa Tanzania”.

Pia, Muwakilishi wa Benki ya Dunia katika nchi za Burundi, Malawi na Somalia Bibi Bella Bird tarehe 4 Desemba mwaka jana akiwa Ikulu Jijini Dar-es-salaam, alimuhakikishia Rais Magufuli kuwa taasisi hiyo, imejipanga kuendelea kutoa mikopo nafuu kwa miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini. 

Hii yote ni kwa sababu ya usimamizi mzuri wa fedha za maendeleo ambazo zinasimamiwa na serikali ya Rais John Pombe Magufuli
Bibi Bird amesema “2016 Benki ya dunia ilitoa mkopo nafuu yenye dhamani za Dola ya Marekani bilioni 1.2, ambazo zilikuwa sawa na trilioni 2.7 fedha ya Tanzania. Fedha hizi zimekwenda katika miradi mbalimbali na tunafurahi kuwa zimetumika vizuri kama ilivyokusudiwa’

Benki ya Dunia imetoa kipaumbele katika miradi ya miundombinu ya barabara na reli, kuongeza usambazaji na uzalishaji wa nishati ya umeme, tekinolojia ya habari na mwasiliano,  elimu, ili kuhakikisha idadi ya wanaopata elimu inaongezeka, uboreshaji wa sekta ya afya,  na kuongeza upatikanaji wa maji safi.

Akizungumzia hali ya uchumi Wilayani Chato Rais Magufuli amesema;”Kwa sasa tupo kwenye mstari sahihi nawaomba Watanzania mvumilie ili tufike mahali ambako Tanzania itakuwa nchi ya asali” 

Rais Magufuli anamaanisha kuwa, Tanzania itakuwa nchi ya asali kweli kutokana na mbio, kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano hii ni dhahiri bila kificho. Mpaka sasa kila kitu cha maendeleo kinachofanywa na Serikali kinawekwa hadharani ili kudhihirisha imedhamiria kutenda inachosema.

“Niliapa kwa Katiba kwamba nchi hii lazima iwe ya amani nataka tujenge uchumi wa kweli” amesema Rais Magufuli.

Haiingii akilini nje ya Tanzania watu wanaona mbio za maendeleo zinavyoshika kasi hapa nchini, na kutabiri matokeo yake kuwa ni ustawi wa nchi na watu wake. Lakini ndani ya Tanzania waone ni mateso, kutoa maneno yasiyofaa na kutaka kufanya vitu vinavyovuruga amani, upendo na mshikamano jambo hili tulikatae.

Vilevile, Rais aliongeza kuwa Tanzania ya viwanda imeanza kupatikana na kinachohitajika ni kuongeza juhudi bila kujali vitisho na maneno ya kukatisha tamaa kutoka kwa yeyote ndani au nje ya nchi.

 “Tunaposema viwanda kuna mataifa yahapendi. Hata tukitaka kujenga viwanda vya nguo hawataki kwa sababu wananufaika. Wanataka tulime Pamba kisha tuwauzie wao watengeneze nguo kisha wazivae halafu watuletee mitumba”. Amesema Rais Magufuli

Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya madini, Royalty Exploration Corporation (TRX) kutoka Canada James Sinclair amesema; “Rais wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli amekaribisha wawekezaji zaidi baada ya kupiga vita rushwa na udanganyifu katika mfumo”.  

Aidha, Sinclair aliongeza kwa kusema kuwa, Serikali imeweka mazingira mazuri ya kiuchumi na kisiasa kuhusu uwekezaji nchini Tanzania. Ambapo kampuni yake imeingia makubaliano na Wakala wa Madini Tanzania (STAMICO) miaka kadhaa iliyopita, lakini haikuathiriwa na mabadiliko ya sheria, kwa kuwa walishaingia katika mabadiliko ya ulipaji wa kodi.  

Akizungumzia suala la viwanda wakati wa uzinduzi wa kiwanda cha sigara cha Philip Moris Tanzania Ltd, kilichopo mjini Morogoro, Rais amekuwa mwalimu mzuri na kutoa somo kwa Watanzania kuwa kiongozi mzuri ni yule anayetatua kero na sio anayetengeneza kero.

“Serikali imejifunza kutokana na makosa ya hapo nyuma ya kuweka kodi kubwa kwenye  viwanda ambapo ilisababisha viwanda vingi kufa, sasa mazingira mazuri yanawekwa ili kulinda viwanda hivyo”; amesema Rais Magufuli

Kitendo ambacho kinashawishi wawekezaji wengi kuja Tanzania kuwekeza pamoja na wazawa kama alivyofanya Philip Moris Tanzania Ltd na Mansoor, au kiwanda cha sukari kinachotarajiwa kuzinduliwa ambacho kinajengwa  na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA).

Tumuunge mkono Rais kwa kila jambo analotekeleza ili tuende sote kwa pamoja, tuweze kutumia fursa mbalimbali za kazi, biashara na uwepo wa soko la uhakika la Afrika Mashariki lenye idadi ya watu takribani milioni 200. Pia, soko lipo la Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) 665.

Mafanikio yote hayo yametokana na usimamizi mzuri wa matumizi ya fedha za umma kwenye wa miradi mikubwa ya maendeleo ambayo ni gumzo ndani na nje ya Tanzania. Miradi hiyo ni pamoja na mradi wa reli ya kisasa unaojengwa kwa fedha za ndani ni mfano wa kuigwa  Barani Afrika, Bomba la Mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga  na mradi wa Umeme wa Stiglers Gorge wa Rufiji.

Miradi mingine ni ununuzi wa ndege 6, ujenzi wa kiwanda cha kimiminika cha gesi Mkoa wa Lindi, Mpango wa Elimu Bure, Mabasi ya mwendo kasi na Tanzania ya viwanda kila Mkoa viwanda 100. Aidha ujenzi wa meli katika ziwa Nyasa, Victoria na Tanganyika, Mpango wa umeme Kinyerezi 11, 111, usambazaji wa umeme vijijini, upanuzi wa viwanja vya ndege na vita dhidi ya rushwa.